1
Uislamu Kwa Kifupi
الإسلام في سطور باللغة السواحيلية –
Dr. MUHAMMAD IBRAHIM AL-MASRI
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema,
Mwenye kurehemu.
MOSI: - UISLAMU NI NINI?:
Uislamu ni kutii anayotaka Mwenyezi Mungu na kufuata sheria yake. Kwa hakika vitu vyote na matukio yote katika ulimwengu huu - ukimtoa mwanadamu – moja kwa moja vinatii kanuni zilizowekwa na Mwenyezi Mungu, yaani vinamtii Mwenyezi Mungu na vinakwenda sambamba na kanuni zake, na hii ndio maana ya Uislamu. Neno Uislamu katika lugha ya Kiarabu linatokana na mzizi wa neno "Salama" linalonyumbulika na kutoa neno: Salamu (amani), utakatifu, unyenyekevu na utiifu.
Mwanadamu anatofautiana na viumbe vingine kwa sifa ya uerevu na uhuru wa kuchagua, kwa hiyo, Uislamu unamlingania (mwanadamu) - baada ya kukinaika kwa akili yake na kuchagua kwa kutaka kwake - afuate uongofu wa Mwenyezi Mungu na maamrisho yake, na aingie katika Uislamu.
Kufuata uongofu wa Mwenyezi Mungu na maamrisho yake ya uongofu ndio dhamana bora kwa usalama wa mwanadamu na kuafikiana na nafsi yake.
Uislamu ndio asili ya ujumbe wote ulitumwa na Mwenyezi Mungu kwa Manabii na Mitume wake wote kwenda kwa wanadamu, na ni ujumbe mmoja kwa Ibrahim, Musa, Issa na Muhammad. Na katika hali yake ya mwisho, uliofunuliwa kwa Mjumbe wa mwisho Muhammad, ujumbe huo umekuja huku ukiwa umeshasahihisha, kutimiza na kuhitimisha ujumbe wote wa kabla yake.
2
Na neno takatifu: "ALLAH" maana yake kwa lugha ya Kiarabu ni: Mungu, na hasa hasa, ni Mungu Mmoja wa Milele, Muumbaji wa ulimwengu, Bwana wa mabwana, Mfalme wa wafalme, Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu, na neno hilo hilo linafahamika na wazungumzaji Kiarabu miongoni mwa Wayahudi na Wakristo.
MBILI: - NGUZO ZA IMANI:
(1) Muislamu anaamini Mungu Mmoja wa pekee, Mtukufu mwenye kubaki milele, Mkubwa mwenye nguvu juu ya viumbe wote, Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu, Muumbaji Mwenye kuruzuku.
- Mwenyezi Mungu hana baba, mama, wala watoto wa kiume au wa kike. Hakuzaa yoyote wala hakuzaliwa na yoyote. Hafanani na kitu chochote. Yeye ni Mola wa wanadamu wote, na sio Mungu wa kundi au jamii maalum.
- Mwenyezi Mungu kwa utukufu wake na ukubwa wake yuko karibu sana na kila muumini mchamungu mwenye kumkumbuka Mwenyezi Mungu, humjibu pindi anapomuomba na anamsaidia pindi anapomtaka msaada. Na Yeye anawapenda wote wanaompenda na anawasamehe makosa yao, na Yeye anawaneemesha waja wake kwa neema ya usalama na kuridhika na uongofu na kufaulu.
- Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kuruzuku, Mkarimu, Mwenye kujitosheleza na kuwatosheleza (viumbe), Mpole Msamehevu, Mwenye subira, Mwenye kudumisha shukrani yake, Mwenye kutegemewa Mwenye kusitiri, Mwenye kuhukumu, Mwenye amani. Na Qur'an Tukufu imebainisha mengine mengi yasiokuwa hayo miongoni mwa sifa za Mwenyezi Mungu Mtukufu.
- Mwenyezi Mungu amemuumba mwanadamu akiwa na akili; ili afahamu na kutambua, na akamuumba na roho na dhamiri ili aongoke kuelekea kwenye kheri na ukweli. Na akamuumba na hisia ili awe mwanadamu kuhisi. Kama tukitaka kuhesabu neema za Mwenyezi Mungu kwetu hatuwezi, kwa kuwa neema zake hazihesabiki.
- Na mkabala wa neema zote za Mwenyezi Mungu na rehema zake kwetu, Yeye (Mungu) haitaji toka kwetu kwa sababu yeye ni Mwenye kujitosheleza, Mwenye cheo cha juu, na yote anayotaka kwetu ni kwamba; tumjue ukweli wa kumjua, na tumpende na tutumie sheria zake, ili zituletee heri.
3
(2) Muislamu anaamini Mitume na Manabii wote kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, habagui baina ya yoyote kati yao.
- Manabii wote ni wanadamu. Mwenyezi Mungu amewapa ufunuo na ujumbe wake, na amewateua ili kuongoza watu.
