Machi 11, 2011 ndio siku nilipojisalimisha kikamilifu kwa Mungu. Nilifanya shahaadah yangu baada ya miezi ya utambuzi. Hali zilizonipeleka kwa Uislamu hazikuwa rahisi. Lakini Alhamdulillah (Sifa zote an Shukrani ziwe kwa Mungu), kwa sasa, hatimye nimekuwa Muslimah (mwanamake Muislamu).
Ningependa kuwaeleza kuhusu safari yangu ya kufikia kwa Uislamu.
Nilikuwa mkatoliki tangu kuzaliwa kwangu. Mama yangu alikuwa mtawa kwa miaka kadhaa kabla ya kuacha konventi, na alitulea katika maisha ya maombi na sala kwa Mungu. Tangu nikiwa na miaka saba, alinifunza tabia ya kujisalimisha kwa Mungu na kukiona kila kitu kinachotendeka kama taratibu za Mungu za kunitayarisha kwa mazuri yanayokuja.
Kwa kuwa nilijijengea uhusiano wa kibinafsi na Mungu, nilikuwa nimejihusisha sana na kazi za kitume. Nilifundisha hata katekisimu na nilipewa tuzo ya Katekista wa Mwaka nilipohitimu Shule ya Upili. Baada ya hapo, maisha yangu yalikuwa safari ya kudumu ya imani.
Katika hatua muhimu sana katika maisha yangu, nilifanya kazi kwa shirika la kibinadamu lililokusudiwa kuelekeza miradi iliyotazamiwa kuunganisha Wafilipino kwa maombi bila kujali dini. Shirika lilikuwa na imani kwamba sisi sote ni ndugu na dada chini ya utunzaji wa Mungu. Hata kabla sijajihusisha na shirika hilo, maisha yangu ya sala yalikuwa yakieleka kwa Mungu Mmoja Mwenye Uwezo. Hata hivyo, bila shaka, baada ya kulelewa kikatoliki nyumbani na shuleni, nilikuwa na mnyenyekeo fulani kwa watakatifu fulani wa kanisa, nikiwatambua sio kama miungu wadogo, lakini kama marafiki katika sala kwa nia yangu. Kulikuwa na wakati ningejiuliza ni nani kati ya watakatifu ndiye mwenye uwezo zaidi katika kuleta baraka. Na hivyo, ningeishia kuomba tena moja kwa moja kwa Mungu - Mlezi Mmoja Mkuu, Mwenye Nguvu, nikijua Yeye ndiye chanzo kikuu cha baraka.
Wakati mama yangu alipopataa lukemia na katika nyakati za mwisho za ugonjwa wake, kilikuwa kipindi cha mapambano tupu. Wakati mmoja, niliamka nikimwomba Mungu aniweke mimi kwa nafasi yake ili nipate kuugua badala yake. Ilikuwa jitihada isiyo na mwisho ya kutafuta rasilimali kwa matumaini ya kupata matibabu ya kisasa ya kumponya mama yangu. Mpaka kasisi wetu wa parokia ambaye alikuwa rafiki wa karibu wa familia alisema - JISALIMISHE... JISALIMISHE KWA MUNGU. Kisha, nilikumbuka tena kujisalimisha, hasa wakati mwili wa mama yangu ulikuwa tayari umeshakataa matibabu ya kemotherapi.
Kifo cha mama yangu kilikuwa hatua muhimu katika maisha yangu. Tangu wakati huo, maisha yangu yamekuwa vita vya kudumu vya kujisalimisha kwa Mungu. Ubinafsi ungenifanya niegemee zaidi kwa mipango yangu - nikipambana kwa ajili ya kuyatimiza na kutafuta kwa ukaidi vile nilivyovitaka mimi licha ya ishara nyingi kutoka kwa Mungu. Katika nyakati hizi, ningepata amani tu nilipojisalimisha. Lakini kwa sababu ya ubinadamu wangu, siku zote ningerudi kuanguka katika mtego wa kutaka mambo yafanyike kwa njia yangu mwenyewe.
Baada ya kifo cha mama yangu, niliitwa kazi huko Qatar. Ilikuwa mwaka wa 2003. Pengine, sikuwa tayari wakati huo. Nilichukua kazi nyingine nchini Ufilipino kwani hakukuwa na haja ya kutafuta kazi nje ya nchi kwa sababu mama yangu alikuwa amekwisha kufa. Je, kuna haja gani ya kupata mapato niliyoyataka kupata wakati alipokuwa hai ili niweze kuendeleza matibabu yake na pia kumpeleka mahali tofauti tofauti? Hakuna.
