SSwali la kwanza kati ya maswali mawili makuu katika maisha ni, “Ni nani aliyetuumba?” Tulizungumzia swali hilo katika makala iliyotangulia na (ninatumai) tulikubaliana kuwa jibu ni “Mungu”. Kwa kuwa sisi ni viumbe, Mungu ndiye Muumba.
Sasa, hebu tugeuke kwa “swali kuu” la pili, ambalo ni, “Kwa nini tuko hapa?”
Naam, kwa nini tuko hapa? Ili tukusanye umaarufu na mali? Kucheza muziki na kuzaa watoto? Kuwa mwanaume au mwanamke aliye tajiri kabisa makaburini, kama tunavyoambiwa kwa utani, “Anayekufa na vinyago vingi zaidi ndiye mshindi?”
Hapana, lazima kuwe na mengi zaidi kwa maisha kuliko hayo, basi hebu fikiria kuhusu hili. Kwanza, angalia vilivyo karibu nawe. Kama wewe huishi pangoni, unazungukwa na mambo ambayo sisi binadamu tuliyatengeneza kwa mikono yetu wenyewe. Sasa, kwa nini tumevitengeneza vitu hivyo? Jibu, bila shaka, ni kwamba tunatengeneza vitu ili vitufanyie kazi fulani maalum. Kwa kifupi, tunatengeneza vitu ili vitutumikie. Hivyo, kwa nini Mungu alituumba, ikiwa sio kumtumikia?
Ikiwa tunamkubali Muumba wetu, na kwamba aliwaumba wanadamu ili wamtumikie, swali linalofuata ni, “Vipi? Tunawezaje kumuabudu Yeye? Bila shaka, swali hili linaweza jibiwa vizuri na yule aliyetuumba. Kama Yeye alituumba tumtumikie, basi anatarajia tufanye kazi kwa namna fulani, ikiwa tutafikia malengo yetu. Lakini tunawezaje kujua namna hiyo ni gani? Tunawezaje kujua kipi Mungu anatarajia kutoka kwetu?
Fikiria hili: Mungu alitupa nuru, ambayo tunaweza kupata njia yetu kupitia kwayo. Hata wakati wa usiku, tuna mwezi unaotoa nuru na nyota za kuongoza watu. Mungu aliwapa wanyama wengine mifumo ya kuongoza yanayofaa kwa mahitaji yao. Ndege zinazohama hama zinaweza kusafiri, hata siku zenye mawingu, zikitumia mbinu ya kuangalia jinsi mwanga unavyogawanyika unapopita kwa mawingu. Nyangumi huhamia kwa “kusoma” viwanja vya sumaku vya Ardhi. Salmoni hurudi kutoka maji makuu ya bahari ili kuzaa katika mahali walipozaliwa wao kwa kutumia harufu. Samaki huhisi harakati za mbali kwa njia ya vipokezi vya shinikizo kwenye miili yao. Popo na pomboo vipofu wa mtoni “huona” kwa kutumia mwangwi. Viumbe fulani vya baharini (kwa mfano Mkunga wa umeme) huzalisha na “kusoma” viwanja vya sumaku, na kuwaruhusu “kuona” katika maji ya matope, au katika weusi wa kina cha bahari. Vidudu vinawasiliana na kemikali. Mimea huhisi jua na kukua kuielekea (phototrophism); mizizi yao huhisi nguvu za mvutano na kukua chini ardhini (geotrophism). Kwa kifupi, Mwenyezi Mungu amewapa uwongofu viumbe vyote katika uumbaji wake. Je, tunaweza kuamini kuwa hangetupa mwongozo wa kipengele kimoja muhimu zaidi cha kuwepo kwetu, yaani raison d'etre—sababu yetu ya kuishi duniani? Kwamba hangetupatia zana za wokovu wetu?
Na mwongozo huu haungekuwa . . . Ufunuo?
Fikiria kwa njia hii: Kila bidhaa ina maelezo na sheria. Kwa bidhaa tata zaidi, ambazo sheria zake hatuelewi, tunategemea miongozo ya mmiliki. Miongozo hii imeandikwa na yule anayejua vizuri bidhaa hizi, ambaye ni mtengenezaji. Mwongozo wa mmiliki kwa kawaida huanza na onyo kuhusu matumizi yasiyofaa ya bidhaa na madhara yake, hatua kuhusu maelezo ya jinsi ya kuitumia bidhaa hiyo vizuri na faida zinazopatikana hapo, na hutoa maelezo zaidi ya bidhaa na mwongozo wa utatuzi wa shida ambapo tunaweza kurekebisha kasoro za bidhaa hiyo.
