Nakala

1


صفةالحج والعمرة


SIFA YA HIJAH NA UMRAH Mtunzi: 


2


بسم الله الرحمن الرحيم


UTANGULIZI: Shukrani zote ni zake Allah, tunashuhudia ya kwamba hakuna apasae kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah na kwamba Muhammad (Rehma na Amani za Allah ziwe juu yake) ni Mtume wake.Ameufikisha ujumbe na kuifikisha amana, kwa hivyo tunakuomba Mola wetu umsalie na kumsalimu Mtume wako huyu mtukufu (Rehma na Amani za Allah ziwe juu yake) na Aali zake na Maswahaba zake watukufu - Aamin. Amma baad, Allah Anasema: {{Kwa ajili ya Mwenyezi Mungu imewajibikia watu wahiji kwenye Nyumba hiyo, kwa yule Mwenye uwezo njia ya kwenda. Na atakaye kanusha basi Mwenyezi Mungu si mhitaji kwa walimwengu}}. [Aali ‘Imraan–97]. Maulamaa wote wamekubaliana kuwa Hija ni moja katika nguzo tano za Kiislamu, na ni faradhi ijulikanayo kuwa ni ya lazima, Atakayekanusha kuwajibika kwake huwa ni kafiri, alieritadi na kutoka katika dini ya Kiislamu.


3


Wanavyuoni wengi wanasema kuwa: Hija imefaradhishwa katika mwaka wa sita baada ya Hijra, (baada ya Mtume wa Allah (Rehma na Amani za Allah ziwe juu yake) kuhamia Madiynah). Mwanachuoni maarufu Ibnil Qayyim, katika kitabu chake kiitwacho Zaadul Ma-ad, yeye amesema kuwa Hija imefaradhishwa mwaka wa tisa, pale ilipoteremshwa aya isemayo: {{Na timizeni Hija na Umra kwa ajili ya Mwenyezi Mungu}}.[Al Baqarah – 196].


1: NI KATIKA AMALI BORA


4


Amesimulia Abu Hurayrah (Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake) kuwa Mtume wa Allah (Rehma na Amani za Allah ziwe juu yake) aliulizwa: "Amali ipi iliyo bora?"Akajibu: "Imani juu ya Allah na Mtume wake" Akaulizwa: “Kisha ipi?”Akasema: "Kisha Jihadi katika njia ya Allah". "Kisha ipi?"Akasema:"Kisha Hija iliyokubaliwa". Anasema As-Sayid Saabiq, mwandishi wa kitabu ‘Fiq-hus Sunnah’: "Hija iliyokubaliwa ni ile isiyochanganyika na maovu.” Al-Hassan Al-Basry, yeye amesema: "Hija iliyokubaliwa ni ile iliyomfanya aliyehiji anaporudi akawa anaipenda akhera yake kuliko dunia”.


2: WAJUMBE WA ALLAH Mtume wa Allah (Rehma na Amani za Allah ziwe juu yake) amesema: ((Mahujaji na wenye kufanya ‘Umra ni wageni wa Allah, Wanachomuomba anawapa, na wakiomba maghfira(msamaha) anawaghufiria)). [Imepokewa na An-Nasai, Ibni Majah, Ibni Khuzaymah na Ibni Hibban]. Kwa hivyo kila aliyebahatika atambue kuwa tokea siku ile alipoamua kwenda kuhiji, kishakuwa mgeni wa Mola wake Mtukufu, na kwa ajili hiyo anatakiwa awe mtu anayekistahiki cheo hicho, Na anapokuwa katika Ibada


5


hiyo tukufu asigombane wala kuzozana na Mahujaji wenzake. Zimepokelewa Hadithi nyingi zinazotufahamisha kuwa atakayehiji bila kufanya maovu wala kugombana wala kuzozana, hapana zawadi nyingine anayoistahiki isipokuwa Pepo.


3: INAWAJIBIKA HAPO HAPO Maimamu wakubwa kama vile Abu Hanifa na Maalik na Ahmad bin Hanbal na baadhi ya wanafunzi wa Imam Shaafi’iy wanasema: "Hija inamwajibikia kila mtu toka pale anapokuwa na uwezo, Kwa sababu Mtume wa Allah (Rehma na Amani za Allah ziwe juu yake) amesema: ((Anayetaka kuhiji basi aharakishe, kwa sababu huenda akaumwa, mnyama wake akazeeka au akapatwa na shida (akazitumia pesa zake).)) Na katika hadithi nyengine amesema: ((Fanyeni haraka mkahiji, maana hajui mmoja wenu atapatwa na nini)). [Imepokewa na Ahmad, Al-Bayhaqiy, At-Twahaawiy na Ibn Maajah].


4: HIJA KWA MALI YA MKOPO


6


Kutoka kwa Abdullahi bin Abu Auf (Radhi za Allah ziwe juu yake) amesema: ((Nilimuuliza Mtume wa Allah (Rehma na Amani za Allah ziwe juu yake) juu ya mtu asiyewahi kuhiji iwapo anaruhusiwa kukopa kwa ajili ya kuhiji?” Akaniambia; “La, (asifanye hivyo)”.)) [Imepokewa na Al-Bayhaqiy].


