Nakala




Muhammad si baba wa yeyote katika wanaume wenu, bali ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na Mwisho wa Manabii, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.” (Kurani 33: 40)





SignsProphethood1.jpgPindi mtu anapoukubali Uislamu, kuthibitisha upya imani yake, au kuswali moja ya sala tano za kila siku, pia inathibitisha imani kwa Muhammad kama mtume wa Mungu; mtume wa mwisho. Mbali na hayo zaidi ya watu bilioni 1.5 duniani kote wanaamini kwamba maisha ya Mtume Muhammad yanastahili kuigwa na kutamaniwa. Hata hivyo watu wengi wanaukubali uislam bila ya kumjua Mtume Muhammad, rehema na baraka za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. Labda wanachojua ni kwamba alizaliwa na kuishi katika Rasi ya Uarabuni na akapokea neno halisi la Mungu katika muundo wa Kurani. Katika makala mawili yafuatayo tutaangalia maisha matukufu ya Mtume Muhammad, tutajifunza kumjua na kumpenda zaidi. Tutayafikia haya kwa kuangalia ishara za Utume katika maisha yake matukufu.





Katika Kiarabu neno nabii (nabi) limetokana na neno naba lenye maana ya habari. Kwa hivyo tunaafikiana kuwa mtume anaeneza habari za Mungu na ujumbe Wake, kwa maana ya kuwa mabalozi wa Mungu duniani. Shughuli zao ni kufikisha ujumbe wa kumwabudu Mungu Mmoja. Hili linahusu kuwaita watu kwa Mungu, kueleza ujumbe, kuleta habari njema au maonyo na kuongoza mambo ya taifa. Mitume wote walikuwa na shauku la kufikisha ujumbe wa Mungu kwa uaminifu na ukamilifu na hii ilijumuisha nabii wa mwisho, Muhammad. Wakati wa khutba yake ya mwisho, Mtume Muhammad aliuuliza umati mara tatu kama ameufikisha ujumbe huo, na akamwita Mwenyezi Mungu ashuhudie jibu lao, ambalo lilikuwa ni “ndiyo!” ya sauti kali.





Pamoja na msingi wa wito wao kwa Mungu Mmoja, ishara nyingine iliyokubaliwa ya ukweli wa manabii ni jinsi wanavyoishi maisha yao. Simulizi za maisha ya Mtume Muhammad ambazo tumezirithi kutoka kwa watangulizi wetu wema zinaonyesha kwamba Utume wa Muhammad uliongozwa na Mungu tangu mwanzo kabisa. Muda mrefu kabla, Utume wa Muhammad ulikuwa unatayarishwa kuwaongoza wanadamu kwenye njia iliyonyooka na uzoefu wake wa maisha ulimsimamisha katika nafasi nzuri kwa ajili ya shughuli hiyo mzito. Kisha akiwa na umri wa miaka 40 alipopewa Utume, Mungu aliendelea kuunga mkono na kuuthibitisha utume wake. Simulizi zozote za maisha ya Muhammad zimejaa mifano ya tabia yake; alikuwa mwenye rehema, mwenye huruma, mkweli, shujaa, na mkarimu huku akijitahidi kupata malipo ya Akhera. Namna Mtume Muhammad alivyoshughulika na masahaba zake, marafiki zake, maadui zake, wanyama, na hata vitu visivyo na uhai vilionyesha bila shaka kwamba alikuwa akimkumbuka Mwenyezi Mungu.





Kuzaliwa kwa Muhammad kuliambatana na matukio mengi yanayoitwa miujiza na mazungumzo ya matukio ya ajabu bila shaka yalionyesha kama ishara za Utume, hata hivyo, ni lazima tuwe waangalifu katika kuamini moja kwa moja katika matukio hayo ya ajabu. Sio matukio yote yanakubaliwa na waandishi wa wasifu na wanahistoria wote wa historia ya Kiislamu hivyo ingawa yanaonyesha mwanzo wa ajabu na maisha yaliyokusudiwa kuongozwa na Mwenyezi Mungu, yanaweza kupambwa au kutiwa chumvi.





Mazingira mahususi lakini sio ya kipekee yaliuzunguka utoto wa Mtume Muhammad  na haya bila shaka yalikuwa na athari katika tabia yake. Wakati alipokuwa na umri wa miaka minane, alikuwa ameteseka kutokana na kifo cha wazazi wake wote wawili na babu yake kipenzi Abdul Muttalib. Aliachwa chini ya uangalizi wa mjomba wake na msaidizi mkuu Abu Talib. Hivyo hata akiwa mvulana mdogo, tayari alikuwa amepatwa na msukosuko mkubwa wa kihisia na kimwili. Waandishi wengi wa historia ya maisha ya Muhammad na Kurani wanakubali maisha yake yaliyovurugika.