- Qur'an imetaja Manabii na Mitume ishirini na watano, na imeashiria kuwa kuna wengine wengi wasiokuwa hao.
- Miongoni mwa Manabii na Mitume waliotajwa ni: Nuhu, Ibrahimu, Ismaili, Is-haqa, Musa, Issa na Muhammad (AS), na wote hao wameleta ujumbe wa kujisalimisha kwa Mwenyezi Mungu Mmoja na kukubali maamuzi yake na kutii amri zake.
(3) Muislamu anaamini vitabu vyote vilivyotoka mbinguni, kama vilivyokuwa katika hali yake ya asili iliyokamili, na kwamba vilishushwa kwa ajili ya kuongoza watu kwenye njia ya Mwenyezi Mungu ilionyooka. Qur'an imeashiria vitabu vilivyofunuliwa kwa Ibrahimu, Musa, Daudi, Issa na Muhammad (AS).
- Na kwa sasa, vitabu vyote miongoni mwa vitabu vilivyotoka mbinguni, ambavyo viliitangulia Qur'an, hakuna chochote kilichobakia katika hali yake ya asili ambayo kilishushwa kwayo. Miongoni mwavyo kuna vilivyopotea, na vingine vimefichwa. Na hayo ni kwa sababu ya zile tofauti na kufuata mataminio ya nafsi kulikotokea kwa wafuasi wa Uyahudi na Ukristu wa karne za mwanzo.
- Mpaka leo hii, Qur'an pekee ndio kitabu cha Mwenyezi Mungu kilichobaki sahihi na kamili, na hakuna yoyote miongoni mwa wenye elimu - Muislamu ao asiyekuwa Muislamu - anayebisha kwamba Qur'an ilivyo leo ndivyo ilivyokuwa tangu karne kumi na nne. Waislamu wanaisoma bila kutofautiana neno wala herufi.
- Hakika Mwenyezi Mungu aliyeishusha Qur'an, ameahidi kuilinda, ikailinda isipatwe na mabadiliko au kupotea au kufichwa.
(4) Muislamu anaamini (kuwepo) kwa Malaika wa Mwenyezi Mungu, nao ni viumbe walioumbwa kwa Nuru nzuri iliyoumbwa na Mwenyezi Mungu.
- Malaika hawahitaji chakula wala kinywaji wala kulala, nao wametakasika kutokana na matamanio ya mwili au tama ya vitu.
4
- Malaika wametiishwa kwa ajili ya kumtii Mwenyezi Mungu kila wakati, na kila mmoja kati yao ana jukumu lake alilopangiwa.
- Wanadamu hawawezi kuwaona Malaika, na hiyo ni kwa sababu ya udhaifu wa hisia zetu, na viungo vya hisia pekee havijitoshelezi kutambua kila kitu kilichopo pembezeni mwetu. Macho yetu hayaoni ispokuwa kiasi cha masafa ya upeo wa mawimbi mekundu mpaka ya zambarau, na hivyo hivyo, masikio na viungo vingine miongoni mwa viungo vya hisia.
(5) Muislamu anaamini (kuwepo) siku ya hesabu (Kiama), na ulimwengu wetu wa kiardhi tunaoujua utaisha katika wakati uliopangwa, na maiti watafufuliwa kwa ajili ya hisabu ya mwisho ya uadilifu.
- Yale yote yanayotoka kwa mwanadamu miongoni mwa maneno, vitendo, fikra au nia, yatahifadhiwa kisha atahesabiwa kwayo siku ya Kiama, pale ambapo kila mmoja wetu atakuta hesabu yake ikiwa imetawanywa, na mwenye waraka msafi kwa mema atalipwa malipo yaliokuwa bora, na Mwenyezi Mungu atampokea mapokezi yaliokuwa mazuri katika Pepo yake. Ama wale ambao nyaraka zao zitakuwa zimejaa mabaya, watapata adhabu ya uadilifu na kutupwa katika Jahanamu.
- Uhakika wa Pepo na Moto hakuna mwenye kuujua ispokuwa Mwenyezi Mungu peke yake. Mola ametaja (Pepo na Moto) katika Qur'an kwa hali yenye kuvifanya vitambulike kwa urahisi na akili ya mwanadamu.
- Yoyote kati yetu anayeona kwamba hapati malipo ya uadilifu wala kuheshimiwa, na kupewa haki kwa yale anayoyafanya miongoni mwa mema katika uhai huu wa kidunia, basi na aelewe kwamba; atapata malipo yakutosha na sifa nzuri (katika) siku ya hesabu (Kiama).
- Na kadhalika, ikiwa imetudhihirikia kwamba: watu miongoni mwa wale wanaofanya maasi na machafu huku wakimsahau Mwenyezi Mungu na ujumbe wake, wanafaulu kupata neema za Dunia, kujinufaisha na kuheshimika. Hikika mwisho wao usio na shaka ni hesabu ya uadilifu yenye kukomesha siku ya hesabu.
- Hakuna ajuaye wakati wa Kiama ila Mwenyezi Mungu pekee yake.
