LAYLATUL-QADRI UTAIPATA VIPI ?.
Swahili.
Imeandikwa na:
Alhidaaya.com
Imepitiwa na :
Yunus Kanuni Ngenda
بسم الله الرحمن الرحيم
Utangulizi
Tunakaribia kuingia kumi la mwisho, kumi ambalo ndani yake
kuna usiku unaojulikana kama ni: Laylatul-Qadr. Ibaada
yoyote itakayotendwa usiku huo, ni bora kuliko ibaada ya
miezi elfu.
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
Hakika Sisi Tumeiteremsha (Qur-aan) katika Laylatil-Qadr
(usiku wa cheo). Na nini kitakachokujulisha ni nini huo (usiku
wa) Laylatul-Qadr? (Usiku wa) Laylatul-Qadr ni (usiku) mbora
kuliko miezi elfu. Wanateremka humo Malaika na Ruwh
(Jibriyl) kwa idhini ya Mola wao kwa kila amri (jambo). (Usiku
huo ni) Amani mpaka kuchomoza Alfajiri (Al-Qadr: 1-5)
Hadiyth mbali mbali zimethibiti kuhusu fadhila za usiku huu
mtukufu na pia hali ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa
aalihi wa sallam) ilivyokuwa masiku kumi ya mwisho ya
Ramadhaan.
Hesabu ya thawabu za usiku huo ni kama ifuatavyo:
Miezi elfu ni sawa na miaka themanini na tatu na miezi
mitatu takriban. (1000 ÷ 12 = 83.3)
Utakapokuwa umo katika ibaada usiku huo wa Laylatul-Qadr,
basi utaandikiwa thawabu za miaka 83! Juu ya hivyo, ibaada
ya usiku huo ni bora zaidi kuliko ibaada ya miaka themanini
na tatu.
Mazingatio kuhusu Laylatul-Qadr:
Mwenye kukosa Laylatul-Qadr atakula hasara kwa dalili ya
Hadiyth ifuatayo:
Kutoka kwa Abu Huraryah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba
ilipofika Ramadhaan, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa
sallam) amesema: ((Umekujieni mwezi wa Ramadhaan, ni
mwezi wa Baraka. Imefanywa Swawm kwenu kuwa ni fardhi,
milango ya Pepo hufunguliwa na milango ya Moto hufungwa
na mashaytwaan hufungwa. Katika mwezi huu, kuna usiku
ulio bora kuliko miezi elfu. Atakayenyimwa kheri zake, basi
hakika amenyimwa!)) [An-Nasaaiy]
Siku hiyo ni siku iliyoteremeshwa Qur-aan. Anasema Allaah
(Subhaanahu Wa Ta'aalaa):
BismiLLaahir-Rahmaanir-Rahiym (Kwa Jina la Allaah Mwingi
wa Rehma, Mwenye kurehemu). Haa Miym. Na Kitabu
kinachobainisha. Hakika Sisi Tumeiteremsha (Qur-aan) katika
usiku uliobarikiwa, (Laylatul-Qadr), hakika Sisi Tumekuwa
Waonyaji. (Usiku) Huo hupambanuliwa kila jambo la hikmah.
(Ad-Dukhaan: 1-4).
Maana ya: “(Usiku) Huo hupambanuliwa kila jambo la
hikma” ina maana: Usiku huo wa Laylatul-Qadr, majaaliwa
yanahamishwa kutoka katika Al-Lawh Al-Mahfuwdhw (Ubao
Uliohifadhiwa) kwenda kwa waandishi (Malaika)
wanaoandika majaaliwa ya mwaka unaokuja; kuhusu uhai,
rizki na yote yatakayomtokea binaadamu mpaka mwisho wa
mwaka [Imesimuliwa na Ibn 'Umar, Mujaahid, Abu Maalik,
Adh-Dhwahaak na wengineo katika Salaf – Ibn Kathiyr: 8:671]
Kufanya juhudi kubwa katika ibaada masiku haya:
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) alikuwa inapoingia
kumi la mwisho akijikaza kwa kufanya ibaada kuliko siku
zozote zingine:
Imepokewa kwa 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anhaa) kwamba:
"Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akijitahidi
katika kumi la mwisho kuliko alivyojitahidi katika siku nyingine zozote" [Muslim]
Na katika Al-Bukhaariy na Muslim:
Imepokewa kwa 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anhaa): "Ilipokuwa inaingia kumi (la mwisho) Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikaza izaar (shuka) yake, akikesha usiku, na akiamsha ahli zake" (Na katika riwaaya nyingine) "Akikesha usiku, akiamsha ahli zake, akijitahidi na akikaza izaar yake" [Al-Bukhaariy na Muslim]
Kwa Nini Umeitwa Laylatul-Qadr?