Kisha mwaka wa 2006, wito wa mahojiano ya kikazi nisioutarajia ulikuja kutoka kwa mwajiri wa Ujerumani mwenye mradi mkubwa huko Qatar. Qatar mara nyingine tena iliniita na ilibidi niyahudhurie mahojiano kwa ushauri wa baba yangu aliyeniambia niyajaribu. Sikutarajia kupata kazi lakini ishara wakati wa taratibu za mahojiano zilinifanya niamini kazi hiyo ilikuwa iwe yangu. Nilienda Qatar baada ya mwezi mmoja. Nilidhani Qatar ilikuwa inipe fursa ya kupata mapato ya zaidi, ila cha kushangaza ni kuwa ilinipa zaidi ya hayo.
Katika malezi yangu ya Kikatoliki, iliingizwa katika vichwa vyetu kwamba kusudi la maisha ni KUMJUA, KUMPENDA na KUMTUMIKIA MUNGU. Hakika, ni hulka ya kiasili ya mwanadamu kuendelea kutafuta maana ya maisha. Utafutaji usio na mwisho wa chemchemi ya ujana umejikita mizizi katika hamu ya mwanadamu ya kuelewa maana na kusudi la kuwepo kwake. Mwanadamu hawezi kamwe kuacha utafiti wake isipokuwa pale atakapopata anachokitafuta. Kwa hivyo, hawezi kusimama kwa ajili ya kitu chochote na kununua angalau muda na afya ili aendelee na kampeni yake. Mamilioni ya wasomaji waliokifanya kitabu cha “Maisha Yanayoongozwa na Lengo” kiwe kati ya vitabu vilivyouzwa sana duniani, ni ushuhuda tosha wa jinsi watu wengi wanatafuta mwelekeo na lengo.
Nilipokuwa na umri wa miaka 8 au 9, nilimuuliza mama yangu - “Mungu alikuwa wapi kabla ya Uumbaji?” Nilimwambia ningetumia muda mrefu nikiwa nimefunga macho yangu na kulowa jasho kutokana na umakini wangu nikiwaza tu kuhusu zifuatazo kwa utaratibu — nafasi yangu na mahali nipo, mawingu, anga ya samawati, mwezi, sayari tisa, nje ya Kundi la nyota la Kilimia, kisha napata kuna nafasi kubwa ya anga ya nje. Licha ya upana na ukubwa wa nafasi hii, Mungu bado yuko juu yake... ”Wakati hapakuwa na kitu alikuwa wapi?” Niliendelea kuuliza. Na mama yangu alitabasamu na kunikumbatia — “Tayari unafikiria mambo hayo?” aliuliza. Kisha akasema, “Hivyo, mpendwa wangu, ndivyo Mungu wetu alivyo mkubwa na Asiye na mwisho. Yeye ni mkubwa kuliko ufahamu wetu, lakini niamini, Yupo mahali yupo.
Tamaa na hamu ya Mwanadamu- vijana na wazee, si kwa ajili ya mambo ya kimwili, wala anasa za kihisia na za kimwili... ni haya yote na zaidi. Sisi sote tangu kuzaliwa kwetu tunamtafuta Mungu. Tumeumbwa ili kumjua, kumpenda, kumtumikia na sasa, kwa kuwa mimi ni Muslimah, wacha niongeze moja zaidi — kumwabudu Mungu kwa Umoja Wake.
Katika safari yangu ya kumtafuta Mungu katika maisha yangu yote, namtukuza kwa kuniongoza kwenye Njia ya Uislamu.
Mwenyezi Mungu amenileta hapa Qatar kwa lengo hili, ili nimalize jitihada zangu na kutumia siku zilizobaki za maisha yangu kumwabudu Yeye kwa njia za Mtume Muhammad, rehema na baraka za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake.
Njia za Mwenyezi Mungu sio njia zetu, kwani Yeye ndiye anayejua zaidi. Hakika, kuhusiana na matukio yaliyotokea katika maisha yangu hapa Qatar, ninatazama nyuma na kuona jinsi alivyonitengenezea njia ambayo imeniongoza kwake.