(6) Muislamu anaamini (kuwepo) Kadari na Uamuzi (wa Mungu).
- Uamuzi na Kadari ni elimu ya Mwenyezi Mungu ya tangu na tangu, navyo ni uwezo wake wa kukadiria na kutekeleza
5
anayotaka, kwa hiyo Mwenyezi Mungu hakuumba ulimwengu kiupuuzi puuzi na hakuuacha hovyo hovyo.
- Mwenyezi Mungu ni Mwenye hekima, Mwadilifu, Mpole, na Kadari yake (aliyokadiriya) yote ni heri, licha ya kuwa, katika baadhi ya wakati tunashindwa kutambua hekima yake katika Kadari zake.
- Yatupasa tumwamini Mwenyezi Mungu kikamilifu, na tukubali anayotufanyia, kwa sababu utambuzi wetu una mpaka, na fikra zetu hazizidi muono wetu wa pekee, lakini elimu yake (Mungu) hakuna kinachoizuia, na hekima yake inaenea ulimwengu wote.
- Mwanadamu analazimika afikiri na kupanga mbinu kwa hekima, kisha aliachie jambo kwa Mwenyezi Mungu. Na ikiwa maisha hayakwenda kama anavyoyatamani, imani yake isiyumbe wala asijisalimishe kwenye mawewe na wasiwasi wenye kuangamiza.
(7) Muislamu anaamini kwamba lengo la maisha haya ni kumwabudu Mwenyezi Mungu.
- Ibada katika Uislamu haimaanishi kujiweka kando (kujitenga), na kutafakari, wala sio kutekeleza matendo ya dini tu, lakini kumwabudu Mwenyezi Mungu inamaanisha tuishi kama alivyoamrisha, wala tusijitenge na maisha.
- Kumwbudu Mwenyezi Mungu ni kwamba: tumjue, tumpende, tutii maamrisho yake na tutekeleze sheria yake katika kila jambo maishani, na katika njia yake tutende kwa usahihi na tujiepushe na shari, na tutekeleze haki yake kwetu, na haki ya nafsi zetu, na haki za ndugu zetu katika wanadamu.
(8) Muislamu anaamini kwamba Mwenyezi Mungu amempa mwanadamu pekee, cheo kikuu kuliko viumbe wenzake tunavyovijua.
- Mwenyezi Mungu amemfadhilisha mwanadamu kwa cheo hiki kwa kuwa amempa uwezo wa kiakili na hisia za kiroho, pia uwezo wa kutenda.
- Mwanadamu si kiumbe aliyelaaniwa tangu kuzaliwa kwake mpaka kufa kwake, bali mwanadamu ni kiumbe mwenye kuheshimiwa (kukirimiwa), mwenye uwezo wa kufanya yote yaliyo mema na mazuri.
6
(9) Muislamu anaamini kwamba kila mwanadamu huwa anazaliwa katika maumbile ya Uislamu, Mwenyezi Mungu amempa kila mwanadamu maandalizi ya kiroho na kiakili ili awe Muislamu mzuri.
- Kila mwanadamu huzaliwa kama vile alivyomtaka Mwenyezi Mungu, kufuatana na yale aliyeamrisha na kukadiria.
(10) Muislamu anaamini kwamba kila mwanadamu huzaliwa akiwa ametakasika na makosa (dhambi), na mwanadamu pindi anapofikia umri wa kukomaa na kuwa mwenye akili na kujitegemea, anakuwa ni mwenye kubeba majukumu ya matendo na nia zake, kwa hiyo, mwanadamu ametakasika (ameepukana) na makosa na dhambi maadam hajayafanya.
- Hakuna dhambi ya kurithi wala dhambi ya mwanzo, ni kweli kuwa Adamu baba wa watu (wote) alifanya dhambi ya kwanza, lakini alimuomba Mwenyezi Mungu amsamehe na akamsamehe.
(11) Muislamu anaamini kwamba ni wajibu kwake kujitahidi kwa ajili ya kuikoa nafsi yake na kufuata Uongofu wa Mwenyezi Mungu.
- Haifai kwa yoyote awe kiunganishi baina ya mtu na Mola wake, kwa hakika uokovu hupatikana kwa imani na matendo, na kwa itikadi nzuri na kutenda. Imani bila matendo mema haina faida, mfano wake ni kama mfano wa matendo mema bila imani.
(12) Muislamu anaamini kwamba Mwenyezi Mungu hatamhukumu mtu (yoyote) kabla ya kumbainishia njia ya kweli.
- Ama mtu asiyejua wala hakupta urahisi wa kujua jambo (lolote) kuhusu Uislamu, habebeshwi jukumu la kujitenga na Uislamu.
- Na kila Muislamu anawajibika amlinganie mwenzake aingie katika Uislamu kwa maneno na matendo (mema).
(13) Muislamu anaamini kwamba imani yake haisihi wala haikamiliki ikiwa ni imani ya upofu isiotegemea ushahidi (maandiko nk).
