Nakala

UJUMBE KWA ALIYEICHOMA KURANI


Dk. Johannes Klumnik (Abdullah Al-Suwaidi)


Tarjama ya Kiswahili ya Dk. Maulid Makokha


Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na rehema na amani ziwe juu ya Mtume wa Mwenyezi Mungu na jamaa zake na maswahaba wake na wenye kumfuata.


Ama baada ya hayo: Hakika, limetokea kwa mara nyingine. Rasmus Paludan ameichoma Qur’ani Tukufu, lakini mara hii, alilifanya hilo mbele ya ubalozi wa Jamhuri ya Uturuki. Haya makala hayatakuwa makala ya kisiasa. Sitaandika kuhusu Paludan kufika kwenye huo ubalozi katika gari la polisi, na akafanya hicho kitendo chake kibaya mno chini ya ulinzi maalumu ambao hakuna mwandamanaji yeyote yule nchini Uswidi atakayeweza kupata.


Na sitaandika kuhusu jinsi wanasiasa wa Uswidi walivyotetea kitendo chake kwa nguvu mno, na kwamba hakuna chama chochote cha kisiasa kilichoinua juu kidole katika Bunge la Uswidi kwa ajili ya kupitisha sheria ya kupiga marufuku hiki kitendo.


Na sitaandika kuhusu kwamba kile Paludan alifanya katika kuichoma Qur’ani na ghasia zilizosababishwa na hilo ni miongoni mwa sababu za chama cha Kidemokrasia cha Uswidi - chama chenye msimamo mkali ambacho asili zake zinarudi kwa Wanazi - kupata idadi kubwa zaidi ya kura katika historia yake katika uchaguzi wa Uswidi mwaka wa 2022, na kwamba serikali ya sasa inatekeleza ajenda ya hiki chama.


Na sitaandika kuhusu yule mwandishi wa habari ambaye hufuatana na Paludan katika mizunguko yake ya kuchoma Qur'ani, alikuwa akifanya kazi katika idhaa yenye uhusiano na serikali ya Urusi, na kwamba (kitendo cha) Paludan kuichomea Qur'ani mbele ya ubalozi wa Uturuki kinazuia Uswidi kujiunga na NATO.


Bali, sitaandika kumhusu Paludan mwenyewe, na kwamba yeye huzungumza kwenye mtandao na watoto wa miaka 13 juu ya maswala yanayohusiana na ngono. Sina haja ya kutaja hilo, kwa maana vyombo vya habari tayari viliwahi kumfedhehsha hapo awali.


Sitaandika kuhusu haya mambo yote katika haya makala, ingawa ni mambo muhimu. Lakini ninataka kuandika kuhusu kile ambacho ni muhimu zaidi kuliko hayo yote. Ninataka kuandika kuhusu hiki Kitabu ambacho anakichoma. Kwa sababu, si kitabu cha kawaida, bali ni Kitabu


cha Mola Mlezi wa walimwengu wote. Ndiyo, ni Kitabu cha Muumba wetu ambaye alituumba na akaumba wanadamu wote, akiwemo Rasmus Paludan ambaye sasa anakichoma hiki Kitabu. “192. Na bila ya shaka hii (Qur’ani) ni Uteremsho wa Mola Mlezi wa walimwengu wote. 193. Ameteremka nao Roho muaminifu. 194. Juu ya moyo wako, ili uwe katika Waonyaji. ” (Qur’ani 26: 192 - 194). Ndiyo, hii Qur’ani inayobainisha iliteremka kwenye moyo wa Mtume wetu Mtukufu rehema na amani zimshukie kwa njia ya Roho mwaminifu ambaye ni Jibril amani iwe juu yake.


