Uislamu hutoa haki nyingi za kibinadamu kwa mtu binafsi. Zifuatazo ni baadhi ya haki hizo za kibinadamu ambazo Uislamu hulinda.
Uhai na mali ya raia wote katika nchi ya Kiislamu huhesabiwa kuwa takatifu, iwe mtu huyo ni Muislamu au asiye Muislamu. Uislamu pia hulinda heshima. Kwa hivyo, katika Uislamu, kutukana wengine ama kuwafanyia mzaha hakuruhusiwi. Mtume Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, alisema: "Kwa hakika damu zenu, na mali zenu, na heshima zenu zisikiukwe."[1]
Ubaguzi wa rangi hauruhusiwi katika Uislamu, kwa sababu Kurani inaongelea kuhusu usawa wa kibinadamu kwa njia ifuatayo:
"Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliye mcha Mungu zaidi katika nyinyi.[2] Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye habari." (Kurani 49:13)
Uislamu unapinga baadhi ya watu binafsi au mataifa fulani kupendelewa kwa sababu ya utajiri wao, nguvu zao ama koo zao. Mwenyezi Mungu aliwaumba wanadamu wakiwa sawasawa, ambao wanapaswa kupambanuliwa na kila mmoja kwa msingi wa imani zao na uchaji Mungu wao. Mtume Muhammad alisema: "Enyi Watu! Mungu wenu ni mmoja na babu mkuu wenu (Adam) ni mmoja. Mwarabu sio bora kuliko asiye Mwarabu na asiye Mwarabu sio bora kuliko Mwarabu, na mtu mwekundu (yaani weupe wa asili ya Uesia) sio bora kuliko mtu mweusi (yaani weusi wa asili ya Uafrika) na mtu mweusi sio bora kuliko mtu mwekundu,[3] isipokuwa katika uchaji Mungu."[4]
Shida moja kuu inayowakabili wanadamu leo ni ubaguzi wa rangi. Mataifa ambayo yameendelea yanaweza kumtuma mtu kwenda mwezini lakini hayawezi kuzuia mtu kumchukia na kupigana na mwanadamu mwenzake. Tangu enzi za Mtume Muhammad, Uislamu umetoa mfano dhahiri wa jinsi ubaguzi wa rangi unaweza kukomeshwa. Hija ya kila mwaka kwenda Makkah inaonyesha udugu halisi wa Kiislamu wa makabila na mataifa yote, ambapo Waislamu wapatao milioni mbili kutoka kote ulimwenguni hukutana Makkah kutekeleza amali ya hija.
Uislamu ni dini ya uadilifu. Mwenyezi Mungu anasema:
"Hakika Mwenyezi Mungu anakuamrisheni mzirudishe amana kwa wenyewe. Na mnapo hukumu baina ya watu mhukumu kwa uadilifu...." (Kurani 4:58)
Vilevile anasema:
"...Na hukumu ni kwa uadilifu. Hakika, Mwenyezi Mungu anawapenda wanao hukumu kwa haki." (Kurani 49:9)
Tunafaa hata kuwa waadilifu kwa wale tunaowachukia, kama vile Mungu anavyosema:
"...Wala kuchukia wengine kusiwafanye kuacha uadilifu. Kuweni Waadilifu; hivyo ndivyo kuwa karibu mno na uchaMungu...." (Kurani 5:8)
Mtume Muhammad alisema: "Enyi watu, jihadharini na dhuluma,[5] kwani udhalimu utakuwa giza siku ya Kiyama."[6]
Na wale ambao hawajapata haki zao (yaani, kwa kudai haki zao) katika maisha ya sasa duniani watazipata Siku ya Kiyama, kama vile Mtume alivyosema: "Siku hiyo ya Kiyama, haki zote zitapewa kwa wale wanaostahiki (na maovu yatalipizwa)..."[7]