“Utayari wa kusamehe na kutokuadhibu” ni tafsiri inayotumika mara kwa mara kwa neno rehema, lakini rehema ni nini katika Uislamu?
Kwa Uislamu, rehema ilipewa maana ya ndani zaidi ambayo ilijenga kipengele muhimu katika maisha ya kila Muislamu, ambacho anazawadiwa na Mungu kwa ajili ya kuonyesha.
Rehema ya Mungu, ambayo vimepewa viumbe Vyake vyote, inaonekana katika kila kitu tunachokitazama: katika jua ambalo hutoa mwanga na joto, na katika hewa na maji ambayo ni muhimu kwa wote walio hai.
Sura nzima katika Quran imepewa jina la sifa ya Mwenyezi Mungu Ar-Rahman au "Mwingi wa Rehema." Pia sifa mbili za Mungu zinatokana na neno la rehema. Nazo ni Ar-Rahman na Ar-Rahim, ambayo ina maana ya “Mwingi wa Fadhila” na “Mwingi wa Rehema.” Sifa hizi mbili zimetajwa katika maneno yaliyosomwa mwanzoni mwa sura 113 za Quran: “Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu.” Maneno haya ni ukumbusho endelevu kwa msomaji wa rehema zisizo na mwisho za Mungu na fadhila kuu.
Mwenyezi Mungu anatuhakikishia kwamba anayefanya dhambi atasamehewa ikiwa atatubu na kuacha kitendo hiki, ambapo anasema:
“Mola wenu Mlezi amejilazimisha rehema, ya kwamba atakaye fanya uovu miongoni mwenu kwa ujinga, kisha akatubu baada yake na akatengenea, basi hakika Yeye ni Mwenye maghfira na Mwenye kurehemu.” (Quran 6:54)
Aya hii inathibitishwa na riwaya ya Mtume Muhammad ambapo amesema kuwa Mwenyezi Mungu alisema:
“Rehema yangu inashinda ghadhabu yangu.”
Malipo ya wema na huruma pia yalihakikishwa na Mtume Muhammad:
“Wenye kurehemu wanahurumiwa na Mwingi wa Rehema. Warehemuni waliomo ardhini, na Yeye aliye mbinguni atakurehemuni” (As-Suyuti).
Rehema ya Mtume
Kuhusu rehema ya Mtume Muhammad ni vyema kutaja kwanza yale ambayo Mwenyezi Mungu amesema juu yake:
“Nasi hatukukutuma ila uwe ni Rehema kwa walimwengu wote.” (Quran 21:107)
…ambayo inahakikisha kwamba Uislamu umejengwa juu ya rehema, na kwamba Mwenyezi Mungu alimtuma Mtume Muhammad, rehema na baraka za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kama rehema kwa viumbe vyote bila ubaguzi.
Katika Quran Mwenyezi Mungu pia anasema:
“Hakika amekwisha kujieni Mtume kutokana na nyinyi wenyewe; yanamhuzunisha yanayo kutaabisheni; anakuhangaikieni sana. Kwa Waumini ni mpole na mwenye huruma.” (Quran 9:128)
Aya hizi zilidhihirika kwa uwazi kabisa katika tabia na matendo ya Mtume, kwani alivumilia matatizo mengi kwa ajili ya kufikisha ujumbe wa Mungu. Mtume pia alikuwa mpole sana katika kuwaongoza watu wake, na kila walipokuwa wakimfanyia ubaya alimwomba Mwenyezi Mungu awasamehe kwa ujinga na ukatili wao.
Maswahaba wa Mtume
Anapowaelezea Maswahaba katika Quran Mungu anasema:
“Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na walio pamoja naye wana nguvu mbele ya makafiri, na wanahurumiana wao kwa wao.” (Quran 48:29).
Baadhi ya watu wanaweza kufikiri ni dhahiri kwa Muhammad kuwa na maadili, kwa sababu yeye ni Mtume, lakini Maswahaba walikuwa ni watu wa kawaida ambao walijitolea maisha yao kwa ajili ya kumtii Mungu na Mtume Wake. Kwa mfano Abu Bakr As-Siddiq alijitolea mali yake yote kwa ajili ya kununua watumwa kutoka kwa mabwana wao wakatili na kisha akawaacha huru kwa ajili ya Mungu.
Wakati mmoja alipokuwa akifafanua dhana sahihi ya rehema kwa Maswahaba zake, Mtume alisema kwamba si kwa wema wa mtu kwa familia na marafiki, bali ni kwa kuonyesha rehema na huruma kwa umma kwa ujumla, iwe unawajua au huwajui.
