Hakika Allah Amemtuma Mtume wake Muhammad (s.a.w) awe dalili iliyo wazi juu ya waja wake, naawabainishie yale aliyoteremshiwa katika Kitabu, na awe mfano mwema wa kuigwa na walimwengu wote, na ili watu wapate kuwa na muongozo mwema katika dini yao na dunia yao. Ametumwa kutufundisha itikadi sahihi pamoja na hekima kwa ajili ya kutengenea hali ya umati wake, na pia kuwaweka juu ya njia safi na sahihi, ili watu wawe juu ya kitanga cheupe, mchana wake sawa na usiku wake, na asiende kinyume na njia hiyo isipokuwa mpotofu. Wakaifuata njia hiyo Maswahaba wake (r.a) na wale waliokuja baada yao na walio wafuatilia kwa wema, Wakaisimamisha sharia ya Allah na kuyakamata vizuri mafundisho hayo kwa magego yao kwa kuifuata itikadi hii iliyo sahihi, na ibada na mwenendo na tabia. Na sisi Alhamdulillah tunaendelea kuufuata mwenendo wao huo kwa kufuata dalili zilizomo ndani ya Qur'ani na zilizomo ndani ya mafundisho yake (s.a.w), na tunamuomba Allah Atuthibitishe juu ya njia hiyo sisi na ndugu zetu wote wa Kiislamu kwa kauli iliyo thabiti katika maisha ya duniani na ya Akhera na atumiminie rehma Zake kwani yeye ni Mwenye kutoa kwa wingi. Kutokana na umuhimu wa maudhui hii, na kutokana na tofauti iliyokuja baadaye, baada ya kuingizwa matamanio ya watu ndani ya itikadi hii, nilipenda kuiandika iwe kama ndiyo itikadi yetu. Itikadi ya Ahlus Sunnah wal Jama’ah, nayo ni imani ya kuwepo kwa Allah na Malaika Wake na vitabu Vyake na Mitume wake na Siku ya Qiyama na Qadar (qudra) kheri yake na shari yake. Namuomba Allah Aijaalie kazi hii iwe halisi kwa ajili yake, Aridhike nayo na iwe funzo kwa waja Wake.
4
ITIKADI YETU Itikadi yetu ni kumuamini Allah na Malaika Wake na Mitume Wake na Vitabu Vyake na Siku ya Mwisho na kila kinachotokea au kutusibu (Qadar) kheri na shari, vyote vinatoka kwa Allah. Kwa hivyo sisi tunaamini kuwa Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye Aliyeumba na ndiye Mfalme Mwenye kukiendesha kila kitu, na ni Yeye peke yake anayestahiki kuabudiwa, na kila kinacho abudiwa kisichokuwa Yeye ni batili. Tunaamini pia kuwa Allah Anayo majina mazuri mazuri na sifa nzuri nzuri na njema, sifa za ukamilifu, na tunaamini kuwa Yeye ni Mmoja Asiye na mshirika katika kuumba Kwake na katika kuabudiwa Kwake na katika majina Yake mazuri na katika sifa Zake njema. Allah Anasema: (Mola wa mbingu na ardhi na vilivyo baina yake. Basi muabudu Yeye tu, na udumu katika ibada yake. Je, mnamjua mwenye jina kama lake?). Maryam -65. Na tunaamini kuwa Yeye ndiye: (Allah - hapana Mungu ila Yeye, Aliye hai, Msimamiaji wa mambo yote milele. Hashikwi na usingizi wala kulala. Ni Vyake pekee vyote viliomo mbinguni na duniani. Ni nani huyo awezaye kuombea mbele yake bila ya idhini Yake? Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao; wala wao hawajui chochote katika vilio katika ujuzi Wake, ila kwa atakalo Mwenyewe. Kiti Chake Cha Enzi kimetanda mbinguni na duniani; na wala haemewi na kuvilinda hivyo. Na Yeye ndiye Aliye juu, na ndiye Mkuu). Al-Baqarah -255. Na tunaamini kuwa: (Yeye ndiye Allah, Muumbaji, Mtengenezaji, Mtia sura, Mwenye majina mazuri kabisa. Kila kilioko katika mbingu na ardhi kinamtakasa, naye ni Mwenye kushinda, Mwenye hekima). Al-Hashri-24.
5
Na tunaamini kuwa:
(Ufalme wa mbingu na ardhi ni wa Allah; Anaumba Apendavyo, Anamtunukia amtakaye watoto wa kike, na Anamtunukia amtakaye watoto wa kiume. Au huwachanganya wanaume na wanawake, na akamfanya amtakaye tasa. Hakika Yeye ni Mjuzi Mwenye uweza). Ash-Shuuraa -49-50. Na tunaamini kuwa:
(Yeye ndiye Muumba mbingu na ardhi, Amekujaalieni mke na mume katika nafsi zenu, na katika wanyama nao (Akawaumba) dume na jike, Anakuzidishieni namna hii. Hapana kitu kama mfano wake. Naye ni Mwenye kusikia Mwenye kuona. Yeye ndiye Mwenye funguo za mbingu na ardhi. Humkunjulia riziki Amtakaye, na humpimia Amtakaye. Hakika Yeye ni Mjuzi wa kila kitu). Ash-Shuuraa -11-12. Na tunaamini kuwa:
(Na hakuna mnyama yoyote katika ardhi ila riziki yake iko kwa Mwenyezi Mungu. Naye Anajua makao yake na mapitio yake. Yote yamo katika Kitabu chenye kubainisha). Huud -6. Na tunaamini kuwa:
(Na ziko kwake funguo za ghaibu; hakuna azijuaye ila Yeye tu. Na Yeye Anajua kilioko nchi kavu na baharini. Na halidondoki jani ila Analijua. Wala punje katikagiza la ardhi, wala kinyevu, wala kikavu ila kimo katika Kitabu kinachobainisha). Al-An’aam -59. Na tunaamini kuwa:
(Hakika ujuzi wa kiama uko kwa Mwenyezi Mungu. Na Yeye ndiye Anayeiteremsha mvua. Na Anavijua viliomo ndani ya matumbo ya uzazi. Na haijui nafsi yoyote itachuma nini kesho. Wala nafsi yoyote haijui itafia nchi gani. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kujua, Mwenye khabari). Luqmaan -34.
6
SIFA YA KUSEMA Tunaamini kuwa Allah Anasema wakati wowote Anapotaka na kwa njia yoyote Anayotaka. Allah Anasema: (Na Mwenyezi Mungu alinena na Musa kwa maneno). An-Nisaa -164. Na Akasema: (Na pindi alipo kuja Musa kwenye miadi yetu, na Mola wake Akamsemeza). Al-A’araf -143. Na Akasema: (Na Tulimwita upande wa kulia wa mlima na tukamsogeza kunong'ona naye). Maryam -52. Na tunaamini kuwa:
(Sema: Laiti kuwa bahari ndio wino kwa maneno ya Mola wangu, basi bahari ingelimalizika kabla ya kumalizika maneno ya Mola wangu, hata tunge ileta mfano wa hiyo kuongezea). Al-Kahf -109. Na tunaamini kuwa: (Na lau kuwa miti yote iliyomo duniani ikawa ni kalamu, na bahari (ikawa wino), na ikaongezewa juu yake bahari nyengine saba, maneno ya Mwenyezi Mungu yasingelikwisha. Hakika Mwenyezi Munguni Mwenye nguvu, Mwenye hikima). Luqmaan -27. Na tunaamini kuwa maneno Yake ni ya ukamilifu uliokamilika na ya ukweli uliokamilika na yenye uadilifu uliokamilika. Allah Anasema: (Yametimia maneno ya Mola wako kwa kweli na uadilifu. Hapana awezaye kuyabadilisha maneno Yake. Na Yeye ndiye Mwenye kusikia na Mwenye kujua). Al-An’aam -115.