5: HIJA YA MWENYE DENI Kamati ya kudumu ya Utafiti wa Kielimu na Utoaji Fat’wa imetoa fat’wa kuhusiana na suala la Hija ya mwenye deni kwa kueleza yafuatayo: Moja ya masharti ya Hija ni uwezo, na mtu kuwa na uwezo wa mali wa kuifanya Hija. Ikiwa mtu ana deni ambalo anadaiwa na mkopeshaji, akawa hakubali yule mtu aende Hija bila kumlipa pesa zake, basi hatoruhusika kwenda Hija hadi alipe deni analodaiwa, kwani mtu huyo atahesabika si mwenye uwezo wa kwenda Hija. Lakini endapo mkopeshaji hatomshikilia alipe pesa zake na ima kamruhusu aende Hija hali ya kuwa ana deni lake, basi anaweza kwenda na Hija yake kwa hali hiyo itakubalika.[Fataawa al-Lajnah ad-Daaimah 11/46]. Na katika Fat’wa nyingine, Kamati ya Kudumu ya Fat’wa walipoulizwa swali kuhusu Hija ya mwenye deni la nyumba ambalo muulizaji alisema anapaswa kulilipa kwa awamu, ilieleza ifuatavyo:Uwezo wa kutekeleza Hija ni moja ya masharti ya kuwa kwake ni waajib. Ikiwa una uwezo wa kulilipa deni hilo kwa awamu ambayo imekutana na wakati wa Hija, basi unaweza kwenda baada ya kulilipa deni katika awamu hiyo,


7


Lakini ikiwa huwezi kulipa deni hilo kwa awamu hiyo, basi ahirisha Hija hadi utakapopata uwezo kwani Allah Anasema:{{Kwa ajili ya Mwenyezi Mungu imewajibikia watu wahiji kwenye Nyumba hiyo, kwa yule Mwenye uwezo njia ya kwenda. Na atakayekanusha basi Mwenyezi Mungu si mhitaji kwa walimwengu}}. [Aal ‘Imraan 3: 97].Na at-Tawfiyq ni kutoka kwa Allah.[Al-Lajnah ad-Daaimah lil Buhuuth al-‘Ilmiyyah wal Iftaa 11/45]. Naye Mwanachuoni Shaykh Muhammad bin Swaalih al-‘Uthaymiyn anasema:Deni linalodaiwa linapaswa kutangulizwa kulipwa kuliko Hija, kwani wajibu wa kulilipa unawekwa mbele kuliko mtu kwenda kutekeleza Hija, Hivyo, anapaswa mtu kulipa kwanza deni kisha ndio kwenda Hija, Na ikiwa hatobakiwa na chochote au kitakachobaki hakitoshelezi gharama za kwenda Hija, basi atasubiri hadi Allah Amjaalie uwezo wa kwendakuitekeleza nguzo hiyo, Lakini likiwa ni deni lenye kuwa na muda mrefu aliopewa mkopeshwa la kulilipa siku za mbele, hivyo, kwa hali hii hata kama mkopeshaji akimruhusu au asimruhusu kwenda Hija, hatoruhusika kwenda Hija ikiwa hana uhakika au dhamana ya kulilipa kwa ule muda aliopewa/waliokubaliana na mkopeshaji. Kwa hali hiyo tunasema: Ikiwa mtu anadaiwa deni, na anafahamu kuwa ana uwezo wa kulilipa kwa muda aliopewa (hata ikiwa ni mbeleni baada ya Hija), basi Hija kwa hali hiyo inakuwa ni wajibu kwake japokuwa ana deni.[Fataawa Ibn ‘Uthaymiyn, 21/96].


8


6: HIJA KWA MALI YA HARAMU Imepokewa kutoka kwa At-Tabarani kuwa Abu Hurayra (Radhi za Allah ziwe juu yake) amesema: kuwa Mtume wa Allah (Rehma na Amani za Allah ziwe juu yake) amesema: ((Anapotoka mwenye kuhiji kwa pesa njema akauweka mguu wake juu ya kipandio cha mnyama wake, akasema: "Labbayka Allahumma labbayk",(Nakuitikia ewe Mola wangu nakuitikia) hujibiwa na msemaji kutoka mbinguni, "Labbayka wa Sa’adayka (Mwitikio wako umekubaliwa na utafurahi kwa amali yako njema hii), kwa sababu zawadi yako (chakula na vifaa vyako) ni vya halali, na mnyama wako ni wa halali, na Hija yako inakubaliwa na haina madhambi". Lakini anapotoka anaehiji kwa pesa za haramu akauweka mguu wake juu ya kipandio cha mnyama wake akasema, "Labbayka Allahumma labbayk", (Nakuitikia ewe Mola wangu nakuitikia), hujibiwa kutoka mbinguni, "Laa labbayka walaa sa’adayka. (Hakukubaliwi kuitikia kwako wala hutolipwa mema), kwa sababu vifaa vyako ni vya haramu na pesa zako niza haramu na Hija yako ni ya dhambi na wala haikubaliwi". (Hadithi Dhaifi).


