1
Kwa Nini Tunauamini Uislamu?
Hoja kwa ufupi
لماذا نؤمن بالإسلام؟ باللغة السواحيلي ة -
Mtungaji: Doctor Nabil Abdissalaam Haruna
2
Utangulizi
Jambo gani linalothibitisha kuwa Qurani ni ufunuo kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwenda kwa mja wake na Mtume wake Muhammad (SAW), Na kuwa kazi ya Mtume ni Msambazaji Mwaminifu Aneyebainisha na Kufafanua ufunuo uliomjia, bila kuchupa mipaka?
Katika ujumbe huu mfupi tutathibitisha – kisayansi na kihistoria – kuwa haiwezekani Quran Tukufu iwe ni neno la Mtume au la mtu yoyote yule wa zama za kuteremshwa kwake. Ushahidi wetu juu hili ni Quran yenyewe iliyoshuka baina ya mwaka 611 na 632, tangu kuzaliwa kwa Masihi, Rehema na amani ziwe juu yake, Quran ambayo, aya zake zimetaja na kurudiarudia ukweli wa kisayansi, ukweli ambao haukujulikana na mtu kwa karne nyingi. Kwa maneno ya wazi, ukweli huo haukubali tafsiri tofauti. Pia aya za Quran zina umakini kisayansi unaoafikiana na ufahamu wa kisayansi na wa kilugha ulio sahihi, bila kuacha upenyo wa kukosea wala kupingana.
"Hebu hawaizingatii hii Qur'ani? Na lau kuwa imetoka kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu bila ya shaka wangelikuta ndani yake khitilafu nyingi." Sura [4] An-Nisa 82.
Hii inabainisha kuwa chanzo cha Quran ni Mwenyezi Mungu Aliyemjuzi kupita kiwango cha wanadamu, Aliyeepukana na makosa, upungufu na uongo. Na hakuna mwenye ukamilifu huo wa moja kwa moja, zaidi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu Muumba wa ulimwengu.
Pokeeni baadhi ya hoja ambazo kila moja inathibitisha ukweli wa kuteremshwa Quran kutoka kwa Mola wa viumbe wote kwenda kwa mja wake na Mtume wake Muhammad, Rehema na amani ziwe juu yake, amabaye ni mbora wa viumbe vyote.
3
HOJA
1- KANUNI ZA KISAYANSI:
Kila kitu ulimwenguni kinaenda kwa hisabu na vipimo makini. Hakuna nafasi ya kibahatisha au kutokea ovyoovyo, na huo ndio msingi wa sayansi ya kisasa. Na kuhusiana na hili Quran Tukufu inasema:
"Kwa hakika Sisi tumekiumba kila kitu kwa kipimo." Sura [54] Al-Qamar 49.
"… na akaumba kila kitu na akakikadiria kwa kipimo." Sura [25] Al-Furqan 2.
"….. Na kila kitu kwake ni kwa kipimo." Sura [13] Ar-Ra‘d 8
"Jua na mwezi huenda kwa hisabu." Sura [55] Ar-Rahman 5.
"Na mbingu ameziinua, na ameweka mizani." Sura [55] Ar-Rahman 7.
"Na tumeteremsha kutoka mbinguni maji kwa kiasi…." Sura [23] Al-Mu’minun 18.
"Na ambaye ndiye aliyeteremsha kutoka mbinguni maji kwa kiasi, …. " Sura [43] Az-Zukhruf 11.
"….wala hatukiteremshi ila kwa kipimo maalumu." Sura [15] Al-Hijr 21.
"Na ardhi tumeitandaza na humo tumeweka milima, na tumeotesha kila kitu kwa kiasi chake." Sura [15] Al-Hijr 19.
2- MZUNGUKO WA MAISHA:
Viumbe hai (wanyama na mimea) pamoja na viumbe visvyo hai (madini, vimiminika na gesi) vinafungamana katika mzunguko wa maisha, Atomi na chembechembe zitokazo kwa viumbe vilivyokufa zinabadilika na kuwa hai. Na kutoka katika uhai kuwa maiti bila kukatika. Mfano wa mzunguko wa kubadilisha seli nzima na kuzitumia ndani ya mwanadamu na mnyama. Na mzunguko wa kaboni katika seli za mnyama na mmea. Na mzunguko wa gesi ya dioksidi kaboni na anga. Na mzunguko wa Nitrojeni katika seli hai kwa upande mmoja na upande mwingine mzunguko wa Nitrojeni ya angani na Samadi ya ardhini.
Yote hayo ni ufafanuzi wa yale yaliyofupishwa na aya zifuatazo:
"….Na humtoa hai kutokana na maiti,na humtoa maiti kutokana na aliye hai…." Sura [3] Aal-‘Imran 27.
"….Humtoa aliye hai kutoka maiti, naye ni mtoaji maiti kutokana na aliye hai…." Sura [6] Al-An‘aam 85.
"….Na nani amtoaye hai kutoka maiti, na akamtoa maiti kutoka aliye hai?..... Sura [10] Yunus 31.
4
"Hukitoa kilicho hai kutokana na kilicho kufa, nahukitoa kilicho kufa kutokana na kilicho hai. Na huihuisha ardhi baada ya kufa kwake….". Sura [30] Ar-Rum 19.
3- VIUMBE HAI NA VIUMBE VISIVYO HAI VIPO VIWILI VIWILI (JOZI):
Qurani imerudiarudia kueleza kuwa kila kitu kipo mbea mbili kwa tamko la kukusasanya "kila kitu":
"Na katika kila kitu tumeumba kwa jozi….." Sura [51] Adh-Dhariyat 49.
Kisayansi, maelezo hayo yanaafikiana na ulimwengu wa Wanyama kuanzia mkubwa kabisa hadi kiumbe mdogo kabisa miongoni mwa virusi, bacteria na microbes vyote vipo viwili viwili. Pia yanaafikiana na mimea kwani mimea ina sehemu za kiume na kike, jambo ambalo halikujulikana wakati iliposhuka Quran. Na kuhusiana na hili inasema Quran:
"…. Na katika kila matunda akafanya dume na jike…." Sura [13] Ar-Ra‘d 3.