Sasa, jinsi gani hiyo inatofautiana na ufunuo?
Ufunuo unatuambia nini cha kufanya, kile ambacho si cha kufanya na kwa nini, kinatuambia kile Mungu anatarajia kwetu, na kutuonyesha jinsi ya kusahihisha mapungufu yetu. Ufunuo ni mwongozo wa mmiliki usio na kifani, unaotolewa kama mwongozo kwa yule atakayetumia, yaani sisi wenyewe.
Katika ulimwengu wetu, bidhaa ambazo zinakidhi au kuzidi maelezo yake zinachukuliwa kuwa nzuri, huku zingine... hmm... hebu fikiria kuhusu hili. Bidhaa yoyote ambayo inashindwa kufikia maelezo ya kiwanda aidha hutengenezwa, ikiwa inawezekana, au hurejeshwa. Kwa maneno mengine, huharibiwa. Ghafla mjadala huu unageuka kuwa wa kutisha sana. Kwa sababu katika mjadala huu, sisi ndio bidhaa-bidhaa ya uumbaji.
Lakini hebu tusite kwa muda na kufikiria jinsi tunavyohusiana na vitu mbalimbali vinavyojaza maisha yetu. Vikifanya kile tunachotaka, tunafurahi. Lakini vinaposhindwa, tunavitupa. Vingine vinarudi kwenye duka, vingine hupeanwa kama sadaka, lakini hatimaye vyote vinaishia kwenye takataka, na baadaye... huzikwa au kuchomwa. Vile vile, mfanyakazi asiye na ufanisi hufutwa kazi, au kwa kiingereza, 'fired' (maana yake ni kuchomwa). Sasa, simama kwa dakika na ufikirie kuhusu hilo. Je, neno hilo la kitasfida lilitoka wapi? Hmm... mtu anayeamini masomo ya maisha haya hutokana na masomo ya kidini anaweza kufurahia sana hilo.
Lakini hiyo haimaanishi mifano kama hii haifai. Bali, kinyume na hayo, tunapaswa kukumbuka kwamba maagano ya Kale na Jipya yamejaa vielelezo, na Yesu Kristo alifundisha kutumia mifano.
Hivyo labda itakuwa bora tukiyatilia haya maanani.
Hapana, ninafaa kusahihishwa. Ni lazima tutilie haya maanani. Hakuna mtu aliyewahi kufikiri kuwa tofauti kati ya furaha ya mbinguni na mateso ya motoni ni jambo la utani.
Katika sehemu mbili zilizopita za mfululizo huu, tulijibu “maswali makuu” mawili. Ni nani aliyetuumba? Mungu. Kwa nini tuko hapa? Ili kumwabudu Yeye na kumtumikia. Swali la tatu kwa kawaida linakuja: “Kama Muumba wetu alituumba ili tumtumikie na kumwabudu, tutafanyaje hivyo?” Katika makala iliyotangulia nilipendekeza kwamba njia pekee tunayoweza kumtumikia Muumba wetu ni katika kutii amri Yake, kama ilivyotajwa kwenye ufunuo.
Lakini watu wengi watajiuliza yafuatayo kuhusiana na hilo: Kwa nini wanadamu wanahitaji ufunuo? Je, haitoshi tu kuwa mzuri? Je! Haitoshi kila mmoja wetu amwabudu Mungu kwa njia yake mwenyewe?
Kuhusiana na umuhimu wa ufunuo, napenda kutaja yafuatayo: Katika makala ya kwanza ya mfululizo huu nilibainisha kuwa maisha yamejaa dhuluma, lakini Muumba wetu ni wa haki na huweka haki yake si katika maisha haya, bali katika maisha ya baadaye. Hata hivyo, haki haiwezi kuwekwa bila vitu vinne—mahakama (yaani, Siku ya Hukumu); hakimu (yaani, Muumba); mashahidi (yaani wanaume na wanawake, malaika, vipengele vya uumbaji); na kitabu cha sheria cha kuhukumu nacho (yaani, ufunuo). Sasa, Muumba wetu atawezaje kuweka haki kama hakuwaamrisha wanadamu wafuate sheria fulani katika maisha yao? Haiwezekani. Katika hali hiyo, badala ya haki, Mungu angekuwa anafanya dhuluma, kwani angewaadhibu watu kwa makosa ambayo hawakuwa na njia ya kujua ni uhalifu.