Rehema "Ndogo"
Baadhi ya mila zisizo na huruma za kabla ya Uislamu zilikuwa zinatoa mtoto kama kafara kwa ajili ya miungu na kuzika wasichana wakiwa hai. Vitendo hivi dhidi ya watoto vilikatazwa vikali na Quran na Sunnah za Kinabii mara nyingi.
Kwa rehema za Mtume kwa watoto, siku moja alikuwa akiongoza swala na wajukuu zake, Al-Hasan na Al-Husein, bado walikuwa ni wavulana wadogo wakicheza na kupanda juu ya mgongo wake, hivyo kwa khofu ya kuwadhuru akiwa anasimama, Mtume akarefusha sajda yake. Wakati mwingine, Mtume aliswali huku akiwa amembeba Umamah, mjukuu wake wa kike.
Wema huu wa Mtume haukutawazwa kwa watoto wake tu bali pia ulienezwa kwa watoto wanaocheza mitaani. Mara tu walipomwona Mtume, walimkimbilia, na alikuwa akiwapokea wote kwa tabasamu mchangamfu na kwa mikono wazi.
Hata wakati wa kuswali wema wa asili wa Mtume ulikuwa wazi, kama alivyowahi kusema:
“(Inatokea kwamba) naanza swala nikikusudia kurefusha, lakini nikisikia kilio cha mtoto, nafupisha Swalah kwa sababu najua kwamba kilio cha mtoto kitachochea matamanio ya mama yake” (Saheeh Al-Bukhari).
Katika hali nyingi Mtume alitufundisha jinsi watoto wanapaswa kulelewa katika hali nzuri na ya upendo, na kwamba wasipigwe, au kupigwa usoni, ili kuepuka unyonge wao. Wakati mtu mmoja alipomwona Mtume akimbusu mjukuu wake, alistaajabishwa na upole wa Mtume na akasema, “Nina watoto kumi lakini sijawahi kumbusu hata mmoja wao.” Mtume akajibu,
“Asiye rehemu hatarehemewa” (Saheeh Al-Bukhari).
Kipande cha Nywele tu
Mungu alipowataja mayatima ndani ya Quran alisema nini maana yake:
“Basi yatima usimwonee!” (Quran 93:9)
Kwa mujibu wa Aya hii zilikuja adabu za Mtume kwa mayatima, kwani alisema:
“Mimi na yule anayemlea yatima na kumruzuku, tutakuwa Peponi namna hii,” akiweka pamoja vidole vyake vya shahada na vya kati. (Abu Dawud)
Ili kumfanya yatima ajisikie kuthaminiwa na kwamba ikiwa amepoteza penzi la wazazi wake bado kuna watu ambao wako tayari kumpenda na kumtunza, Mtume alihimiza wema kwa kusema kwamba mtu hulipwa kwa matendo mema kwa kila nywele anayopiga katika kichwa cha yatima.
Ulinzi wa mali ya yatima ulithibitishwa wazi na Mungu na Mtume Wake. Kwa mfano, Mungu anasema maana yake:
“Hakika wanao kula mali ya mayatima kwa dhulma, hapana shaka yoyote wanakula matumboni mwao moto, na wataingia Motoni.” (Quran 4:10)
Kauli ya Mtume pia inatufahamisha kwamba moja ya madhambi saba makubwa ni kula mali ya yatima.
Rehema ya kimungu inafunika uwepo wote katika zizi lake, lenye kudumu milele. Mola Mlezi wa watu ni mwenye kuwarehemu, mwenye huruma. Jina la Mwenyezi Mungu, Ar-Rahman, linapendekeza rehema Yake ya upendo ni kipengele kinachobainisha nafsi Yake; utimilifu wa huruma zake hauna kikomo; bahari isiyo na mwisho isiyo na ufukwe. Ar-Razi, mmoja wa wasomi wa kiislamu wa kitambo aliandika, ‘Haiwezekani kwa viumbe kuwa na rehema zaidi kuliko Mwenyezi Mungu!’ Hakika Uislamu unafundisha kwamba Mungu ni mwenye huruma zaidi kwa mwanadamu kuliko mama yake mwenyewe.