Pia yanaafikiana na vitu visivyo na uhai: Vitu vinavyounda Atomi kila kimoja kina vigololi viwili. Na anga za juu zilizokubwa mno, kwa sasa inaminiwa kuwa zina mwenza aitwayo "maada kiza"
4- TABIA YA ULIMWENGU:
Ardhi haipo kama vile walivyoidhania watu wa kale – kuwa ndio mhimili wa ulimwengu. Na hii Ardhi haipo vingine ila ni tone katika upana usio na mwisho wa ulimwengu. Zingatia aya ifuatayo:
"Malaika na Roho hupanda kwendea kwake katika siku ambayo kadiri yake ni miaka khamsini elfu!" Sura [70] Al-Ma‘arij 4.
Jambo hili linawekwa wazi na uelezaji wa Quran ikitaja mbingu kabla ya Ardhi katika aya 178 zilizotaja mbingu na ardhi kwa pamoja ukitoa aya nne ambazo muktadha wake ulitaka kinyume cha hivyo. Miongoni mwa aya hizo ni:
"Hatukuziumba mbingu na ardhi wala yaliyomo baina yake ila kwa haki na kwa muda maalumu…." Sura [46] Al-Ahqaf 3.
Ni jambo linalofahamika na kila mtu, kuwa ulimwengu huu mpana umejaa viumbe na aina mbalimbali za maisha tusizozijua. Na juu ya hili, Aya zinasema:
"Na vyote viliomo katika mbingu na katika ardhi, tangu wanyama mpaka Malaika, vinamsujuidia Mwenyezi Mungu…" Sura [16] An-Nahl 49.
"Na katika Ishara zake ni kuumba mbingu na ardhi, na wanyama aliowaeneza…" Sura [42] Ash-Shura 29.
"Na litapulizwa baragumu, wazimie waliomo mbinguni na waliomo katika ardhi…" Sura [39] Az-Zumar 68.
5
"Zinamtakasa zote mbingu saba na ardhi na vyote viliomo ndani yake…" Sura [17] Al-Isra’ 44.
Mwanzo wa Ardhi – na maumbo mengine ya anga za juu zinazoonekana – kutoka katika pande moja kubwa. Na hili linafikiana na Aya ifuatayo:
"Je! Hao walio kufuru hawakuona kwamba mbingu na ardhi zilikuwa zimeambatana, kisha Sisi tukazibabandua?...." Sura [21] Al-Anbiya’ 30.
Pande hilo lilitawanyika na kuwa wingu kubwa la moshi, kama ilivyokuja katika Aya ifuatayo:
"Kisha akazielekea mbingu, na zilikuwa moshi, akaziambia hizo na ardhi: Njooni, kwa khiari au kwa nguvu…." Sura [41] Fussilat 11.
Kisha sehemu za hilo pande zikajikusanya na kuwa nyota, sayari na miezi zikienda katika njia zao katika anga linalopanuka moja kwa moja kama ilivoashiria aya ifuatayo:
"Na mbingu tumezifanya kwa nguvu na uwezo na hakika Sisi bila ya shaka ndio twenye uwezo wa kuzitanua." Sura [51] Adh-Dhariyat 47.
5 - ANGA ZA JUU:
Maumbo yote, kuanzia Nyota, Sayari na Miezi yanatembea mfululizo huko angani katika njia maalumu na kwa speed tofauti tofauti. Kwa kutembea huku kwenye uiano, mwendo wa mstari myofu wa msafiri wa anga za juu wa kukata masafa baina ya eneo anga moja na jingine unakuwa mstari ulioinama. Ndio maana maelezo ya Quran yanatumia neno "al-uruuji" yaani kupinda na kuinama. Katika kuelezea mwendo wa angani:
"Kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mwenye mbingu za daraja. Malaika na Roho hupanda kwendea kwake katika siku ambayo kadiri yake ni miaka khamsini elfu!" Sura [70] Al-Ma‘arij 3 - 4.
"… na yanayoteremka kutoka mbinguni, na yanayopanda humo…" Sura [57] Al-Hadid 4.
Kimsingi – Quran imeashiria uwezekano wa mwanadamu kwenda anga za juu pale atakapopewa na Mungu uwezo wa nguvu na nyenzo za kufanya hivyo, pamoja na kumzindua juu ya yale ambayo huenda akakabiliana nayo huko anga za juu katika hatari za vimondo, meteorites na mionzi ya kuangamiza.
"Enyi makundi ya majini na watu! Mkiweza kupenya kwenye mbingu na ardhi, basi penyeni! Hamtapenya ila kwa kupewa madaraka." Sura [55] Ar-Rahman 33. Kisha:
"Mtapelekewa muwako wa moto na shaba; walahamtashinda…" Sura [55] Ar-Rahman 35.
6
Aya nyinginezo zinathibitisha kuwa mbingu zimejaa vimondo. Vimondo ambavyo imethibitika kuwa, vile vinavyopenya tabaka la anga ya ardhi pekee, kila siku, ni maelfu milioni ya vipande vya ukubwa tofauti tofauti. Na aghlabu ya vipande hivyo vinaunguzwa wakati vikipenya tabaka la anga. Zingatia aya hizi:
"Nasi tulizigusa mbingu, na tukaziona zimejaa walinzi wenye nguvu na vimondo." Sura [72] Al-Jinn 8.
"Isipokuwa mwenye kusikiliza kwa kuibia, naye hufuatwa na kijinga cha moto kinachoonekana." Sura [15] Al-Hijr 18.
Qurani imebainisha kuwa kuna ugumu wa kupumua na kifua kubana unaompata mtu anayepanda anga za juu zilizombali na nguvu za mvutano:
"…Na anayetaka apotee hukifanya kifua chake kina dhiki, kimebana, kama kwamba anapanda mbinguni…" Sura [6] Al-An‘aam 125.