Mwaka wa 2009, kampuni iliyonileta Qatar ilikuwa imekutana na matatizo na kuanza kuwafuta watu kazi na kuwapa hiari ya kutafuta kazi nyingine. Jinsi nilivyokuja kufanya kazi katika kampuni ambayo nipo kwa sasa pia ni mojawapo ya maajabu mazuri aliyoniwekea Mwenyezi Mungu. Jinsi nilivyobadilisha kazi kutoka kampuni yangu ya awali hadi hii yangu ya sasa ilikuwa njia nyepesi sana. Taasisi ambayo ninafanya kazi ni taasisi ya Kiislamu inayoongozwa na sharia (sheria ya Kiislamu) na idara ninayofanya kazi kwa sasa imenipa fursa ya kutua katika kazi yangu ya ndotoni - mawasiliano ya kikampuni. Kwa kuwa nimezama katika utayarishaji wa majarida na matangazo ya kibiashara, ilibidi nijue vizuri maadili ya ushirika yaliyo katika mwongozo wa Sharia, ambayo imenipelekea kusoma zaidi kuhusu Uislamu. Katika hatua hiyo, Nilijikuta nikifurahia kile nilichokuwa nikifanya na ningesoma chochote nilichoweza kupata.
Mnamo mwaka wa 2010, nilikutana na Muislamu wa Kifilipino. Hakukuwa na mazungumzo yoyote kuhusu dini yetu. Alijua jinsi nilivyokuwa na maombi na sala nyingi kwa sababu ya Rozari yangu na vijitabu vya Novena. Aliniambia kuwa katika familia yake, kuna Waislamu na Wakristo pia. Alinihakikishia kwamba sikuwa na haja ya kuwa na wasiwasi wowote kuhusu hilo kabisa. Nilipata kwake sifa ambazo nimekuwa nikizitafuta. Maoni yake kuhusu uhusiano ni sawa na yangu. Kwa hivyo, dini haikuwa suala na sisi sote tuliheshimu imani zetu.
Wakati mmoja, nilikwenda kwa Fanar (kituo cha utamaduni wa Kiislamu cha Qatar) na bosi wangu wakati wa maonyesho ya sanaa za kaligrafia ili kununua vitu kadhaa kwa ajili ya kampuni yetu. Nilipata nakala ya kitabu cha MUSLIMAH BORA na kuanza kuisoma miezi mitatu baada ya kukipata kitabu huku mchumba wangu hakuwepo Qatar wakati huo. Nilihisi aya za Qur'an zinazungumza nami moja kwa moja. Niliposoma sifa za Muslimah Bora (mwanamke wa Kiislamu), nilitambua kwamba njia yangu ya maisha ilikuwa kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu. Kisha, nilipata nakala ya Qur'an katika lugha ya Tagalog na ningehisi aina fulani ya amani kubwa moyoni mwangu ambayo ingenifanya nitokwe na machozi. Nilijiambia mwenyewe itabidi niifuatilie. Nilitafuta mwongozo kutoka idara ya Shari'a na kutoka kwa wenzangu wenye nia nzuri kuhusu vitabu vipi vya kusoma. Ningeingia mtandaoni na kusoma kila kitu nilichopata. Mpaka siku moja, nilipoamua kuacha. Niliacha kutafuta maarifa kwa sababu sikutaka kutekeleza kitu chochote nikiwa bado nina uhusiano na mchumba wangu ambaye alikuwa amefika kutoka Ufilipino wakati huo. Ingawa hakuzungumzia kuhusu suala la dini yangu, nilijiambia, ilibidi niangalie kwa makini kama nilikuwa ninaathiriwa na uwepo wake maishani mwangu au kama kukumbatia kwangu kwa Uislamu kunatokana na chaguo langu mwenyewe... kutoka kwa kina cha ndani kabisa cha moyo wangu na roho yangu.
Wakati huo nilipoacha kutafuta maarifa zaidi, nilikuwa napitia mgogoro pia. Matatizo yaliendelea kuongezeka na nilichanganyikiwa kuhusu jinsi ya kusali. Nifanye maombi ya Rozari au nifanye swalaah (maombi ya Waislamu) ambayo sikujua chochote kuhusu jinsi ya kuifanya? Kwa miezi kadhaa, nilikuwa na utata, mpaka usiku mmoja nilipoamka na nikamwomba Mungu na kusema - “Mungu wangu, nimechanganyikiwa. Sijui tena jinsi ya kuomba. Angalia moyo wangu. Ninajisilimu kwako!“ Baada ya hapo, nilihisi amani fulani.