Kwani hakukukuta yatima akakupa makaazi? (Kurani 93:6)





Mjomba wake Muhammad Abu Talib alikuwa masikini na alijitahidi kutunza familia yake, hivyo wakati wa ujana wake, Muhammad alifanya kazi kama mchungaji. Kutokana na kazi hii, alijifunza kuukubali upweke na kukuza sifa kama vile uvumilivu, tahadhari, utunzaji, uongozi, na uwezo wa kuhisi hatari. Uchungaji ni kazi ambayo manabii wote wa Mungu tunaowajua walikuwa nayo kwa pamoja. ‘…Masahaba wakauliza, “Je, ulikuwa mchungaji?” Akajibu, “Hapakuwa na nabii ambaye hakuwa mchungaji."’[1]





Katika ujana wake wakati mwingine Muhammad alisafiri na Abu Talib, akifuatana na misafara hadi kwenye vituo vya biashara. Katika tukio moja, inasemekana alisafiri hadi kaskazini mwa Syria. Wafanyabiashara wakubwa walitambua tabia yake na kumpa jina la utani Al-Amin, yule unayeweza kumwamini. Hata katika ujana wake, alijulikana kuwa mkweli na mwaminifu. Hadithi moja ambayo inakubaliwa na wanazuoni wengi wa Kiislamu na wanahistoria ni simulizi ya moja ya safari za Mtume Muhammad kwenda Syria.





Hadithi inaelezea kuwa mtawa Bahira alitabiri Utume na akamshauri Abu Talib “kumlinda mpwa wake kwa uangalifu”. Kwa mujibu wa mwandishi wa wasifu Ibn Ishaq, wakati msafara aliokuwa akisafiria Mtume Muhammad ukikaribia ukingo wa mji, Bahira aliweza kuona wingu ambalo lilionekana kuwa na kivuli na kumfuata kijana mmoja. Pindi  msafara uliposimama chini ya vivuli vya miti fulani, Bahira “aliona wingu likiufunika mti, na matawi yake yalikuwa yakiinama na kumuinamia mtume wa Mungu hadi alipokuwa kwenye kivuli cha chini yake.” Baada ya Bahira kushuhudia hili alimtazama Muhammad kwa karibu na akamuuliza maswali mengi kuhusu idadi ya tabiri za Kikristo alizozisoma na kuzisikia.





Kijana Muhammad alijitofautisha miongoni mwa watu wake kwa unyenyekevu, tabia zuri, na tabia njema, hivyo haikuwa ajabu kwa masahaba zake kumuona, hata akiwa kijana miaka mingi kabla ya Utume, akiepuka vitendo vya ushirikina na kujiepusha na kunywa pombe, kula nyama iliyochinjwa kwenye madhabahu ya mawe au kuhudhuria sherehe za ibada za masanamu. Pindi alipofikia utu uzima Muhammad alifikiriwa kuwa mtu wa kutegemewa na kuaminiwa zaidi katika jamii ya Makka. Hata wale waliojihusisha na mizozo ya kikabila walikubali uaminifu na uadilifu wa Muhammad.





Maadili ya Muhammad na tabia njema zilikuwepo tangu umri mdogo, na Mungu aliendelea kumuunga mkono na kumuongoza. Alipokuwa na umri wa miaka 40 Muhammad alipewa nyenzo za kubadilisha ulimwengu, nyezo za kuwanufaisha wanadamu wote.





Katika makala ifuatayo, tutaangalia jinsi maisha ya Muhammad yalivyobadilika baada ya Utume na kuhitimisha kuwa si jambo la busara kutoa uthibitisho kwa wale wanaodai kuwa Muhammad alikuwa Mtume wa uongo. Hakudai Utume ili kupata starehe, mali, ukuu, utukufu, au nguvu.Mbali na muujiza mkubwa zaidi aliopewa, Kurani Mtume Muhammad alifanya miujiza mingi ya halisi iliyoshuhudiwa na watu wa zama zake waliofikia mamia, na katika visa fulani maelfu.[1]  Ripoti za miujiza zimetufikia kwa njia ya kuaminika na dhabiti ya uenezaji wa kifanisi katika historia ya ulimwengu. Ni kana kwamba miujiza ilifanywa mbele ya macho yetu. Njia ya upokezaji ndiyo inayotusadikisha kuwa Muhammad kwa hakika alifanya miujiza hii mikubwa kwa usaidizi wa kimungu na, hivyo, tunaweza kumwamini aliposema, ‘Mimi ni Mtume wa Mungu.’