7
Na Akasema: (Na nani Mkweli kuliko Mwenyezi Mungu?). An-Nisaa -87. Na tunaamini kuwa Qur-ani ni maneno ya Allah, Aliyo yatamka kwa uhakika kabisa kwa kumfundisha Jibriyl aliyeiteremsha ndani ya kifua cha Mtume wa Allah Muhammad (s.a.w). Allah Anasema: (Sema: Ameiteremsha hii (Qur-aan) Roho takatifu kutokana na Mola wako kwa haki). An-Nahl -102. Na Akasema: (Na kwa hakika huu ni Uteremsho wa Mola wa walimwengu wote. Ameuteremsha Roho muaminifu, (Jibrilu) Juu ya moyo wako, ili uwe katika Waonyaji. Kwa ulimi wa Kiarabu ulio wazi). Ash-Shu’araa-192-195.
SIFA YA KUWEPO KWAKE JUU Tunaamini kuwa Allah yupo juu kabisa mbali na viumbe vyake kwa dhati Yake na kwa sifa Zake, na hii inatokana na kauli Yake Mwenyezi Mungu Mtukufu Aliposema:
(Na Yeye ndiye Aliye juu, na ndiye Mkuu). Al-Baqarah -255. Na Akasema: (Malaika na roho hupanda Kwake katika siku ambayo muda wake ni miaka elfu hamsini). Al-Ma’aarij -4. Na Akasema: (Je! Mnadhani muko salama kwa (Allah) Ambaye Yuko mbinguni ya kuwa Yeye hatokudidimizeni ardhini tahamaki hiyo inataharaki?). Al-Mulk -16.
Na Akasema: (Naye Ndiye Mwenye nguvu (Yuko) juu ya waja Wake). Al-An’aam -18.
8
Na imekuja katika Sunnah (Mafundisho ya Mtume wa Allah (s.a.w): (Mrehemu aliye ardhini Atakurehemu aliye mbinguni). Kaipokea Abu Ya’ala na Atw-Twabaraaniy na Al-Haakim Na kuwepo mbinguni hakuna maana kuwa yupo katika mojawapo ya sayari zilizopo juu kama baadhi ya watu wanavyoweza kudhania, bali dunia yetu ukiilinganisha na mbingu ni mfano wa doa dogo sana, bali hata haionekani. Kwani huko juu kuna nyota na sayari zilizoenea hata kama mtu atasafiri kwa kasi ya kupita kiasi (speed of light) basi atachukua mamilioni ya miaka na hatoweza kufika mwisho wake, na hata kama ataufikia mwisho wake, basi atakuta kuwa bado ipo anga isiyo na mwisho. Kwa hivyo ni Allah Peke Yake ndiye Mwenye kuelewa mfano wa kuwa juu Kwake Subhaanahu wa Ta’ala.
ALLAH ANAYO ARSHI Allah Anasema: (Hakika Mola wenu ni Allah, Ambaye Ameziumba mbingu na ardhi kwa siku sita, kisha Akawa juu ya ‘Arshi Yake). Yunus -3.
Na kuwa juu ya ‘Arshi Yake ni kuwa kunakonasibiana na utukufu wake Subhaanahu wa Ta’ala, hapana anaejua mfano wake isipokuwa Yeye. Na tunaamini kuwa Allah Akiwa juu ya ‘Arshi Yake, Yupo pamoja na viumbe Vyake kwa elimu Yake. Anasikia kauli zao na kuona vitendo vyao, huku Akiyaendesha mambo yao. Anamruzuku fakiri na Anampa ufalme Amtakaye na Anamuondolea ufalme amtakaye, Anamnyanyua amtakaye na Anamuangusha amtakaye, na tunaamini kwamba kheri yote imo mikononi Mwake Subhaanahu wa Ta’ala, na kwamba Yeye ni muweza wa kila jambo.
9
Na Yeyote mwenye uwezo huo, basi bila shaka yupo pamoja na viumbe vyake kikweli huku akiwa juu ya Arshi yake kikweli, na ni Yeye Peke yake ndiye mwenye kuujua uhakika wake. Allah Anasema: (Hapana kitu kama mfano wake. Naye ni Mwenye kusikia Mwenye kuona). Ash-Shuuraa -11.
Na Anasema: (Na Malaika watakuwa kandoni mwake (hizo mbingu) na Malaika wa namna nane watachukua 'Arshi ya Mola wako juu yao). Al-Haaqqah -17.
Sisi hatusemi kama wanavyosema wengine kuwa eti Allah yupo ardhini pamoja na viumbe Vyake, kwani tunaona kuwa kusema hivyo ni kukufuru au ni upotofu, kwa sababu kumpa Allah wasifu usiolingana naye ni kupunguza katika sifa Zake.
SIFA YA KUSHUKA Tunaamini pia yale aliyotujulisha Mtume wake (s.a.w) kuwa Allah Anashuka katika mbingu za dunia kila usiku katika thuluthi ya mwisho na kusema:
(Nani mwenye kuniomba nimkubalie, nani mwenye kuniomba nimpe, nani mwenye kuniomba maghfira nimghufirie). Alipoulizwa Imaam Ash-Shaafi’iy: 'Vipi Allah Anashuka? Akajibu: Kwani vipi Alipanda? Na tunaamini kuwa Allah Atakuja Siku ya Qiyaamah kuwahukumu viumbe wake. Allah Anasema: (Sivyo hivyo! Itakapovunjwa ardhi vipande vipande. Na Akaja Mola wako na Malaika safu safu. Na ikaletwa Jahannamu siku hiyo, siku hiyo mtu atakumbuka! Lakini kukumbuka huko kutamfaa nini?). Al-Fajr -21-22.
11
SIFA YA IRAADA (ATAKAVYO ALLAH) Tunaamini kuwa Allah Anatenda Atakavyo. Allah Anasema: (Atendaye Ayatakayo). Al-Buruuj -16. Na tunaamini kuwa zipo Irada namna mbili.
Ya kwanza Anatujulisha katika kauli Yake :
(Na lau kuwa Allah Alipenda wasingelipigana (Lau shaa'a Alaahu). Lakini Allah Hutenda Atakavyo). Al-Baqarah -253.
Na hapa maana yake ni ‘kutaka’, kama ilivyo katika kauli Yake :
(Wala nasaha yangu haikufaini kitu nikitaka kukunasihini, ikiwa Allah Anataka (In Kaana Allaahu Yuriydu) kukuachieni mpotee). Huud -34.
Na uwezo mwingine ni wa kisharia, na Hamtakii isipokuwa Anayempenda, kamailivyo katika kauli Yake Subhaanahu wa Ta’ala: (Na Mwenyezi Mungu anataka kukukhafifishieni kwenye ut’iifu wake, na wanaotaka kufuata matamanio wanataka mkengeuke makengeuko makubwa). (Na maana yake hapa ni kuwa 'Hivi Ndivyo Anavyotaka Allah' lakini kakupeni uhuru wa kuchagua wenyewe mnakotaka kwenda). An-Nisaa -27.
Na tunaamini kuwa Atakacho Allah katika mambo ya kilimwengu na ya kisharia yote ni katika hekima Yake, na hafanyi kitu bila ya kuwa na hekima kubwa ndani yake, na sisi huenda tukaijua hekima hiyo au tusiijue kutokana na upungufu wa akili zetu. Allah Anasema: (Kwani Allah si muadilifu kuliko mahakimu wote?). Atw-Twiyn -8.
11
Na Akasema: (Na nani aliye mwema zaidi katika kuhukumu kuliko Allah kwa watu wenye yakini?). Al-Maaidah -50.
SIFA YA KUPENDA Na tunaamini kuwa Allah Subhaanahu wa Ta’ala Anawapenda wacha Mungu wake wanaompenda. Allah Anasema: (Sema: Ikiwa nyinyi mnampenda Allah basi nifuateni mimi, Allah Atakupendeni na Atakufutieni madhambi yenu). Al-‘Imraan -31.
Na Akasema: (Basi Allah atakuja leta watu anao wapenda nao wanampenda). Al-Maaidah -54.
Na Akasema: (Hakika Allah Anawapenda wanaosubiri). Al-‘Imraan -146.
Na tunaamini kuwa Allah Huridhika zinapofuatwa sharia Zake na huchukizwa zisipofuatwa. Allah Anasema: (Mkikufuru basi Mwenyezi Mungu si mwenye haja nanyi, lakini hafurahii kufuru kwa waja Wake). Az-Zumar -7.