Na zilikuwa aya za mwanzo alizomteremka nazo Jibril kwa Mtume wetu Muhammad rehema na amani zimshukie ni “1. Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, 2. Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, 3. Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! 4. Ambaye amefundisha kwa kalamu. 5. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui. ” (Qur’ani 96: 1 - 5). Hizi aya zinaashiria kwamba inamlazimu mtu kusoma kwa ujumla, na akisome hiki Kitabu hususan. Kwa sababu, hiki Kitabu ni kitabu cha Mola wetu Mlezi ambaye alituumba kutokana na tone la damu, na akatutia sura katika matumbo ya mama zetu kwa namna apendavyo. Hata hivyo, Mwenyezi Mungu Mwenye Nguvu, Mtukufu alitaja baada ya hayo, katika muktadha wa hizi aya, tatizo la mtu, ambalo ni “6. Kwani! Hakika mtu bila ya shaka huwa jeuri 7. Akijiona katajirika.” (Qur’ani 96: 6 - 7). Kwa hivyo, ubabe na kiburi cha mtu humzuia kusoma, kujifunza na kufaidika. Kama sivyo, lau kuwa angelikisoma hiki Kitabu, angepata ndani yake dalili na nuru: “174. Enyi watu! Umekufikieni ushahidi kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Na tumekuteremshieni Nuru iliyo wazi.” (Qur’ani 4: 174). Na angepata ndani yake uponyaji wa yale yaliyomo vifuani: “57. Enyi watu! Yamekujieni mawaidha kutoka kwa Mola wenu Mlezi, na uponyaji kuponyesha yaliyomo vifuani, na uwongofu, na rehema kwa Waumini.” (Qur’ani 10: 57). Na angepata ndani yake uwongofu kwa yaliyo nyooka kabisa: “Hakika hii Qur'ani inaongoa kwenye ya yaliyo nyooka kabisa”. (Qur’ani 17: 9).


Qur’ani Tukufu inatuongoa kwenye kila heri, bali ndiyo chimbuko la sayansi zote. Huyu hapa Mwingereza mtaalamu wa mambo ya mashariki Hartwig Hirschfeld anasema akikubali athari ya Qur'ani katika kuendeleza maarifa (elimu) licha ya chuki yake juu ya Uislamu: "Na hatupaswi kushangaa wakati Qur'ani inapoangaliwa kuwa ndiyo chanzo cha sayansi. Wakati mwingine, Qur'ani huangukia kwenye kila maudhui yanayounganisha kati ya mbingu na ardhi, na maisha ya kibinadamu, biashara na taaluma nyinginezo. Na hili nalo lilipelekea kutolewa kwa makala kadhaa ya kisayansi yanayounda ufafanuzi wa sehemu za hiki Kitabu kitukufu. Na kwa hii njia, Qur'ani ilikuwa sababu ya mijadala mikubwa, na inahusishwa kwa njia isiyo ya moja kwa moja na maendeleo ya ajabu ya matawi yote ya elimu katika ulimwengu wa Kiislamu".


Lakini, mwanadamu hatanufaika na Qur’ani kwa kiasi hiki isipokuwa baada ya kufikiri na kufahamu; “Namna hivi Mwenyezi Mungu anakubainishieni Aya zake mpate kufikiri.” (Qur’ani 2: 219). “Namna hivi anakubainishieni Mwenyezi Mungu Aya zake ili mpate kufahamu.” (Qur’ani 2: 242). Lakini inaonekana kuwa wewe kwa hakika, ewe Paludan, hufikirii wala hutumii akili yako aliyokupa Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo, huelewi yaliyomo ndani yake ya uwongofu na uponyaji: “Sema: Hii Qur'ani ni uwongofu na uponyaji kwa wenye kuamini. Na wasioamini, umo uziwi katika masikio yao, nayo kwao imezibwa hawaioni. ” (Qur’ani 41: 44).


Mimi ni Mswidi, na nimekulia katika familia isiyokuwa ya Kiislamu. Na wakati fulani vivyo hivyo sikuwa ninajua chochote kuhusu Qur'ani Tukufu. Lakini Mwenyezi Mungu akanihurumia, na akaufungua moyo wangu kuisoma, kuitafakari na kuizingatia. Hivyo, nikagundua kuwa hiki Kitabu hakikuwa ni chenye kuandikwa na mwanadamu. Ni Kitabu chenye ushindi, Kitabu kisicho cha kawaida, Kitabu chenye nuru, mwongozo, rehema na heri. Na hili ndilo ninalotaka kutoka kwako pia, ewe Paludan, na kutoka kwa Waswidi wengineo pia, kwamba mkitazame kwa makini na mkitafakari.