7
- Ni wajibu kwa mwanadamu aijenge imani yake kwenye msingi imara wa kukinaika kiakili bila kuwepo shaka yoyote au wasiwasi.
- Uislamu unasisitiza (kuwepo) uhuru wa Itikadi (imani), na wala hakuna kulazimishana katika (kufuata) dini, na inatosha kuwa katika ulimwengu wa Kiislamu kuna baadhi ya masinagogi ya kale ya Wayahudi, na baadhi ya makanisa ya kale sana. Bado yapo mpaka leo hii.
(14) Muislamu anaamini kwamba Qur'an ni maneno ya Mwenyezi Mungu aliomfunulia Nabii Muhammad (S.A.W) kupitia kwa Malaika Jibrilu.
- Qur'an ilishuka kidogo kidogo katika matukio mbalimbali ili ijibu maswali, iweke suluhisho, itatue mizozo, na imuongoze mwanadamu katika mambo yake yote kuelekea njia ya haki.
- Qur'an imeshuka kwa lugha ya Kiarabu, na bado ingali kamilifu na sahihi katika tamko lake la Kiarabu mpaka leo hii, na mamilioni ya watu wanaihifadhi kimoyomoyo.
(15) Muislamu anaamini na anatafautisha baina ya Qur'an na Sunna ya Nabii Muhammad (S.A.W), ambapo Qur'an ni maneno ya Mwenyezi Mungu, na Sunna za Nabii (Ni maneno ya Mtume na mafunzo yake pamoja na vitendo vyake) nayo ndio ubainifu na muundo wa kuifanyia kazi Qur'an.
- Vyote viwili Qur'an na Sunna za Nabii Muhammad (S.A.W) ndivyo chimbuko (asili) la msingi la kuutambua Uislamu.
TATU: - MATENDO YA IBADA:
Mwenyezi Mungu amempangia Muislamu aina nne za ibada, na hizo ibada ndio kuitekeleza imani. Baadhi ya ibada hutekelezwa kila siku, nyingine kwa wiki, na baadhi zinaambatana na miezi au zinarejearejea kila mwaka, na baadhi hutekelezwa kwa uchache mara moja katika umri wote.
Na hizo Ibada ni:
1. Sala
8
2. Funga
3. Zaka
4. Hija.
1- SALA:
- Kusali kwa ajili ya Muumba kila siku ndio njia nzuri ya kuulea utu bora kwa mwanadamu, na kuboresha hisia zake.
- Mwenyezi Mungu hana haja ya sala zetu kwa sababu ametakasika na kuhitaji. Hakika Sala ni kwa manufaa yetu sisi, nayo ni manufaa yasiokuwa na mpaka, na fadhila zake zinazidi taswira (mtizamo muono).
- Katika Sala ya Muislamu, viungo vyote katika mwili vinaafikiana na roho na akili katika kumwabudu Mwenyezi Mungu na kumtukuza.
- Sala ndio moyo wa Ibada.
- Hakuna njia yoyote nyingine inayofanana wala kuipiku Sala, kwa namna inavyokusanya kati ya uzingatiaji wa kifikra na ikhilaswi (nia safi) rohoni, na kutukuka kitabia na uchangamfu wa mwili, yote hayo yanapatikana katika kitendo kimoja.
- Kutekeleza Sala ni wajibu (lazima) kwa kila Muislamu mwanaume au mwanamke, mwenye akili, aliye balehe (kukomaa, pevuka, kuwa mkubwa), hakuna mwenye kusameheka aache sala, ispokuwa mwanamke wakati wa damu ya hedhi na nifasi.
YANAYOTAKIKANA KWENYE SALA:
- Udhu, Usafi wa mwili, mavazi na sehemu ya kusalia, vazi linalofaa (lenye kusitiri uchi), nia, kuelekea upande wa Kibla; nao ni upande wa Al-Kaaba iliyopo Makka.
SALA ZA FARADHI (LAZIMA):
- Ni Sala Tano, mchana na usiku, na Sala ya Ijumaa ambayo hutekelezwa wakati wa Adhuhuri, na Sala ya Kumsalia maiti.
SALA ZA SUNNA (ZILIZOSISITIZWA):
- Ni zile sala za ziada zinazotekelezwa pamoja na Sala za Faradhi, ukiongezea Sala za Idi mbili.
9
SALA ZA SUNNA ZISIZOKUWA ZA MKAZO (ZA KUJITOLEA):
- Ni Sala nyinginezo nyingi kwa atakaye mchana na usiku.
NYAKATI ZA SALA ZA FARADHI:
SALA YA AL-FAJIR: Kuanzia Al-Fajir mpaka kabla ya kuchomoza kwa jua.
SALA YA ADHUHUR: Pindi jua linapoanza kupinda kutoka katika (hali ya wima - utosini) mpaka linapokuwa katikati ya njia yake (kiasi kidogo) katika upande wa magharibi.
SALA YA LAASIR: Baada ya kuisha wakati wa Adhuhuri mpaka kuzama kwa jua.
