WASIA KWA WENYE KUFUNGA
RAMADHAN
Imeandaliwa na Raudhwah Islamic
Group
Imepitiwa na Ust.Abubakari Shabani
Rukonkwa.
Ilipokaribia kuingia Ramadhan Mtume swalla Allahu alayhi
wasalam aliwausia maswahaba zake kuhusu Ramadhan,
wasia tutakaouona katika mada zijazo Inshaa Allah. Na sisi
tukiwa tumeuanza mwezi huu mtukufu ni muhimu
kukumbushana yafuatayo ili uwe wasia wetu kwa ajili ya
kufaidika na Ramadhan.
1-Kumshukuru Allah subhanahu wataala kwa
kutuwafikisha kuidiriki Ramdhan. Hakika kushukuru ni
miongoni mwa ibada azipendazo Allah, na akaahidi kwa
waja wake wakimshukuru basi atawaongeza neema
alizowapa. Amesema Allah subhanahu wataala“Na
alipotangaza Mola wenu : Kama mtanishukuru
nitakuzidishieni, na mkikufuru hakika adhabu yangu ni kali
sana” (Suratu Ibrahim: 7) na akasema tena katika Suratul
Baqarah aya ya 152 “….na nishukuruni wala msinikufuru”.
Uhakika hatuwezi kufikia upeo wa kushukuru neema za
Allah, kwani neema zake hazihesabiki wala hazipimiki.
Amesema Ibnul Qayyim rahimahullah: “Kuwafikishwa
kushkuru neema za Allah, nayo ni neema inayohitaji
shukrani, na kuwafikishwa kushkuru neema ya shukrani, ni
neema nyengine inayohitaji shukrani, na hivyo hivyo
inaendelea kua muislamu aendelee kumshkuru Allah
mpaka mwisho wa pumzi zake”. Miongoni mwa neema hizo
ni kuwafikishwa kuidiriki ramadhan, alau siku moja na usiku
wake, kwani wangapi walitamani alau waweze kufunga
lakini maradhi yamewaweka vitandani, hawawezi kufunga,
na kula yao mpaka watumie mirija? Wangapi walitamani
waidiriki ramadhan na family zao, lakini sasa wako kaburini
ima katika viwanaja vya pepo au mashimo ya moto?
Hatutojua neema mpaka ikiondoka. Tumepewa nafasi ya
kujirekebisha matendo yetu ,kwa kuitumia vizuri
Ramadhan,ili siku ya Qiyama tupate ujira mkubwa apatao
mfungaji, ujira ambao mimi na weye wakati huu
tumewafikishwa na Allah kuupata,na tuukimbilieni huku
tukiomuomba Allah atuwafikishe tuimalize Ramadhan kwa
salama, asitunyime ujira wake wote, na atuwafikishe
tuidiriki Ramadhan inayokuja. Tumshukuruni Allah si kwa
maneno tu, bali na kwa matendo kwa kuonesha kuithamini
Ramadhan.
2-Kufunga kwa Imani na kutarajia malipo
Amesema Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam)katika
hadith sahihi, iliyopokelewa na Bukhari,Muslim na Nasai
rahimahumullah na kusimuliwa na Abu-Hurayra radhiallahu
anhu :“Yoyote atakaefunga Ramadhan, kwa imani na kwa
kutarajia malipo atasamehewa dhambi zake zilotangulia”.
Kufunga kwa Imani ni kukiri kua funga ni amri ya Allah, na
ni miongoni mwa nguzo za kiislamu, atakaesimamisha basi
atakua ameusimamisha uislamu wake, na atakaevunja basi
atakua kaubomoa uislamu wake. Allah hataki kula yetu na
wala hana haja ya kukaa na njaa kwetu lakini anachotaka ni
ibada na kama anavyosema katika lengo la funga ni kuwa
anataka watu wawe wacha-Mungu yani wamuogope yeye
Subhanah.
Kutarajia malipo ni kutaraji kuwa kutokana na funga
tunayofunga basi kuna malipo mazuri yaliyoandaliwa kwa
wafungaji,na malipo ya mwanzo ni kusamehewa dhambi na
mengine yanafuatia Akhera. Ni madhambi mangapi
tumeyafanya ya dhahiri na siri,makubwa na madogo yote
hayo yatasamehewa kwa atakaefunga kwa imani na kutaraji
malipo. Amesema Mtume wa Allah (swalla Allahu alayhi
wasallam) katika Hadith inayosimuliwa na Anas(radhia
Allahu anhu) :“Hakuna amali kwa asiekua na nia na hakuna
na malipo kwa asiyeyatarajia” .
Na tumkumbukeni Allah na ukubwa wake na kwamba
akatayarisha malipo mazuri kwa wafungaji na papo hapo
tuyatarajie malipo hayo.
