Nakala

Isa Mtume


“Semeni nyinyi: ‘Tumemuamini Mwenyezi Mungu na yale tuliyoteremshiwa sisi, na yaliyoteremshwa kwa Ibrahim na Ismail na Is-haka na Yaakub na wajukuu zake, na waliyopewa Musa na Isa, na pia waliyopewa manabii wengine kutoka kwa Mola wao Mlezi; hatutofautishi baina ya yeyote katika hao, na sisi tumesilimu kwake.’” (Kurani 2:136)





“Hakika Sisi tumekuletea wahyi wewe kama tulivyowapelekea wahyi Nuhu na manabii waliokuwa baada yake. Na tulimpelekea wahyi Ibrahim na Ismail na Is-haka na Yaakub na wajukuu zake, na Isa na Ayub na Yunus na Harun na Suleiman, na Daud tukampa Zaburi.” (Kurani 4:163)





“Masihi mwana wa Maryamu si chochote ila ni mtume. Wamekwishapita mitume kabla yake. Na mama yake ni mwanamke mkweli.[1]  Wote wawili walikuwa wakila chakula.[2]  Angalia jinsi tunavyowabainishia Aya, kisha angalia vipi wanavyogeuzwa.” (Kurani 5:75)





“Hakuwa yeye (Isa) ila ni mtumishi tuliyemneemesha, na tukamfanya ni mfano kwa Wana wa Israili.” (Kurani 43:59)





Ujumbe wa Isa


“Na tukawafuatishia hao Isa mwana wa Maryamu, kuyahakikisha yaliyokuwa kabla yake katika Taurati, na tukampa Injili, iliyomo ndani yake uongofu, na nuru na inayosadikisha yaliyokuwa kabla yake katika Taurati, na uongofu na mawaidha kwa wacha Mungu.” (Kurani 5:46)





“Enyi watu wa Kitabu! Msipite kiasi katika dini yenu, wala msimseme Mwenyezi Mungu ila kwa lililo kweli. Hakika Masihi Isa, mwana wa Maryamu, ni mtume wa Mwenyezi Mungu, na neno lake tu alilompelekea Maryamu, na ni roho iliyotoka kwake.[3]  Basi muaminini Mwenyezi Mungu na mitume wake. Wala msiseme: ‘Utatu.’ Komeni! Itakuwa kheri kwenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mungu mmoja tu. Ametukuka Yeye na kuwa na mwana. Ni vyake Yeye vyote viliyomo katika mbingu na katika ardhi. Na Mwenyezi Mungu ni Mtegemewa wa kutosha. Masihi hataona uvunjifu kuwa mtumwa wa Mwenyezi Mungu, wala malaika waliokaribishwa.[4]  Na watakaoona uvunjifu utumwa wa Mwenyezi Mungu na kufanya kiburi, basi atawakusanya wote kwake.” (Kurani 4:171-172)





“Huyo ndiye Isa mwana wa Maryamu. Ndiyo kauli ya haki ambayo wanaifanyia shaka. Haiwi kwa Mwenyezi Mungu kuwa na mwana, Subhanahu, Yeye ametakasika! Anapolihukumia jambo basi huliambia tu: Kuwa! Likawa.[5]  Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mola wangu Mlezi, na Mola wenu Mlezi. Basi muabuduni Yeye. Hii ndiyo njia Iliyonyooka. Lakini makundi yakakhitalifiana wao kwa wao. Basi ole wao hao waliokufuru kwa kuhudhuria Siku iliyo kuu!” (Kurani 19:34-37)





“Na alipokuja Isa na dalili zilizo wazi, alisema: ‘Nimekujieni na hekima, na ili nikuelezeni baadhi ya yale mliyokhitalifiana. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na mnitii mimi. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mola wangu Mlezi, na ni Mola wenu Mlezi. Basi muabuduni Yeye tu. Hii ndiyo njia Iliyonyooka.’ Lakini makundi kwa makundi yao yalikhitalifiana wao kwa wao. Ole wao waliodhulumu kwa adhabu ya Siku chungu.” (Kurani 43:63-65)





“Na Isa mwana wa Maryamu aliposema: ‘Enyi Wana wa Israili! Hakika mimi ni mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu, ninayethibitisha yaliyokuwa kabla yangu katika Taurati, na mwenye kubashiria kuja mtume atakayekuja baada yangu; jina lake ni Ahmad.’[6]  Lakini alipowaletea hoja zilizo wazi, walisema: ‘Huu ni uchawi ulio dhahiri!’”[7] (Kurani 61:6)





