SHARTI ZA KUSIHI KWA FUNGA -
SEHEMU YA KWANZA
Makala imeandaliwa na Raudhwah islamic
Group
Imepitiwa na Abubakari Shabani Rukonkwa.
Ili swaum isihi kuna sharti zake zitimizwe ndipo funga hiyo
itasihi. Na sharti hizi zisipokamilika basi funga haitosihi au
funga itabatilika na itamlazimu mwenye kufunga aje kuilipa
funga hiyo.
Hivyo hatutokuja kueleza yanayofunguza. Bali makala hii in
shaa Allah itamtosheleza msomaji kujua sharti za kusihi kwa
funga na kubatilika kwa funga. Pia katika baadhi ya vitabu
wametumia neno NGUZO ZA FUNGA zote hizo ni sawa na
wanakusudia kukieleza kitu hicho hicho.
1-KUTIA NIA KILA SIKU
Ni lazima kwa mwenye kufunga atie nia kwa kila siku
anayofunga. Iwe funga hiyo ya sunna au faradhi kama
Ramadhan. Na hatokuwa na funga yule atakaekuwa hajatia
nia. Kwani katika hadithi kutoka kwa Sayyidina Omar (radhi
za Allah ziwe juu yake) amesema: “Nimemsikia Mjumbe wa
Allah akisema: “ Hakika kila jambo huambatana na nia na
kila mtu atalipwa kutokana na kile alichokinuwia … .”
[Bukhari na Muslim].
Na inamuwajibikia mwenye kufunga Ramadhan atie nia
kabla ya kuanza kwa alfajiri ya kweli. Na endapo mwenye
kutaka kufunga hatotia nia kabla ya wakati huo basi
hatokuwa na funga. Na itamuwajibikia kwake yeye kuja
kuilipa funga hiyo. Kwa ushahidi wa Hadithi ya Mtume
(swalla Allahu alayhi wasallam): “Yeyote ambae hatoweka
nia ya kufunga kabla ya alfajiri hatokuwa na funga.”
Imepokewa na Imam Ahmad na An-Nasai.
Hivyo inamlazimu atie nia kwa kuzingatia kabla ya kuanza
kwa funga na nia hiyo iwe kwa kila siku atakayoifunga.
Ama mwenye kufunga sunna anaweza kutia nia kabla ya
kupambazukwa kwa jua,mpaka wakati wa zawali (kabla ya
Adhuhuri)
Kwa nini mtu atie nia kila siku ndani ya Ramadhani? Swala
humalizika kwa mtu kutoa salam. Na anapotaka kuingia
katika swala nyengine basi analazimika kutia nia ya swala
nyengine. Hivyo hivyo kwa mwenye kufunga, swaumu
humalizika kwa kuzama kwa jua hivyo basi anaetaka
kufunga siku ya pili lazima atie nia nyengine. Kwani
anakuwa ameanza swaumu nyengine. Na hii ndio kauli
yenye nguvu.
Imethibiti hadithi ya mtume (swalla Allahu alayhi wasallam)
akisema:
م NRZ "[رواه ا QF ا R ST ا UVW م NL Y : " FG و IFJ لله KFL ل NO
. Nًb`O`R J لله iVJ jWi R ج ١ ص ٢٨٨ ^ ط` ا ab cNR
Alisema mtume (swalla Allahu alayhi wasallam):Hana funga
yoyote ambae alie lala bila kuweka nia usiku.
[Imepokelewa na imamu maliki katika kitabu chake cha
muwatwaa 1/288]
Je kutia nia ni kwa kutamka au moyoni tu inatosha?
Kwanza ni jambo lisilokuwa na shaka kuwa nia mahali pake
ni moyoni. Ama suala la kutamka kwa kauli za maulamaa
wengi ni jambo ambalo halikuthibiti katika dini. Hivyo basi
mwenye kufunga atatia nia moyoni mwake kwani Allah
anajua yale yote yaliyomo ndani ya nafsi zetu na hakifichiki
kwake kitu chochote.
Nakauli iliyo sahihi nikwamba kutamka niya ni BIDAA
kwasababu nia nikatika matendo ya moyo.
2- KUJIZUIA KULA NA KUNYWA
Ni lazima kwa mtu mwenye kufunga ajizuie kula na kunywa
kuanzia kuingia kwa alfajiri ya kweli hadi kuzama kwa jua.
Kwa kauli ya Allah (subhanahu wata‘ala): “Na kuleni na
kunyweni mpaka kubainike kwenu weupe wa alfajiri katika
weusi wa usiku, Kisha timizeni saumu mpaka usiku.”
(Suratul Baqara : 187).