SALA YA MAGHARIBI: Baada ya kuzama jua mpaka kuzama kwa mawingu mwekundu upande wa magharibi.
SALA YA INSHA: Baada ya kuisha wakati wa Sala ya Magharibi mpaka kuchomoza Al-Fajir.
- Ni wajibu kuitekeleza kila Sala kwa wakati wake uliopangiliwa (na sheria), ispokuwa pakiwepo udhru wenye kukubalika (kisheria), na mtu atayepitwa na sala ya faradhi inampasa aitekeleze kwa wakati wa karibu iwezekanavyo.
- Sala inatekelezwa kwa harakati za mwili, zikiambatana na maneno na kusoma aya za Qur-an.
- Zaidi ya sala za faradhi na za sunna, Muislamu anamtaja Mola wake kila wakati, akielezea shukrani yake kwa Mola wake na kukumbuka neema zake, na kuomba msamaha wake kila wakati. Na Muislamu huwa anamtaja Mola wake kwa wingi katika kila tukio: Kama vile kuzaliwa kwa mtoto, ndoa, kuelekea kitandani (kulala), kuamka, kutoka na kurudi nyumbani, kusafiri, kufika mjini, kupanda (kipandwa), kuendesha chombo, kabla na baada ya kula na kunywa, wakati wa mavuno, kutembelea makaburi, au katika nyakati za huzuni na maradhi.
10
2- FUNGA:
Funga ni kujizuia kikamilifu na kuacha kula, kunywa, kuingiliana mke na mume na kuvuta sigara, kuanzia kuchomoza kwa Al-Fajir mpaka kuzama kwa jua. Funga ni ibada ya Kiislamu isyo na mfano katika kumlea mwanadamu awe na subira, upendo, ukweli na nia safi (Ikhlas) kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.
- Mwanadamu anajifunza katokana saumu: Hisia ya ubunifu yenye matumaini, nia nzuri (Ikhlas), subira, kuwapenda wangine, uadilifu, kujiwekea akiba kwa hekima, matumizi mazuri, nguvu za utashi, maafikiano mazuri, na uhai wenye afya, kujidhibiti, moyo wa kushikamana na jamii, umoja na undugu.
FUNGA YA FARADHI:
- Funga ya lazima inatekelezwa kila mwaka katika mwezi wote wa Ramadhani, ambao ni mwezi wa tisa katika mwaka wa Kiislamu (kwa miezi mwandamo).
FUNGA YA SUNNA:
- Funga ya Jumatatu na Alhamis kila wiki, na siku Tatu katikati ya kila mwezi wa Kiislamu, na siku sita baada ya kuisha Ramadhan na Idi Fitri, na funga ya baadhi ya siku katika miezi ya Rajab na Shaaban ambayo hutangulia mwezi wa Ramadhan.
- Funga ya Ramadhan ni faradhi (lazima) kwa kila Muislamu balehe, mwanaume au mwanamke, mwenye akili timamu, mzima (si mgonjwa), mkazi wa mji (si msafiri).
- Wanawake wamekatazwa kufunga wakiwa katika siku za damu ya hedhi na nifasi (watalipia baada ya kumaliza hizo damu) na wanaruhusiwa kufunga au kuacha kufunga katika kipindi cha kunyonyesha. Msafiri na mgonjwa wanaruhusiwa kufunga na kuacha kufunga.
3- ZAKA:
Zaka ni ibada, nayo ni aina ya kuwekeza kiroho.
11
- Maana ya sisisi ya "ZAKA" kwa lugha ya Kiarabu ni: twahara (usafi) yaani kuisafisha mali. Zaka maana yake ni: Kiwango maalum cha mali kinachotolewa na mwenye mali kutoka katika chumo la mali yake, kilimo au wanyama, ili awagawie wenye kustahiki miongoni mwa wenye kuhitaji.
- Zaka haisafishi mali peke yake, lakini pia inasafisha moyo wa mwenye mali kutokana na ubinafsi na tamaa. Pia inasafisha moyo wa mwenye kupewa kutokana na husuda na wivu, na nyongo na chuki, na nafasi zao zinachukuliwa na upendo uliotakasika kumuombea dua mwenye mali.
- Pia zaka ina faida kubwa kibinadamu, kijamii na kisiasa. Kwa mfano, Zaka inaifanya jamii kuepukana na migogoro ya kitabaka, hisia za nyongo, chuki, dhana mbaya, na ufisadi.
- Kwa kila Muislamu mwanaume na mwanamke, kama mali anayoimiliki hadi kufikia mwishoni mwa mwaka, inazidi kiasi cha Gram 75 za Dhahabu, (karibu sawa na Dollar 820 katika hesabu ya mwaka 1997). Sawa sawa iwe ni mali alizozilimbikiza au bidha za biashara, (inawajibika) atoe Zaka kwa uchache kiasi cha (2, 5%) asilimia mbili na nusu.