Miujiza ya Isa


“(Maryamu) akawaashiria (mtoto). Wakasema: ‘Vipi tumsemeze aliye bado mdogo yumo katika mlezi.’ Akasema (Isa): ‘Hakika mimi ni mtumishi wa Mwenyezi Mungu, amenipa Kitabu na amenifanya mtume.[8]  Na amenijaalia ni mwenye kubarikiwa popote pale niwapo. Na ameniusia sala na zaka maadamu ni hai. Na nimtendee wema mama yangu. Wala hakunifanya niwe jeuri, mwovu. Na amani iko juu yangu siku niliyozaliwa, na siku nitakayokufa, na siku nitakayofufuliwa kuwa hai.’” (Kurani 19:29-33)





(Miujiza zaidi imetajwa chini ya kichwa: Habari njema ya mtoto mchanga aliyezaliwa)





Meza Iliyoandaliwa (vyakula) kutoka Mbinguni kwa idhini ya Mungu


“Wanafunzi waliposema: ‘Ewe Isa mwana wa Maryamu! Je, Mola wako Mlezi anaweza kututeremshia chakula kutoka mbinguni?’ Akasema: ‘Mcheni Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi ni waumini wa kweli.’ Wakasema: ‘Tunataka kukila chakula hicho, na nyoyo zetu zitue, na tujue kwamba umetuambia kweli, na tuwe miongoni mwa wanaoshuhudia.’ Akasema Isa mwana wa Maryamu: ‘Ewe Mwenyezi Mungu, Mola wetu Mlezi! Tuteremshie chakula kutoka mbinguni ili kiwe Sikukuu kwa ajili ya wa mwanzo wetu na wa mwisho wetu, na kiwe ni ishara itokayo kwako. Basi turuzuku, kwani Wewe ndiye mbora wa wanaoruzuku.’ Mwenyezi Mungu akasema: ‘Hakika Mimi nitakuteremshieni hicho. Lakini yeyote katika nyinyi atakayekana baadaye, basi hakika Mimi nitampa adhabu nisiyopata kumpa yeyote katika walimwengu.’” (KuranI 5:112-115)





Isa na Wanafunzi Wake


“Enyi mlioamini! Kuweni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu, kama alivyosema Isa mwana wa Maryamu kuwaambia wanafunzi wake: ‘Nani wasaidizi wangu kwa Mwenyezi Mungu?’ Wakasema wanafunzi: ‘Sisi ni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu!’ Basi taifa moja la Wana wa Israili liliamini, na taifa jingine lilikufuru. Basi tukawaunga mkono walioamini dhidi ya maadui zao, wakawa wenye kushinda.”[9] (Kurani 61:14)





“Na nilipowafunulia wanafunzi kwamba waniamini Mimi na Mtume wangu, wakasema: ‘Tumeamini na shuhudia kuwa sisi ni Waislamu.’” (Kurani 5:111)





“Tena tukafuatisha nyuma yao mitume wetu wengine, na tukamfuatisha Isa mwana wa Maryamu, na tukampa Injili. Na tukajaalia katika nyoyo za waliomfuata upole na rehema. Na umonaki (utawa wa mapadri) wameuzua wao. Sisi hatukuwaandikia hayo, ila kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu. Lakini hawakuufuata inavyotakiwa kuufuata. Basi wale walioamini katika wao tuliwapa ujira wao. Na wengi wao ni wapotovu. Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na muaminini mtume wake, atakupeni sehemu mbili katika rehema yake, na atakujaalieni muwe na nuru ya kwenda nayo. Na atakusameheni. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. Ili watu wa Kitabu wajue kwamba wao hawana uweza wowote juu ya fadhila za Mwenyezi Mungu. Na fadhila zote zimo mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Humpa amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye fadhila kuu.”[10] (Kurani 57:27-29)





Shauku ya Kristo


“Isa alipohisi kuwa kati yao pana ukafiri alisema: ‘Ni nani wasaidizi wangu kwa Mwenyezi Mungu?’ Wanafunzi wake wakasema: ‘Sisi ni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu. Tumemuamini Mwenyezi Mungu, na shuhudia kwamba sisi hakika ni Waislamu.’[1]  Mola wetu Mlezi! Tumeyaamini uliyoyateremsha, na tumemfuata huyu mtume, basi tuandike pamoja na wanaoshuhudia.’ Na makafiri walipanga mipango, na Mwenyezi Mungu akapanga mipango, na Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa wenye kupanga.[2]  Pale Mwenyezi Mungu aliposema: ‘Ewe Isa! Mimi nitakufisha, na nitakunyanyua kwangu, na nitakutakasa na wale waliokufuru, na nitawaweka wale waliokufuata juu ya wale waliokufuru, mpaka Siku ya Kiyama. Kisha marejeo yenu yatakuwa kwangu, nikuhukumuni katika yale mliyokuwa mkikhitalifiana.’” (Kurani 3:52-55)