Pia Quran imeashiria kuwa Safari za angani zinaathiri balanzi ya macho na kufanya vitu kuonekana vinatikisika. Na jambo hili walimelishuhudia wanaanga pale walipojaribu kuelea anga za juu wakiwa nje ya chombo cha anga:
"Na lau tungeliwafungulia mlango wa mbingu, wakawa wanapanda, Basi wangeli sema: Macho yetu yamelevywa, bali sisi wenyewe tumerogwa…." Sura [15] Al-Hijr 14 – 15.
6 - UWIANO WA WAKATI:
Katika dunia yetu, wakati unarekebishwa kwa mujibu wa ardhi kujizunguka yenyewe (masiku) na kulizunguka jua (miaka). Na mwezi kuizunguka dunia (miezi na miaka ya mwezi mwandamo), ama miezi ya mfumo wa jua, masaa, dakika na sekunde hivi ni vitu vilivyopewa majina na watu. Yote haya yaliyoko ardhini hayana maana yoyote huko anga za mbali zilizopana, kwani Sayansi ya kisasa imedhihirisha kuwa wakati ni wa uwiano, na hili ndilo lililothibitishwa kwa uwazi kabisa na aya za Quran tangu karne nyingi:
"…Nahakika siku moja kwa Mola wako Mlezi ni kama miaka elfu mnavyo hisabu nyinyi." Sura [22] Al-Hajj 47.
"…. kisha yanapanda kwake kwa siku ambayo kipimo chake ni miaka elfu kwa mnavyohisabu nyinyi." Sura [32] As-Sajdah 5.
"Malaika na Roho hupanda kwendea kwake katika siku ambayo kadiri yake ni miaka khamsini elfu!" Sura [70] Al-Ma‘arij 4.
7 – JUA NA MWEZI:
7
Jua ni nyota inayowaka na kuangaza sayari zilizopo pembezeni mwake, mwanga wake unaakisiwa katika mwezi ambao ni baridi na kutoa nuru ardhini wakati wa usiku. Tofauti hizi za tabia ya kazi za jua na mwezi zimetajwa na aya zifuatazo:
"Na akaufanya mwezi ndani yake uwe nuru, na akalifanya jua kuwa taa." Sura [71] Nuh 16.
"….na akajaalia humo taa na mwezi unaong'ara." Sura [25] Al-Furqan 61.
"Na tukaifanya taa yenye mwanga na joto;" Sura [78] An-Naba 13.
Umbo la mwezi linaloonekana linabadilika badilika mara mwezi mchanga hadi mwezi mpevu kulingana na maweko yake ya kiuwiano (vituo) baina yake na jua na ardhi:
"…na mwezi ukawa na nuru, na akaupimia vituo…" Sura [10] Yunus 5.
"Na mwezi tumeupimia vituo, mpaka unakuwa kama karara kongwe." Sura [36] Ya-Sin 39.
Mwaka wa mfumo wa jua ni siku 365, 2422. huku mwaka wa mfumo wa mwezi ni siku 354, 036. Na kwa hapa tunapata kuwa miaka 300 ya mfumo wa jua ni sawa na miaka 309 ya mfumo wa mwezi nayo ni sawa na siku 109573 bila kupunguza wala kuoingeza. Na katika hili, unadhihirika umakini wa kisayansi ulio mwujiza wa melezo ya Quran katika kisa cha watu wa pangoni:
"Na walikaa katika pango lao miaka mia tatu, na wakazidisha tisa." Sura [18] Al-Kahf 25.
Yaani kubakia kwao ndani ya pango kulichukua miaka 300 ya mfumo wa jua sawa na 309 ya mfumo wa kalenda ya mwezi.
8- MAUMBILE YA ARDHI:
Ardhi ni gololi inayojizungusha na kwa hiyo kuna kupishana usiku na mchana. Na juu ya hili, aya inasema:
"…Hufunika usiku juu ya mchana, na hufunika mchana juu ya usiku…" Sura [39] Az-Zumar 5.
Vilevile, mwendo wa ardhi unadhihirika katika maelezo ya Quran katika Surat Shamsi:
"Naapa kwa jua na mwangaza wake! Na kwa mwezi unapolifuatia! Na kwa mchana unapolidhihirisha! Na kwa usiku unapolifunika!" Sura [91] Ash-Shams 1 – 4.
Yaani kuja kwa mchana (kutokana na kutembea kwa ardhi) ndiko kunakolidhihirisha jua na sio kinyume chake. Na hivyo hivyo, kuja kwa usiku (kutokana na kutembea kwa ardhi) ndiko kunakolificha jua. Kama mwendo unavyodhihiri katika tamko "salakha" (ameuchuna/vua) mchana kutoka katika usiku:
8
"Na usiku ni Ishara kwao. Tunauvua humo mchana..." Sura [36] Ya-Sin 37.
Na kwa "mwendo wa milim" kutokana na kutembea kwa ardhi angani – bila ya sisi kuhisi – kama ilivyotajwa katika aya ifuatayo:
"Na unaiona milima unaidhania imetulia; nayo inakwenda kama mwendo wa mawingu…" Sura [27] An-Naml 88.
9 – MILIMA:
Milima ina kazi kubwa katika kuimarisha gamba la ardhi wakati ardhi ijanapojizunguka yenyewe na inapolizunguka jua kwa vile inavyovipata miongoni mwa kuyeyuka na kutoa mvuke pamoja na kuwepo nyufa na mikunjo, kwa hiyo milima inafanya kazi ya kuituliza ardhi na kuzuia mavolkeno na matetemeko ya ardhi. Na haya yametajwa katika aya za Quran zifuatazo:
"Na kaweka katika ardhi milima ili ardhi isiyumbeyumbe nanyi…" Sura [16] An-Nahl 15. na Sura [31] Luqman 10.
Na tukaweka katika ardhi milima iliyothibiti ili isiwayumbishe..." Sura [21] Al-Anbiya’ 31.
