1
بسم الله الرحمن الرحيم
WALIVYOOMBA MASWAHABA ILI WAKUBALIWE SWAUM YA MWEZI WA RAMADHANI Imeandikwa na: Imaam Swaalih Bin Fawzaan Al-Fawzaan Imetafsiriwa na: Idara ya Wanachuoni.com Imepitiwa na: Yunus Kanuni Ngenda Salaf-us-Swaalih (Rahimahumu Allaah) walikuwa wakimuomba Allaah miezi sita Awafikishe katika Ramadhaan, kisha wanamuomba tena kwa miezi sita Awakubalie Swawm ya Ramadhaan. Walikuwa wakitilia umuhimu wa matendo kukubaliwa zaidi kuliko utekelezaji. Allaah (Jalla wa ´Alaa) Amesema: إِنَّمَا يَتَقَبَّلُ اللَّهُ مِنَ الْمُتَّقِينَ
“Hakika Allaah Anatakabalia wenye uchaji Allaah”. (05:27) Allaah Anakubali kutoka kwa wachaji Allaah ambao wanamcha Allaah, wanamukhofu, wanamuogopa na wanamuabudu ukweli wa kumuabudu. Wameitwa ´wachaji Allaah` kwa kuwa wamechukua kinga inayowakinga na adhabu na khasira za
2
Allaah kwa kumtii, kutekeleza maamrisho Yake na kujiepusha
na makatazo Yake.
Salaf (Rahimahumu Allaah) walikuwa wakiogopa matendo yao
kurudishwa kwa sababu ya upungufu wake, ima kwa sababu ya
kutotakasa nia kwa kuingiliwa ndani yake na Riyaa au Sum´aa.
Hii ni khatari kubwa ambayo inayoweza kumsibu mwanaadamu.
Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:
“Hakika ya kila ´amali inalipwa kwa nia na kila mmoja atalipwa
kwa kile alichonuia.”
Nia ndio msingi wa ´amali. Inaweza kuingiwa ndani yake na
kitu katika Riyaa au Sum´aa au ´amali inayofanyiwa asiyekuwa
Allaah (´Azza wa Jalla) na hivyo ´amali hiyo iwe ni yenye
kurudishwa kwa mwenye nayo. Kuna khatari vilevile ´amali
ikawa sio yenye kuafikiana na Sunnah za Mtume (Swalla
Allaahu ´alayhi wa sallam) na hivyo ikawa ni yenye kurudishwa.
Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:
“Mwenye kufanya ´amali isiyokuwa humo Amri yetu
itarudishwa.”
Vilevile wanaogopa kuwa wamewadhulumu watu na hivyo
matendo yao wakapewa wale waliowadhulumu. Inawezekana
wakawa wamemdhulumu mtu katika mali yake au heshima yake
au wamemfanyia uadui. Katika hali hii siku ya Qiyaamah yule
mdhulumiwaji atapewa matendo mazuri ya yule mdhulumaji.
Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:
“Yule aliyemdhulumu ndugu yake basi amrudishie haki yake leo
kabla [ya Siku] ambapo hakutokuwa dinari wala dirhamu. Ikiwa
alifanya matendo mazuri yatachukuliwa na apewe yule
3
aliyemdhulumu na ikiwa hana matendo mazuri yatachukuliwa
madhambi ya yule rafiki yake na apewe yeye.” (al-Bukhaariy
(2317)
Imesimuliwa katika Hadiyth ya kwamba kuna watu watakuja
siku ya Qiyaamaha na matendo mfano wa jibali katika Swalah,
Swadaqah na Swawm, lakini amemdhulumu huyu, amempiga
huyu na amechukua mali ya huyu. Wote hawa watachukua
sehemu ya matendo yake mazuri. Yakiisha kabla ya
kuhukumiwa yatachukuliwa madhambi yao na kuongezewa.
Baada ya hapo atupwe Motoni. Hii ni khatari kubwa. Kwa ajili
hiyo ndio maana Salaf walikuwa wakitilia umuhimu mkubwa
katika ´ibaadah na hata hivyo wakiogopa isije kukubaliwa.