Na Akasema: (Lakini Mwenyezi Mungu Kachukia kutoka kwao, na kwa hivyo Akawazuia na ikasemwa: Kaeni pamoja na wanao kaa!). At-Tawba -47. Na tunaamini kuwa Allah Huridhika na wale wanaoamini na kufanya mema. Allah Anasema: (Mwenyezi Mungu Yu radhi nao, na wao wako radhi naye. Hayo ni kwa anayemwogopa Mola wake). Al-Bayyinah -6.
12
Na tunaamini kuwa Allah Anamkasirikia kila mwenye kustahiki kukasirikiwa katika makafiri na wasiokuwa makafiri. Allah Anasema: (Wanaomdhania Mwenyezi Mungu dhana mbaya. Utawafikia mgeuko mbaya, na Allah Awakasirikie).Al-Fat-h -6.
Na Akasema: (Lakini aliyekifungulia kifua chake kukataa - basi hao ghadhabu ya Allah ipo juuyao, na wao watapata adhabu kubwa). An-Nahl -106.
WAJHI WA ALLAH Na tunaamini kuwa Allah Anao wajihi wenye utukufu na ukarimu. Allah Anasema: (Unabaki Wajihi wa Mola wako wenye utukufu na ukarimu). Ar-Rahmaan -27.
MIKONO Tunaamini kuwa Allah Anayo mikono miwili mitukufu. Allah Anasema: (Bali mikono yake (miwili - yadaahu) iwazi. Hutoa Apendavyo). Al-Maaidah -64.
Na Akasema: (Na wala hawakumhishimu Allah kama Anavyostahiki kadiri Yake. Na Siku ya Qiyaamah ardhi yote itakuwa mkononi Mwake, na mbingu zitakunjwa katika mkono Wake wa kuume. Subhaanahu wa Ta’ala Ametakasika na Ametukuka na hayo wanayomshirikisha nayo). Az-Zumar -67.
13
(Siku ya Ridhwaan Waislamu walipofungamana na Mtume wa Allah (s.a.w) chini ya mti kwa kumpa mkono wote kwa pamoja, mmoja baada ya mwengine, na Allah Akateremsha kauli Yake:
(Bila Shaka wale wanaofungamana nawe, kwa hakika wanafungamana na Allah. Mkono wa Allah uko juu ya mikono yao). Al-Fat-h -10.
Ieleweke kuwa Allah Anaposema Anayo mikono au macho, haina maana kuwa mikono Yake ni sawa na mikono yetu, au macho Yake ni sawa na macho yetu - AstaghfiruLlaah. Meza inayo miguu na viti vina miguu, lakini miguu ya viti na ya meza ni tofauti na miguu ya mwanaadamu aloitengeneza meza ile, kwani sifa ya mtengenezaji lazima iwe tofauti na sifa ya kilichotengenezwa, ama sivyo mtengenezaji na kilichotengenezwa watakuwa kitu kimoja. Na Allah Ndiye mwenye kupigiwa mifano bora, sifa Zake Subhaanahu wa Ta’ala haziwezi kufananishwa na sifa zetu. Lakini wakati huo huo lazima tukikubali kila Alichojinasibisha nacho Subhaanahu wa Ta’ala).
MACHO Na tunaamini kuwa Allah Anayo macho mawili kikweli, na hii inatokana na kauli Yake Subhaanahu wa Ta’ala Aliposema kumwambia Nuuh (s.a.w): (Na unda jahazi mbele ya macho yetu na kwa mujibu wa ufunuo wetu). Huud -37.
Na Mtume wa Allah (s.a.w) amesema: (Pazia yake ni nuru, na lau kama Ataiondoa basi nuru ya Wajihi Wake ingeunguza kila ilichokifikia). Na alipokuwa akihadithia juu ya Ad-Dajjaal alisema:
(Dajjaal ana chongo na Mola wenu Hana chongo). Na tunaamini kuwa macho yetu hayamfikii kumuona Allah. Allah Anasema:
14
(Macho hayamfikilii, bali Yeye anayafikilia macho. Naye ni Mjuzi, Mwenye khabari."Al-An’aam -103.
WAISLAMU WATAMUONA ALLAH SIKU YA QIYAMA Na tunaamini kuwa Waislamu watamuona Mola wao Siku ya Qiyaamah. Allah Anasema: (Zipo nyuso siku hiyo zitang'ara. Zinamwangallia Mola wao). Al-Qiyaamah -22-23.
Na tunaamini kuwa Allah Subhaanahu wa Ta’ala hana mfano wake katika ukamilifu wa sifa Zake. Allah Anasema: (Hapana kitu kama mfano Wake. Naye ni Mwenye kusikia Mwenye kuona). Ash-Shuuraa -11.
Na tunaamini kuwa Allah Hashikwi na usingizi wala halali. Allah Anasema:
(Hashikwi na usingizi wala kulala). Al-Baqarah -255.
Na tunaamini kuwa Allah Hamdhulumu mtu, na hii inatokana na ukamilifu wa uadilifu Wake Subhaanahu wa Ta’ala, na kwamba hapana Asichokijua katika matendo ya waja Wake, na kwamba Hashindwi na chochote, kwani Anapotaka chochote kiwe hukiambia tu; 'Kuwa' na kikawa. Allah Anasema: (Hakika amri Yake Anapotaka kitu ni kukiambia tu: Kuwa! Na kikawa). Yaasiyn -82.
Na tunaamini kuwa Allah Haguswi na uchovu wala tabu ya aina yoyote ile. Allah Anasema:
15
(Na bila ya shaka Sisi tumeziumba mbingu na ardhi na vilio baina yao mnamo siku sita; na wala hayakutugusa machofu). Qaaf -38.
Na tunakiamini kila Alichojithibitishia nafsi Yake, Akasema kuwa Anacho, basi sisi tunaamini kuwa Anacho kwa uhakika, na tunaamini pia kila alichotujulisha Mtume wake (s.a.w) juu ya Mola wake, katika Majina Yake mazuri mazuri na Sifa Zake njema. Lakini tunakataa mambo mawili, nayo ni:
1. Kufananisha (kushabihisha). Nako ni kutamka kwa ulimi au kwa moyo kuwa wasifu wa Allah unafanana na wasifu wa viumbe Vyake. 2. Na pia tunakataa kukisia. Nako ni kujisemeza moyoni au kutamka kwa ulimi kuzikisia sifa za Allah kuwa labda ni hivi au vile. Na tunakanusha kila Allah Alichojikanushia nafsi Yake, au kile alichokikanusha Mtume wake (s.a.w), na tunakinyamanzia kila Alichokinyamazia, na tunaamini kuwa hii ndiyo njia sahihi, kwani kila Alichojikanushia nafsi Yake ni habari kutoka Kwake, na Yeye Subhaanahu wa Ta’ala ndiye mwenye kuijua nafsi Yake na ndiye Msema kweli kupita wote, Mwenye mazungumzo bora kupita wote, waja Wake hawana uwezo wa kujua chochote juu Yake bila Yeye kuwajulisha.
TANBIIH Kila tulichokitaja katika sifa za Allah, iwe kwa urefu au kwa ujumla, katika kuthibitisha au katika kukanusha, yote tumeyanukuu kutoka katika kitabu cha Allaah (Qur-aan) au mafundisho ya Mtume Wake (s.a.w) (Sunnah) iliyo sahihi nayo pia ni itikadi waliyokuwa nayo Maimamu wetu wema waliotangulia.
16
Tunaona kuwa inawajibika kuzifasiri nassw (dalili) zilizomo ndani ya Qur-aan kwa uhakika wake kama Anavyozistahiki Allah, na tunajitenga mbali na njia ya wageuzaji wa maana wale waliozigeuza maana na kuzifasiri kwa njia Asiyoitaka Allah Subhaanahu wa Ta’ala, na tunajitenga mbali na njia ya wabadilishaji waliobadilisha, mbali na maana iliyokusudiwa, na pia tunajitenga mbali na wazidishaji waliozidisha na kuzifanya sifa zake kuwa ni za kumfananisha. Tuna hakika kuwa yale yaliyomo ndani ya Kitabu cha Allah na ndani ya mafundisho ya Mtume Wake (s.a.w) ni haki isiyopingana, na hii inatokana na kauli Yake Subhaanahu wa Ta’ala Aliposema:
(Hebu hawaizingatii hii Qur-aan? Na lau kuwa imetoka kwa asiye kuwa Allah bila ya shaka wangeli kuta ndani yake khitilafu nyingi). An-Nisaa -82.
