NYAKATI TATU MUHIMU ZA IBADA
ZISIKUPITE KATIKA RAMADHANI
Imeandaliwa na Alhidaya.com
Imepitiwa na Abubakari shabani
Rukonkwa
Nyakati tatu hizi ni muhimu sana za kufanya
ibada kutokana na fadhila zake kuu. Mwenye
kupenda kuchuma thawabu nyingi asizikose
khaswa katika mwezi huu Mtukufu Wa
Ramadhaan ambao ni mwezi wenye malipo
maradufu
1-Wakati wa mwanzo: Baina ya Alfajiri na
jua kuchomoza:
Usimulizi uliothibiti kutoka katika Swahiyh
Muslim (564/1) kwamba Mtume (Swalla Allaahu
'alayhi wa sallam) na Maswahaba walikuwa
2
wakibakia macho wakati huo hadi jua
kuchomoza kwani ni wakati mja anapogaiwa
rizki yake, na ni wakati wenye kheri nyingi,
unampa siha nzuri ya mwili binaadamu, na kwa
ujumla ni wakati wenye baraka nyingi za kila
aina kwani Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa
sallam) aliomba:
((Ee Allaah, wabarikie Ummah wangu nyakati za
asubuhi mapema)) [At-Tirmidhiy, Ahmad, Abu
Daawuud, Ibn Maajah na imethibitishwa kuwa ni
Hadiyth Swahiyh na Shaykh Al-Albaaniy]
Usimulizi huu umetoka kwa Maswahaba kadhaa
ambao wameelezea kwamba: "Mtume (Swalla
Allaahu 'alayhi wa sallam) alipotaka kupeleka
kikosi au jeshi aliwapeleka mwanzo wa asubuhi".
3
Vile vile wamesimulia kwamba:"Swakhar
alikuwa mtu tajiri ambaye alikuwa akipelekea
biashara zake mwanzo wa asubuhi na matokeo
yake ilikuwa ni kufuzu katika biashara na kupata
faida kubwa sana".
Wamesimulia Salafus-Swaalih kwamba Ibn
'Abbaas naye alimkataza mtu kulala nyakati hizo
alipomwambia:
"Inuka! Je, unalala katika saa ambayo rizki
inagaiwa?"
Ikiwa wakati huo ni kama hivyo ilivyoelezwa
juu, basi vipi Muislamu aache wakati huu umpite
hasa katika mwezi huu mtukufu wa Ramdhaan?
Ibnul-Qayyim (Rahimahu-Allaah) katika kitabu
chake 'Zaad Al-Ma'aad' amesema: "Usingizi wa
4
asubuhi unanyima rizki kwani huo ni wakati
ambao Muumba anaombwa rizki na wakati wa
kugaiwa rizki. Hivyo usingizi unanyima rizki
isipokuwa kwa dharura. Usingizi wakati huo pia
ni madhara kwa mwili…"
Faida nyingine kubwa ya kubakia
macho ukimdhukuru Allaah wakati huu:
Kwa muda wa saaa moja na nusu takriban
utakuwa umepata thawabu za Hajj na ‘Umrah
zikiwa kamilifu:
Imetoka kwa Anas kwamba Mtume (Swalla
Allaahu 'alayhi wa sallam) amesema:
((Atakayeswali Alfajiri katika Jamaa'ah kisha
5
akakaa anamdhukuru Allaah mpaka likachomoza
jua kisha akaswali Raka'ah mbili, atapata ujira
kama ujira wa kwenda Hajj na 'Umrah ulio
kamili kamili kamili)) [Imetolewa na At-
Tirmidhiy na kaisahihisha Al-Albaaniy]
Pindi ukifanya hivyo kwa mwezi mzima utakuwa
umechuma thawabu za Hajj na ‘Umrah za muda
wa mwezi mzima. Hizo ni fadhila za siku za
kawaida, seuze ukifanya mwezi mtukufu huu wa
Ramadhaan? Jitahidi ndugu Muislamu kadiri
uwezavyo kuchuma hizi thawabu kubwa ambazo
zingelikukalifu mali, tabu za safari na mashaka
ya kufika Makkah kutekeleza ibada hizo. Lakini
kwa Rehma ya Allaah Amejaalia thawabu hizo
ziweze kuchumwa tukiwa majumbani mwetu
tena kwa wepesi kabisa. Wanaume inawapasa
waswali msikitini kuzipata thawabu hizo kwa
kuwa Hadiyth imetaja atakayeswali jamaa’ah.