Nini hukmu ya kula kwa kusahau
Yule ambae atakula kwa kusahau iwe kidogo au sana basi
haitobatilika funga yake kwa ushahidi wa hadithi ya Abu
Hurayrah (radhi za Allah ziwe juu yake) amesema :
Amesema Mtume (Swalla Allahu alayhi wa sallam):
“Mwenye kusahau nae amefunga, basi akala au akanywa na
aikamilishe funga yake.”
[Al Bukhariy na Muslim].
Na katika riwaya nyengine “Kwani hakika Allah amemlisha
na amemnywisha.” Ila Muislamu azingatie asije kujiigiza
kuwa amesahau kwani ataweza kuwadanganya watu lakini
Allah hawezi kumdanganya hata kidogo.
Je kupiga mswaki ndani ya Ramadhan kwa kutumia dawa
inasihi?
Ama Kupiga mswaki ndani ya funga hilo linasihi kwani
Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) alikuwa akipiga
mswaki nae amefunga. Ama suala linakuja kwenye kupiga
mswaki kutumia dawa.
Dawa ya mswaki haibatilishi swaum ikiwa wakati anasafisha
meno atatema na wala hamezi. Ama ikiwa atakusudia
kumeza, swaumu yake itabatilika.
Na yule ambae anakhofia anaweza kumeza basi bora
asitumie dawa. Na kilichopendekezwa zaidi na maulamaa
mtu apige mswaki kwa kutumia dawa kabla ya kuanza kwa
saumu na itakapoingia saumu apige mswaki bila ya kutumia
dawa ili asije kutumia dawa na kuimeza.
Je kuonja chakula wakati mtu amefunga inasihi?
Kuonja chakula wakati mtu amefunga inasihi kwa sharti
ahakikishe kuwa hamezi kile alichokiweka kwenye ulimi
kwa ajili ya kuonja.
Je kukoga katika mchana wa Ramadhan inasihi?
Kukoga au kukosha uso ikiwa mtu yumo kwenye funga
inasihi. Ila ahakikishe maji hayaingii katika matundu ya
mwili kama masikioni nk.
Ama yakiingia bila ya kukusudia hilo halina tatizo. Na
yakiingia kwa kusudia basi atakuwa amefungua.
Ni ipi hukmu ya mwenye kufunga kutia dawa kwenye
macho?
Anaruhusika kutumia na haitobatilika funga yake.
Nini hukmu ya kuchoma sindano wakati mtu amefunga?
Ikiwa sindano ni ya dawa tu basi haifunguzi. Ila sindano
ikiwa imewekewa kitu chochote ambacho ndani yake
kitampa mwenye kufunga nguvu kama glucose basi hapo
itakuwa amefungua. Allah ni mjuzi zaidi.
3-KUJIZUIA NA KUJITAPISHA KWA MAKUSUDI
Pia ni wajibu kwa mwenye kufunga kujizuia na kujitapisha
kwa makusudi. Ama akitapika bila ya kukusudia basi
ataendelea na funga yake kama kawaida. Na akijitapisha
kwa makusudi ni lazima ailipe funga hiyo.
Kutoka kwa Abu Hurayrah (radhiya Allahu anhu) amesema:
Amesema Mtume (Swalla Allahu alayhi wa sallam): "... na
mwenye kujitapisha basi inamuwajibikia kulipa." Bukhari na
Muslim.
4-KUWA MUISLAMU
Ikiwa mtu sio Muislamu basi kwake yeye haimuwajibikii
kufunga. Na akija kusilimu basi hatolipa kwa zile siku
ambazo hakufunga kwani alipokuwa sio Muislamu
haikumuwajibikia kufunga.
Ama Muislamu ambae ataritadi wakati amefunga basi moja
kwa moja funga yake itabatilika na akija kutubu na kuamua
kurudi kwenye Uislamu basi inamuwajibikia kuzilipa siku
zote ambazo aliziwacha wakati ametoka kwenye Uislamu.
5-KUWA NA AKILI KATIKA MCHANA MZIMA WA
RAMADHAN
Pia ili swaumu isihi lazima mwenye kufunga awe na akili na
ikiwa atarukwa na akili basi funga yake itabatilika. Na
hakuna tatizo kwa mtu kuzimia kwa muda mchache katika
mchana wa mwezi wa Ramadhan.
SHARTI ZA KUSIHI KWA FUNGA- SEHEMU YA PILI
3 – KUJIZUIA KUFANYA TENDO LA NDOA KWA
MAKUSUDI NA KUJITOA MANII
Ikiwa mtu atafanya jimai bila ya kukusudia basi mtu huyo
atakuwa amesameheka. Kwa kauli ya Allah:
رًا `ُz| نَ للهَُّ َ N وَ َ ْ ُ ُ `ُFُO تْ iَ َّ َ َ NR َ ْ َ ِ وَ Iِ ِ ُ ْ ْ^َ أَ ْ N َ ِb حٌ NَT ُ ْ ُ َ ْ FJ َ َ ْ ...{و
}N ً رَ ِ
''Wala si lawama juu yenu kwa mlivyo kosea. Lakini ipo
lawama katika yale ziliyo fanya nyoyo zenu kwa makusudi.
Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye
kurehemu''
(Suratul Ahzaab : 5).
Ama yule ambae atafanya jimai kwa makusudi basi huyo
funga yake itabatilika na itamlazimu kwake yeye kuilipa
funga hiyo pamoja na kutoa kafara.
Kafara kwa yule ambae atafanya tendo la ndoa katika
mchana wa Ramadhani ni :
i. Kuacha huru mtumwa.
ii. Kufunga miezi miwili mfululizo.
iii. Alishe maskini 60 kila mmoja kibaba kimoja.
Ikiwa mke au mume mmoja wao amemlazimisha kwa nguvu
mwenzake kufanya tendo la ndoa ndani ya mchana wa
Ramadhan na wamo katika funga basi yule aliemlazimisha
mwenzake ndio itamuwajibikia kutoa kafara.
Na mwanamke hatakiwi akubali kufanya tendo la ndoa
wakati amefunga ndani ya Ramadhani. Na maulamaa
wengine wakaengeza kwa kusema hata ikiwa anaweza
kupigana na mume wake basi ampige, Kuonesha uzito wa
funga.
Na wala mtu asitumie kivuli kuwa amelazimishwa kujitetea
ajue kuwa Allah (subhanahu wata‘ala) anajua kila kilichomo
ndani ya nafsi ya mja wake.
Ikiwa mtu atafanya tendo la ndoa hali ya kuwa amefunga
ndani ya Ramadhani kwa siku mbili tofauti basi ni juu yake
kafara mbili. Kila funga moja basi na kafara yake moja.
Pia ikiwa mtu anafanya tendo la ndoa na baadae
ikambainikia kuingia kwa alfajiri basi kinachotakiwa ni
kuacha tendo la ndoa hapo hapo akakoge janaba na aendelee
na funga yake.
Je ni wakati gani jimai ya mchana wa Ramadhani
inaruhusika?
Ikiwa mke na mume wote wana dharura za kisheria za
kutofunga kwa mfano wote wamesafiri basi hakuna ubaya
na hawatotoa kafara. Kwani ruhusa ya kutofunga
ishakuwepo kwao wao.
Ikiwa mume amerudi safari na mke wake hakufunga siku
hiyo kwa sababu ya hedhi na ametwaharika baada ya funga
kuanza, basi tendo la ndoa kwao wao linaruhusika kwani
mume hajafunga na mke hakufunga.
Ama kinyume na hali hizo wakifanya tendo la ndoa ndani ya
mchana wa Ramadhani wakiridhia wenyewe basi kwa kila
mmoja juu yake kafara ama mmoja amemlazimisha
mwenzake basi yule aliyemlazimisha mwenzake ni juu yake
kutoa kafara.
Kujitoa maniii kwa makusudi kunabatilisha funga. Hivyo
basi yeyote ambae amefunga anatakiwa ajizuie na kujitoa
manii kwa makusudi. Na mfano wa kujitoa manii kwa
makusudi ni puunyeto, au kwa kumkumbatia au kumchezea
mkewe au mwanamke mpaka akatokwa na manii.
1-SUALI
Walifanya jimai kabla ya kuanza kwa funga na baadae
hawakuwahi kukoga janaba wakalala mpaka ikaingia alfajiri.
Je nini hukmu ya funga yao?
JIBU
Ikiwa walitia nia ya kufunga basi funga yao itasihi.
Kinachowalazimu ni kukoga janaba ili waweze kuswali na
waendelee na funga yao.
Na hili ni kwa ushahidi wa hadithi ya Bibi Aysha na Ummu
Salamah (radhiya Allahu anhuma) “kwamba Mtume (Swalla
Allahu alayhi wasallam) alikuwa akiamka na janaba
kutokana na kukutana kimwili na wake zake, kisha anakoga
na kufunga.”
(Al Bukhariy na Muslim).
2-SUALI
Alifanya jimai bila ya kujua kwamba alfajiri imeingia. Na
baadae akajua kuwa alifanya jimai wakati tayari alfajiri
ishaingia. Nini hukmu yake?
Ikiwa wakati anafanya hajui kama wakati umeingia basi
atakoga na ataendelea na funga yake. Kwani hakuna kosa
kwa mtu kutojua.Ama akifanya kwa kusudi basi funga
itabatilika funga yake na itamlazimu kutoa kafara na kuilipa
funga hiyo.