Na kwa vile kauli zinazopingana huwa zinabishana, na hili ni jambo lisiliowezekana katika habari Anazotupa Allah Subhaanahu wa Ta’ala na anazotupa Mtume wake (s.a.w). Na yeyote anaedai kuwa ndani ya Kitabu cha Allah au ndani ya mafundisho ya Mtume Wake (s.a.w) yamo maneno yanayopingana, akasema hayo kwa kukusudia au kwa vile moyo wake umekwenda upande, basi huyo anatakaiwa atubu kwa Mola wake na atoke ndani ya upotofu wake. Na yeyote anayedhani kuwa kuna upungufu wowote ndani ya Kitabu cha Allah au ndani ya mafundisho ya Mtume wake (s.a.w) au baina yao, basi huyo ima ana upungufu wa elimu au uchache wa fahamu au ana upungufu katika kuzingatia kwake, kwa hivyo aitafute elimu na ajitahidi katika kuzingatia mpaka ukweli utakapombainikia. Na kama haukumbainikia, basi amtafute mwenye elimu kupita yeye na aachane na upotofu wake, na aseme kama wanavyosema wale waliobobea katika elimu: (Tumeamini, zote zimetoka kwa Mola wetu). Al-Imran -7.
17
Na ajue ya kuwa Qur'aan na Sunnah haviwezi kugongana wala kupingana wala hapana hitilafu baina yake.
MALAIKA Na tunaamini juu ya Malaika wa Allah kama ulivyokuja wasfu wao ndani ya Qur-aan kwamba wao ni: (Bali hao ni watumwa walio tukuzwa. Hawamtangulii kwa neno, nao wanafanya amri Zake).………… Allah Amewaumba ili wamuabudu na kumtii. Allah Anasema: (Hawafanyi kiburi wakaacha kumuabudu, wala hawachoki. Wanamtakasa usiku na mchana, wala hawanyong'onyei). Al-Anbiyaa -19-20.
Allah Akatujaalia tusiweze kuwaona, na Aliwafanya wengine kati ya waja Wake kuweza kuwaona, kwani Mtume (s.a.w) alimuona Jibriyl (s.a.w) akiwa katika umbile lake la kweli ana mbawa mia sita, akiwa ameifunika anga yote juu yake. Jibriyl (s.a.w) aliwahi pia kuonekana na Bibi Maryam akiwa katika umbile la binaadamu aliyekamilika, akazungumza naye, na aliwahi pia kumjia Mtume (s.a.w) akiwa pamoja na Maswahaba wake (r.a) akiwa katika umbile la mwanamume asiyejulikana wala hapakuwa na ishara yoyote usoni mwake kama ni mtu aliyetoka safari ndefu, akaliegemeza goti lake juu ya goti la Mtume wa Allah (s.a.w) na kuuweka mkono wake juu ya paja la Mtume wa Allaah (s.a.w), kisha akazungumza naye huku Mtume (s.a.w) akimjibu, na baada ya kuondoka ndipo Mtume (s.a.w) akawaambia Maswahaba wake (r.a) kuwa yule alikuwa Jibriyl (s.a.w). Na tunaamini kuwa Malaika wana kazi zao maalum walizopewa na Mola wao. Jibriyl (s.a.w)ni mletaji wahyi kwa Mitume. Anawateremshia kutoka kwa Allah na kuwafikishia anaotumwa kuwafikishia katika Mitume wake Subhaanahu wa Ta’ala. Na yupo Mikaaiyl aliyepewa kazi ya kuteremsha mvua na ya mazao
18
anapopewa amri na Allah. Na yupo Israafiyl mwenye kazi ya kupuliza parapanda (baragumu) siku ya Qiyaamah. Na yupo Malaika wa kifo aliyepewa kazi ya kutoa roho wakati wa kufa, na yupo Malaika wa majabali, na yupo Malik mlinzi wa mlango wa Motoni, na wapo Malaika wanaowashughulikia watoto wachanga matumboni mwa mama zao, na wengine waliopewa kazi ya kuwahifadhi wanaadamu na wengine wenye kuandika ‘amali zao, na kila mtu ana Malaika wawili. Allah Anasema: (Wanapopokea wapokeaji wawili, wanaokaa kuliani na kushotoni, Hatamki neno ila karibu yake yupo mwangalizi tayari (kuandika)). Qaaf -17-18.
Na wengine wana kazi za kuwauliza maiti baada ya kufikishwa kaburini, wanajiwa na Malaika wawili na kumuuliza Nani Mola wake, nini dini yake, nani mtume wake? Allah Anasema: (Allah Huwatia imara wenye kuamini kwa kauli imara katika maisha ya dunia na katika Aakhirah. Na Allah huwaacha kupotea hao wenye kudhulumu. Na Allah Hufanya apendavyo). Ibraahiym -27.
Na wapo Malaika waliopewa kazi ya kuwashughulikia watu wa Peponi. Allah Anasema: (Na Malaika wanawaingilia katika kila mlango. (Wakiwaambia) Assalaamu ‘Alaykum! Amani iwe juu yenu, kwa sababu ya mlivyosubiri! Basi ni mema mno malipo ya Nyumba ya Aakhirah). Ar-Ra’ad -23-34.
Na Mtume wa Allah (s.a.w) alitujulisha kuwa ndani ya 'Baytul Ma’amuur', iliyopo mbinguni wanaingia na kuswali ndani yake kila siku Malaika elfu sabini wakishamaliza hawaipati fursa ya kurudi humo tena.
19
VITABU Na tunaamini kuwa Allah Amewateremshia Mitume Vitabu ili viwe hoja na mwangaza kwa walimwengu kwa ajili ya kuwafundisha hekima na kwa ajili ya kuwatakasa. Na tunaamini kuwa Allah Amemteremshia kila Mtume Kitabu. Allah Anasema: (Kwa hakika tuliwatuma Mitume Wetu kwa dalili waziwazi, na tukateremsha Kitabu pamoja nao na Mizani, ili watu wasimamie uadilifu). Al-Hadiyd -25.
Na katika vitabu hivyo tunavyovijua ni: 1. Taurati; Allah Alimteremsia Nabii Muusa (s.a.w), na hiki ni Kitabu kitukufu kupita vyote vya Bani Israaiyl. Allah Anasema: (Hakika Sisi Tuliteremsha Taurati yenye uongofu na nuru, ambayo kwayo Manabii walionyenyekea Kiislamu, na wacha Mungu, na Wanachuoni, waliwahukumu Mayahudi; kwani walikabidhiwa kukihifadhi Kitabu cha Allah. Nao wakawa ni mashahidi juu yake). Al-Maaidah -44.
2. Injili; Allah alimteremshia Nabii ‘Issa (s.a.w), na hiki kinakisadikisha Taurati na kukikamilisha. Allah Anasema: (Na tukampa Injili iliyomo ndani yake uongofu, na nuru na inayosadikisha yaliyokuwa kabla yake katika Taurati, na uongofu na mawaidha kwa wacha Mungu). Al-Maaidah -46.
3. Zaburi; Aliyopewa Nabii Daawuud (s.a.w). 4. Sahifa (Suhuf); Walizoteremshiwa Nabii Ibraahiym na Muusa (s.a.w). 5. Qur-aan tukufu; Aliyoteremshiwa Mtume wetu Muhammad (s.a.w) mwisho wa ma Nabii.
21
Allah Anasema: (Ni uongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uongofu na upambanuzi). Al-Baqarah -185.
Na Akasema: (Kinachosadikisha yaliyokuwa kabla yake katika Vitabu na kuyalinda). Al-Maaidah -48.