- Zaka huhesabiwa katika pato safi baada ya kukata makato yote yakiwemo matumizi yake binafsi, matumizi ya familia, madeni yenye kustahiki, na ushuru … n.k.
- Zaka inastahiki apewe kila: Fakiri, maskini, na waislamu wapya, kutoa, fidia ya kuwakomboa mateka Waislamu), wenye madeni, na wenye kusimamia ukusanyaji wa Zaka, wale walowekeza maisha yao katika kufanya tafiti za kielimu, uchunguzi na kuueneza Uislamu, na watoto wa njiani nao ni wageni wenye shida (kuhitaji).
- Kodi zitozwazo na serekali hazihesabiwi kuwa ni badala ya faradhi ya Zaka. Na kwa mwenye kutoa Zaka inampasa ajichunge wakati wa kuitoa Zaka asitafute kujifakharisha, kujisifu au kujijengea jina, ila kama ikiwa katika kutangaza kwake anakusudia kuwahimiza wangine wamuige.
12
4- HIJA:
Hija ni kwenda kuhiji Makka mara moja kwa uchache katika umri wa mtu, nayo ni wajibu kwa kila Muislamu mwanaume na mwanamke mwenye akili timamu na uzima wa mwili, mwenye uwezo wa mali (pesa).
- Hija ndio mkusanyiko wa watu ulio mkubwa kabisa duniani kwa waumini, kila mwaka tena kwa wakati mmoja (mnamo mwaka 1989: walihiji watu million 2, 5 mbili na laki tano).
- Amani ndio kauli mbiu ya mkusanyiko huo: Amani pamoja na Mwenyezi Mungu, pamoja na nafsi, pamoja na wangine, na pamoja na viumbe hai wote. Ni marufuku kabisa kuvunja amani hiyo kwa kufanya uadui wa aina yoyote ile dhidi ya mwanadamu, kiumbe hai au mmea, kwa namna yoyote ile.
- Huko Makka Waislamu wanakusanyika kutoka sehemu mbalimbali, na pande zote wanazoishi watu, kwa ajili ya kuitika wito wa Mwenyezi Mungu. Kwa hakika Waislamu wanaelekea huko Makka kwa ajili ya kumtukuza Mwenyezi Mungu pekee yake, sio kwa ajili ya mwanadamu.
- Hija ni mkusanyiko unaowakumbusha watu siku ya mkusanyiko mkubwa wa siku ya Kiama pindi watu wote watasimama wakiwa sawa sawa mbele ya Mwenyezi Mungu.
- Vilevile Hija ni kuadhimisha matendo ya ibada yaliyofanywa na Nabii Ibrahimu na mwanawe mkubwa Ismaili, wote wawili ndio waliokuwa wa kwanza kuhiji kwenye Al-Kaaba: Nyumba ya kwanza ya Mwenyezi Mungu Ardhini.
- Na inapendeza sana kutembelea msikiti wa Nabii Muhmmad (S.A.W) "uliopo Madina", ijapokuwa sio sharti ya kusihi kwa Hija wala kukamilika kwake.
NNE: - UISLAMU NI MFUMO WA MAISHA:
1. Maisha ya tabia (njema).
2. Maisha ya kifikra.
3. Maisha ya kibinafsi.
4. Maisha ya kifamilia.
13
5. Maisha ya kijamii.
6. Maisha ya kiuchumi.
7. Maisha ya kisiasa.
8. Maisha ya kimataifa.
1- MAISHA YA TABIA (NJEMA) KATIKA UISLAMU:
- Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa wakati wote wa kulingania kwake, kiasi cha miaka ishirini na tatu, alikuwa ni mfano hai wa Uislamu kwa binadamu. Kama vile mafundisho ya Uislamu yaliyofafanuliwa na Sunna za Mtume. Mafundisho yaliyokuwa mfumo kamili wenye kukusanya pande zote za mwenendo wa tabia njema.
- Uislamu unamuongoza Muislamu awe: mwaminifu, mkweli, mwenye nia njema (ikhlas), mwema, myenyekevu, mwenye huruma, mwadilifu, mstaarabu, mwenye haya, mwenye kutekeleza ahadi zake.
- Pia Uislamu unakataza mambo yote yenye kupingana na sifa hizi, vilevile unakataza: husuda, unafiki, kujionesha, dharau, uzinzi, utesi, usengenyaji na kudanganyika.
2- MAISHA YA KIFIKRA KATIKA UISLAMU:
- Vyanzo vya maarifa katika Uislamu ni Ushahidi wa wazi au ni hoja thabiti zinazofikiwa kwa majaribio au uzoefu au vyote viwili kwa pamoja.
- Qur'an inawahimiza waumini wajitafutie maarifa katika ulimwengu kwa upana wake.
- Imani ya Muislamu kwa Mwenyezi Mungu inajengeka kwa maarifa ya kiakili na utafiti wa kiuchambuzi, kisha baada ya hapo unaacha mlango wazi kwa ajili ya kujiongezea nyanja zote za maarifa.