3-Kuchunga ulimi na mambo ya kipuuzi.
Anasimulia kwamba amesema Mtume swalla Allahu alayhi
wassalam katika hadithi iliyopokewa na Bukhari na Abu-
Daud na kusimuliwa na Abu-Hurayra:“Yoyote asiewacha
maneno ya upuuzi, na kuyafanyia kazi,basi Allah hana haja
ya kuacha chakula chake na kinywaji chake”. Je
tumeizingatia hadithi hii tukafumba midomo yetu?
Amesema Mtume wa Allah (swalla Allahu alayhi wasallam)
kuwa “Yoyote anaemuamini Allah, na siku ya mwisho basi
na aseme la kheri au anyamaze” .(Muttafaqun alayhi). La
kusikitisha Ramadhan ndio imekua mwezi wa
porojo,Ramadhan imekua ndio mwezi wa kusengenyana,
Ramadhan ndio mwezi wa watu kukaa barazani na kuanza
kutaja sifa za wapita njia,na wengine kukaa maskani na
kuhadithiana uongo. Tumejiweka wapi na hadithi hii?
Tokea hapo mwanzo Allah hahitaji chakula chetu wala
kukaa kwetu na njaa lakini analolitaka ni ucha-mungu,na
haupatikani kwa kuzungumza ovyo,na kwa mwenye kusema
uongo na kufanya upuuzi mwengine basi ni bora kwake kula
kwani Allah hahitaji kulifungia tumbo akauwachia
ulimi,kama kufunga basi na viungo vyote vifungwe.
Hatopata hasara anaenyamaza kimya lakini hasara kwa
asiweza kuumiliku ulimi wake.
Kumiliki ulimi ni jambo alousiwa Muadh bin Jabal na
kaambiwa kuumiliki ulimi ndio itakua sababu ya kutengenea
matendo yote iwe sala,swaumu,hajj na hata Jihad. Aliulizwa
Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam):” Ni kipi
kitachowaingiza wengi motoni ? Akajibu kua ulimi na utupu
ndivyo vitakaowaingiza wengi motoni. Na akasema
atakaenidhamini viungo hivyo basi na yeye amemdhamini
Jannah,(Hadith imepokewa na Bukhari). Basi na tuanze
kumdhamini Mtume wa Allah viungo hivi ndani ya
Ramadhan hii kwa kutosema uongo,kutosengenya,kutukana
na porojo nyenginezo.
4-Kutia nia ya kuzidisha kheri, na kushindana katika
mazuri.
Muumini wa kweli hatasheki na kufunga tu ndio ikawa
basi,wala hatosheki na kusali sala zake tano, kisha ikawa
ndio kishamuabudu Allah. Kumuabudu Allah hakutoshi kwa
dakika 25 kwa sala zote tano, ndani ya masaa 24. Allah
hahitaji kupangiwa au kutengewa muda kwani muda wote ni
wake na anastahiki muda wote kuabudiwa. Alipotaja pepo
na starehe zake akamalizia kwa kusema na washindane
wenye kushindana(Muttafifin :26) na kwengine akasema
Kwa mfano wa haya nawatende watendao. (swaaffaat :61).
Pepo inahitaji kushindaniwa kwani kama anavyosema
Rasuul (swalla Allahu alayhi wasallam) kuwa “….Hakika
bidhaa ya Allah ni ghali na bidhaaa ya Allah ni
pepo.(Tirmidhy). Ikiwa kushindana kwenyewe sisi ndio
tutaenda na sala tano tu ambazo hazina khushui ndani yake,
na haikutimizwa rukuu wala sijdah, mbele ya wale ambao
wanaswali mpaka kuvimba miguu yao, na kuroa ndevu zao
kwa kulia na kukesha usiku mzima, kwa kumuabudu Allah
hivi tutakua sawasawa? Au ndo sisi tunashindana kwa aina
za vyakula na nani kapika vingi na vizurii?
Wengi wetu kabla ya Ramadhan tulitia nia ya kuzidisha
kufanya kheri, na wengine baada ya kufanya vibaya
Ramadhan zilopita, tukajiapiza Ramadhan ijayo nitafanya
vizuri, na nitamuabudu Allah kikamilifu, lakini
tunayakumbuka haya au pia tunasubiri ya mwakani, ili
tufanye vizuri kwa kua Ramadhan hii tuko na mishughuliko
ya world cup, hatuna muda wa kumuabudu Allah.
Na tuipambeni Ramadhan yetu kwa Qur-an na qiyamul-layl.