Kwa Kitabu hiki Allah Akavifuta vilivyotangulia na Akachukua Yeye mwenyewe jukumu la kukilinda ili kibaki kuwa hoja kwa viumbe wote mpaka siku ya Qiyaamah. Allah Anasema: (Hakika Sisi ndio Tulioteremsha Ukumbusho huu, na hakika Sisi ndio Tutaoulinda). Al-Hijr -9.
Ama Vitabu vilivyotangulia, vilikuwa vikiletwa kwa ajili ya wakati maalum, na ukishamalizika wakati wake vinaletwa vingine kuchukua nafasi yake, na hii ndiyo maana havikuwa na uwezo wa kujilinda kutokana na ubadilishaji. Allah Anasema: (Miongoni mwa Mayahudi wamo ambao hubadilisha maneno na kuyatoa mahala pake). An-Nisaa -46.
Na Akasema: (Basi ole wao wanaoandika kitabu kwa mikono yao, kisha wakasema: Hiki kimetoka kwa Allah, ili wachumie kwacho pato dogo. Basi ole wao kwa yale iliyoandika mikono yao, na ole wao kwa yale wanayoyachuma). Al-Baqarah -79.
Na Akasema: )Sema: Nani aliyeteremsha Kitabu alichokuja nacho Muwsaa, chenye nuru na uongofu kwa watu, mlichokifanya kurasa kurasa mkizionyesha, na mengi mkiyaficha). Al-An’aam -91.
21
Na Akasema: (Na wapo baadhi yao wanaopindua ndimi zao katika kusoma Kitabu ili mdhanie kuwa hayo yanatoka Kitabuni, na wala hayatoki Kitabuni. Na husema: Haya yametoka kwa Allah. Na wala hayatoki kwa Allah. Na wanamsingizia Allah uongo na wao wanajua. Haiwezi kuwa mtu aliyepewa na Allah Kitabu na hikima na Unabii kisha awaambie watu: Kuweni wa kuniabudu mimi badala ya Allah. Bali atawaambia: Kuweni wenye kumuabudu Mola wa viumbe vyote, kwa kuwa nyinyi mnafundisha Kitabu na kwa kuwa mnakisoma). Aali-‘Imraan -78-79.
Na Akasema: (Enyi Watu wa Kitabu! Amekwishakujieni Mtume wetu anayekufichulieni mengi mliyokuwa mkiyaficha katika Kitabu, na anayesamehe mengi. Bila shaka imekujieni kutoka kwa Allah nuru na Kitabu kinachobainisha). Al-Maaidah -15.
MITUME Na tunaamini kuwa Allah Amewatuma kwa waja Wake Mitume ili wawe wabashiri na waonyaji. Allah Anasema: (Mitume hao ni wabashiri na waonyaji, ili watu wasiwe na hoja juu ya Allah baada ya kuletewa Mitume. Na Allah ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima). An-Nisaa -165.
Na tunaamini kuwa Muhammad ni mbora wa Mitume wote, kisha Ibrahim kisha Mussa kisha Nuh kisha Issa mwana wa Maryam, na hawa ndio waliohusishwa katika aya ifuatayo. Allah Anasema: (Na tulipochukua ahadi kwa Manabii na kwako wewe (Muhammad), na Nuuh na Ibraahiym na ‘Iysaa mwana wa Mariamu, na tulichukua kwao ahadi ngumu). Al-Ahzaab -7.
22
Na tunaamini kuwa shari’ah ya Muhammad (s.a.w) imekusanya fadhila zote walizokuja nazo Mitume waliotangulia. Allah Anasema: (Amekuamrisheni Dini ile ile aliyomuusia Nuwh na tuliyokufunulia wewe, na tuliyowausia Ibraahiym na Muwsaa na ‘Iysaa, kwamba shikeni Dini wala msifarikiane kwayo). Ash-Shuuraa -13.
Na tunaamini kuwa Mitume wote ni watu, viumbe na hawana uwezo wowote wa kuumba au kugawa rizki wala hawajui ghaibu nk. Allah Anasema: (Wala sikwambiini kuwa nina khazina za Allah; wala kuwa mimi najua mambo ya ghayb; wala sisemi: Mimi ni Malaika). Huud -31.
Allah Alimuamrisha Muhammad (s.a.w) atamke maneno yafuatayo:
(Sema: Mimi sikwambiini kuwa ninazo khazina za Allah. Wala sijui mambo yaliyofichikana. Wala sikwambiini kuwa mimi ni Malaika). Al-An’aam -50.
Na akaamrishwa pia atamke:
(Sema: Siimilikii nafsi yangu manufaa wala madhara, ila apendavyo Allah). Al-A’araaf -188.
Na akaamrishwa pia atamke: (Sema: Mimi sina mamlaka ya kukudhuruni wala kukuongozeni. Sema: Hakika hapana yeyote awezaye kunilinda na Allah, wala sitapata pa kukimbilia isipokuwa kwake Yeye tu). Al-Jinn -21-22.
Na tunaamini kuwa wao ni waja wa Allah Aliowakirimu kwa kuwapa ujumbe. Allah Anasema: (Enyi kizazi tuliyowachukua pamoja na Nuwh! Hakika yeye alikuwa mja mwenye shukrani). Al-Israa -3.
23
Na Akasema: (Ametukuka Aliyeteremsha Furqaan kwa mja Wake, ili awe mwonyaji kwa walimwengu wote). Al-Furqaan -1.
Na juu ya Mitume wengine Akasema: (Wakumbuke waja wetu, Ibraahiym na Is-haaq na Yaa'quwb waliokuwa na nguvu na busara). Swaad -45.
Na Akasema: (Na Daawuwd Tukamtunukia Sulaymaan. Alikuwa mja mwema. Na hakika alikuwa mwingi wa kutubia). Swaad -30.
Na juu ya ‘Issa mwana wa Maryam Allah Anasema: (Hakuwa yeye (‘Iysaa) ila ni Mtumwa Tuliyemneemesha na tukamfanya ni mfano kwa Wana wa Israili). Az-Zukhruf -59.
Tunaamini pia kuwa Allah Subhaanahu wa Ta’ala Amekamilisha ujumbe wake kwa kumleta Muhammad (s.a.w) kama ni Mtume kwa watu wote. Allah Anasema: (Sema: Enyi watu! Hakika mimi ni Mtume kwenu nyinyi nyote, niliyetumwa na Allah Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi. Hapana mungu ila Yeye Anayehuisha na Anayefisha. Basi muaminini Allah na Mtume Wake asiyejua kusoma na kuandika, ambaye anamuamini Allah na maneno Yake. Na mfuateni yeye ili mpate kuongoka). Al-A’araf -158.
DINI YA ALLAH Na tunaamini kuwa dini aliyokuja nayo ni Islam aliyoridhika nayo Allah kwa waja Wake. Na kwamba Allah Haikubali dini nyingine isipokuwa hii. Allah Anasema: (Bila ya shaka Dini mbele ya Allah ni Uislamu). Aali-‘Imraan -19.
24
Na Akasema: (Leo Nimekukamilishieni Dini yenu, na Nimekutimizieni neema Yangu, na Nimekupendeleeni Uislamu uwe ndiyo Dini). Al-Maaidah -3.
Na Akasema:
(Na anayetafuta dini isiyokuwa Uislamu haitakubaliwa kwake. Naye Aakhirah atakuwa katika wenye khasara). Aali-‘Imraan -85.
Na tunaamini kuwa yeyote atakayedai kuwa ipo dini nyengine inayokubaliwa na Allah isiyokuwa Islamu, kama vile dini ya Kiyahudi au ya Kinasara au dini nyengine yoyote, huyo anakuwa amekufuru, na lazima atubu kwa kufru yake hiyo. Akitubu anasamehewa, ama asipotubu huyo anauliwa kama ni Murtaddi, kwa sababu anakuwa ameikadhibisha Qur-aan tukufu. Na tunaamini kuwa hapana tena Mtume baada ya Muhammad (s.a.w), na yeyote atakayejidai utume baada yake au akamsadiki mwenye kujidai utume anakuwa kafir, kwa sababu anakuwa amemkadhibisha Allaah na Mtume Wake na Waislamu wote.