9


7: KWANZA -UMRA Miyqaat (Mipaka) Mtume wa Allah (Rehma na Amani za Allah ziwe juu yake) ameweka Miyqaat, mipaka, maalum ambayo yeyote anayekwenda Makkah kwa nia ya kuhiji au kufanya Umra haruhusiwi kuivuka kabla ya kutia nia ya Ihraam, mahala hapo. Amewawekea watu wa Madina mji wa Dhul Hulayfah kuwa ni Mpaka wao. Mji huu unajulikana pia kwa jina la Abaar-Ali, nao upo Madina, kiasi cha Kilomita 450 mbali na Makkah. Akawawekea watu wa Sham, mji wa Al-Juhfa kuwa ni Miyqaat yao. Na Miyqaat ya watu wa Najd niQarn al Manaazil. Amma watu wa Yemen Miyqaat yao ni mji wa Yalamlam. Na watu wa Iraaq Miyqaatyao ni Dhaata ‘Irq. Hii ni mipaka aliyoiweka Mtume wa Allah (Rehma na Amani za Allah ziwe juu yake) kisha akasema: ((Hiyo ni mipaka yao na ya kila apitae njia hizo, kwa wasio wakazi wa miji hiyo, kwa kila atakaye kuhiji au kufanya ‘Umra)). Mtu anapowasili katika mipaka hiyo anatakiwa aoge, ajisafishe, akate kucha na kunyoa sehemu ya siri na kujitia manukato akitaka. (Si vizuri kujitia manukato katika vazi la Ihraam, ingawaje si haram kufanya hivyo,


11


isipokuwa sharti iwe kabla ya kutia nia ya ibada ya hija au umra). Unaweza kuoga na kuvaa Ihraam (vazi la kuhijia) pamoja na kufanya yote hayo ukiwa nyumbani kwako, hotelini au popote ulipofikia kabla ya kuifikia mipaka hiyo, isipokuwa nia lazima uitie ufikapo penye mipaka hiyo.


8: VIZURI KUSWALI KABLA YA KUTIA NIA Utakapofika katika mojawapo ya mipaka iliyotajwa ukiwa bado hujaswali Swala ya faradhi ya wakati huo, basi ni bora kuswali kwanza kisha utie nia, Amma ukiwa umekwishaswali, basi ni vizuri (si lazima) kusali rakaa mbili,za Sunnah ikiwa wakati huo si katika nyakati zinazokatazwa kuswali, kisha unatia nia kwa kusema: “Labbayka ‘Umra” Kisha unaanza kufanya Talbiya kwa kusema:


“Labbayka Allahumma Labbayk, Labbayka Laa Shariyka Laka Labbayka, Inna Lhamda Wanni-‘mata Laka Wal Mulk Laa Shariyka Laka.” Unaendelea hivyo njia yote, wanamume wanasema kwa sauti kubwa na wanawake kwa sauti ndogo huku ukimuomba Allah maghfira (msamaha) na kumdhukuru kwa wingi (kumtaja).


11


Unatakiwa pia uwe ukimswalia Mtume wa Allah (Rehma na Amani za Allah ziwe juu yake) kwa wingi pamoja na kuamrisha mema na kukataza maovu unapokuwa safarini mpaka utakapowasili Makkah.


9: HUKUMU YA TAL’BIA Talbiyah ni kutamka "Labbayka Allahumma Labbayka. Labbayka Laa Shariyka Laka Labbayka, InnaL-hamda Wanni-‘mata Laka Wal Mulk Laa Shariyka Laka.” Maulamaa wote wamekubaliana kuwa Talbiyah ni kitendo kilichotolewa amri juu yake. Kutoka kwa Ummus-Salama (Radhi za Allah ziwe juu yake) amesema: ((Nilimsikia Mtume wa Allah (Rehma na Amani za Allah ziwe juu yake) akisema: ‘Enyi watu wa nyumba ya Muhammad, anayehiji kati yenu anyanyuwe sauti yake anapofanya Talbiyah)). [Imepokewa na Imam Ahmad na Ibni Hibban]. Maulamaa wamekhitilafiana katika hukumu yake, katika wakati wake, na katika kuichelewesha. Imam Shaafi’iy na Imam Ahmad wanasema kuwa kitendo hicho ni Sunnah na kwamba mtu anatakiwa aanze kufanya Talbiyah mara baada ya kutia nia ya Ihraam, Na iwapo ametia nia ya Hija kisha asifanye


12


Talbiyah, basi Hija yake inasihi na wala haina tatizo lolote. Imam Maalik, yeye anaona kuwa kitendo hicho ni Wajibu na mtu asipofanya Talbiyah baada ya kutia nia ya Ihraam, akaendelea hivyo muda mrefu bila kufanya Talbiyyah, basi inampasa kuchinja mnyama.