Miujiza mikubwa ya Muhammad ilishuhudiwa na maelfu ya waumini na wenye kutilia shaka, kufuatia aya za Kurani zilifunuliwa zikitaja matukio ya ajabu. Kurani ilifanya baadhi ya miujiza kuwa ya milele kwa kuitia katika fahamu za waumini. Wapinzani wa zamani wangekaa kimya tu wakati aya hizi zilikaririwa. Lau miujiza hii isingetokea, wangechukua muda wa kuichafua na kumsingizia Muhammad. Lakini badala yake, kinyume cha matarajio kilifanyika. Waumini walikua na uhakika zaidi wa ukweli wa Muhammad na Kurani. Ukweli kwamba waumini walikua na nguvu zaidi katika imani yao na kunyamaza kwa wasioamini na kutokataa kutokea kwao ni kukiri kutoka kwa wote wawili kwamba miujiza ilifanyika sawa na Kurani inavyoelezea.





      Katika sehemu hii tutazungumzia baadhi ya miujiza halisi aliyoifanya Muhammad, rehema na baraka za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake.





Miujiza inatokana na Nguvu ya Mungu


      Muujiza ni mojawapo ya mambo ambayo yanaimarisha zaidi madai ya nabii wa Mungu. (nukta inahitajika) Miujiza haipaswi kuwa kiini pekee cha imani, kwani matukio ya kiungu yanaweza pia kutokea kwa kutumia uchawi na ushetani. Ukweli wa utume uko wazi na dhahiri katika ujumbe halisi unaoletwa, kwani Mungu ameweka uwezo, ingawa ni mdogo, kwa wanadamu kutambua ukweli kwa jinsi ulivyo, hasa katika suala la monotheazimu (imani kwamba kuna Mungu mmoja tu)  Lakini ili kuimarisha zaidi hoja ya Utume, Mwenyezi Mungu alifanya miujiza mikononi mwa Mitume wake kuanzia Musa, Yesu hadi Muhammad. Kwa sababu hii, Mungu hakuleta miujiza kwa matakwa ya watu wa Makkah, lakini Mungu Mwenye Busara alimpa Muhammad miujiza Aliyotaka wakati aliouchagua:





“Na walisema: Hatutakuamini mpaka ututimbulie chemchem katika ardhi hii. Au uwe na kitalu cha mitende na mizabibu, na utupitishie mito kati yake ikimiminika. Au utuangushie mbingu vipande vipande kama ulivyo dai; au utuletee Mwenyezi Mungu na Malaika uso kwa uso Au uwe na nyumba ya dhahabu, au upae mbinguni. Wala hatutaamini kupaa kwako mpaka ututeremshie kitabu tukisome. Sema: Subhana Rabbi, Ametakasika Mola wangu Mlezi! Kwani mimi ni nani isipo kuwa ni mwanaadamu na Mtume?’’’ (Kurani 17:90-93)





Jibu lilikuwa:





“Na hapana kinacho tuzuia kupeleka miujiza ila ni kuwa watu wa zamani waliikanusha. Na tuliwapa Wathamudi ngamia jike kuwa ni Ishara iliyo dhaahiri, lakini walidhulumu kwaye. Nasi hatupeleki Ishara ila kwa ajili ya kuhadharisha.” (Kurani 17:59)





Walipotaka kwa nguvu, Mungu kwa hekima yake alijua kwamba hawataamini, kwa hiyo alikataa kuwaonyesha miujiza:





“Na waliapa kwa Mwenyezi Mungu kwa ukomo wa viapo vyao, kuwa ikiwafikia Ishara wataiamini. Sema: Ishara ziko kwa Mwenyezi Mungu. Na nyinyi hamjui kuwa zitapo kuja hawato amini. Nasi twazigeuza nyoyo zao na macho yao. Kama walivyo kuwa hawakuamini mara ya kwanza, tunawaacha katika maasi yao wakitangatanga.’” (Kurani 6:109-110)





Tunakusanya hapa baadhi ya miujiza halisi mikubwa iliyofanywa na Mtume Muhammad.