MAKHALIFA WAONGOFU Na tunaamini kuwa Mtume wa Allah (s.a.w) anao Makhalifa waongofu waliouongoza ummah baada ya kufa kwake kwa kueneza elimu na da’awah na uongozi, na kwamba mbora wao ni Abu Bakr Asw-Swiddiyq (r.a) akifuatiwa na ‘Umar Bin Al-Khattwaab (r.a) kisha ‘Uthmaan Bin ‘Affaan (r.a), kisha ‘Aliy Bin Abi Twaalib (r.a), na huu ndio mpangilio wao katika kufadhilishwa kwao. Na tunaamini kuwa ummah ule ndio umma bora kupita zote, na hii inatokana na kauli yake Allah Alipowaambia: (Nyinyi ndio ummah bora kuliko umma zote waliodhihirishiwa watu, kwa kuwa mnaamrisha mema na mnakataza maovu, na mnamuamini Allah). Aali-‘Imran -110.
25
Na tunaamini kuwa walio bora kupita wote ni Maswahaba (r.a), kisha waliokuja baada yao, kisha waliokuja baada yao, na kwamba wangali wapo watu wenye kuidhihirisha haki bila kujali lawama za wanaowalaumu, mpaka siku Allaah atakapoleta amri Yake. Na tunaitakidi kuwa yaliyotokea baina ya Maswahaba (r.a) katika fitna na mapambano, yanatokana na jitihada zao katika uamuzi. Wapo waliosibu na wapo waliokosea, na kama alivyosema Mtume wa Allah (s.a.w): "Mwenyezi kusibu anapata ujira mara mbili, na mwenye kukosea anapata ujira mara moja." Na kwamba Allah Atawasamehe makosa yao, na tunaamini kuwa lazima tuache kuwasema vibaya, na badala yake tuwaseme kwa wema, na tusiwataje isipokuwa kwa kuzitaja sifa wanazozistahiki, na tuziondoe chuki zetu juu yao. Allah Anasema: (Hawawi sawa miongoni mwenu wenye kutoa kabla ya Ushindi na wakapigana vita. Hao wana daraja kubwa zaidi kuliko wale ambao waliotoa baadae na wakapigana. Na wote hao Allah Amewaahidia wema). Al-Hadiyd -10.
Na Akasema: (Na waliokuja baada yao (wakawa wanawapenda Waislamu waliotangulia wanawaombea du’aa) wanasema: Mola wetu! Tughufirie sisi na ndugu zetu waliotutangulia (kufa) katika Uislamu, wala usijaalie ndani ya nyoyo zetu undani kuwafanyia Waislamu (wenzetu). Mola wetu! Hakika Wewe ni Mpole na Mwenye kurehemu). Al-Hashr -10.
SIKU YA MWISHO Tunaamini kuwa Siku ya Mwisho ndiyo Siku ya Qiyaamah, ambapo hapana tena siku nyingine baada yake, na siku hiyo Allah Atawafufua waja wake kwa ajili ya kuwaingiza katika
26
nyumba ya neema 'Peponi', au katika nyumba ya adhabu iumizayo 'Motoni'. Tunaamini kuwa watu watafufuliwa baada ya baragumu kupigwa, kama Allah Alivyosema:
(Na litapulizwa barugumu, wazimie waliomo mbinguni na waliomo katika ardhi, isipokuwa Aliyemtaka Allah. Kisha litapulizwa mara nyengine. Hapo watainuka wawe wanangojea). Az-Zumar -68.
Kisha watu watasimamishwa mbele ya Allah wakiwa kama siku waliyozaliwa bila viatu wala nguo (kama ilivyoelezwa katika Swahiyh Al-Bukhaariy na Muslim – Imepokelewa kuwa Bibi ‘Aaishah (r.a) alimuuliza Mtume (s.a.w): (Watu watafufuliwa wakiwa uchi kila mmoja anamtizama mwenzake?" Mtume (s.a.w) akamwambia: "Ewe Aisha! mambo siku hiyo yatakuwa magumu kuliko hivyo." Watu hawatakuwa na wakati wa kutazamana - mambo yatakuwa magumu sana- Ya rabbi sallim). Allah Anasema: (Siku Tutakapozikunja mbingu kama mkunjo wa karatasi za vitabu. Kamatulivyoanza umbo la mwanzo tutalirudisha tena. Ni ahadi iliyo juu yetu. Hakika Sisi ni watendao). Al-Anbiyaa -104.
Na tunaamini kuwa watu watapewa madaftari yao kwa mkono wa kulia au nyuma ya migongo yao au kushotoni mwao. Allah Anasema: (Ama atakayepewa daftari lake kwa mkono wa kulia. Basi huyo atahesabiwa hisabu nyepesi. Na arudi kwa ahli zake na furaha. Na ama atakayepewa daftari lake kwa nyuma ya mgongo wake. Basi huyo ataomba kuteketea. Na ataingia Motoni). Al-Inshiqaaq -7-12.
27
Na Akasema: (Na kila mtu tumemfungia ‘amali yake shingoni mwake. Na Siku ya Qiyaamah tutamtolea kitabu atakachokikuta kiwazi kimekunjuliwa. Ataambiwa: Soma kitabu chako! Nafsi yako inakutosha leo kukuhesabu). Al-Israa -13-14.
Na tunaamini kuwa mizani zitawekwa Siku ya Qiyaamah na kwamba hapana atakayedhulumiwa. Allah Anasema: (Basi anayetenda chembe ya wema, atauona! Na anayetenda chembe ya uovu atauona!). Zilzaal -7-8.
Na Akasema: (Ama wale ambao mizani zao zitakuwa nzito, hao ndio wenye kufanikiwa. Na wale ambao mizani zao zitakuwa nyepesi, hao ndio walio zitia khasarani nafsi zao, na katika Jahannamu watadumu. Moto utababua nyuso zao, nao watakuwa na nyuso zilizokunjana). Al-Muuminuun -102-104.
SHAFA’AH Na tunaamini kuwa ipo Shafa’ah (msamaha) mkubwa wa Mtume wa Allah (s.a.w) atakapowaombea umma wake baada ya kupewa idhini hiyo na Mola wake Subhaanahu wa Ta’ala, na baada ya watu kuona dhiki na kuanza kuwaendea Manabii (kama Nabii) Nuuh kisha Ibraahiym kisha Muusa kisha ‘Issa (s.a.w) mpaka watakapoishia kwake Muhammad (s.a.w). Na tunaamini pia kuwa wale watakaoingia Motoni katika Waislamu (tu) nao pia wataombewa Shafa’ah watolewe humo, na Shafa’ah hii ni kwa ajili ya Mtume wa Allah (s.a.w) na Mitume wengine na watu wema na Malaika, na tunaamini kwamba Allah Atawatoa Motoni pia makundi kwa makundi ya Waislamu kwa fadhila Zake tu na rehma Zake, bila hata kuombewa Shafa’ah.
28
HODHI NA SWIRAAT Na tunaamini kuwa Mtume wa Allah (s.a.w) ana hodhi lake, na maji yake ni meupe kuliko maziwa na matamu kuliko asali, na yenye harufu nzuri kuliko miski. Urefu wake hodhi hilo ni mwendo wa mwezi mzima, na upana wake mwendo wa mwezi mzima na vyombo vyake vinang'aa kama nyota za mbinguni. Waislamu watakunywa humo, na atakayekunywa hatopata kiu tena. Tunaamini kuwa ipo 'Swiraat' itakayowekwa juu ya Jahannam, na watu watapita juu yake, na kasi zao zitakuwa kiasi cha ‘amali zao. Wapo watakaopita kama umeme, na wengine kama upepo, na wengine kama ndege, na Mtume wa Allah (s.a.w) atakuwa juu yake huku akisema: "Ya rabbi Sallim sallim" (Allah Salimisha Salimisha). Na tunaamini kila kilichokuja katika mafundisho ya Mtume (s.a.w) kuhusu Siku hiyo pamoja na vitisho vyake - Tunamuomba Allah Atusaidie. PEPO NA MOTO Na tunaamini juu ya Pepo na Moto, na kwamba Pepo ni nyumba ya neema Aliyowaandalia Allah waja wake wema wamchao. Ndani yake mna yale ambayo macho hayajapata kuyaona, wala masikio kuyasikia wala halijapata kumpitikia mtu yeyote nafsini mwake. Allah Anasema: (Nafsi yoyote haijui waliyofichiwa katika hayo yanayofurahisha macho - ni malipo ya yale waliyo kuwa wakiyatenda). As-Sajdah -17.