10: FADHILA ZAKE Imesimuliwa na Jaabir (Radhi za Allau ziwe juu yake) kuwa Mtume wa Allah (Rehma na Amani za Allah ziwe juu yake) amesema:((Muislamu yeyote atakayefanya Talbiyah tokea asubuhi mpaka jua linapozama, dhambi zake zitafutwa na atarudi (akiwa hana dhambi) kama alivyokuwa siku aliozaliwa na mama yake)). [Imepokewa na Ibni Majah]. Imesimuliwa pia na Abu Hurayrah(Radhi za Allahziwe juu yake) kuwa Mtume wa Allah (Rehma na Amani za Allah ziwe juu yake) amesema: ((Kila Mwenye kuinyanyua sauti yake kwa kufanya Talbiyah, anapewa bishara (njema), na kila Mwenye kufanya Takbir (kutamka 'Allahu Akbar) anapewa bishara (njema)” Akaulizwa: “Ewe Mtume wa Allah, bishara ya Pepo?” Akasema: “Ndiyo”)). [Imepokewa na At-Tabaraniy na Sa’iyd bin Mansuur].


13


11: KUNYANYUA SAUTI KATIKA TAL’BIA Mtume wa Allah (Rehma na Amani za Allah ziwe juu yake) amesema:((Alinijia Jibriyl (Rehma na Amani za Allah ziwe juu yake) akaniambia: “Waamrishe swahaba zako wanyanyuwe sauti zao katika Talbiyah, kwani hiyo ni katika alama za Hija)). [Imepokewa na Ibni Majah, Imam Ahmad, Ibni Khuzaymah na Al Hakim]. Na kutoka kwa Abubakar (Radhi za Allahziwe juu yake)amesema:((Mtume wa Allah (Rehma na Amani za Allah ziwe juu yake) Aliulizwa: “Amali gani iliyo bora katika Hija?” Akajibu: “Al ajji wa thajji” (Kunyanyua sauti katika kufanya Talbiyah na kuchinja).)) [Imepokewa na At-Tirmidhiy na Ibni Majah].


12: TWA’WAFU YA UMRA Unapowasili Makkah unaanza kufanya, Umra kwa taratibu zifuatazo:‘Unatufu’, kwa kuizunguka Al-Ka’abah mizunguko saba ukianzia penye jiwe jeusi (Al Hajar al aswad), ukiwa mbali na jiwe hilo anzia sawa na jiwe jeusi. Kabla ya kuanza kutufu lielekee Jiwe jeusi kisha linyooshee mkono (ukiweza kulifikia na kulibusu au


14


kuligusa bila ya kuumiza watu ni vizuri), la kama utasababisha madhara kwa watu au kwa nafsi yako, inatosha kuliashiria tu kwa mkono wa kulia kwa mbali huku ukisema: “Bismillahi Allahu Akbar” Kisha unaizunguka Al-Ka’abah ikiwa kushotoni kwako mizunguko saba. Kwa wanamume ni vizuri katika mizunguko mitatu ya mwanzo kukimbia kidogo kidogo mfano wa mtu anayekimbia juu ya mchanga, na mizunguko minne iliyobaki unakwenda mwendo wa kawaida. Wanawake wanakwenda mwendo wa kawaida katika mizunguko yote saba. Wakati wote huo unatakiwa uwe ukisoma dua zozote ulizohifadhi, Hakuna kisomo maalumu au dua maalumu, bali unaweza kuomba dua yoyote na kwa lugha yoyote, na unaweza pia kusoma sura ulizohifadhi katika Qur-aan. Al-Ka’abah ina nguzo nne, na maarufu katika hizo ni nguzo ya jiwe jeusi na nguzo iliyo kabla yake ambayo ni nguzo ya Yaman (Ar-Rukn al-Yamani). Na unapokwenda baina ya nguzo ya Yamani na Jiwe Jeusi ni vizuri kuomba na kuikariri dua ifuatayo: “Rabbana Aatina Fiddunyaa Hasanatan Wa Fil Aakhirati Hasanatan Wa Qinaa ‘Adhaaba Nnaar”. Na maana yake ni: (Mola wetu tupe katika dunia yaliyo mema, na katika akhera (tupe) yaliyo mema, na utuepushe na adhabu ya Moto).


15


Unaendelea hivyo mpaka utakapolifikia Jiwe jeusi, Hapo utakuwa umekwishamaliza mzunguko wa mwanzo, na utaanza mzunguko wa pili kwa kunyanyua mkono wa kulia huku ukiliashiria tena jiwe jeusi na kusema: “Allahu akbar”, kisha utafanya yale yale uliyo fanya katika mzunguko wa mwanzo, mpaka umalize mizunguko saba. Kila unapolifikia jiwe jeusi au unapokuwa sawa nalo, unanyanyuwa mkono wa kulia na kulielekea jiwe huku ukisema: “Allahu Akbar”.


13: MAQAAM IBRAAHIM Ukishamaliza kutufu (kuzunguka) mara saba, unakwenda kuswali raka’a mbili nyuma ya Maqaam Ibraahim, Katika raka’a ya mwanzo unasoma Alhamdu na Qul ya ayyuha l kaafiruun, na katika raka’a ya pili unasoma Alhamdu na QulhuwAllahu ahad, au sura yoyote tofauti na hizo. Usipoweza kuswali penye Maqaam Ibraahim kwa sababu ya msongamano mkubwa wa watu, unaweza kuswali popote karibu na hapo au popote mbali na hapo sharti iwe ndani ya muskiti.


