Hapo zamani za kale, mwanamke akiota katika ndoto kuwa mwanamume anazima taa ya kandili ndani ya nyumba, au akiota kuwa nyumba kubwa imeangukia nguzo zake, angetabiriwa na mtabiri wa ndoto kuwa mwanamume mwenye nyumba hiyo atafariki!
Mtu mmoja alisema: "Niliota katika ndoto nikitembea kwa magongo asubuhi, na saa moja baadaye niliarifiwa kuwa baba yangu alikuwa amekufa."
Waarabu wa zamani walimdhania kunguru ni ndege kisirani. Huu wote ulikuwa ushirikina uliomea mizizi siku za ujahili kabla ya Uislamu.
Mtume Muhammad alisema katika hotuba moja: "Mwenyezi Mungu alimpa mtumishi wake uchaguzi kati ya kupewa ua la Dunia na kile Alichokuwa amemwekea, na akachagua kile Alichokuwa amemwekea." Watu walikanganyika, lakini Abu Bakr alianza kulia, akielewa kuwa Mtume alikuwa akiwaambia watu kwamba maisha yake yalikuwa yanafika mwisho."[1]
Msichana mdogo aliulizwa: "Kuna watoto wangapi katika familia yenu?"
Alijibu msichana huyo: "Tuko saba."
Akaulizwa tena: "Wako wapi?"
Akajibu msichana: "Sisi watano tuko hapa, na wawili wetu wako pale chini ya mti ule."
Aliyeuliza akatazama upande ambao msichana aliashiria na kuona mawe mawili ya makaburi chini ya mti.
"Nyinyi ni watano, basi," akajibiwa. "Hapana," akajibu, "Sisi ni saba."
Kifo sio kufutilia mbali wala sio mwisho. Ni mpito kutoka hali moja ya kuwa kiumbe kwenda nyingine. Ni kuzaliwa upya katika ulimwengu mwingine. Ingawa inaonekana kama plagi imeunganishwa kwenye kifaa cha umeme, ni hali ya muda mfupi sana. Tunawaambia watoto kwamba marehemu "ameenda kwa Mola wao". Ni njia nzuri ya kuielezea. Ni mtazamo mwafaka unaokubaliana vizuri na imani yetu.
Maana ya Uhai
Albert Camus, mwanafalsafa Mfaransa aliyeitakidi maisha ya huria, alisema kwamba kwa kuwa sisi sote lazima tufe, hakuna chochote kilicho na maana yoyote.
Kabla yake, al-Khayyam alisema: "Kioo hiki kilitengenezwa kwa umbo zuri la kiufundi, basi kwa nini lazima kikubali kuvunjika?"
Haya ni mawazo potofu, ya kukana dini na sheria za kibinadamu. Kinyume chake, Mtume Muhammad alisema: "kuwa katika ulimwengu huu kama mgeni au msafiri."
Ibn Umar alikuwa akisema: "Unapoenda kulala usiku, usingoje alfajiri, na unapoamka, usingoje usiku ufike. Faidi afya yako kabla ya kufikwa na nyakati za ugonjwa na tumia vizuri maisha yako kabla ya kifo chako."[2]
Maisha ni kama uwanja wa ndege; ni maandalizi tu ya safari ndefu inayokuja.
Mwenyezi Mungu anasema: "Ambaye ameumba mauti na uhai ili kukujaribuni ni nani miongoni mwenu mwenye vitendo vizuri zaidi..." (Kurani 67:2)
Hii ni njia bora ya kuliangalia suala hili. Badala ya kuonekana kama hukomesha shughuli, hali hii isiyoepukika ionekane kama kichocheo cha harakati. Tunahitaji kushughulika na kutengeneza majina yetu wakati bado tunaweza.
Tunapotambua kuwa maisha ni mafupi, itatusaidia kuwa watu wanaosamehe zaidi. Tutaamua kuweka chuki za kibinafsi kando, tukijua kwamba wakati wetu tunaoishi na wengine ni mdogo.
Tunalazimika kujiuliza maswali matatu muhimu:
1. Tunawezaje kuishi maisha ya furaha na ya manufaa?
2. Watu watasema nini baada ya sisi kuondoka duniani? Wataathirika vipi na hadithi za maisha yetu?
3. Matendo yetu mema yatakuwaje siku ya Akhera?
Mmoja wa Watu Wema Waliotangulia alisema: "Kuna watu ambao wanafanya matendo mengi mazuri, laiti wangejua watakufa kesho, wasingeweza kuongeza kile wanachofanya."
Ali ibn Abi Talib alisema: "Kwa kila pumzi, mtu hufikia karibu sana na kifo." Alisema pia: "Fanyeni kazi katika ulimwengu huu kana kwamba mtaishi milele, lakini fanyeni kazi kwa ajili ya Akhera kana kwamba mtakufa kesho."
Steve Jobs alitoa hotuba ya kwanza ambapo alielezea jinsi alivyozoea kulala sakafuni katika vyumba vya marafiki zake, jinsi alivyolazimika kutembea kwa maili kupata chakula cha bure, jinsi mama yake mchanga alivyolazimika kuhangaika kupata watu wa kumchukua yeye kama mtoto wa kupanga pindi alipozaliwa, jinsi alivyosukumwa kwa urahisi nje ya kampuni aliyoanzisha, na jinsi alivyohisi ilipobainika ana saratani ya kongosho. Kisha akasema: "ikiwa unaishi kila siku kana kwamba ni siku yako ya mwisho, ipo siku moja itakuthubutikia kuwa kweli."
Jinsi ya Kuangalia Mauti kwa Uwazi
1. Inatosha kuyafikiria mauti kama safari ya kwenda mahali ambapo hakuna maonevu au dhuluma. Itasemwa Siku ya Kiyama: "Leo, kila nafsi italipwa kulingana na iliyochuma. Hapana dhuluma leo..." (Kurani 40:17)
2. Ni kuungana tena na wapendwa wetu ambao walikufa. Kabla tu ya kufa, Muadh ibn Jabal alisema: "Kesho, nitakutana na wale ninaowapenda, Muhammad na Masahaba wake."
3. Ni ukombozi kutoka gereza la uwepo wa mali. Mtume alisema: "Ulimwengu ni gereza la muumini."[3]
4. Ni rehema kwa wale ambao maisha yao yamekumbwa na maradhi yanayodhoofisha, ukosefu na kunyimwa au kutoweza kufanya kazi au wakati akili ya mtu huzorota sana kiasi cha wao kutoweza tena kutangamana na wapendwa wao.
5. Mauti ni sawa na kulala. Yote mawili ni mabadiliko katika hali yetu ya kuishi. Moja ni kuhama kabisa kwenda maisha mengine, na ile nyingine ni dalili kuwa ya kwanza ipo na ni hakika.
6. Kujua kwamba tutakufa siku moja hutusaidia kushikilia maadili yetu tunapokabiliwa na shida za maisha, na huturahisishia kufanya maamuzi sahihi tunapokabiliwa na uchaguzi usiofaa lakini unaovutia.