Shaykh Ibn 'Uthaymiyn (Rahimahu-Llaah) Amesema:
Kwanza: Kutokana na uwezo; nao ni utukufu kama vile kusema “fulani mwenye uwezo mkubwa" yaani mwenye hadhi au utukufu.
Pili: Ni usiku ambao una majaaliwa ya mwaka mzima na huandikwa yote yatakayotokea mwaka huo, na hii ni Hikma ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kuonyesha usanifu wa utengenezaji Wake na Uumbaji Wake.
Tatu: Usiku huo una uwezo mkubwa kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam):
((Atakayesimama usiku wa Laylatul-Qadr kwa iymaan na kutaraji malipo, ataghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia))[Al-Bukhaariy na Muslim]
Sababu Ya Kupewa Waislamu Laylatul-Qadr:
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliona umri wa Ummah za mwanzo ni mrefu, na umri wa Ummah wake ni mfupi akapewa usiku wa Laylatul-Qadr uwe ni bora kuliko miezi elfu. [Muwatw-twaa 1/321 (Muhammad Fuad 'Abdul-Baaqy]
Ibaada Za Kufanya Masiku Kumi Ya Mwisho:
1-Qiyaamul-Layl: (Kisimamo cha usiku kuswali):
((Atakayesimama (Kuswali) Ramadhaan kwa iymaan na kutaraji malipo, ataghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
2-Kuosma Qur-aan:
Hasa kwa vile usiku wa Laylatul-Qadr ndio usiku ulioteremeshwa Qur-aan kama tulivyoona katika Aayah hizo za juu katika Suratul-Qadr na Suratud-Dukhaan. Pia Muislamu inampasa aisome Qur-aan Ramadhaan nzima kwa sababu ndio mwezi ulioteremshwa Qur-aan kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
Mwezi wa Ramadhaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan ili iwe Hidaaya kwa watu na hoja bayana za Hidaaya na Al-Furqaan (Upambanuzi). [Al-Baqarah: 185]
Jibriyl ('Alayhis-Salaam) alikuwa akimteremkia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) kila usiku wa Ramadhaan akimsomesha na kumsikiliza Qur-aan:
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) alikuwa ni mbora (mwenye matendo mema) wa watu, na alikuwa mbora zaidi katika Ramadhaan kwa sababu Jibriyl alikuwa akimjia kila usiku wa Ramadhaan akimfundisha Qur-aan)) [Al-Bukhaariy]
3- I'tikaaf Msikitini:
Kutia niyyah kubakia Msikitini kwa kufanya ibaada humo kwani Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) alikuwa akifanya hivyo:
Imepokewa kwa ‘Aaishah (Radhiya Allaahu 'anhaa) kwamba: Mtume (swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) alikuwa akifanya I'tikaaf kila Ramadhaan siku kumi, ulipofika mwaka wake wa kuaga dunia alifanya I'tikaaf siku ishirini" [Al-Bukhaariy]
4-Kuomba Maghfirah:
Kwa sababu ni hatari mtu atokea Ramadhaan bila ya Allaah kumghufuria madhambi!