14: KUNYWA MAJI YA ZAM ZAM


16


Baada ya kumaliza kutufu na kuswali raka’a mbili penye Maqam Ibrahim, ni vizuri kunywa maji ya Zam zam, Unaweza kunywa kutoka katika majagi ya maji yaliyoenezwa msikitini hapo, na unaweza pia kwenda penye mifereji (mabomba) ya maji ya Zamzam yaliyokuwepo penye uwanja wa Swafaaa na Marwah. Imepokewa kutoka kwa Bukhari na Muslim kuwa Mtume wa Allah (Rehma na Amani za Allah ziwe juu yake) alikunywa maji ya Zamzam kisha akasema: ((Maji haya yamebarikiwa, Yanamshibisha Mwenye njaa na yanamponesha Mgonjwa)).


15: SA’AY BAINA YA SWAFAA NA MAR’WA Swafaa na Marwah ni vilima viwili vilivyoelekezana, vilivyomo ndani ya msikiti upande wa kisima cha Zamzam. Ukimaliza kutufu na kunywa maji ya Zamzam, unakwenda penye jabali Swafaa kwa ajili ya kuanza kufanya ibada ya Sa'ayi, baina ya majabali Swafaa na Marwah. Unaanza kwa kupanda Swafaa huku ukisema: “Inna Swafaa wal’Mar’wata min shaairi llahi". kisha unasema "Abdau bimaa badaa llahu bihi”, na maana yake ni: (“Hakika Swafaa na Mar’wa ni katika alama za kuadhimisha dini ya Allah, Ninaanza pale alipoanzia Allah, (Ambaye ndani ya Qur-an tukufu ameanza kulitaja jabali Swafaa kisha Mar’wa).


17


Si lazima kutamka maneno hayo, lakini hi ni kwa sababu Mtume wa Allah (Rehma na Amani za Allah ziwe juu yake) alisema na kufanya hivyo. Unapowasili juu ya Swafaa unaelekea Qibla kisha unasema: “La Ilaha Illa Llahu Wahdahu Laashariyka lahu, Lahul’mulku walahul’hamdu Wahuwa Alaa Kulli Shay-In Qadiir, La Ilaha Illa Llahu Wahdahu, Anjaza Waadahu Wanaswara ‘Abdahu Wahazamal Ahzaaba Wahdahu” Unasema hivyo mara tatu. *Ukimaliza kusema maneno haya mara moja waomba dua,unanyanyua mikono, ukielekea kibla, kisha warejea kusema hayo maneno waomba tena dua hadi mara tatu. Hivi ndivyo alivyofanya Mtume wa Allah (Rehma na Amani za Allah ziwe juu yake). Kama hukuweza (kutokana na zahma au kama hujaweza kuhifadhi vizuri) basi unasoma hata mara moja tu, au unaomba du’aa yoyote na kusoma chochote unachoweza kusoma, Kisha teremka na ufanye "Sa’ayya Umra”. Na Sa’ay ni kwenda baina ya Swafaa na Marwah mara saba (Kwenda, inahisabiwa mara moja, na kurudi mara moja). Ni vizuri kukimbia kidogo kidogo kila unapozifikia alama za kijani zilizo ukutani baina ya Swafaa na Marwah, lakini wanawake, wao wanakwenda mwendo wa kawaida. UkifikaMar’wa, unapanda juu na kusema pamoja na kufanya yale ulioyasema na kufanya ulipokuwa juu ya Swafaa.


18


Hakuna katika Twawaafu wala katika Sa’ay, dua au kisomo maalum, Soma chochote na omba dua yoyote.


16: KUJI HALALISHA Ukishamaliza kufanya Sa’ay, unapunguza nywele zako au unazinyoa zote, Kwa wanamume ni vizuri kunyoa, kama alivyofanya na kupendekeza Mtume (Rehma na Amani za Allah ziwe juu yake). Lakini wanawake, wao wanapunguza kidogo tu.Hapo utakuwa umekwisha maliza ibada ya ‘Umra na unaweza kuvua nguo za Ihraam na kuvaa nguo zako za kawaida, Na kinakuhalalikia kila kitu ulichoharamishiwa ulipokuwa katika Umra, hata mkeo. (Kama ni ‘Umra ya Hija unasubiri tarehe 8 Dhul-Hija ili uanze ibada ya Hija).


17: FADHILA ZA KUNYOA NYWELE ZOTE Kutoka kwa Abdillahi bin ‘Omar (Radhi za Allah ziwe juu yake) kuwa Mtume wa Allah (Rehma na Amani za Allah ziwe juu yake) amesema:((“Allah Awarehemu walionyoa (nywele zote)” Masahaba (Radhi za Allah ziwe juu yao) wakasema: “Na waliopunguza ewe Mtume wa Allah?” Akasema: “Allah awarehemu walionyoa (nywele zote).” Wakasema: “Na waliopunguza ewe Mtume wa Allah?” Akasema: “Allah awarehemu walionyoa (nywele zote)” Wakasema: “Na waliopunguza ewe Mtume wa Allah?” Akasema: “Na waliopunguza”)).


19


Katika Hadithi hii Mtume wa Allah (Rehma na Amani za Allah ziwe juu yake) amewaombea Rehma mara tatu walionyoa nywele zote na akawaombea mara moja tu waliopunguza. Tunamuomba Allah atuingize katika Rehma Zake – Aamin.