4-KUEPUKANA NA HEDHI NA NIFASI
Ni lazima kwa mwanamke anaetaka kufunga awe
ametwaharika kutokana na hedhi na nifasi. Na pindi
mwanamke anapokuwa na hedhi au nifasi basi huwa ni
wajibu kwake kuacha kufunga. Na hii ni amri kutoka kwa
Allah (subhanahu wata‘ala) na mwanamke akitwaharika
ataendelea na kufunga.
Pia siku ambazo ameziacha kwa kutofunga atakuja kuzilipa
baada ya Ramadhani.
SUALI
Bado muda mdogo sana kumalizika kwa funga. Mwanamke
akapatwa na hedhi. Je itahesabika funga yake ile?
JIBU
Hapana, haitohesabika funga ile kwa sababu wakati
haujatimia. Na itamlazimu mwanamke huyo aje kuilipa
funga hiyo baada ya kumalizika kwa Ramadhani.
SUALI
Mwanamke amepatwa na maumivu au dalili nyengine za
kuonyesha atapatwa na hedhi ila hakupata wala hakutokwa
na damu. Nini hukmu yake?
JIBU
Hatowajibika kuilipa na funga yake itakuwa sahihi.
SUALI
Ikiwa mwanamke siku zake za hedhi zimekaribia. Akaona
matone ya damu ila damu haikutoka. Nini hukmu ya funga
yake?
JIBU
Lazima ailipe funga hiyo kwani matone hayo ya damu
yatahesabika kama ni damu ya hedhi.
SUALI
Miaka yote Ramadhan napata kufunga siku 10 tu au 11. Na
zinazobaki nakuwa katika siku za hedhi. Sipati kufanya
ibada ambazo zina fadhila kubwa kuliko miezi mingine.
Nakuwa mnyonge kutokana na hali hiyo.
Je naweza kutumia vidonge vya kuzuia hedhi ?
JIBU
Kuhusu hedhi muda wake wajuu kabisa ni siku kumi na
tano, zikizidi hapo huwa ni ugonjwa, kwa maelezo yako
unakuwa ukitokwa na damu kwa takriban siku 20, hii
inaonesha una tatizo jitahidi kutafuta tiba ya ugonjwa huo.
Ama ikiwa zitabaki siku 15 au chini ya hapo tutaizingatia
kuwa ni hedhi, na kipindi unachokua ndani ya hedhi kuacha
yale sheria iliokutaka kuyaacha ni ibada, hivyo ibada
iliyokuzuilia kufanya ibada nyengine fadhila zake ni kubwa
zaidi kwa wakati huo.
Pili.
Kuhusu kutumia vidonge vya hedhi wako maulamaa
wanasema kuwa haifai kutumia vidonge hivyo kwani
vimethibitika vina madhara.
Ama tukisema havina madhara basi ushauri wetu ni bora
kuiacha hedhi katika utaratibu wake ndio bora zaidi kiibada
na kiafya pia. Kwani ndio maumbile yake mwanamke
alivyoumbwa na Allah (subhanahu wata‘ala). Na Allah ndie
mjuzi zaidi.
SUALI
Ikiwa mwanamke amemaliza nifasi kwa siku chache mfano
siku saba je anaweza kufunga?
JIBU
Ikiwa kweli imesita damu ya nifasi mwanamke huyo
anaweza kufunga. Na Allah ni mjuzi zaidi.
SUALI
Ni ipi hukmu ya funga kwa mwanamke aliyeharibu mimba?
JIBU
Ikiwa mimba imeharibika kabla ya mtoto kuumbika basi
damu hiyo si damu ya nifasi na mwanamke atakoga
kujisafisha na kuendelea na funga yake.
Ikiwa mimba imeharibika baada ya mtoto kuumbika basi
damu hiyo itakuwa ni ya nifasi na itambidi ajizuie kufunga
mpaka pale itakaposita damu ya nifasi. Na Allah ni mjuzi
zaidi.
SUALI
Mwanamke ametoharika kabla ya kuanza kwa alfajiri ya
kweli. Akatia nia ya kufunga ila akachelewa kukoga josho.
Je anaweza kufunga?
JIBU
Ndio anaweza kufunga. Kitakachomlazimu ni kukoga josho
kabla ya kutoka kwa swala ya alfajiri ili asiache swala na
ataendelea na funga yake. Na Allah ni mjuzi zaidi.
Hayo ndio masharti ambayo yanalazimika kutimizwa ili
funga ya Muislamu isihi. Na kinyume cha masharti hayo ni
kubatilika kwa funga hiyo. Na kama tulivyoeleza
itamuwajibikia mtu huyo kulipa. Ama yule ambae kwa
sababu ya kufanya tendo la ndoa yeye itamuwajibikia kulipa
pamoja na kafara. Na Allah ni mjuzi zaidi.