Adhkaar na madarsa na vikao vya kheri,Tutieni nia ya
kuzidisha kheri na miongoni mwa mambo tunaotakiwa
kuyaazimia kuyafanya ni kutekeleza sunna ya itikafu, sunna
ambayo hakuiachapo Mtume baada ya kuhamia Madina na
mwaka aloiwacha ikabidi ailipe lakini ndio sunna
iliyokimbiwa na wengi.
5-Kuwahurumia wanyonge na kuacha israfu.
Anasema Allah (subhanahu wataala) “…. Na
amewanyanyua daraja baadhi yenu juu ya wengine ili
akufanyieni mtihani kwa hayo alokupeni…” (An-aam
165).Na akasema tena katika Suratu-Nahli aya ya 71 “Na
Allah amewafadhilisha baadhi yenu kuliko wengine katika
rizki, Je wale walofadhilishwa,hawarejeshi rizki zao,kwa
wale wanaowamiliki kwa mikono yao ya kulia?”.
Kutofautiana kwa kipato ni dalili za uwepo wa Allah
kuonesha anampa amtakae na humnyima amtakae na
kwamba kupata si kwa utashi wa mtu, bali ni mipango ya
Allah. Na akawataka waja wake wasaidiane. Bila shaka
miongoni mwa jamii za kiislamu tunazoishi nazo wako
wanaofunga lakini wasijue wataftari nini, na wanafunga
hawana daku ya kula ili waweze kufunga vizuri.
Wanafunga kwa kua ni amri ya Allah (subhanahu wataala)
lakini kipato chao na uwezo wao hauwaruhusu kufanya
hivyo. Watu aina hiyo wanahitaji kuangaliwa kwa jicho la
huruma na wale wenye uwezo. Si vibaya kila siku kumlisha
maskini mmoja kwani sadaka ya kulisha chakula ina
thamani kubwa mbele ya Allah (subhanahu wataala). Na
Amesema Mtume wa Allah katika hadithi inayosimuliwa na
Saad bin Khalid:”Atakaemfutarisha aliefunga, basi atapata
ujira sawa na wake, pasi na kupungua ujira wa mfungaji
chochote”(Tirmidhy,Nasai na Ibnu-Majah).
Ikiwa ni hivyo basi na kuftarsha kwetu tusiwasahau maskini
na sio shughuli zetu za kuftarisha kujazwa matajiri na wenye
uwezo wao ambao hata hicho chakula hawakihitaji. Kwa
kutumia kiyasa ya hadith ya Rasuul inayosimuliwa na Abu-
Hurayrah kua chakula kibaya ni chakula cha harusini, kwani
wanaalikwa wasiokihitaji; basi na ftari zetu kesi ndio
hiyohiyo, tunawasahau maskini na wote wanaoalikwa
hawakihitaji. Tusitosheke na thawabu za kuftarisha mtu bali
tutake na thawabu za kulisha maskini kwani tukialika
matajiri tutapata thawabu za kuftarisha tu lakini kualika
maskini itakua ni thawabu za kuftarisha na za kulisha
maskini.
Ama kuhusu israfu tumeona maudhui yake katika mada
zilopita
6-Kukumbuka njaa na kiu siku ya Qiyamah.
Moja kati ya mambo walohusishwa Mitume na ndo ikawa
kama zawadi yao hapa duniani amesema Allah subhanah
“Hakika tuliwachagua kwa lile jambo zuri kabisa la
kuikumbuka Akhera” (Swaad :46). Ni zawadi ambayo
imewafanya kutojali maisha ya dunia ni kutoshughulishwa
na starehe za duniani.
Amesema Allah (subhanahu wataala) hii kuonesha kua kila
kitu chao walikua wakifiri akhera.Na hivyo ndio
anavyotakiwa muislamu wa kweli awe. Awe anafikiri
akhera,kwani nguzo zote za kiislamu kuanzia sala,swaumu
na hata hajji vinamkumbusha mtu mambo yatakayotokezea
siku ya kiyama. Funga inatakiwa imkumbushe mtu njaa na
kiu, kitakachowakuta watu wa motoni na kutokana na kiu
hiyo wataomba kwa watu wa peponi kama anavyotusimulia
Allah (subhanahu wataala) katka suratu A’raf aya ya 50 “Na
watanadi watu wa motoni kuwaita wa peponi: Tumiminieni
maji au chochote katika alivyokuruzukuni Allah. Watasema
watu wa peponi: Hakika Allah ameviharamisha vyote viwili
(yani chakula na maji) kwa makafiri”. Hivyo basi mtu
anapokaa na njaa na kiu akumbuke kua akhera watu waovu
watakaa na njaa na kiu.(Allah atuhifadhi)
Allah atuwafikishe kuyatekeleza haya na mengineyo ya
kheri.