18: HIJA Tarehe nane Dhul Hija inaitwa "Siku ya Attar’wiyah”, nayo ni siku inayoanza Ibada za Hija. Likishatoka jua la siku hiyo, oga na uvae nguo zako za Ihraam ukiwa nyumbani, hotelini au popote ulipofikia mjini Makkah au nje yake kisha sema: “Labbayka Hijjah”. Masharti ya Ihraam ni yale yale tuliyoyataja hapo mwanzo katika ibada ya ‘Umra. Asubuhi ya siku hiyo Mahujaji wanaondoka Makkah kuelekea Minaa na wanaswali mahali hapo Swala ya Adhuhuri, Alasiri, Magharibi, Ishaa ya siku hiyo, pamoja na Swala ya Alfajiri ya siku ifuatayo, Kila Swala inaswaliwa katika wakati wake Qasran, (kwa kupunguza). Unazifupisha Swala za raka’a nne unaziswali raka’a mbili, ama Swala ya Magharibi unaiswali kwa ukamilifu – raka’a tatu.


21


19: ARAFAA Hukumu yake:


Kusimama ni nguzo kubwa kupita zote katika nguzo za Hija, na hii inatokana na Hadithi ya Mtume wa Allah (Rehma na Amani za Allah ziwe juu yake)aliposema: ((Al Haju ‘Arafah – (Kusimama) Arafa ndiyo Hija yenyewe - atakayewahi usiku wa kujikusanya kabla ya kuingia alfajiri (ya siku ya ‘Arafah) basi amewahi”)). [Imepokewa na Imam Ahmad pamoja na maImam wengine wa Hadithi].


20: KUSIMAMA ARAFAA Likishatoka jua la tarehe tisa Dhul Hija, Mahujaji wanaondoka Minaa na kuelekea ‘Arafa kwa utulivu huku wakisema: “Allahu akbar” – au “Laa ilaaha illa -llah” au huku wakilabiy kwa kusema: “Labbayka Allahumma Labbayk, Labbayka Laa Shariyka Laka Labbayk - Inna Lhamda Wannii’mata Laka Wal Mulk Laa Shariyka Laka.” Wanakwenda kwa utulivu bila kuwaudhi wenzao, na wanaswali Swala ya Adhuhuri na Alasiri wakati mmoja hapo ‘Arafa, Qasran, (kwa kupunguza) zote wakati wa Adhuhuri, kwa adhana moja na iqama mbili. Ni vizuri kubaki katika sehemu ya Namira, mahali ulipo msikiti mkubwa wa Namira na wasiingie ‘Arafah mpaka


21


baada ya wakati wa zawaal. (Kiasi cha saa sita za mchana). Hii siyo lazima, hasa kutokana na zahma za hapo ‘Arafa, siku hiyo, isipokuwa ni bora kama ikiwezekana, Hakikisha kuwa umo ndani ya mipaka ya ‘Arafa, na unapokuwa mahali hapo patakatifu, zidisha kuomba dua na kumtaja Mola wako hukuukiwa umeelekea Qiblah, kwa sababu siku hiyona mahali hapo ndipo watu wanapoghufiriwa (samehewa) madhambi yao yote na kurudi makwao kama siku waliyozaliwa. Nyakati za jioni tafuta sehemu za juu juu. Panda, kisha au ndani ya hema kisha elekea Qiblah na unyanyue mikono yako juu huku ukiomba, kama alivyofanya Mtume wa Allah (Rehma na Amani za Allah ziwe juu yake). Imesimuliwa na Jaabir (Radhi za Allahziwe juu yake) kuwa Mtume wa Allah (Rehma na Amani za Allah ziwe juu yake) amesema: ((“Hakuna siku bora kwa Allah kuliko siku kumi za (mwanzo) za Dhul Hija”. Mtu mmoja akamuuliza: “Siku hizo ni bora, au mtu anapokuwa katika Jihadi kwa muda huo?” Mtume wa Allah(Rehma na Amani za Allah ziwe juu yake) akamuambia: “Siku hizo ni bora kuliko idadi ya siku hizo katika Jihadifiy sabiili Llah. Na hapana siku iliyo bora kwa Allah kuliko siku ya ‘Arafah, Allahhuwaambia Malaika wake kwa fahari: “Tazameni waja wangu, wamekuja nywele zao zikiwa zimetimka, wamejaa mavumbi, wametoka kila sehemu za mbali wakitaraji Rehma Zangu na wala hawakuwahi kuiona adhabu Yangu”. Hakuna siku ambayo Allah anawaepusha watu wengi na moto kuliko siku