Katika rehema nyingi za Mungu, Huteremsha mvua ili kuzalisha matunda kutoka kwenye bustani ili kuupa mwili wa mwanadamu. Nafsi pia inahitaji lishe nzuri ya kiroho kama vile mwili unavyohitaji chakula. Katika rehema zake nyingi, Mungu alituma manabii na wajumbe kwa wanadamu na kuwafunulia maandiko ili kutendeleza roho ya mwanadamu. Rehema ya Mwenyezi Mungu imejidhihirisha katika Torati ya Musa:
"…Na katika maandiko yake mna uwongofu na rehema kwa wanao mwogopa Mola wao Mlezi." (Kurani 7:154)
Na ufunuo wa Kurani:
"…Hii (Kurani) ni hoja zinazo toka kwa Mola wenu Mlezi, na uwongofu na rehema kwa watu wanao amini." (Kurani 7:203)
Rehema haitolewi kwa sifa fulani za mababu. Huruma ya Kimungu inatolewa kwa kutenda kulingana na Neno la Mungu na kusikiliza kisomo chake:
"Na hichi ni Kitabu tulicho kiteremsha, kilicho barikiwa. Basi kifuateni, na mchenimngu, ili mrehemewe." (Kurani 6:155)
"Na isomwapo Kurani isikilizeni na mnyamaze ili mpate kurehemewa." (Kurani 7:204)
Rehema ni matokeo ya utiifu:
"Na shikeni Swala, na toeni Zaka, na mt'iini Mtume, ili mpate kurehemewa." (Kurani 24:56)
Rehema ya Mungu ni tumaini la mwanadamu. Kwa hiyo waumini wanamwomba Mwenyezi Mungu rehema yake.
"Mimi yamenipata madhara. Na Wewe ndiye unaye rehemu kuliko wote wanao rehemu!" (Kurani 21:83)
Wanaomba rehema ya Mungu kwa uaminifu:
"Mola wetu Mlezi! Usizipotoe nyoyo zetu baada ya kwisha tuongoa, na utupe rehema itokayo kwako. Hakika Wewe ndiye Mpaji." (Kurani 3:8)
Na wanawaombea rehema ya Mwenyezi Mungu wazazi wao:
"…Mola wangu Mlezi! Warehemu kama walivyo nilea utotoni.!" (Kurani 17:24)
Ugawaji wa Rehema za Mungu
Huruma ya kimungu inawafunga mikononi waaminifu na wasio na imani, watiifu na waasi, lakini katika maisha yajayo itawekwa akiba kwa ajili ya waaminifu. Ar-Rahman ni mwenye huruma kwa viumbe vyote duniani, lakini rehema yake imehifadhiwa kwa waaminifu katika maisha yajayo. Ar-Raheem atasambaza rehema zake kwa waumini siku ya kiama:
"…Adhabu yangu nitamsibu nayo nimtakaye. Na rehema yangu imeenea kila kitu. Lakini nitawaandikia khasa wanao mchamngu, na wanao toa Zaka, na wale ambao wanaziamini Ishara zetu- Ambao kwamba wanamfuata huyo Mtume, Nabii, asiye soma wala kuandika, wanaye mkuta kaandikwa kwao katika Taurati na Injili…." (Kurani 7:156-157)
Ugawaji wa rehema za Mwenyezi Mungu umeelezewa na Mtume wa Uislamu:
"Mwenyezi Mungu ameumba sehemu mia za rehema. Akaweka sehemu moja kati ya viumbe vyake kwa ajili ya kuhurumiana wao kwa wao. Mwenyezi Mungu amehifadhi sehemu tisini na tisa zilizosalia kwa ajili ya Siku ya Hukumu ili kuwafadhilisha waja Wake." (Saheeh Al-Bukhari, Saheeh Muslim, Al-Tirmidhi, na wengineo.)
Sehemu ndogo tu ya rehema ya Mwenyezi Mungu inajaza mbingu na ardhi, wanadamu wanapendana, wanyama na ndege wanakunywa maji.