10 - TABAKA LA ANGA:
Ardhi inazungukwa na tabaka mbalimbali za gesi zinazotofautiana kitabia za kifizikia na mjengo wake wa kikemia. Hili limegundulika na sayansi hivi karibuni, huku likiwa limeshaashiriwa na aya zifuatazo:
"Kwani hamwoni jinsi Mwenyezi Mungu alivyoziumba mbingu saba kwa matabaka? Sura [71] Nuh 15.
"Na tukajenga juu yenu saba zenye nguvu?" Sura [78] An-Naba 12.
"Aliyeumba mbingu saba kwa matabaka…" Sura [67] Al-Mulk 3.
Na hizi ni tabaka zilizoungana wala hazina kuachana:
"Je! Hawaangalii mbingu zilizo juu yao! Vipi tulivyozijenga, na tukazipamba. Wala hazina nyufa." Sura [50] Qaf 6.
Pia hizo ni tabaka zinazolindwa na zinalindwa na mvutano (huenda milima nayo ikawa ina kazi katika jambo hili). Vilevile zinalindwa na balanzi madhubuti ya mwenendo na matendo kati ya gesi na ardhi:
"Na tukaifanya mbingu kuwa dari iliyo hifadhiwa…" Sura [21] Al-Anbiya’ 32.
Wala hazitanduliwi ila kuwepo kuharibika kwa mambo na matukio ya siku ya kiama:
9
"Na mbingu itapotanduliwa." Sura [81] At-Takwir 11.
"Mbingu itapochanika." Sura [84] Al-Inshiqaq 1.
"Mbingu itapochanika." Sura [82] Al-Infitar 1.
Na hilo tabaka la anga linatunza hewa ya ardhini – yenye gesi muhimu kwa maisha ya viumbe – ili isipenye na kwenda anga za nje. Na katika tabaka hizo kunapatikana wingi wa mvuke wa maji utokanao na uwanda wa mimie na maji "kisha yanarejea" ardhini. Pia tabaka hizo zinaakisi mionzi ya joto itokayo ardhini na kuigeuza "na kuirejesha" tena ardhini bila kuiacha ijiingize huko. Na vivyo hivyo, yanafanya mawambi yasiyotumia nyaya. Soma:
"Naapa kwa mbingu yenye marejeo!" Sura [86] At-Tariq 11.
11 – MVUA:
Mvuke wa maji unajikusanya angani na kujirundika katika punje punje zilizosheheni umeme. Na hivyo ni kutokana na matendo ya hewa. Matendo amabayo yanatimua hizi punje punje – zikiwa ni vumbi vumbi katika uso wa ardhi au rasharasha za mawimbi ya bahari, au gesi zinazoainishwa na miale ya jua – na kwa hivyo mawimbi yanaanzishwa. Na katika hili, Quran inasema:
"Mwenyezi Mungu ndiye anayezituma pepo zikayatimuamawingu…" Sura [30] Ar-Rum 48.
"Na Mwenyezi Mungu ndiye anayezituma Pepo ziyatimue mawingu…" Sura [35] Faatir 9.
Hapa ni kana kwamba pepo zinapandisha (chavusha) mawingu kwa hizi punje punje. Kama ilivyoelezwa katika maelezo ya Quran:
"Na tunazipeleka pepo za kupandishia, na tunateremsha kutoka mbinguni maji…" Sura [15] Al-Hijr 22.
Baada ya hapo, Pepo zinasukuma mawingu huko angani hadi kunatokea kuvutana kati ya umeme hasi na chanya. Kwa maana "zinaambatana":
"Je! Huoni ya kwamba Mwenyezi Mungu huyasukuma mawingu, kisha huyaambatisha, kisha huyafanya mirundi?..." Sura [24] An-Nur 43.
Huko kuambatana kunapelekea kuundwa kwa mawingu mazito yaliyotayari kuanguka yakiwa ni mvua. Na jambo hilo linaambatana na kutolewa kwa umeme mkali ukiwa katika sura ya Radi na mmeto:
"Yeye ndiye anayekuonyesheni umeme kwa khofu na tamaa, na huyaleta mawingu mazito. Na radi inamtakasa Mwenyezi Mungu kwa kumhimidi…" Sura [13] Ar-Ra‘d 12 – 13.
10
Na mawingu katika kujitanua kwake yapo aina mbili: moja yanajikunjua kiupana (mawingu mtandazo) na ya pili kiwima (mawingu mpandano) ambayo yanajitandaza angani kama milima. Kama inavyodhihiri anagani katika zama zetu za sasa. Maelezo ya Quran yanapambanua kati ya aina mbili hizo kwa kueleza "yabsutwuhu - anayatandaza" kwa aina ya kwanza:
"Mwenyezi Mungu ndiye anayezituma pepo zikayatimua mawingu, kisha akayatandaza mbinguni kama apendavyo…" Sura [30] Ar-Rum 48.
Na maelezo "mipandano" na "milima" kwa ajili ya aina ya pili:
"Je! Huoni ya kwamba Mwenyezi Mungu huyasukuma mawingu, kisha huyaambatisha, kisha huyafanya mirundi? Basi utaona mvua ikitoka kati yake. Na huteremsha kutoka juu kwenye milima ya mawingu mvua ya mawe..." Sura [24] An-Nur 43.
Mawingu mpandano pekee ndiyo yanayoweza kuteremsha mvua ya vipande vya mawe ya barafu kama ilivyoelezwa na hiyo aya ya pili, ambayo imethibitisha vilevile kuwa mvua (wadqa) inaanguka kutoka ndani ya mawingu "kati yake" na siyo kutoka nje yake kwa upande wa chini kama inavyofahamika haraka haraka na watu wa kawaida.
12 - VYANZO VYA MAJI:
Watu wa kale hawakujua kuwa mito inaanzia katika milima mirefu pale mawingu yanapogongana na vilele vya milima vilivyobaridi. Na kuangusha shehena yake ikiwa ni mvua au barafu na kuyeyuka kidogo kidogo na maji yanaanza kutiririka katika mto kuelekea anapopataka Allah kwa muda atakao. Na katika kukutana baina ya milima mirefu na kuanza kwa mito, Quran inasema:
"Na ndani yake tukaweka milima mirefu yenyekuthibiti, na tunakunywesheni maji matamu…" Sura [77] Al-Mursalat 27.