22


hiyo”)). [Imepokewa na Abu Ya’ala – Al-Bazzaar – Ibn Khuzaymah na Ibn Hibbaan]. Imepokewa pia kuwa Anas bin Maalik (Radhi za Allahziwe juu yake) amesema: (Mtume wa Allah (Rehma na Amani za Allah ziwe juu yake) alisimama ‘Arafah wakati jua linakaribia kuzama, akasema: “Ewe Bilaal! Ninyamazishie watu.” Bilaal (Radhi za Allah ziwe juu yake), akainuka na kuwataka watu wanyamaze, Kisha Mtume wa Allah (Rehma na Amani za Allah ziwe juu yake) akasema: “Enyi watu! Alinijia Jibril hivi punde na kunipa salam zitokazo kwa Mola wangu, (Kisha) Akasema: ‘Allah amewaghufiria watu wa Arafah na watu wa Masha'ari l haram (Muzdalifah).” Akainuka ‘Omar bin Khattab (Radhi za Allah ziwe juu yake)akauliza: “Hizi (salam na haya maghfira) ni kwa ajili yetu peke yetu?” Mtume wa Allah (Rehma na Amani za Allah ziwe juu yake) akasema: “Hizi ni zenu na za wote watakaokuja (hapa) baada yenu mpaka siku ya Qiyama.” ‘Omar (Radhi za Allahziwe juu yake) akasema: “Kheri za Allah ni nyingi na nzuri”)). Imesimuliwa na Ibnul Mubarak kutoka kwa Sufyaan Ath-Thawriy kuwa: 'Mtu anapokuwa hapo anatakiwa ajishughulishe na kuomba dua pamoja na kumtaja Allah sana ili arudi akiwa amefaidika na ameghufiriwa, na asiwe katika waliokula hasara siku hiyo kwa kuyakosa maghfira ya Allah'. Jua likishazama Mahujaji wanaondokaArafah na kuelekea Muzdalifah.(Usiswali MagharibihapoArafah).


23


21: MUZ’DALIFA Unapokuwa Muzdalifah utaswali Swala ya Magharibi na ‘Ishaa wakati wa ‘Ishaa, raka’a tatu za Magharibi kisha mbili za ‘Ishaa kwa adhana moja na Iqama mbili, Kisha utabaki hapo mpaka baada ya Swala ya Alfajiri. Ukiwa hapo utaomba dua kwa wingi huku ukinyanyua mikono yako juu, na kuelekea Qiblah kama alivyofanya Mtume wa Allah (Rehma na Amani za Allah ziwe juu yake). Ukiwa Muzdalifah utaokota mawe ya kupigia Jamaraat. (Jamaraat ni milingoti mikubwa mitatu ya mawe yanayopigwa hapo Minaa ambayo watu wengine huyaita Mashetani)!!!,Unaokota mawe saba tu, (si lazima kuokota mawe yote hapo Muzdalifah), na mawe mengine unaweza kuokota ukiwa Minaa, Unaweza pia kuokota mawe yote ukiwa hapo kama ukitaka.


22: MINAA


24


Utaondoka Muzdalifa kwa utulivu na kuelekea Minaa baada ya Swalah ya Alfajiri na kabla ya kutoka jua. Utakapowasili Minaa unafanya yafuatayo: 1. Unalipiga Jamaratul ‘Aqabah ambalo watuwanaliita Shetani Mkubwa, lililo karibu na Makkah kwa mawe saba, moja baada ya jingine. Kila unaporusha jiwe unasema:“Allahu Akbar". (Haijuzu kutupa mawe yote saba kwa pamoja). *‘Jamaraat’ si mashetani kama wanavyoitakidi baadhi ya watu wenye kutupa mawe kwa ghadhabu na kutokana na wengine hutupa mawe makubwa wakidhani kuwa wanampiga na kumkomesha Shetani, Hayo yote hayajuzu, kwa sababu ‘Jamaraat’ yamewekwa kwa ajili ya kumtaja Mwenyezi Mungu na kujikumbusha tu namna gani Nabii Ibraahiym mahali hapo alivyompiga mawe shetani aliyejaribu kumshawishi asimchinje Mwanawe kama alivyoamrishwa na Mola wake. Kwa hivyo mtu anatakiwa arushe mawe madogo sana na kuyapiga Jamaraat kwa nia ya kutii amri ya Allah tu, bila ya kuingiza fikra nyingine. Kwa wale wasiojiweza wanaweza kumwakilisha mtu awapigie, na mtu mmoja anaweza kuwakilishwa na wengi. (Kumbuka siku ya mwanzo unalipiga mawe Jamarat moja tu, tofauti na siku zinazobaki unapiga mawe Jamaraat zote tatu). 2. Chinja mnyama wako, na ni vizuri kama utakula katika nyama hiyo na nyengine utawapa masikini.


25


3. Punguza au nyoa nywele zako. (kunyoa nywele zote ni bora zaidi), Na Mwanamke anakata nywele zake kidogo tu. Utaratibu huu ni bora zaidi ingawa unaweza kutanguliza hiki kabla ya kile, Ukimaliza kupiga mawe, kuchinja na kunyoa, unakuwa umekwisha jihalalisha uhalalisho mdogo, na unaweza kuvaa nguo zako za kawaida na kufanya yote uliyokatazwa ulipokuwa na Ihraam, ispokuwa tu huwezi kumwingilia mkeo mpaka umalize Twawaaful Ifaadhwah (Twawaafu ya Hija).