Ama wanawake, wanazipata fadhila hizo hata
wakiswali majumbani mwao. Hata hivyo, juu ya
kuweko fadhila kama hiyo, tusisahau kuwa
haivunji wala haifuti fardh ya kwenda Hajj kwa
6
mwenye uwezo, asije mtu akadhani kufanya hayo
kutakuwa kumetengua wajibu wake wa kuhiji au
kufanya ‘Umrah.
2- Wakati wa pili: Kabla ya Jua kuzama
(Magharibi):
Huu ni wakati ambao bado Muislamu yuko
katika Swawm na du'aa yake anayoiomba
hairudi:
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam)
amesema: (([Watu] watatu du'aa zao hazirudi;
mwenye kufunga Swawm hadi afuturu. Kiongozi
muadilifu na aliyedhulumiwa)) [At-Tirmidhiy
kwa isnaad nzuri]
7
Ni fursa kwa Muislamu atumie wakati huo
kuomba du'aa wakati huu hasa kwa vile ni wakati
ambao Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)
Amehimiza Atukuzwe kama Anavyosema:
... na msabbih kwa kumsifu Mola wako kabla ya
kuchomoza jua na kabla ya kuchwa [Qaaf: 39]
…Na msabbih Mola wako kwa kumsifu kabla ya
kuchomoza jua, na kabla halijachwa, na nyakati
za usiku pia umsabbih na ncha za mchana ili
upate ya kukuridhisha [Twaahaa: 130].
Na omba maghfirah kwa dhambi zako, na
umsabbih Mola wako kwa kumsifu jioni na
asubuhi)) [Ghaafir: 55]
3- Wakati wa tatu: Suhuur - Kabla ya Alfajiri
Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amewaaahidi
wenye taqwa Pepo kwa sababu miongoni mwa
sifa zao ni kuomba maghfira kabla ya Alfajiri:
Hakika wenye taqwa watakuwa katika Jannaat na
chemchem. Wanapokea Aliyowapa Mola wao.
Kwa hakika hao walikuwa kabla ya haya
9
wakifanya mema. Walikuwa wakilala kidogo tu
usiku. Na kabla ya Alfajiri wakiomba
maghfira. [Adh-Dhaariyaat: 15-18]
Kisha wamesifiwa tena kwa sifa kama hiyo
pamoja na nyinginezo:
Wanaosubiri, wanaosema kweli, na watiifu, na
wanaotoa sadaka, na wanaoomba maghafira
kabla ya Alfajiri.[Al-'Imraan: 17]
Muislamu asiache wakati huo umpite kwani ni
wakati muhimu na wenye fadhila na faida kubwa
kwa vile Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)
Huteremka wakati huo kutoka mbingu ya saba na
kuweko mbingu ya ardhi kututakabalia maombi
ya anayemuomba:
10
Imetoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu
'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi
wa sallam) amesema: (Allaah (Subhaanahu wa
Ta'ala) Huteremka (kwa namna inavyolingana na
utukufu Wake) kila siku katika mbingu ya dunia
(mbingu ya kwanza) inapobakia thuluthi ya
mwisho ya usiku na Husema: Nani ananiomba
Nimtakabalie? Nani ana shida Nimtekelezee?
Nani ananiomba maghfirah Nimghufurie?)) [Al-
Bukhaariy na Muslim]
Nani miongoni mwetu asiyemhitaji Mola wake
kumtakabalia haja zake au kumuondeshea shida
zake? Nani asiyekuwa na madhambi asiyemhitaji
Mola wake kumghufuria? Hivyo usiache wakati
huu ukakupita hasa kwa vile ni mwezi wa
Ramadhaan ambao kila jambo ulifanyalo lina
fadhila na thawabu marudufu.
11
Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)
Atuwezeshe kudiriki nyakati hizo tatu na
nyingine, tuwe katika ibada katika mwezi huu wa
Ramadhaan na miezi yote mingineyo na
Atujaalie kheri na Baraka nyingi, Atutakabalie
haja zetu, Atuondoshee shida zetu na Atughufurie
madhambi yetu yote. Aamiyn.