Ama kuhusu maji ya visima na chemchem zinazotoka katika hazina za maji ya ndani ya ardhi, binadamu hakulijua hilo ispokuwa hivi karibuni, alipojua kuwa chanzo cha maji hayo vilevile ni maji ya mvua kutoka mawinguni kisha yanapenya katika tabaka za arfdhi na kujikusanya katika hazina hizo. Huku Quran ikiwa imeshalitaja hilo kwa uwazi na kufupisha:
"Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu ameteremsha maji kutoka mbinguni. Kisha akayapitisha kwenye chemchem katika ardhi…" Sura [39] Az-Zumar 21.
Mwanadamu tangu kuwepo kwake anajua mito ya juu ya aardhi na maji ya ndani ya ardhi kuwa ndio chanzo cha maji matamu kwa ajili ya kunywa yeye, wanyama na kumwagilia mimiea, kama anavyojua kuwa bahari ndio vyanzo vya uchumi wa samaki na vito vya thamani mpaka hatimaye alipokujagundua kuwa katika mito ya maji matamu vilevile kuna aina za vito vya thamani: Kama lulu iliyopo katika mito ya visiwa vya Uingereza, Chekoslavakia na Japani. Na aina mbalimbali ya vito mfano alamasi, yakuti na zarkoni katika mito na matabaka ya mito mabalimbali, ni hili linathibitisha kile kilichothibitishwa na Quran Tukufu:
11
"Na bahari mbili haziwi sawa; haya ni matamu yenye ladha, mazuri kunywa. Na haya ni ya chumvi, machungu. Na kutokana na bahari zote mnakula nyama mpya (isiyo chacha). Na mnatoa mapambo mnayo yavaa…" Sura [35] Faatir 12.
"Anaziendesha bahari mbili zikutane; Baina yao kipo kizuizi, zisiingiliane. Basi ni ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayoikanusha? Katika hizo bahari mbili zinatoka lulu na marijani." Sura [55] Ar-Rahman 19 – 22.
13 - KILIMO:
Wakati wa kumwagilia ardhi iliyolimwa maji yanapenya katika vipenyo vya ardhi na kujipanua hadi juu na chini ya ardhi kunapasuka na kutikisika na maji yanatembea na harakati za mizizi ya mimea na vinyweleo vyake. Harakati za mchwa wanaofanyakazi ya kufungua vipenyo udongoni. Matukio yote haya hayaonekani kwa macho matupu. Ispokuwa yamebainishwa na tafiti na mitazamo yakini ambayo haikuwepo kwa wahenga. Lakini Quran Tukufu imeelezea jambo hilo kam umakini mkubwa
"…Na unaiona ardhi imetulia kimya, lakini tunapoyateremsha maji juu yake husisimka nakututumka, na kumea kila namna ya mimea mizuri." Sura [22] Al-Hajj 5.
Udongo wa kilimo unatofautiana kutoka eneo moja hadi lingine: kimuundo wa kifizikia, kikemia na kibaiolojia. Na katika kufaa kwa kilimo na uzuri wa mazao yake. Hayo yanalingana na yaliyotajwa na aya ifuatayo:
"Na katika ardhi vimo vipande vilivyo karibiana, na zipo bustani za mizabibu, na mimea mingine, na mitende yenye kuchipua kwenye shina moja na isiochipua kwenye shina moja, nayo inatiliwa maji yale yale. Na tunaifanya baadhi yao bora kuliko mengine katika kula…" Sura [13] Ar-Ra‘d 4.
Pia Qurani imeashiria yale yaliyogunduliwa na maarifa ya kisasa ya kuwa Ardhi iliyoinuka ni bora kuliko zisizoinuka:
"… Ni kama mfano wa bustani iliyo mahali pa juu, ikaifikia mvua kubwa na ikaleta mazao yake mardufu…" Sura [2] Al-Baqarah 265.
14 – ULIMWENGU WA WANYAMA:
Tafiti za elimu ya wanyama zimegundua kuwa kuna tofauti kubwa katika falme za wanyama, tofauti ambazo wanazuoni wanazigawanya kama ifuatavyo: Vyeo, vikundi, jamii, aina na kila moja ni jamii yenye kujitegemea, ina mafungamano, desturi na lugha yake kama jamii za kibinadamu, na hii ni kuthibitisha aya ifuatayo:
"Na hapana mnyama katika ardhi, wala ndege anayeruka kwa mbawa zake mbili, ila ni umma kama nyinyi…" Sura [6] Al-An‘aam 38.
12
Mtu anayezingatia mienendo ya wanyama, ndege, samaki na wadudu na namna wanavyotendeana na mazingira yaliyowazunguka, wanavyosaidiana na kugombana anayakinisha ukweli wa aya zifuatazo:
"Aliye umba, na akaweka sawa. Na ambaye amekadiria na akaongoa." Sura [87] Al-A‘la 2 – 3.
"Akasema: Mola wetu Mlezi ni yule aliyekipa kila kitu umbo lake, kisha akakiongoa." Sura [20] Ta-Ha 50.
Vilevile maelezo yaliokuja kuhusiana na nyuki:
"Na Mola wako Mlezi amemfunulia nyuki: Jitengenezee majumba yako katika milima, na katika miti, na katika wanayojenga watu. Kisha kula katika kila matunda, na upite katika njia za Mola wako Mlezi zilizo fanywa nyepesi kuzipita…" Sura [16] An-Nahl 68 – 69.
Maji ni msingi wa maisha kwa kila kiumbe: mnyama na mmea hata vile visivyoonekana ila kwa darubini. Na hili ndilo lililotajwa na Quran tangu karne nyingi:
Na Mwenyezi Mungu ameumba kila kinyama kutokana na maji…" Sura [24] An-Nur 45.
"Na tukajaalia kwa maji kila kilichohai…" Sura [21] Al-Anbiya’ 30.
