Nakala

Katika kusimulia kisa cha Yesu, Qur'ani inaeleza jinsi Maryamu, mama wa Yesu, alikujiwa na malaika kutoka kwa Mungu, akimletea habari ambazo hajawahi kamwe kuzifikiria: kwamba angemzaa mtoto wa kiume, Masihi, ambaye atakuwa mcha Mungu na atakuwa nabii wa Mungu, akiwaita Wana wa Israeli (Waisraili) kwenye Njia Iliyo Nyooka ya Mungu.





“Na pale Malaika walipo sema: Ewe Maryamu! Hakika Mwenyezi Mungu anakubashiria (mwana) kwa neno litokalo kwake. Jina lake ni Masihi Isa mwana wa Maryamu, mwenye hishima katika dunia na Akhera, na miongoni mwa walio karibishwa (kwa Mwenyezi Mungu). Naye atazungumza na watu katika utoto wake na katika utuuzima wake, na atakuwa katika watu wema.” (Kurani 3:45-46)





Kwa kawaida, habari hii kwa Maryamu, ilikuwa ya ajabu na ilionekana kuwa isiyowezekana.





“Maryamu akasema: Mola wangu Mlezi! Vipi nitampata mwana na hali hajanigusa mwanaadamu? Mwenyezi Mungu akasema: Ndivyo vivyo hivyo, Mwenyezi Mungu huumba apendacho. Anapo hukumu jambo, huliambia: Kuwa! Likawa. Na atamfunza kuandika na Hikima na Taurati na Injili.” (Kurani 3:47-48)





Asili ya Yesu yenyewe ni ya kipekee, hadi kwamba Mungu analinganisha upekee wa uumbaji wake na ule wa mwanadamu na nabii wa kwanza, Adamu.





“Hakika mfano wa Isa kwa Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa Adam; alimuumba kwa udongo kisha akamwambia: Kuwa! Basi akawa.” (Kurani 3:59)





Yesu na Miujiza Yake





Yesu akawa mmoja wa manabii wakuu wa Mungu, na akatumwa kwa Wana wa Israeli ili kuthibitisha mafundisho ya mtangulizi wake, Mtume Musa. Kuzaliwa kwake kulikuwa muujiza, na, kama manabii wote wa Mungu, alipewa miujiza kadhaa. Akawaendea watu wake, akiwaambia:





“Na ni Mtume kwa Wana wa Israili kuwaambia: Mimi nimekujieni na Ishara kutoka kwa Mola Mlezi wenu, ya kwamba nakuundieni kwa udongo kama sura ya ndege. Kisha nampuliza anakuwa ndege kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na ninawaponesha vipofu wa tangu kuzaliwa na wakoma, na ninawafufua maiti kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na ninakwambieni mnacho kila na mnacho weka akiba katika nyumba zenu. Hakika katika haya ipo Ishara kwenu ikiwa nyinyi ni wenye kuamini. Na ninasadikisha yaliyo kuwa kabla yangu katika Taurati, na ili nikuhalalishieni baadhi ya yale mlio harimishiwa, na nimekujieni na Ishara kutokana na Mola Mlezi wenu. Kwa hivyo mcheni Mwenyezi Mungu na nit'iini mimi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mola wangu Mlezi na ni Mola wenu Mlezi. Basi muabudni Yeye. Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka.” (Kurani 3:49-51)





Wafuasi wa Yesu





Qurani inaendelea na hadithi ya Yesu kwa kusimulia matukio kadhaa ya maisha yake na ya wanafunzi wake.





“Isa alipo hisi kuwa kati yao pana ukafiri alisema: Nani wasaidizi wangu kwa Mwenyezi Mungu? Wanafunzi wake wakasema: Sisi ni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu. Tumemuamini Mwenyezi Mungu, na shuhudia kwamba sisi hakika ni Waislamu. Mola wetu Mlezi! Tumeyaamini uliyo yateremsha, na tumemfuata huyu Mtume, basi tuandike pamoja na wanao shuhudia.” (Kurani 3:52-53)





Katika tukio lingine, ambalo (sura) nzima ya Qurani imepewa jina kutokana nalo, wanafunzi wa Yesu walimwomba muujiza mwingine.