Rehema za Mungu zikaanza. Mchumba wangu alikwenda nyumbani kwa Ufilipino mapema kabla ya wakati aliopanga kuenda. Mungu alinipa muda niliohitaji kwa utambuzi wangu.
Sikutarajia kwamba siku ambayo tsunami kubwa ingepiga Japani ingekuwa siku nitakayofanya Shahaadah yangu (ushuhuda wa imani unaotamkwa ili kuingia kwa Uislamu). Nilihisi tu moyo wangu ulikuwa kimya sana. Nilikwenda kwa Fanar nikiwa na nia ya kuhudhuria madarasa ya kimsingi ya Uislamu. Nilichukua hatua hii nilipokuwa na uwezo hatimaye wa kujibu maswali ya kimsingi niliyokuwa nayo. Kwanza, iwapo mchumba wangu na mimi tusingeweza kuishia pamoja, ningeweza kuendelea kuwa Muislamu? Nitakapokufa, familia yangu ingesitiri vipi mabaki yangu? Na kisha, niliona akilini mwangu wenzangu wa kiislamu wa kike na nilihisi utangamano fulani wa kijamii. Kisha nilijiambia , kuna uwezekano wa kupoteza mtu mmoja, lakini ningepata wengi zaidi. Pili, kwa nini wanaume wa Kiislamu wanaruhusiwa kuoa hadi wake wanne? Je! Hawajui ni uchungu kwa mwanamke ikiwa mwanamke mwingine anapendwa zaidi kuliko yeye? Swali hili lilibaki bila majibu kwa miezi kadhaa mpaka siku hiyo nilipokuwa nikijiandaa kwenda Fanar. Kwa kweli, swali hili daima lingenizuia kukubali masomo niliyoyapata kuhusu Uislamu na nilikuwa na matumaini ya kupata jibu mara nilipopewa fursa ya kuhudhuria masomo katika Fanar. Hatimaye, asubuhi hiyo nilipokuwa nikijiandaa kuenda Fanar, nilijiuliza maswali mengine kwa akili yangu - je, hisia ya wivu ndio itakuwa ya kunivuta nyuma kutoka kwa Mwenyezi Mungu? Je! Kwani kitu cha kidunia kama hicho kitanizuia nimjue Mwenyezi Mungu? Sikujijibu mwenyewe. Badala yake, nilikimbilia kujiandaa kuondoka. Hatua hiyo peke yake ilikuwa jibu.
Baada ya kufika Fanar, nilikuwa na fursa ya kuwa na mazungumzo ya moja kwa moja na washauri wao wawili - Dada Zarah na Dada Maryam. Hamu ya moyo wangu ilianza kujifunua. Dada Maryam alisema kuwa ninaonekana niko tayari. Aliponiuliza kama ningependa kufanya shahaadah, nilijibu tu kwa kusema - JE, KUNA MTU YEYOTE AMBAYE ANGEWEZA KUNIONGOZA KUIFANYA? Tena, hisia hiyo ya uhakika - sio kuhusu NDIO au HAPANA, ni kuhusu upatikanaji wa mtu ambaye angeweza kuniongoza kuifanya shahadah.
Baada ya kusema Shahadah, machozi yalianza kutirirka. Dada Maryam aliponikumbatia na kuniambia tayari nimeshakuwa Muislamu, Nilimshukuru kwa machozi. Familia yangu ya karibu ilinikaribisha kama Muslimah na namshukuru Allah kwa hilo. Ingawa wanabaki kuwa Wakatoliki, kukubali kwao, msaada na upendo wao unanisaidia sana. Kwa upande wa mchumba wangu, alishangaa kupokea ujumbe kutoka kwangu dakika chache baada ya mimi kuingia kwa Uislamu. Hakutarajia kupokea habari kama hizo kutoka kwangu.
Kuingia kwangu kwa Uislamu kulisisitizwa na tsunami kubwa. Ninaiangalia kama ishara ya kuwa Mwenyezi Mungu ameniosha kabisa na kunitakasa kutoka kwa dhambi zangu. Ningekuwa nini leo kama nisingelijisalimisha kwake? Ningekuwa wapi?