“Na kwa kusema kwao: ‘Sisi tumemuuwa Masihi Isa, mwana wa Maryamu, mtume wa Mwenyezi Mungu - nao hawakumuuwa wala hawakumsulubu, bali walifananishiwa tu.[3]  Na hakika waliokhitalifiana katika haya wamo katika shaka nayo. Wao hawana ujuzi wowote nayo, ila ni kufuata dhana tu. Wala hawakumuuwa kwa yakini. Bali Mwenyezi Mungu alimtukuza kwake.[4]  na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.” (Kurani 4:157-158)





Wafuasi wa Yesu


“Watakaokuhoji katika haya baada ya kukufikilia elimu hii waambie: ‘Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu, na wake zetu na wake zenu, na sisi wenyewe na nyinyi wenyewe, kisha tuombe kwa unyenyekevu tutake laana ya Mwenyezi Mungu iwashukie waongo.’ Hakika haya ndiyo maelezo ya kweli. Na hakuna mungu ila Mwenyezi Mungu tu, na hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye nguvu na Mwenye hekima. Na kama wakigeuka, basi Mwenyezi Mungu anawajua waharibifu. Sema: ‘Enyi Watu wa Kitabu! Njooni kwenye neno lililo sawa baina yetu na nyinyi[5]  Ya kwamba tusimuabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu, wala tusimshirikishe na chochote; wala tusifanyane sisi kwa sisi kuwa Waola Walezi badala ya Mwenyezi Mungu[6].’  Na, wakigeuka basi semeni: ‘Shuhudieni ya kwamba sisi ni Waislamu.’” (Kurani 3:61-64)





“Hakika wamekufuru waliosema: ‘Mwenyezi Mungu ni Masihi mwana wa Maryamu.’ Sema: ‘Ni nani mwenye kumiliki chochote mbele ya Mwenyezi Mungu ikiwa Yeye angetaka kumuangamiza Masihi mwana wa Maryamu, na mama yake, na wote waliomo katika ardhi?’ Na mamlaka ya mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake ni vya Mwenyezi Mungu. Huumba apendavyo. Na Mwenyezi Mungu anao uweza juu ya kila kitu. Na Mayahudi na Wakristo wanasema: ‘Sisi ni wana wa Mwenyezi Mungu na vipenzi vyake.’ Sema: ‘Basi kwa nini anakuadhibuni kwa ajili ya madhambi yenu?’ Bali nyinyi ni watu tu kama wale wengine aliowaumba. Humsamehe amtakaye na humuadhibu amtakaye. Na ni wa Mwenyezi Mungu tu ufalme wa mbingu na ardhi. Na marejeo ni kwake Yeye.” (Kurani 5:17-18)





“Hakika wamekufuru waliosema: ‘Mwenyezi Mungu ni Masihi mwana wa Maryamu!’ Na hali Masihi mwenyewe alisema: ‘Enyi Wana wa Israili! Muabuduni Mwenyezi Mungu, Mola wangu Mlezi na Mola wenu Mlezi. Kwani anayemshirikisha Mwenyezi Mungu, hakika Mwenyezi Mungu atamharimishia Pepo, na mahala pake ni Motoni. Na waliodhulumu hawatakuwa na wa kuwanusuru.’ Kwa hakika wamekufuru waliosema: ‘Mwenyezi Mungu ni wa tatu wa Utatu.’[7]  Hali hakuna mungu ila Mungu Mmoja. Na ikiwa hawaachi hayo wanayoyasema, kwa yakini itawakamata adhabu chungu wale wanaokufuru. Je, hawatubu kwa Mwenyezi Mungu na wakamwomba msamaha? Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghfira na Mwenye kurehemu.” (Kurani 5:72-74)