29
Na Moto ni nyumba ya adhabu Aliyoitayarisha Allah Subhaanahu wa Ta’ala kwa ajili ya makafiri madhalimu. Ndani yake mna kila aina ya adhabu ambazo hazijapata kumpitikia mtu yeyote nafsini mwake. Allah Anasema: (Na wakiomba msaada watasaidiwa kwa kupewa maji kama mafuta yaliyotibuka. Yatayowababua nyuso zao. Kinywaji hicho ni kiovu mno!). Al-Kahf -29.
Na Akasema: (Hakika Allah Amewalaani makafiri na Amewaandalia Moto unaowaka kwa nguvu. Watadumu humo milele. Hawampati mlinzi wala wa kuwanusuru. Siku ambayo nyuso zao zitapinduliwa pinduliwa katika Moto. Watasema: Laiti tungelimtii Allah, na tungelimtii Mtume!). Al-Ahzaab -64-66.
MASWALI YA KABURINI Na tunaamini juu ya mtihani wa kaburini, wakati mtu atakapoulizwa nani Mola wake na ipi dini yake na yupi Mtume wake. Allah Anasema: (Allah Huwatia imara wenye kuamini kwa kauli imara katika maisha ya dunia na katika Aakhirah). Ibraahiym -27.
Na tunaamini juu ya neema za kaburini. Allah Anasema: (Wale ambao Malaika huwafisha katika hali njema, wanawaambia: Amani iwe juu yenu! Ingieni Peponi kwa sababu ya yale mliyokuwa mkiyatenda). An-Nahl -32.
31
ADHABU YA KABURINI Na tunaamini juu ya adhabu ya kaburini kwa madhalimu na makafiri. Allah Anasema: (Na lau ungeliwaona madhaalimu wanavyokuwa katika mahangaiko ya mauti, na Malaika wamewanyooshea mikono wakiwambia: Zitoeni roho zenu! Leo mtalipwa adhabu ya fedheha kwa sababu ya mliyokuwa mkiyasema juu ya Allah yasiyo ya haki, na mlivyokuwa mkizifanyia kiburi Ishara Zake). Al-An’aam -93.
Katika mlango huu zipo Hadiyth nyingi zilizo sahihi, na kila Muislamu anatakiwa aamini yote yaliyomo ndani ya Qur-aan na ndani ya Sunnah (Mafundisho ya Mtume wa Allah (s.a.w) yanayohusu mambo ya ghaibu na wala asiyakatae kwa sababu hayalingani na mambo yanayotendeka duniani, kwani ya Aakhirah hayakisiwi na haya ya duniani kutokana na hitilafu kubwa sana iliyopo baina ya mawili hayo- Wa Allaahu l Musta’aan.
QADAR Tunaamini juu ya Qadar (kudra – majaliwa - yale yaliyokwisha andikwa) kheri yake na shari yake kuwa yote yamekwisha andikwa na yote yanatokana na Allah na kwamba kisha waqadiria waja wake kwa elimu yake iliyokienea kila kitu. Na Qadar imegawika sehemu nne. 1. Ujuzi: Tunaamini kuwa Allah ni Mjuzi wa kila kitu, Anajua kilichotokea na kitakachotokea na namna inavyotokea, na hii inatokana na elimu yake isiyo na mwanzo wala mwisho ilichokienea kila kitu. Hakitokei kipya ikawa Allah Hakuwa na elimu nacho, na tunaamini kuwa Allah hasahau.
31
2. Maandishi: Tunaamini kuwa Allah Ameandika katika ubao wa Lawhu al-Mahfuudh yote yaliyotokea na yatakayotokea mpaka siku ya Qiyaamah. Allah Anasema: (Je! Hujui kwamba Allah Anayajua yaliyomo mbinguni na katika ardhi? Hakika hayo yamo Kitabuni. Hakika (kuyadhibiti) hayo kwa Allah ni mepesi). Al-Hajj -70.
3. Kutaka: Tunaamini kuwa Allah Ametaka kiwepo kila kilicho mbinguni na ardhini, kwani hakiwezi kuwepo kitu chochote bila Yeye kutaka kiwepo. Anachokitaka kinakuwa na Asichokitaka hakiwi. 4. Kuumba: Tunaamini kuwa Allah ndiye Aliyeumba kila kitu. Allah Anasema: Allah ndiye Muumba wa kila kitu, na Yeye ndiye Mlinzi juu ya kila kitu.Yeye Anazo funguo za mbingu na ardhi). Az-Zumar -63.
KUTAKA KWA ALLAH Na sehemu hii ya tatu imekusanya kutaka kwa Allah Subhaanahu wa Ta’ala na kutaka kwa viumbe wake, kwa sababu Allah Anakijua kila kinachotendwa na waja Wake, na kwamba Yeye mwenyewe Ametaka kiwepo, ama sivyo kisingewezekana kutendeka. Allah Anasema: (Kwa yule miongoni mwenu anayetaka kwenda sawa. Wala nyinyi hamtataka isipokuwa Atake Allah Mola wa walimwengu wote). At-Takwiyr -28-29.
Na Akasema: (Na lau kuwa Allah Alipenda wasingelipigana. Lakini Allah Hutenda atakavyo). Al Baqarah -253.
32
Na Akasema: (Na lau kuwa Allah Angelipenda wasingefanya hayo. Basi waache na hayo wanayoyazua). Al-An’aam -112 Lakini juu ya yote hayo, tunaamini pia kuwa Allah Amempa mwanaadamu uhuru wa kuamua na Akampa uwezo wa kutenda. Na ufuatao ni ushahidi kuwa mwanaadamu amepewa uwezo huo. Allah Anasema: (Basi ziendeeni konde zenu mpendavyo). Al-Baqarah -223.
Na Akasema: (Na ingelikuwa kweli walitaka kutoka bila ya shaka wangelijiandalia maandalio). At-Tawbah -46.
Kwa hivyo Allah Amempa mwanaadamu uwezo wa kutaka, kuamua na wa kwenda atakapo na kujiandalia atakavyo. Pili, kule kuamrishwa kufanya mema na kukatazwa kufanya mabaya ni dalili kuwa mwanaadamu anao uwezo wa kufanya atakalo, maana kama asingekuwa na uwezo huo kule kukatazwa na kuamrishwa kusingekuwa na maana yoyote. Allah Anasema: (Allah Haikalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri iwezavyo). Al-Baqarah -286.
Tatu, Allah Anamsifia Atendaye mema kwa wema wake, na Anamlaumu atendaye ovu kwa ovu lake. Mwanaadamu asingekuwa na uwezo wa kutenda atakalo basi pasingekuwa na haja ya kumsifia mwema wala kumlaumu muovu kwa sababu huko ni kumpa mtu sifa asiyoistahiki. Nne, Allah Ameleta Mitume. Allah Anasema: (Mitume hao ni wabashiri na waonyaji, ili watu wasiwe na hoja juu ya Allah baada ya kuletewa Mitume). An-Nisaa -165.
33
Yangelikuwa matendo ya watu hayafanyiki kwa uwezo wao na uchaguzi wao, hoja yao isingebatilika kwa kuletewa Mitume.
Tano, kila mtu anapotenda jambo huhisi kuwa ametenda au ameacha kutenda. Utamuona anaposimama, anapokaa, anapoingia, anapotoka, anaposafiri, anapolala. Anapotenda lolote katika haya hufanya kama anavyotaka na wala hahisi kama yupo yeyote anayemlazimisha kufanya hayo, bali anaiona tofauti iliyopo anapofanya jambo kwa hiari yake mwenywe na anapolazimishwa, na hata shari’ah inatofautisha pale mtu anapofanya jambo kwa hiari yake na anapolazimishwa wakati Allah Hamuhesabii kuwa ametenda kosa mtu anayefanya jambo kwa kulazimishwa. Wakati huo huo anayefanya maasi kwa hiari yake huyo anahesabiwa kama ni mkosa, kwa sababu amechagua kufanya hayo kwa hiari yake mwenyewe bila kuelewa kuwa Allah Keshamuandikia. Kwa hivyo hapana anayejua nini alichoandikiwa ila baada ya kutenda. Allah Anasema: (Na haijui nafsi yoyote itachuma nini kesho). Luqmaan -34.