Kuna sababu nyingine kwa nini tunahitaji ufunuo? Mwanzo, bila ya kuongozwa na kuonyeshwa njia, wanadamu hawawezi hata kukubaliana juu ya masuala ya kijamii na ya kiuchumi, kisiasa, sheria, n.k. hivyo tunawezaje kukubaliana kuhusu Mungu? Pili, hakuna mtu anayeandika mwongozo wa mtumiaji kwa njia bora zaidi kuliko yule aliyetengeneza bidhaa hiyo. Mungu ndiye Muumba, sisi ni viumbe, na hakuna mtu anayejua mpango wa viumbe kwa njia bora kuliko Muumba. Je, wafanyakazi wanaruhusiwa kubuni majukumu yao ya kazi, mshahara na fidia kama wanavyotaka? Je, sisi wananchi tunaruhusiwa kuandika sheria zetu wenyewe? Hapana? Vizuri basi, kwa nini turuhusiwe kuandika dini zetu wenyewe? Kama historia imetufundisha chochote, ni kuhusu majanga yanayotokea wakati wanadamu wanafuata matamanio yao. Ni wangapi ambao wamedai kuwa na bendera ya mawazo huru wameunda dini zilizowaletea wao wenyewe na wafuasi wao majanga na maafa duniani na katika Akhera?
Hivyo kwa nini haitoshi tu kuwa mzuri? Na kwa nini haitoshi kila mmoja wetu kumwabudu Mungu kwa njia yake mwenyewe? Mwanzo, maelezo ya watu kuhusu kitu “kizuri” hutofautiana. Kwa baadhi, ni maadili ya viwango vya juu na maisha safi, kwa wengine ni wazimu na ghasia. Vilevile, dhana za jinsi ya kumtumikia na kumwabudu Muumba wetu zinatofautiana pia. Muhimu zaidi na kwa uhakika, hakuna mtu anayeweza kutembea kwenye duka au hoteli na kulipa kwa fedha tofauti kuliko ile mfanyabiashara anakubali. Dini pia ni hivyo. Ikiwa watu wanataka Mungu akubali utumwa wao na ibada zao, wanapaswa kulipa kwa fedha ambazo Mungu anadai. Na fedha hiyo ni utii kwa ufunuo Wake.
Fikiria kuhusu kulea watoto katika nyumba ambapo umeanzisha “sheria za nyumba.” Kisha, siku moja, mmoja wa watoto wako anakuambia yeye amebadilisha sheria, na atafanya mambo tofauti. Utajibu vipi? Huenda ukamjibu kwa, “Unaweza kuchukua sheria yako mpya na kwenda Jahannamu!” Naam, fikiria kuhusu hilo. Sisi ni viumbe wa Mungu, tunaishi katika ulimwengu Wake, chini ya sheria Zake, na “kwenda Jahannamu” ndicho kile Mungu atamwambia yeyote anayepuuza sheria Zake.
Ukweli huwa ngumu katika hatua hii. Tunapaswa kutambua kwamba neema zote ni zawadi kutoka kwa Muumba wetu, na hustahili shukrani. Nani hutumia zawadi kabla ya kutoa shukrani? Hata hivyo, wengi wetu hutumia neema za Mungu kwa maisha yetu yote na kamwe hatushukuru. Au tunapeana shukrani baada ya muda kuisha. Mshairi wa Kiingereza, Elizabeth Barrett Browning, alikejeli maombi ya mwanadamu akiwa msibani katika Kilio cha Binadamu:
Na midomo inasema “Mungu nihurumie,”
Ambayo hayajawahi kusema: Mwenyezi Mungu atukuzwe!
Je, hatufai kuonyesha tabia njema na kumshukuru Muumba wetu kwa neema Zake sasa, na hatimaye kwa maisha yetu yote? Je, Yeye hatudai deni hilo?
Ulijibu “Ndiyo.” Lazima uwe umejibu hivyo. Hakuna aliyesoma hadi hapa bila kukubaliana, lakini tatizo ni hili: Wengi wenu walijibu “Ndiyo,” mkijua vizuri kwamba moyo wenu na akili zenu hazikubaliana kabisa na dini za matamaduni yenu. Unakubali kuwa tuliumbwa na Muumba. Unajitahidi kumfahamu. Na unatamani kumtumikia na kumwabudu Yeye kwa namna anavyotaka. Lakini hujui jinsi gani, na hujui ni wapi pa kutafuta majibu. Na hilo, kwa bahati mbaya, sio suala ambalo linaweza kujibiwa katika makala hii. Kwa bahati mbaya, hiyo inapaswa kushughulikiwa katika kitabu, au labda hata katika mfululizo wa vitabu.
Habari njema ni kwamba nimeandika vitabu hivi. Nawakaribisha kuanza na The Eighth Scroll. Kama umependa nilichokiandika hapa, utayapenda niliyoyaandika huko.