- Katika Uislamu hakuna taasisi yoyote kama vile kanisa au inayofanana na kanisa, wala hakuna ukiritimba wa maarifa kwa Makuhani au Viongozi wa kidini.
- Kila Muislamu ajitahidi kujifunza Uislamu ili aufanyie kazi.
3- MAISHA YA KIBINAFSI KATIKA UISLAMU:
- Twahara na Usafi, chakula cha afya, mavazi yenye kustahiki, mwenendo mzuri, uhusiano wa kingono ulio sahihi katika wigo wa ndoa.
14
- Uislamu umeharamisha vyakula na vinywaji vyote vyenye kudhuru, Vikiwemo pombe na mihadarati (madawa ya kulevya), vilevile nyama ya mzoga na wanyama wasiochinjwa kwa njia sahihi, wanyama wakali wenye kushambulia, nyama ya nguruwe na damu yenye kutolewa.
- Pia Uislamu umehusia kuchunga njia za kiafya katika kusambaza chakula na kukihifadhi, kusafisha mdomo na mikono, na kula chakula kwa usawa, na yasiokuwa hayo katika maelekezo ya afya njema.
4- MAISHA YA KIFAMILIA KATIKA UISLAMU:
- Familia ndio kiini (seli) cha kwanza cha jamii, wanafamilia wanaunganishwa kwa udugu wa damu na uhusiano wa ndoa. Hakuna kitu kingine kinyume na hayo, miongoni mwa uhusiano usiokuwa wa kawaida (kama kuasili mtoto, na ndoa ya jinsia moja "ushoga na usagaji", na ndoa ya majaribio…n.k).
- Mwenyezi Mungu amewakirimu baba na mama, na hasa mama, kwa (kumpa) heshima kubwa mno, hata kama watakuwa si Waislamu.
- Uislamu umeweka (sheria ya) ndoa kama vile wajibu wa kidini kwa kila mwenye kuweza kubeba majukumu yake, na kila mtu katika familia ana haki zake na wajibu wake.
- Kufunga ndoa hakusihi (hakufai) bila kuridhiana kikamilifu kuliko huru kati ya mume na mke.
- Mume ndio mwenye jukumu kamili la kumtunza (kumpa matumizi) mkewe, hata kama mkewe ni tajiri, na mume hana haki ya kuingilia matumizi ya mali za mke.
- Uislamu umeruhusu kuoa wake wengi - kwa kiwango kisichozidi wanne katika hali ya dharura maalum tu, na umefanya (kuoa wake wengi) kwa sharti mume awe na uwezo wa kutekeleza mahitajio yote ya lazima ya wake zake na kiuadilifu kamili baina yao katika matendo, nalo ni sharti lililo mbali mno kwa wanaume wengi.
- Wala haifai kukimbilia talaka ispokuwa kama itakuwa ndio suluhisho la mwisho baada ya kushindikana majaribio yote ya suluhu na kuhukumiana kwa njia ya familia ya mume na mke.
15
5- MAISHA YA KIJAMII KATIKA UISLAMU:
- Mwenyezi Mungu amemwamrisha kila mtu kusaidia na kufanyia wema watu wa familia yake, ndugu zake, watumishi wake na majirani zake.
- Ubora wa mtu katika Uislamu hautokani na tabaka au rangi, wala nasaba au mali, bali hutokana na uchamungu na matendo mema, na kinyume cha hayo hakuna.
- Wanadamu wote ni ukoo mmoja kutoka kwa baba mmoja na mama mmoja, na ubinadamu ni kitu kimoja, sio katika nasaba tu, bali ni katika yale uliyoumbiwa kwa ajili yake.
6- MAISHA YA KIUCHUMI KATIKA UISLAMU:
- Mwanadamu anapaswa ajitahidi kutafuta rizki yake kutokana na kazi halali, na hayo sio kwamba ni wajibu tu, bali pia ni fadhila kubwa.
- Kile anachokichuma mwanadamu kwa kazi yake ni milki yake, lakini analazimika kutekeleza haki za umma katika milki hio, na umma nao kwa nafasi yake unabeba jukumu lake la kuwatoshelezea watu wake waepukane na kuomba.
- Mfumo wa kiuchumi katika Uislamu haujengeki kwa mahesabu matupu, lakini pia wajengeka kwa maadili na misingi mema. Zaka na Sadaka zinaunda jiwe la msingi katika mfumo huu.
- Mwanadamu huja duniani mikono mitupu, na hivyo hivo hutoka duniani, kwa hiyo mmiliki wa uhakika wa kila kitu ni Mwenyezi Mungu, na mwanadamu amewakilishwa tu katika mali. Ingawa Uislamu haukatazi kufanya miradi ya kujitegemea wala hauharamishi haki ya kumiliki kwa mtu binafsi, ispokuwa Uislamu hauruhusu ubinafsi na tamaa ya kibepari.
- Uislamu unachukua njia ya kati na kati iliyo nzuri baina ya mtu na na jamii, baina ya mwananchi na taifa, baina ya ujamaa na ubepari na baina ya mwili na roho.