Na lau kuwa mlifanya hivyo, mngepata kwamba hiki Kitabu kina uponyaji wa magonjwa ya jamii ya Uswidi ambayo tunaishi ndani yake. Je, si kweli kwamba watu wengi wa Uswidi wanapatwa na maisha ya taabu, na kwamba asilimia 10% ya watu wanameza vidonge vya kupunguza mfadhaiko, na kwamba Waswidi 100,000 wanajaribu kujiua kila mwaka? Mwenyezi Mungu huhuisha roho zilizokufa kwa Qur’ani Tukufu: “Je, aliyekuwa maiti kisha tukamhuisha, na tukamjaalia nuru inakwenda naye mbele za watu, mfano wake ni kama aliyeko gizani akawa hata hawezi kutoka humo?” (Qur’ani 6: 122).


Ewe Paludan, muulize Mswidi yeyote aliyesilimu kuhusu furaha kuu ambayo alihisi, na utulivu wa kiroho ambao anahisi anapoisoma Qur’ani. Je, wewe hutaki furaha?


Ewe Paludan, je, si kweli kwamba jamii ya Uswidi husumbukana na mgawanyiko mbaya wa kifamilia na kutotii wazazi kwa kushangaza? Je, si kweli kwamba baadhi ya baba na mama hufia ndani ya ghorofa yao na kukaa humo kwa miezi, bali miaka, na watoto wao hawaulizi habari zao? Ama Qur’ani Tukufu, ndani yake kuna uponyaji wa huu ugonjwa usiokuwa na tiba: “23. Na Mola wako Mlezi ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu, na wazazi wawili muwatendee wema. Mmoja wao akifikia uzee, naye yuko kwako, au wote wawili, basi usimwambie hata: Ah! Wala usiwakemee. Na sema nao kwa msemo wa hishima. 24. Na uwainamishie bawa la unyenyekevu kwa kuwaonea huruma. Na useme: Mola wangu Mlezi! Warehemu kama walivyo nilea utotoni. ” (Qur’ani 17: 23-24).


Ewe Paludan, je! Si kweli kwamba jamii ya Uswidi inasumbukana na kuongezeka kwa ukali, wasiwasi, chuki na uadui? Ni haja kubwa iliyoje tuliyo nayo ya amri za kimwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu: "Shikamana na kusamehe, na amrisha mema, na jitenge na majaahili. ” (Qur’ani 7: 199). "Na semeni na watu kwa wema” (Qur’ani 2: 83). Bali ni haja kubwa iliyoje tuliyo nayo ya kuiga mfano wa Mtume Mtukufu rehema na amani zimshukie ambaye wewe mara nyingi umekuwa ukimtusi kila wakati: “Basi ni kwa sababu ya rehema itokayo kwa Mwenyezi Mungu ndio umekuwa laini kwao. Na lau ungeli kuwa mkali,


mwenye moyo mgumu, bila ya shaka wangelikukimbia. Basi wasamehe, na waombee maghfira, na shauriana nao katika mambo. ” (Qur’ani 3: 159).


Ewe Paludan, ni nini kinachokukimbiza kutoka kwa Qur’ani Tukufu? Unachukia nini? Je, ni hii Aya: “Hakika Mwenyezi Mungu anaamrisha kufanya uadilifu, na hisani, na kuwapa jamaa; na anakataza uchafu, na uovu, na dhulma. Anakuwaidhini ili mpate kukumbuka.” (Qur’ani 16: 90). Au je, ni hii Aya: “Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliye mchamngu zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye khabari. ” (Qur’ani 49: 13).


Sidhani kama ni hii Aya au ile. Kwa sababu, tatizo lako ni kwamba wewe husomi Qur’ani, na wala hufahamu ujumbe wake. Bali umejishughulisha na kuichoma na kuidunisha. Ndio maana ninakuita, na ninawaita Waswidi wote, bali watu wote kukisoma hiki Kitabu. Kwani ndicho njia ya kutuongoa hapa duniani na kutuokoa Akhera.


Na rehema na amani ziwe juu ya Nabii wetu Muhammad na jamaa zake na maswahaba wake.



Machapisho ya hivi karibuni

UJUMBE KUTOKA KWA MUH ...

UJUMBE KUTOKA KWA MUHUBIRI MUISLAMU KWA MKRISTO

FADHILA YA KUFUNGA SI ...

FADHILA YA KUFUNGA SIKU SITA ZA SHAWAL

Masuala kumi muhimu n ...

Masuala kumi muhimu na mafupi kuhusu mwezi wa Muharram

UJUMBE KWA ALIYEICHOM ...

UJUMBE KWA ALIYEICHOMA KURANI