Akiwa na umri wa miaka 40, Mtume Muhammad alikuwa mfanyabiashara imara na mwanafamilia aliyepewa vipindi vya kutafakari na kujitathmini. Alikuwa ni raia mwenye kuheshimika sana Makka na watu walikuwa na desturi ya kuja kwake ili kusuluhisha mabishano, ushauri, na kuhifadhi vitu vyao vya thamani. Haya yote hata hivyo yalikuwa karibu kubadilika kwa sababu katika moja ya vipindi vyake vya kutengwa na kutafakari alitembelewa na malaika Jibrili na aya za Kurani zilianza kufunuliwa kwake. Kazi yake ilikuwa imeanza; maisha yake hayakuwa yake tena - sasa yalikuwa yamejitolea kueneza neno la Uislamu. 





Labda kwa sasa baadhi ya matukio katika maisha yake yalianza kuwa na maana. Labda aliweza kuona kuwa Mungu alikuwa ameyapanga mambo kwa ajili yake, kwa kuangalia nyuma tunaweza kuona kuwa dalili za Utume zilikuwa zikionekana katika nyanja nyingi na matukio mengi katika maisha yote ya Mtume Muhammad. Kabla ya kazi yake, maisha ya Muhammad yalikuwa mepesi. Alikuwa na ndoa nzuri na yenye furaha, watoto, hakuwa na wasiwasi wa kifedha na bila shaka alizungukwa na marafiki na familia ambayo ilimpenda na kumheshimu.





Kutangaza Utume wake kwa haraka kulimfanya kuwa masikini, mtu aliyetengwa na jamii, na maisha yake yalitishiwa kwa zaidi ya tukio moja. Ukuu, nguvu, mali, na utukufu vilikuwa vitu vya mbali zaidi kuwepo kwenye akili yake. Kwa hakika, tayari alikuwa na vitu hivi, ingawa kwa kiwango kidogo. Hakuwa apate faida yoyote kwa kuutangaza Utume wake pamoja na azma ambazo hazikuwa za ukweli. Mtume Muhammad, familia yake, na wafuasi wake walidhihakiwa, kukashifiwa, na kupigwa kimwili, mtindo wake wa maisha ulibadilika sana na kuwa mbaya zaidi.





Mmoja wa sahaba wa Muhammad, alisema, “Mtume wa Mwenyezi Mungu hakuona mkate uliotengenezwa kwa unga laini tangu Mungu alipomtuma (kama Mtume) hadi alipokufa.”[1] Mwingine amesema kuwa" Mtume alipofariki, hakuacha pesa wala kitu kingine chochote isipokuwa punda wake mweupe, silaha zake na kipande cha ardhi alichokiacha kama sadaka."[2]





Kabla ya  Mtume Muhammad kufa, alikuwa kiongozi wa himaya, iliyokuwa na uwezo wa kupata hazina ya kitaifa lakini aliishi maisha ya kawaida, akishughulika tu na kukamilisha kazi yake na kumwabudu Mungu. Licha ya majukumu yake kama Mtume, mwalimu, mwanasiasa, jenerali, hakimu, na mpatanishi, Muhammad alikuwa akiwakamua mbuzi wake mwenyewe, akitengeneza nguo na viatu vyake, na pia kusaidia kazi za jumla za nyumbani.[3]  Maisha ya Mtume Muhammad yalikuwa ni mfano bora wa utu na ukawaida. Mavazi na mtindo wake wa maisha haukumtofautisha na wafuasi wake. Pindi Mtu alipoingia kwenye mkusanyiko hapakuwa na kitu chochote kuhusu Mtume Muhammad ambacho kilimtofautisha na watu wengine kwenye mkusanyiko huo.





Katika miaka ya mwanzo ya kazi yake, muda mrefu kabla hata ya kuwa na uwezekano wa kufanikiwa, Muhammad alipokea ahadi ya kuvutia kutoka kwa viongozi wa Makka. Wakifikiri kuwa lazima Muhammad anasema madai hii ya Utume kwa ajili ya manufaa ya kibinafsi, kisha mjumbe alimjia na kusema “...Kama unataka pesa, tutakusanya pesa za kukutosha ili uwe tajiri kuliko sisi. Ukitaka uongozi, tutakuchukua wewe kama kiongozi wetu na kamwe tusiamue jambo lolote bila kibali chako. Ukitaka ufalme, tutakutawaza kuwa mfalme juu yetu...”. Kwa mwanadamu yeyote, katika kipindi chochote cha kihistoria, hii itakuwa ni ahadi ngumu sana kukataa; hata hivyo, Muhammad hakuwa na hamu ya kujinufaisha binafsi au kutambuliwa. Ingawa kulikuwa na sharti moja tu la ukarimu huu lilikuwa linakwenda kinyume na kila kitu ambacho Muhammad alikisimamia. Viongozi wa Makka walitarajia akate tamaa na mwito wake wa Uislamu na kuacha kumwabudu Mungu peke yake, bila mshirika yeyote. [4]  Mtume Muhammad alikataa kabisa ahadi hiyo. 