Quran imeelezea kwa umakini mkubwa mtambo wa kutengeza maziwa kwa wanyama kama ng`ombe na nyati, namna chakula kilichosagwa kinavyotawanywa katika mishipa ya damu, maziwa katika chuchu na mabaki yatolewayo, na hilo lipo katika aya ifuatayo:
"Na hakika katika nyama hoa nyinyi mna mazingatio. Tunakunywesheni katika vile viliomo matumboni mwao, vikatoka baina ya mavi na damu, maziwa safi mazuri kwa wanywao…" Sura [16] An-Nahl 66.
15 - MIMBA:
Aya za Quran zimegusia kuanza kwa mimba na hatua za kuendelea kwake kwa umakini zaidi unaoafikiana na elimu ya viinitete ya kisasa. Mwanzo wa mimba ni seli iliyochanganyika..." Sura [76] Al-Insan 2.
Kijidudu cha manii kimoja tu katika mamilioni ya vijidudu vya manii ndicho kinachofanikiwa kuchavusha yai. Na juu ya kiwango hiki kidogo aya zimekielezea kuwa:
"Kwani hakuwa yeye tone ya manii lilio shushwa." Sura [75] Al-Qiyamah 37.
Na tone kilugha ni: maji kidogo mno. Na kwa sababu hii ni vigumu sana kisayansi kujua mapema jinsia ya mimba kabla ya kuwa wazi alama zake. Na kwa
13
hiyo imesema kweli Quran katika aya hii na aya zilizo kama hii zenye maana hiyo hiyo ambazo ni nyingi:
"Mwenyezi Mungu anajua mimba abebayo kila mwanamke…" Sura [13] Ar-Ra‘d 8.
Mimba inaanza kwa "kuning`inia" kidudu cha manii katika ukuta wa yai, na pale yai linapochavushwa kikawaida linajisukuma kuelekea mji wa mimba pale "litakaponing`inia " na ukuta wa mji wa mimba kwa kutumia seli inayomeng`enya ambayo inamea ndani yake. Jambo ambalo linathibitisha ukweli wa Quran, kwani Quran inataja uumbwaji wa mwanadamu kutokana na pande linaloning`inia katika aya za kwanza kuteremka:
"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu linaloning`inia." Sura [96] Al-‘Alaq 1 – 2.
Aya zifuatazo zimetaja maendeleo ya mimba baada ya hapo na inakuwa kipande cha nyama kilichotafunwa kisichowazi ni kitu gani "hakijaundwa" na baadaye kinaanza kuonesha kidogo kidogo, alama za viungo hadi kinakuwa mchanganyiko wa viungo vilivyotengenezwa na vingine havijatengenezwa, kisha kunatokea seli za Cartilaginous ambazo zinabadilika na kuwa umbo la mifupa, kisha kidogo kidogo mifupa inavishwa viungo:
"…hakika Sisi tulikuumbeni kutokana na udongo, kisha kutokana na manii, kisha kutokana na kipande cha damu ilio gandana, kisha kutokana na kipande cha nyama chenye umbo na kisicho kuwa na umbo…" Sura [22] Al-Hajj 5.
"Kisha tukaiumba tone kuwa damu iliyoganda, na tukaiumba damu kuwa pande la nyama, kisha tukaliumba pande la nyama kuwa mifupa, na mifupa tukaivika nyama. Kisha tukamfanya kiumbe mwengine…" Sura [23] Al-Mu’minun 14.
Mtoto akiwa tumboni – kwa kipindi chote cha kukua kwake – anaogelea katika kimiminika chenye chakula chote anachokihitaji. Na hicho kimiminika kinalindwa na utando imara (utando wa amniotiki). Na hicho kimiminika kinapata chakula kwa njia utando mwingine (utando wa Placenta) utando unaoratibu namna mtoto atakavyopata vitu vya kumnufaisha na kusafisha mabaki kupitia ukuta wa fuko la uzazi ambalo limevishwa utando kama sponji nene (utando poromoka). Hiyo mitando mitatu, imetajwa na aya ifuatayo:
"…Anakuumbeni katika matumbo ya mama zenu, umbo baada ya umbo, katika viza vitatu…" Sura [39] Az-Zumar 6.
16 - KNYONYESHA:
Aya za Quran zimeamrisha kuzingatia ukamilishaji wa kumnyonyesha mtoto kwa muda wa miaka miwili kamili. Na muda huo ndio ulioafikiwa na tiba ya kisasa. Tiba iliyothibitisha umuhimu wa kumnyonyesha mtoto mchanga kwa maziwa ya mama ili kumpatia chanzo "Aydahia" yaani maziwa yenye virutubisho muhimu, yanayonasibiana na maendeleo ya ukuaji wa mtoto, na yenye kukinga na kuzuia
14
maradhi. Pia tafiti zimethibitisha umuhimu wa kuendelea kunyonyesha kwa muda wa miaka miwili, na jambo hilo ndio lililokuja katika aya ifuatayo:
"Na wazazi wanawake wawanyonyeshe watoto wao miaka miwili kaamili kwa anayetaka kutimiza kunyonyesha…" Sura [2] Al-Baqarah 233.
17 - CHAKULA NA AFYA:
Quran tukufu imesisitizia faida za kitabibu kwa kutumia asali ya nyuki:
"…Na kutoka matumbo yao kinatoka kinywaji chenye rangi mbali mbali; ndani yake kina matibabu kwa wanaadamu…" Sura [16] An-Nahl 69.
Utabibu wa kisasa umegundua matumizi mbalimbali yenye faida kubwa katika kutibu, kukinga na kusafisha vidonda kwa kutumia asali.
Hayo yote, Ukiachilia mbali kanuni za kitabibu zinazogundulika siku baada ya siku zinazokubaliana na Quran katika kukataza kula nyamafu, damu, nyama ya nguruwe, na kanuni zinazohimiza kuchinja (yaani kumwaga damu ya mnyama kupitia shingoni) kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu. Pia kukataza uzinzi na ushoga (mapenzi kinyume cha maumbile) na kukataza kufanya mapenzi wakati wa hedhi, na kukataza kutumia pombe na vilevi vingine.