- Uislamu umeweka muongozo uliofafanuliwa kwa shughuli za kibiashara ili kudhamini uadilifu baina ya wenye kuuziana.
- Katika Uislamu mali hazichumwi ispokuwa kwa uwekezaji wa kweli wa vyanzo vya mali, kazi au fikra. Mali peke yake haizalishi
16
mali zingine. Mbadala wa Kiislamu kwa faida thabiti kwenye mali iliyowekwa (benki) ni kushiriki katika (kuizalisha) jambo ambalo Uislamu umelipangilia kwa aina mbalimbali.
- Uislamu unahimiza kutoa mikopo mizuri (bila malipo au faida) kwa ajili ya kuwasaidia wangine.
7- MAISHA YA KISIASA KATIKA UISLAMU:
- Kxatika taifa la Kiislamu utawala ni wa Mwenyezi Mungu, na watu wamewakilishwa katika taifa kwa ajili ya kusimamia sheria yake.
- Ujumbe wa kimsingi kwa umma ni kuweka jamii ya Kiislamu, na kufikisha wito wa Uislamu kwa wanadamu wa kila eneo, na kila Muislamu - kulingana na hali yake na uwezo wake - ana jukumu katika kuamrisha mema na kukataza mabaya.
- Kiongozi ni msimamizi mtekelezaji tu anayechaguliwa na watu ili awahudumie kulingana na sheria ya Mwenyezi Mungu. Na jukumu la taifa ni kudumisha uadilifu na kuhifadhi usalama wa wananchi wote.
- Inawajibika kumchagua kiongozi na wasimamizi kutoka miongoni mwa wananchi bora zaidi wenye vigezo stahiki, na pindi hao wasimamizi (viongozi) wakipoteza uaminifu wa Mwenyezi Mungu na uaminifu wa watu, inawajibika kuwatoa na kuwabadilisha na kuwaweka wanaofaa zaidi.
- Uislamu umeweka adhabu kwa makosa yote yanayodhuru amani na usalama wa jamii, na miongoni mwa makosa hayo ni: kuuwa, ugaidi, wizi, uzinzi, ushoga, usagaji, kunywa pombe na mfano wake na kumtangaza mwingine kwa ubaya.
- Ama wasiokuwa Waislamu wana haki ya kupangilia mambo ya maisha yao kama vile ndoa, talaka, vyakula, na mirathi kulingana na mafundisho ya dini zao, au kulingana na sheria ya Kiislamu kama wakitaka.
- Vilevile wasiokuwa Waislamu wana haki ya kuchagua baina ya kutoa Zaka iliofaradhishwa kwa Waislamu, au badala yake watoe ushuru maalumu unaoitwa jizya. Na katika hali zote mbili taifa la
17
Kiislamu linalazimika kuwapa hifadhi na himaya kamili na uhuru wa kiimani.
8- MAISHA YA KIMATAIFA KATIKA UISLAMU:
- Watu wote ni wana wa Adamu, watu wote ni sawa: katika hali zao za kibinadamu na katika yale waliyoumbiwa.
- Waislamu wanaheshimu maslahi ya wangine na haki yao ya kuishi, na wanazilinda mali zao na hadhi zao maadam hawajagusa haki za Waislamu, na Uislamu unapiga marufuku uadui kwa aina zake zote.
- Jihadi katika Uislamu ni kuwasaidia watu wenyekutenzwa nguvu (wanyonge) ili kuwarejeshea uhuru wao na haki zao za kisheria, ili wajichagulie kwa hiari yao. Yale wanayoyaridhia miongoni mwa itikadi na mfumo wa maisha. Uislamu hata siku moja haujaruhusu wala hauruhusu kumlazimisha, kumchokoza au kutoa rushwa kwa mtu yoyote ili abadilike na kuingia Uislamu.
- Na kinyume cha hayo, hakika Waislamu ndio waliosumbuliwa na bado wanasumbuliwa na aina nyingi za ukandamizwaji, mibinyo ya kiuchumi na uchokozi ili waache dini yao. Andalus (Spain), Palestina, India, Burma, na Bosnia, (yote hayo) ni baadhi ya mifano ya makosa makubwa ya wakati uliopita na wa sasa. Wakati ambapo wasiokuwa Waislamu: Wayahudi na Wakristu katika jamii za Kiislamu, daima wanapata usalama na himaya, na haki (zao) kuheshimika.
- Waislamu wanaelekea katika vita pindi usalama wa taifa unapokuwa hatarini. Na vitani ni marufuku kabisa kuharibu mimea na wanyama, au kuua wasiopigana (wasio wanajeshi) miongoni mwa wanawake, watoto na wazee.
- Katika Uislamu mikataba ya kimataifa hueshimiwa kwa makini, ispokuwa kama wengine wataanza kuivunja. Haifai kuvunja mkataba kwa ajili ya tamaa ya kunufaika kisiasa au kiuchumi kwa muda (mchache).