Katika tukio jingine, Abu Talib, ambaye ni ami yake Muhammad  alihofia maisha ya mpwa wake na akamsihi aache kuwaita watu kwenye Uislamu. Tena jibu la Muhammad lilikuwa la maamuzi na la kweli, akasema, “Naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu, Ewe Mpwa wangu!, hata kama wataliweka jua kwenye mkono wangu wa kulia na mwezi katika mkono wangu wa kushoto kwa malipo ya kuacha jambo hili (kuwalingania watu katika kujiunga kwenye Uislamu), sitaacha kamwe mpaka Mwenyezi Mungu aushinde au niangamie nikiutetea.”[5]





Njia nyingi zilichukuliwa na makafiri wa Makka kuchafua tabia ya Muhammad na kudharau ujumbe aliokuwa akijaribu kueneza. Hawakuwa na huruma walipoidharau Kurani yenyewe. Walidai kwa dhati kuwa Kurani haikufunuliwa na Mwenyezi Mungu na kuwa Mohammad aliiandika yeye mwenyewe. Hili lilifanyika ili kuwakatisha tamaa watu kumfuata Muhammad au kuamini madai yake ya kuwa Mtume wa Mungu. Mtume Muhammad hakuandika Kurani. Alikuwa mtu asiye na elimu, asiyejua kusoma wala kuandika kabisa. Hakuweza kujua au hata kukisia baadhi ya ukweli wa kisayansi ambao Kurani inataja kwa urahisi na mara kwa mara.





Zaidi ya hayo, inaleta mantiki kusema kwamba lau kuwa Kurani ingeandikwa na Muhammad angejisifu na kujitaja zaidi. Kurani kwa hakika inawataja Manabii wawili Isa na Musa mara nyingi zaidi kwa majina kuliko inavyomtaja Mtume Muhammad. Kurani pia inamkemea na kumsahihisha Mtume Muhammad. Je, nabii muongo anaweza kujihatarisha kujifanya aonekane kama mtu anayeweza kufanya makosa?





Mtume Muhammad alikuwa mfanyabiashara wa Kiarabu asiye na elimu. Huenda maisha yake hayakuwa ya ajabu isipokuwa kwamba tangu mwanzo wa kuwepo kwake Mungu alikuwa pamoja naye, akimtayarisha kwa ajili ya Utume na kumwandaa kuuongoza ulimwengu wote katika enzi mpya ya ukuaji wa kidini. Muhammad alipokua, alijulikana kuwa mkweli, mwaminifu, muadilifu, mkarimu, na mpole. Pia alijulikana kuwa mtu wa kiroho sana na kwa muda mrefu alikuwa amechukia upotovu wa waziwazi na ibada ya sanamu katika jamii yake.





Tunapoyatazama maisha ya Mtume Muhammad kwa umbali wa muda tunaweza kuona kwa uwazi kwamba maisha yake yalikuwa ya kumtumikia Mwenyezi Mungu, lengo lake pekee lilikuwa kufikisha ujumbe. Uzito wa ujumbe huo ulimlemea sana mabegani mwake na hata kwenye mahubiri yake ya mwisho alikuwa na shaka na kuwataka watu washuhudie kwamba alikuwa ameufikisha ujumbe wa Mungu. Kama Muhammad angetaka madaraka au umaarufu angelikubali ahadi ya kuwa kiongozi wa Makka. Kama angekuwa anatafuta utajiri hangeishi maisha ya kawaida, akifa akiwa hana mali yoyote, tofauti na kiongozi mwingine yeyote mwenye mamlaka. Ukawaida wa maisha ya Mtume Muhammad na hamu yake isiyoyumba ya kueneza ujumbe wa Uislamu ni dalili zenye nguvu za uhalali wa madai yake ya Utume.



Machapisho ya hivi karibuni

UJUMBE KUTOKA KWA MUH ...

UJUMBE KUTOKA KWA MUHUBIRI MUISLAMU KWA MKRISTO

FADHILA YA KUFUNGA SI ...

FADHILA YA KUFUNGA SIKU SITA ZA SHAWAL

Masuala kumi muhimu n ...

Masuala kumi muhimu na mafupi kuhusu mwezi wa Muharram

UJUMBE KWA ALIYEICHOM ...

UJUMBE KWA ALIYEICHOMA KURANI