Uongofu wa Mtume (SAW) umeongoza – kwa elimu kutoka katika ufunuo – kufikia katika mambo mengi yanayotumiwa na utabibu wa kisasa ili kuhifadhi afya ya mtu na jamii: sawa katika suala la usafi wa viungo vya mwili – na hii ikiwa ni sehemu ya ibada na sunna – kwa kuoga, kutia udhu, kupiga mswaki, kusafisha pua kwa maji (ndani ya pua), au kula chakula cha kiasi, au kula kwa njia nzuri, kuosha viganja kabla na baada ya kula, kusukutua, usafi wa nguo na makazi, kutumia dawa, kujiepusha na maambukizi, kuweka karantini za kiafya kwa magonjwa ya kuambukiza, kutunza mazingira dhidi ya mabaki (kinyesi, mkojo) ya wanadamu ili kujikinga na vimelea vya magonjwa. Na kujihadhari na ugonjwa kutoka kwa mbwa.
Tutosheke na kuashiria kwa (ufupi) maneno haya bila maelezo. Na yote haya ni sehemu za sheria za Quran na mafundisho ya Mtume (SAW), yaliyolazimishwa na Uislamu kuyafuata.
18 – HISTORIA ASILIA:
Tafiti za mabaki ya kale ndio msingi wa kujua historia ya viumbe hai, na historia za zama za kijiolojia za sayari ya ardhi, mfumo huo unaofuatwa katika tafiti za kisayansi za kisasa – aya ya Quran tayari imeshatoa wito wa kufuatwa:
"Sema: Tembeeni katika ardhi na tazameni jinsi alivyo anzisha uumbaji…" Sura [29] Al-‘Ankabut 20.
15
19 - FIRAUNI NA MUSA:
Baada ya tumbo la ardhi kufukia historia ya Wamisri wa kale, zimepita karne nyingi mpaka kugunduliwa "jiwe rosetta" halafu makaburi ya wafalme, maiti za mafirauni zilizokaushwa. Kwa hivyo zikagundulika siri zilizopita, na mwanadamu akaona namna miili ya mafirauni ilivyosalia ikiwa imekaushwa. Ukiwemo mwili kaushwa wa Umnifataahu: Yule Firauni aliyezama wakati akimfukuza Musa Rehema na amani ziwe juu yake. Pia zikiwemo maiti kaushwa zote za familia ya wafalme wa kumi na mbili, familia iliyokuwepo wakati wa mapambano baina ya wana wa Israeli na wafalme wa Misri. Na mwujiza wa Quran katika suala hili unawakilishwa pale Qurani Tukufu iliposisitiza kubakia kwa mwili wa "Firauni wa Kutoka" ukiwa kamili uliosalimika ili iwe mazingatio kwa kila kizazi kitakachokuja:
"Leo, basi, tutakuokoa kwa mwili wako, ili uwe Ishara kwa ajili ya walionyuma yako…" Sura [10] Yunus 92.
20 - UTABIRI WA KIHISTORIA:
Qurani imetabiri utabiri wa kweli – na Quran isingeweza kusema kweli - kama ingekuwa sio kutoka katika ufunuo wa Mjuzi wa siri: Utabiri wa kwanza ni kuhifadhiwa Quran Tukufu baada ya muda, ijapokuwa imeteremka kwa umma wenye wingi wa wasiojua kusoma na kuandika, nayo ndio kitabu cha pekee cha Mungu kisichobadilishwa wala kupotoshwa wala kupingana katika vifungu vyake kwa upana wa muda na eneo:
"Hakika Sisi ndio tulioteremsha Ukumbusho huu, na hakika Sisi ndio tutaoulinda." Sura [15] Al-Hijr 9.
Pili: kutabiri kuwa wanadamu wa zama zote na maeneo yote, wakiwemo Warabu watu wa lugha ya ufasaha na uwazi, watashindwa kuleta maneno yaliyo sawa na umbuji (ubora wa hali ya juu) wa Quran. Yenye maana na matamko bora kabisa, ukamilifu wa maelezo, muundo bora wa kilugha, uzuri wa midundo na athari zake, Na kwa hakika hadi kufikia sasa watu wote wameshindwa na hili ni kwa ushahidi wa hali halisi ya kihistoria. Na kwa hiyo vifungu vya Quran vinaendelea kuwa ndio aina ya kipekee iliyobora, sio kama mashairi ya wanadamu wala makala zao. Ispokuwa Quran ni "Quran" tu!:
"Au wanasema: Ameizua? Sema: Basi leteni Sura kumi zilizozuliwa mfano wa hii, na waiteni muwawezao badala ya Mwenyezi Mungu, ikiwa mnasema kweli." Sura [11] Hud 13.
"Je! Ndiyo wanasema ameizua? Sema: Hebu leteni sura moja mfano wake na muwaite (kukusaidieni) muwawezao, isipokuwa Mwenyezi Mungu, ikiwa nyinyi mnasema kweli." Sura [10] Yunus 38.
"Na ikiwa mna shaka kwa hayo tuliyomteremshia mja wetu basi leteni sura moja ya mfano wake, na muwaite mashahidi wenu badala ya Mwenyezi Mungu, ikiwa mnasema kweli." Sura [2] Al-Baqarah 23.
16
"Sema: Wangelikusanyika watu na majini ili walete mfano wa hii Qur'ani basi hawaleti mfano wake, hata wakisaidiana wao kwa wao." Sura [17] Al-Isra’ 88.
Quran imetabiri kuwa ndani ya Quran kuna maana na hakika na siri ambazo zilifichikana kwa kizazi cha zama za Ufunuo, mambo amabyo yatagundulika kidogo kidogo:
"Tutawaonyesha Ishara zetu katika upeo wa mbali na katika nafsi zao wenyewe mpaka iwabainikie kwamba haya ni kweli…" Sura [41] Fussilat 53.
"Kila khabari ina kipindi chake. Nanyi mtakuja jua." Sura [6] Al-An‘aam 67.