Na Akasema: (Watasema walioshirikisha: Lau kuwa Allah Angetaka tusingelishiriki sisi, wala baba zetu; wala tusingeliharimisha kitu chochote. Vivi hivi walikanusha waliokuwa kabla yao mpaka walipoonja adhabu yetu. Sema: Je, nyinyi mnayo ilimu mtutolee? Nyinyi hamfuati ila dhana. Wala hamsemi ila uongo tu). Al-An’aam -148.
Kwa hivyo tunamuambia mwenye kufanya maasi; 'Kwa nini usitende mema huku ukitegemea kuwa Allah ndiye Alokuandikia uyatende? Kwa sababu hapana tofauti kwako baina ya mema na maovu kwa vile hujui nini ulichoandikiwa kabla ya kukitenda.' Mtume wa Allah (s.a.w) alipowaambia Maswahaba (r.a):
34
(Kila mmoja keshaandikiwa makao yake ya Peponi na ya Motoni." Maswahaba (r.a) wakamuuliza: "Si bora tuache kufanya ‘amali na tuyategemee tuliyokwishaandikiwa?" Mtume (s.a.w) akawaambia: "Hapana! Bali fanyeni, kwani kila mtu amewepesishiwa yale ambayo kwa ajili yake ameumbiwa). Na tunamuuliza mwenye kutenda maasi: 'Kwa mfano wewe unasafiri kwa gari kuelekea Makkah, ukakuta mbele yako njia mbili, mtu mkweli akakuambia kuwa ukipita njia ya mwanzo utakutana na vitisho vingi na utapambana na tabu, ama njia ya pili ni nyepesi na haina matatizo yoyote. Bila shaka utapita njia ya pili, na haiwezekani ukapita ya mwanzo ukasema; 'Nishaandikiwa', na kama utafanya hivyo, watu watakuona mwendawazimu. Mfano mwengine; Ukifanikiwa kupata kazi mbili, mojawapo ina mshahara mkubwa sana na nyengine mshahara mdogo, ukaambiwa uchague, bila shaka utachagua ile yenye mshahara mkubwa. Basi vipi unajichagulia nafsi yako katika ‘amali za Aakhirah zile zilizo duni kisha unasema kuwa 'Hivi ndivyo nilivyokadiriwa (nishaandikiwa)? Unapoumwa kwa mfano, utawatafuta madaktari bora na utakubali kustahamili kupigwa sindano zenye kuuma au kufanyiwa operesheni na kustahamili kunywa dawa chungu, unafanya yote hayo ili upate kupona. Kwa nini basi huachi kujitibia na kusema; 'Nishaandikiwa?' BAADHI YA FAIDA Itikadi hii tukufu yenye mizizi mitukufu ina matunda mengi yenye faida nyingi ndani yake, na zifuatazo ni baadhi tu ya faida hizo: Imani ya kumuamini Allah na majina Yake na sifa Zake vinaongeza mapenzi yetu kwa Allah na kumtukuza. Mambo ambayo kupatikana kwake kunasababisha kuzidisha hima ya
35
kuisimamia dini na kujiepusha na makatazo ya Allah na kufuata maamrisho Yake Subhaanahu wa Ta’ala kwa ajili ya kupata furaha ya duniani na ya Aakhirah. Allah Anasema: (Mwenye kutenda mema, mwanamume au mwanamke, naye akawa ni Muumini, tutamhuisha maisha mema; na tutawapa ujira wao kwa bora ya waliyo kuwa wakiyatenda). An-Nahl -97.
MATUNDA YA KUAMINI MALAIKA Kwanza: Tunapata kujua utukufu wa Aliyewaumba Subhaanahu wa Ta’ala na kuzijua nguvu Zake na Ufalme wake. Pili: Kumshukuru Allah kwa kuwalinda waja Wake, kwani Malaika hawa wamo miongoni mwao wenye kazi ya kuwalinda Waislamu na kuandika ‘amali zao n.k. Tatu; Kuwapenda Malaika kwa kumuabudu kwao Allah kwa ukamilifu, na kwa kuwaombea kwao maghfira Waislamu. MATUNDA YA KUVIAMINI VITABU Kwanza: Tanapata kuielewa rehma ya Allah juu ya waja Wake, kwa vile Amewateremshia Kitabu kila umati kwa ajili ya kuwaongoza. Pili: Tunaiona hekima ya Allah Aliyeweka ndani ya Vitabu hivi shari’ah zenye kunasibiana na kila umati, na akakifanya Kitabu cha mwisho kuwa Qur-aan tukufu ili kiwe kwa umati wote uliobaki katika zama zote na wakati wote mpaka Siku ya Qiyaamah. Tatu: Tunapata kumshukuru Allah kwa neema Yake hiyo.
36
MATUNDA YA KUAMINI MITUME Kwanza: Tunaijua rehma ya Allah kwa waja wake Aliyewapelekea Mitume kwa ajili ya kuwaongoza. Pili: Tunapata kumshukuru Allah kwa neema Yake hiyo. Tatu: Kuwapenda Mitume na kuwaheshimu na kuwapa sifa wanazozistahiki, kwani wao ni Mitume wa Allah waliochaguliwa miongoni mwa watu wote, wakamuabudu Allah kama Anavyostahiki kuabudiwa, wakaifanya kazi ya kuwalingania watu huku wakisubiri na kustahamili udhia. MATUNDA YA KUAMINI SIKU YA QIYAMA Kwanza: Kumtii Allah kwa kutegemea kupata thawabu zitakazokufaa Siku ya Qiyaamah, na kuepukana na kufanya madhambi kwa kuihofia adhabu ya Siku hiyo. Pili: Kumliwaza Muislamu kwa yale anayoyakosa katika neema za hapa duniani na anasa zake, akitegemea neema na anasa za Siku ya Aakhirah. MATUNDA YA KUAMINI QADAR Kwanza: Kumtegemea Allah katika kila jambo, kwa vile vyote ni kwa uwezo Wake Allah. Pili: Starehe ya nafsi na utulivu wa moyo, maana mtu anapotambua kuwa hapana kinachoweza kutokea bila Allah kutaka, moyo hutulia na nafsi huingiwa na matumaini akaridhika na kile alichomuandikia Mola wake. Na hapana mtu anayeishi maisha mazuri na mwenye nafsi iliyotulia kupita yule mwenye kuamini juu ya Qadar. Tatu: Kuondoa majisifu pale mtu anapofanikiwa kupata analolitaka, kwani kupata chochote ni neema itokayo kwa Allah na kwa kuwa keshaandikiwa (keshajaaliwa) mtu huyo kuyapata
37
mafaniko yale au kheri ile, kwa hivyo mtu huyo anatakiwa amshukuru Allah badala ya kujisifu. Nne; Kuondosha hofu na uoga pale mtu anapokikosa anachokitaka au anapopata msiba kwani yote hayo yanatokana na Allah. Allah Anasema: (Hautokei msiba katika ardhi wala katika nafsi zenu ila umekwishaandikwa katika Kitabu kabla hatujauumba. Hakika hayo kwa Allah ni mepesi). Al-Hadiyd -22.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu Atuthibitishe katika itikadi hii na Atuonjeshe matunda yake na atuongezee katika fadhila Zake na asizipoteze nyoyo zetu baada ya kuziongoza, na atumiminie rehma kutoka Kwake kwani Yeye ndiye Mpaji. WalhamduliLlaahi Rabbil ‘aalamin – Mola wetu mswalie na msalimie Mtume wako Muhammad pamoja na Maswahaba wake na ‘Aali zake wema, na kila atakayemfuata kwa wema na uongofu mpaka Siku ya Qiyama.