Pia, rehema ya Mungu ambayo itadhihirika Siku ya Hukumu ni kubwa kuliko yale tunayoyaona katika maisha haya, kama vile adhabu ya Mungu itakuwa kali zaidi kuliko ile tunayoipata hapa. Mtume wa Uislamu alielezea jinsi hizi sifa mbili tukufu zilivyokithiri:
"Iwapo Muumini angejua ni adhabu gani aliyoiweka Mwenyezi Mungu, basi atakata tamaa na hakuna hata mmoja atakayetazamia kuingia Peponi. Kama kafiri angejua rehema nyingi za Mwenyezi Mungu, hakuna hata mmoja atakayekata tamaa kuifikia Pepo." (Saheeh Al-Bukhari, Saheeh Muslim, Al-Tirmidhi)
Hata hivyo, katika mafundisho ya Kiislamu, rehema ya Mungu inapita hasira ya Mungu:
"Hakika rehema yangu imepita adhabu yangu." (Saheeh Al-Bukhari, Saheeh Muslim)
Huruma ya Mungu iko karibu sana na kila mmoja wetu, inatusubiri kuipata tunapokuwa tayari. Uislamu unatambua mwelekeo wa mwanadamu kufanya dhambi, kwani Mungu amemuumba mwanadamu dhaifu. Mtume amesema:
"Watoto wote wa Adamu hukosea kila mara ..."
Wakati huo huo, Mungu hutujulisha kuwa anasamehe dhambi. Tukiendeleza Hadithi hiyo hiyo:
"...lakini walio bora zaidi kwa wanao wanaokosea daima ni wale wanaotubu daima." (Al-Tirmidhiy, Ibn Majah, Ahmad, Hakim)
Mungu anasema:
"Anasema: ‘Enyi waja wangu walio jidhulumu nafsi zao! Msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote. Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.’" (Kurani 39:53)
Muhammad, Mtume mwenye Rehema, alipewa jukumu la kufikisha habari njema kwa watu wote:
"Waambie waja wangu ya kwamba Mimi ndiye Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu." (Kurani 15:49)
Toba huvutia Rehema ya Kimungu:
"…Kwa nini mnauhimiza uwovu kabla ya wema? Kwa nini hamuombi msamaha kwa Mwenyezi Mungu ili mrehemewe?" (Kurani 27:46)
"…Hakika rehema ya Mwenyzi Mungu iko karibu na wanao fanya mema.!" (Kurani 7:56)
Tangu nyakati za kale, rehema ya Mungu ya kuokoa imewaokoa waaminifu kutokana na maangamizi yanayo wasubiri:
"Ilipo fika amri yetu, tulimwokoa Huud na walio amini pamoja naye, kwa rehema itokayo kwetu…." (Kurani 11:58)
"Na ilipo fika amri yetu, tulimwokoa Shua'ibu na wale walio amini pamoja naye kwa rehema yetu…." (Kurani 11:94)
Ukamilifu wa huruma ya Mungu kwa mwenye dhambi unaweza kuonekana katika yafuatayo:
1. Mungu Anakubali Toba
"Na Mwenyezi Mungu anataka kukurejezeni kwenye ut'iifu wake, na wanao taka kufuata matamanio wanataka mkengeuke makengeuko makubwa." (Kurani 4:27)
"Je! Hawajui ya kwamba Mwenyezi Mungu anapokea toba ya waja wake, na anazikubali sadaka, na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kupokea toba na Mwenye kurehemu." (Kurani 9:104)
2. Mungu Anampenda Mwenye Dhambi Anayetubu
"…Kwa maana Mungu huwapenda wale wanaomgeukia daima…." (Kurani 2:22)
Mtume akasema:
"Kama wanadamu hawakuwa wakifanya madhambi, Mwenyezi Mungu angeumba viumbe wengine wanaofanya madhambi, kisha angewasamehe, kwani Yeye ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu." (Al-Tirmidhi, Ibn Majah, Musnad Ahmed)