"…Yeye atakuonyesheni Ishara zake, na mtazijua…" Sura [27] An-Naml 93.
"Na bila ya shaka mtajua khabari zake baada ya muda." Sura [38] Saad 88.
"Bali wameyakanusha wasioyaelewa ilimu yake kabla hayajawajia maelezo yake…" Sura [10] Yunus 39.
Pia Quran imetabiri kukombolewa Makka, huku wito wa kuutangaza Uislamu ukiwa bado upo katika hali dhaifu sana, kiasi cha kuteswa na kuzingirwa na maadui kila pande:
"Hakika aliyekulazimisha kuifuata Qur'ani hapana shaka atakurudisha pahala pa marejeo…" Sura [28] Al-Qasas 85.
"Hakika Mwenyezi Mungu amemtimizia Mtume wake ndoto ya haki. Bila ya shaka nyinyi mtauingia Msikiti Mtakatifu, Inshallah…" Sura [48] Al-Fath 2.
Pia Quran imetabiri ushindi wa Warumi dhidi ya Wafarsi na hiyo ikiwa ni kinyume na matarajio, kwa uthibitisho wa wataalamu wa historia:
"Warumi wameshindwa, Katika nchi iliyo karibu. Nao baada ya kushindwa kwao watashinda, Katika miaka michache…" Sura [30] Ar-Rum 2 – 4.
Pia Quran, hatimaye imetabiri uharibifu wa mazingira – nchi kavu na baharini – kwa mikono ya wanadamu. Huenda isiwe ajabu kutajwa uharibifu wa nchi kavu, ama kutaja uharibifu wa bahari (na bahari kwa lugha ya kiarabu: ni neno linalokusanya bahari na mito) na yale yaliyoikumba bahari kwa sasa miongoni mwa uchafuzi na kuangamiza mazingira ya bahari. Na dunia yote inataabika kwa hali hiyo katika kipindi cha mwishoni mwa karne ya ishirini. Kweli jambo hilo ni mwujiza wa kisayansi na kihistoria na ni jambo ambalo haliwezi kuja ila kutoka kwa Muumba wa ulimwengu Aliye Mjuzi aliyesema kweli pale aliposema:
"Ufisadi umedhihiri bara na baharini kwa iliyoyafanya mikono ya watu…" Sura [30] Ar-Rum 41.
HITIMISHO – KUTULIA NA KUJIULIZA.
17
Mpenzi msomaji - kwa sasa umeshapitia makala hii yenye vifungu vya hoja za kisayansi juu ya ujumbe wa Uislamu, tangu sasa umeshakuwa mwanadamu utakayeulizwa mbele ya Mola wako aliyekuumba ambaye ni Allah Mmoja Peke yake. Natarajia utainasihi nafsi yako katika kipindi cha ukweli, ukijiweka huru na fikra zote zilizotangulia, ili ujue kuwa jambo hili ni muhimu wala sio la mchezo:
"Je! Mlidhani ya kwamba tulikuumbeni bure na ya kwamba nyinyi kwetu hamtarudishwa?" Sura [23] Al-Mu’minun 115.
Kwa hakika ukizisikia hoja unakuwa mtu unayestahiki kuhesabiwa, Jambo ambalo linakutaka uharakishe kufuata wito wa kweli kabla hujapitwa na wakati:
"Wala Mwenyezi Mungu hataiakhirisha nafsi yoyote inapofika ajali yake..." Sura [63] Al-Munafiqun 11.
"(Aambiwe): Kwa hakika ulikuwa umeghafilika na haya; basi leo tumekuondolea pazia lako, na kwa hivyo kuona kwako leo ni kukali." Sura [50] Qaf 22.
Katika kipindi hicho hazitokufaa nguvu zako, uwezo wako, mali yako wala watoto wako:
"Siku ambayo kwamba mali hayatofaa kitu wala wana." Sura [26] Ash-Shu‘ara’ 88.
Wala halitokufaa: kundi (lako), wazazi, au wakuu. Wala hutasameheka kwa kufuata watu kibubusa:
"Walio fuatwa watakapowakataa wale waliowafuata, na hali ya kuwa wamekwishaiona adhabu; na yatakatika mafungamano yao. Na watasema wale waliofuata: Laiti tungeweza kurudi tukawakataa wao kama wanavyotukataa sisi! Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu atakavyowaonyesha vitendo vyao kuwa majuto yao; wala hawatakuwa wenye kutoka Motoni." Sura [2] Al-Baqarah 166 – 167.
"Na wote watahudhuria mbele ya Mwenyezi Mungu. Wanyonge watawaambia walio takabari: Sisi tulikuwa wafwasi wenu; basi hebu hamtuondolei kidogo hivi katika adhabu ya Mwenyezi Mungu? Watasema: Lau Mwenyezi Mungu angelituongoa basi hapana shaka nasi tungelikuongoeni. Ni mamoja kwetu tukipapatika au tukisubiri; hatuna pa kukimbilia." Sura [14] Ibraheem 21.
"Bali wanasema: Hakika sisi tuliwakuta baba zetu wanashika dini makhsusi, basi na sisi tunaongoza nyayo zao. Sura [43] Az-Zukhruf 22.
Mlango wa toba upo wazi, haya tuiendee:
"Sema: Enyi waja wangu walio jidhulumu nafsi zao! Msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote…" Sura [39] Az-Zumar 53.
18
Uislamu ni wito kwa watu wote, katika Uislamu anaingia yoyote atakaye, bila muunganishi kati ya mja na Mola wake. Wala hakuna kuomba ruhusa kutoka kwa mamlaka ya kidini au kiongozi:
"Na hatukukutuma ila kwa watu wote, uwe mbashiri, na mwonyaji…" Sura [34] Saba’ 28.
Mwisho, kumbuka kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:
Hapana kulazimisha katika Dini. Kwani Uwongofu umekwisha pambanuka na upotofu…" Sura [2] Al-Baqarah 256.
Chagua mwenyewe kwa Akili yako, ukitakacho kielekea.