“Na Mayahudi wanasema: ‘Uzeir ni mwana wa Mungu,’[8]  Na Wakristo wanasema: ‘Masihi ni mwana wa Mungu.’ Hiyo ndiyo kauli yao kwa vinywa vyao. Wanayaiga maneno ya waliokufuru kabla yao. Mwenyezi Mungu awaangamize! Wanageuzwa namna gani hawa! Wamewafanya makuhani wao na wamonaki wao kuwa ni marabi badala ya Mwenyezi Mungu, na pia Masihi mwana wa Maryamu. Na wala hawakuamrishwa isipokuwa wamuabudu Mungu Mmoja, hapana mungu ila Yeye. Subhanahu, Ametakasika na hayo wanayomshirikisha nayo.”[9] (Kurani 9:30-31)





“Enyi mlioamini! Hakika wengi katika makuhani na wamonaki wanakula mali za watu kwa batili na wanazuilia njia ya Mwenyezi Mungu. Na wanaokusanya dhahabu na fedha, wala hawazitumii katika njia ya Mwenyezi Mungu, wabashirie khabari ya adhabu iliyo chungu.” (Kurani 9:34)





Ujio wa Pili


“Na hawi katika watu wa Kitabu ila hakika atamuamini yeye kabla ya kufa kwake.[10]  Naye Siku ya Kiyama atakuwa shahidi juu yao.”[11] (Kurani 4:159)





“Na kwa hakika yeye (Isa) ni alama ya Saa ya Kiyama. Basi usiitilie shaka,[12]  na nifuateni. Hii ndiyo njia Iliyonyooka.” (Kurani 43:61)





Yesu Siku ya Kiyama


“Na pale Mwenyezi Mungu atakaposema: ‘Ewe Isa mwana wa Maryamu! Kumbuka neema yangu juu yako, na juu ya mama yako, nilipokutia nguvu kwa Roho Takatifu, ukazungumza na watu katika utoto na utuuzimani. Na nilivyokufunza kuandika na hekima na Taurati na Injili. Na ulipotengeneza udongo sura ya ndege, kwa idhini yangu, kisha ukapuliza ikawa ndege kwa idhini yangu; na ulipowaponesha vipofu na wakoma kwa idhini yangu; na ulipowafufua wafu kwa idhini yangu; na nilipokukinga na Wana wa Israili ulipowajia na hoja zilizo wazi,’ na wakasema waliokufuru miongoni mwao: ‘Haya si lolote ila ni uchawi mtupu!’” (Kurani 5:110)





“Na pale Mwenyezi Mungu atakaposema: ‘Ewe Isa mwana wa Maryamu! Ati wewe uliwaambia watu: ‘Nifanyeni mimi na mama yangu kuwa ni miungu badala ya Mwenyezi Mungu?’[13]’  (Na Isa) atasema: ‘Subhanaka, Wewe umetakasika! Hainifalii mimi kusema ambayo si haki yangu. Ikiwa nilisema basi bila ya shaka umekwisha yajua. Wewe unayajua yaliyo ndani ya nafsi yangu, lakini mimi siyajui yaliyo katika nafsi yako. Hakika Wewe ndiye Mjuzi mkubwa wa yaliyofichikana.’[14]  ‘Sikuwaambia lolote ila uliyoniamrisha, nayo ni: ‘Muabuduni Mwenyezi Mungu, Mola wangu Mlezi na Mola wenu Mlezi.’ Na mimi nilikuwa shahidi juu yao nilipokuwa nao. Na uliponifisha ukawa Wewe ndiye Muangalizi juu yao. Na Wewe ni shahidi juu ya kila kitu. Ukiwaadhibu basi hao ni waja wako. Na ukiwasamehe basi Wewe ndiye Mwenye nguvu na Mwenye hikima.’[15]  Mwenyezi Mungu atasema: ‘Hii ndiyo Siku ambayo wasemao kweli utawafaa ukweli wao. Wao watapata bustani zipitazo mito kati yake. Humo watadumu milele. Mwenyezi Mungu amewawia radhi, nao wawe radhi naye. Huku ndiko kufuzu kukubwa.’ Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi na vilivyomo. Naye ni Muweza wa kila kitu.” (Kurani 5:116-120)



Machapisho ya hivi karibuni

UJUMBE KUTOKA KWA MUH ...

UJUMBE KUTOKA KWA MUHUBIRI MUISLAMU KWA MKRISTO

FADHILA YA KUFUNGA SI ...

FADHILA YA KUFUNGA SIKU SITA ZA SHAWAL

Masuala kumi muhimu n ...

Masuala kumi muhimu na mafupi kuhusu mwezi wa Muharram

UJUMBE KWA ALIYEICHOM ...

UJUMBE KWA ALIYEICHOMA KURANI