23: TWA WAAFUL-IFAADHWA Hukmu yake:


Maulamaa wote wamekubaliana kuwa Twawaaful Ifaadhwah (Twawaafu ya Hija) ni katika nguzo za Hija, na kwamba asiyetufu Twawafu hiyo Hija yake inabatilika. Na hii inatokana na kauli Yake Mwenyezi Mungu Mtukufu Aliposema: {{Kisha wajisafishe taka zao, na watimize nadhiri zao, na waizunguke Nyumba ya Kale (Nyumba kongwe – Al-Ka’abah).}} [Al Hajj – 29]. Ukishamaliza shughuli za hapo Minaa, unakwenda Makkah na unafanya Twawaaful Ifaadhwah, nako ni kuizunguka Al-Ka’abah mara saba na kufanya kama ulivyofanya katika Twawaafu ya ‘Umrah. Kisha unafanya Sa’ay, kutembea baina ya Swafaa na Marwah


26


na kufanya kama ulivyofanya mara ya kwanza ulipofanya ‘Umrah. Ukishamaliza, unakuwa umekwisha jihalalishia halalisho kubwa, na kwa hivyo hata mkeo anakuhalalikia, Unaweza kuiahirisha Twawaafu ya Ifaadhwah mpaka baada ya kumaliza shughuli zote za Minaa. Ukishamaliza Twawaafu ya Ifaadhwah unarudi Minaa na unabaki hapo usiku wa tarehe 11, 12 na 13 kwa wasiokuwa na haraka. Hizo zinaitwa siku za Tashriyq. Inatosha kama utabaki hapo usiku wa tarehe 11 na wa 12 tu. Katika siku 2 au 3 hizo unapiga mawe Jamaraati zote tatu kila siku kwa mpangilio ufuatao: Anza kupiga Jamaraat lambali na Makkah, (Jamaraat dogo) kisha la kati, kisha Kubwa (Jamarat al Aqaba). Kila moja piga mawe saba huku ukisema: "Allahu Akbar", kila unaporusha jiwe. Hii ni kwa siku tatu zilizobaki.


24: NYAKATI ZA KUPIGA MAWE Siku ya An-Nahr – Sikukuu mosi, usipige mawe mpaka jua lichomoze. ((Mtume wa Allah (Rehma na Amani za Allah ziwe juu yake) alipokuwa Muzdalifah aliwatanguliza Minaa watu dhaifu na wazee na wanawake, akawaambia: “Musirushe mawe mpaka jua litoke”)).[Imepokewa na At-Tirmidhiy].


27


Mwenye udhuru anaweza kuchelewesha mpaka kabla ya Magharibi, lakini ni vizuri kupiga mawe baada ya kutoka jua na kabla haijaingia Magharibi kwa asiyekuwa na udhuru. (Baadhi ya Maulamaa wanajuzisha kupiga mawe baada ya Magharibi kwa udhuru, lakini bora ujaribu kupiga kabla jua kuzama). Wakati wa kurusha mawe kwa siku mbili zilizobaki au siku tatu kwa wale wasiotaka kuharakisha, ni baada ya Zawal (wakati wa adhuhuri pale jua linaposogea kidogo baada ya kuwa katikati).


25: KUOMBA DUA Ni vizuri kuelekea Qiblah na kuomba dua baada ya kumaliza kupiga kila Jamaraat isipokuwaJamaraat la mwisho. Hadithi iliyosimuliwa na Bukhari na Imam Ahmad inasema: ((Mtume wa Allah (Rehma na Amani za Allah ziwe juu yake) Alikuwa akeshapiga kila Jamaraat kwa mawe saba akisimama na kuelekea Qiblah na kuomba dua, isipokuwa baada ya kulipiga Jamaraat la mwisho hakusimama)).


26: SIKU YA KUHARAKISHA


28


Ikiwa unataka kubaki hapo kwa mda wa siku mbili tu, basi siku ya tarehe Kumi na mbili Dhul Hijaambayo hujulikana kama ni "Yawmul isti’ijaal" - Siku ya Kuharakisha – unapiga mawe na kuondoka Minaa kabla ya jua kuzama, na ikiwa utakawia kuondoka ukawepo hapo baada ya juwa kuzama itakubidi ubaki hapo siku moja zaidi. Ni vizuri kubaki usiku wa tatu ikiwa huna cha kukushughulisha.


27: TWAWAFUL-WADA’A Unapotaka kurudi nchini kwako baada ya kumaliza shughuli za Hija, unatufu Twawaful wada’a, (Twawafu ya kuaga) nayo ni kama ifuatavyo: Unatufu Al-Ka’abah mara saba na kufanya kama ulivyofanya katika Twawafu za mwanzo, lakini mara hii bila ya kufanya Sa’ay baina ya Swafaa na Marwah. Kwa kufanya hivyo ibada ya hija itakua imekwishaa. Tunamuomba Allah Mtukufu Azikubali Ibada zetu, Atusamehe yote tulio mkosea na Aifanye Hija yetu iwe HijaMabruur. Aameen!!



Machapisho ya hivi karibuni

Uislamu Ni dini ya ma ...

Uislamu Ni dini ya maumbile na akili na furaha

UJUMBE KUTOKA KWA MUH ...

UJUMBE KUTOKA KWA MUHUBIRI MUISLAMU KWA MKRISTO

FADHILA YA KUFUNGA SI ...

FADHILA YA KUFUNGA SIKU SITA ZA SHAWAL