Imepokewa kwa Anas na wengineo kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) alipopanda juu ya minbar aliitikia ((Aamiyn, Aamiyn, Aamiyn)). Alipoulizwa kwa nini ameitikia hivyo akasema: ((Amenijia Jibriyl akasema: “Ee Muhammad, ole wake yule ambaye unapotajwa hakuswalii, hivyo sema Aamiyn”. Nikasema Aamiyn. Kisha akasema: “Ole wake yule ambaye umeingia mwezi wa Ramadhaan kisha akatoka bila ya kughufuriwa, kwa hiyo sema Aamiyn”. Nikasema Aamiyn. Kisha akasema: “Ole wake yule ambaye amewakuta wazazi wake au mmoja wa wazazi wake lakini wasimuingize Peponi. Hivyo sema Aamiyn”. Nikasema Aamiyn)) [Swahiyh At-Tirmidhiy na kasema Shaykh Al-Albaaniy kuwa Hadiyth hiyo ina daraja ya Hasan Swahiyh]
5-Du'aa Ya Kuomba Katika Siku Kumi Hizi za Mwisho:
Imepokewa kwa 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anhaa) kwamba alisema "Ee Mtume wa Allaah je, nitakapojaaliwa kufika usiku wa Laylatul-Qadr niombe nini?" Akasema, ((Sema: Allaahumma Innaka 'Afuwwun Tuhibbul-'Afwa fa'afu 'anniy - Ee Allaah Hakika Wewe Ndiye Mwenye Kusamehe Unapenda Kusamehe basi Nisamehe)) [Ibn Maajah na kaisahihisha Al-Albaaniy]
6-Kumkdhukuru Allaah Kwa wingi:
Kwa Tasbiyh (Kumsabbih kwa kusema; Subhaanah Allaah) kwa Tahmiyd (kumsifu kwa kusema; AlhamduliLLaah), Tahliyl (kumpwekesha kwa kusema; Laa ilaaha illa-Allaah), Takbiyr (Kumtukuza kwa kusema: Allaahu Akbar).
7- Kuomba Du'aa:
Ramadhaan ni mwezi wa kuomba kwa sababu Aayah za kuomba du’aa zipo kati ya Aayah za kuhusu Swawm:
Na watakapokuuliza waja Wangu kuhusu Mimi, basi Mimi ni Qariyb (Yu karibu daima kwa elimu Yake); Naitikia maombi ya muombaji anaponiomba. Basi waniitikie Mimi na waniamini Mimi, wapate kuongoka. [al-Baqarah: 186]
Usiku Gani Unapatikana Laylatul-Qadr?
Hadiyth kadhaa zimetaja kuhusu usiku wa Laylatul-Qadr. Imetajwa kuwa ni katika masiku kumi ya mwisho; siku ya
ishirini na moja, au ishirini na tatu, au ishirini na tano au ishirini na saba kwa dalili zifuatazo:
Hadiyth ya 'Aiashah (Radhiya Allaahu 'anhaa) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) amesema: ((Utafuteni usiku wa Laylatul-Qadr katika siku za witiri kwenye siku kumi za mwisho)) [Al-Bukhaariy]
Hadiyth ya Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu 'anhumaa) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) amesema: ((Utafuteni usiku wa Laylatul-Qadr katika siku kumi za mwisho za Ramadhaan; katika (usiku wa) tisa, saba, na wa tano utakaobakia [mwisho wa Ramadhaan])) [al-Bukhaariy]
Imaam Ahmad amepokea kutoka kwa 'Ubaydah bin As-Swaamit kwamba alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) kuhusu usiku wa Laylatul-Qadr akasema:
((Katika Ramadhaan, utafuteni siku kumi za mwisho, hakika umo katika siku za witiri; siku ya ishirini na moja, au ishirini na tatu, au ishirini na tano, au ishirini na saba, au ishirini na tisa, au usiku wa mwisho)) [Ahmad]
Alama Zinazobainisha Laylatul-Qadr:
1. Usiku huo unakuwa na mwanga zaidi.
2. Upepo siku hiyo hutulia, yaani siku hiyo hautokei upepo mkali.
3. Hali ya hewa huwa nzuri.
4. Nyoyo za Waumini usiku huo huwa zina utulivu kuliko siku nyingine.
5. Baadhi ya watu wema huoteshwa usiku huo kama walivyokuwa wakioteshwa Maswahaba na Salafus-Swaalih (wema waliotangulia)
Asubuhi Yake:
Hadiyth ya ‘Ubay bin Ka'ab (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba: "Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) ametuambia kuwa, jua siku hiyo hutoka likiwa halina mishale (mikali)" [Muslim]
Pia,
((Laylatul-Qadr ni usiku ulio katika hali ya ukunjufu, usio na baridi wala joto, asubuhi yake jua huwa jekundu na dhaifu))[Swahiyh Ibn Khuzaymah]
((Laylatul-Qadr usiku wa kung'aa [yaani wenye mwanga] sio joto wala baridi, na vimondo (nyota za kufyatuliwa) havitotumwa)) [At-Twabaraaniy na Ahmad]
Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atuwezeshe kukesha masiku kumi ya Ramadhaan ili tujaaliwe kuupata usiku huu mtukufu, tutoke katika Ramadhaan tukiwa tumeghufuriwa madhambi yetu yote. Aamiyn