“Wanafunzi walipo sema: Ewe Isa bin Maryamu! Je, Mola wako Mlezi anaweza kututeremshia chakula kutoka mbinguni? Akasema: Mcheni Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi ni Waumini. Wakasema: Tunataka kukila chakula hicho, na nyoyo zetu zitue, na tujue kwamba umetuambia kweli, na tuwe miongoni mwa wanao shuhudia. Akasema Isa bin Maryamu: Ewe Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wetu! Tuteremshie chakula kutoka mbinguni ili kiwe Sikukuu kwa ajili ya wa mwanzo wetu na wa mwisho wetu, na kiwe ni Ishara itokayo kwako. Basi turuzuku, kwani Wewe ndiye mbora wa wanao ruzuku.’” (Kurani 5:112-114)





Na Mwenyezi Mungu aliwatumia chakula walichokuwa wakikitaka, lakini sio kabla ya kuwaonya.





“Mwenyezi Mungu akasema: Hakika Mimi nitakuteremshieni hicho. Lakini yeyote katika nyinyi atakaye kanya baadae, basi hakika Mimi nitampa adhabu nisiyopata kumpa yeyote katika walimwengu.’” (Kurani 5:115)





Mwisho wa Kisa?





Hadithi ya Yesu haina mwisho katika Qurani, kwani tunaambiwa kwamba Yesu hakuuawa, bali, Mungu alimuinua nabii Wake mpendwa Kwake.





“Pale Mwenyezi Mungu aliposema: Ewe Isa! Mimi nitakufisha, na nitakunyanyua kwangu, na nitakutakasa na wale walio kufuru, na nitawaweka wale walio kufuata juu ya wale walio kufuru, mpaka Siku ya Kiyama. Kisha marejeo yenu yatakuwa kwangu, nikuhukumuni katika yale mliyo kuwa mkikhitalifiana. Ama wale walio kufuru, nitawaadhibu adhabu kali katika dunia na Akhera, wala hawatapata wa kuwanusuru. Na ama wale walio amini na wakatenda mema basi Mwenyezi Mungu atawalipa ujira wao kaamili. Na Mwenyezi Mungu hawapendi madhaalimu.” (Kurani 3:55-57)





Qurani pia inaonyesha kwamba Yesu hakuuawa wala kusulubiwa. Akizungumzia Wana wa Israeli, Mungu anakosoa madai yao dhidi ya Maryamu pamoja na madai yao kwamba walimuua Yesu.





“Na pia kwa kufuru zao na kumsingizia kwao Maryamu uwongo mkubwa. Na kwa kusema kwao: Sisi tumemuuwa Masihi Isa, mwana wa Maryamu, Mtume wa Mwenyezi Mungu - nao hawakumuuwa wala hawakumsalibu, bali walifananishiwa tu. Na hakika walio khitalifiana katika haya wamo katika shaka nayo. Wao hawana ujuzi nayo wowote, ila ni kufuata dhana tu. Wala hawakumuuwa kwa yakini. Bali Mwenyezi Mungu alim- tukuza kwake, na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.” (Kurani 4:156-158)





Qur'ani inathibitisha kwamba Yesu aliinuliwa na Mwenyezi Mungu, na Mtume Muhammad, rehema na baraka za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, anatuhakikishia kwamba Yesu atateremshwa duniani mara nyingine kabla ya Siku ya Kiama. Katika kauli ya Mtume Muhammad, iliyosimuliwa na Abu Huraira, Mtume alisema:





“Naapa kwa Yule ambaye nafsi yangu imo Mkononi Mwake, ni hakika mwana wa Maryamu hivi karibuni atashuka kati yenu kama hakimu wa haki, na atavunja msalaba, kuua nguruwe, na kukomesha Jizyah (ushuru), na mali itakuwa nyingi sana hadi kwamba hakuna mtu atakayeikubali, hadi sajda moja itakuwa bora kuliko ulimwengu na kila kitu ndani yake.” (Saheeh Al-Bukhari)



Machapisho ya hivi karibuni

UJUMBE KUTOKA KWA MUH ...

UJUMBE KUTOKA KWA MUHUBIRI MUISLAMU KWA MKRISTO

FADHILA YA KUFUNGA SI ...

FADHILA YA KUFUNGA SIKU SITA ZA SHAWAL

Masuala kumi muhimu n ...

Masuala kumi muhimu na mafupi kuhusu mwezi wa Muharram

UJUMBE KWA ALIYEICHOM ...

UJUMBE KWA ALIYEICHOMA KURANI