3. Mungu Hufurahi Mwenye Dhambi Anapotubu Maana Anatambua Anaye Bwana Anayesamehe Dhambi!
Mtume akasema:
“Mwenyezi Mungu hufurahishwa sana na toba ya mja wake anapotubia kuliko yeyote miongoni mwenu ikiwa (angemkuta) ngamia wake ambaye alikuwa amempanda katika jangwa lisilo na maji baada ya kumtoroka akiwa amebeba chakula chake na kinywaji chake. Baada ya kukata tamaa akauendea mti na akajilaza katika kivuli chake, kisha alipokuwa katika kukata tamaa kwake, akaja ngamia na kusimama ubavuni mwake, akazishika hatamu zake na akapiga kelele kwa furaha: Ewe Mola. Wewe ni mja wangu, na mimi ni Bwana wako’ – kufanya kosa hili (kwa maneno) kutokana na furaha yake iliyopitiliza.” (Saheeh Muslim)
4. Lango la Toba liko wazi Mchana na Usiku
Huruma ya Mwenyezi Mungu inatoa msamaha kila siku na kila usiku kwa mwaka. Mtume akasema:
“Mwenyezi Mungu hunyoosha mkono wake usiku ili kupokea toba ya aliye fanya dhambi mchana, na hunyoosha mkono wake mchana ili kupokea toba ya aliye fanya dhambi usiku mpaka [siku itakapofika] jua kutoka Magharibi (moja ya alama kuu za Siku ya Kiyama). (Saheeh Muslim)
5. Mungu Anakubali Toba Hata Dhambi Zikirudiwa
Mara kwa mara Mungu huonyesha huruma yake kwa mwenye dhambi. Fadhili za upendo za Mungu kwa Wana wa Israeli zinaweza kuonekana kabla ya dhambi ya ndama wa dhahabu kufanywa, Mungu alishughulika na Israeli kulingana na huruma yake, hata baada ya kutenda dhambi, aliwatendea kwa rehema. Ar-Rahman anasema:
"…Na tulipo muahidi Musa masiku arubaini, kisha mkachukua ndama (mkamuabudu) baada yake, na mkawa wenye kudhulumu: Kisha tukakusameheni baada ya hayo, ili mpate kushukuru." (Kurani 2:51-52)
Mtume anasema:
“Mtu mmoja alifanya dhambi, kisha akasema, ‘Ewe Mola wangu nisamehe dhambi yangu,’ Mwenyezi Mungu akasema, ‘Mja wangu ametenda dhambi, kisha akatambua kwamba ana Mola anayeweza kusamehe dhambi na anaweza kumuadhibu kwa hilo. Kisha yule mtu akairudia dhambi hiyo, kisha akasema: ‘Ewe Mola wangu, nisamehe dhambi yangu. Yule mtu akarudia dhambi hiyo (mara ya tatu), kisha akasema, ‘Ewe Mola wangu nisamehe dhambi yangu,’ na Mwenyezi Mungu akasema, ‘Mja wangu ametenda dhambi, kisha akatambua kwamba ana Mola awezaye kusamehe dhambi na anayeweza kuadhibu. Fanya upendavyo, kwani mimi nimekusamehe." (Saheeh Muslim).
6. Kuingia Uislamu Hufuta Dhambi Zote Zilizotangulia
Mtume ameeleza kwamba kuukubali Uislamu kunafuta dhambi zote za awali za Muislamu mpya, bila kujali jinsi zilivyokuwa kubwa kwa sharti moja: Muislamu mpya anaukubali Uislamu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu tu. Baadhi ya watu walimuuliza Mtume wa Mungu, ‘Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Je, tutawajibishwa kwa yale tuliyoyafanya wakati wa siku za ujinga kabla ya kusilimu?’ Akajibu:
"Yeyote anayeukubali Uislamu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu tu hatahesabiwa, lakini mwenye kufanya hivyo kwa sababu nyingine atawajibika kwa muda kabla ya Uislamu na baada yake." (Saheeh Al-Bukhari, Saheeh Muslim)
Ingawa rehema ya Mungu inatosha kufunika dhambi yoyote, haimwachii mwanadamu kutoka kwenye wajibu wake wa kutenda ifaavyo. Nidhamu na bidii inahitajika katika njia ya wokovu. Sheria ya Wokovu katika Uislamu inatilia maanani imani na kushika Sheria, si imani tu katika Mungu. Sisi si wakamilifu na ni dhaifu na Mungu alituumba hivi. Tunapokosa kushika Sheria takatifu, Mungu Mwenye Upendo yuko tayari kusamehe. Msamaha unapokelewa kwa urahisi kupitia kuungama dhambi kwa Mungu peke yake na kuomba rehema zake, akiwa na nia thabiti ya kutofanya tena. Lakini mtu anapaswa kukumbuka daima kwamba Pepo haipatikani kwa matendo ya mtu pekee, bali hutolewa kwa rehema ya Mwenyezi Mungu. Mtume wa Rehema aliweka wazi ukweli huu:
“Hataingia Peponi hata mmoja wenu kwa vitendo vyake peke yake.’ Wakauliza, ‘Hata wewe ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?’ Akasema, ‘Hata mimi, isipokuwa Mwenyezi Mungu amenifunika kwa fadhila na rehema zake." (Saheeh Muslim)
Imani katika Mungu, kushika Sheria Yake, na matendo mema, yanazingatiwa kuwa kama sababu, sio njia ya kuingia Peponi.