Kurani nzima hata hivyo ilirekodiwa kwa maandishi wakati wa ufunuo kutoka kwa imla ya Mtume, rehema na baraka za Mungu ziwe juu yake. Ilirekodiwa na baadhi ya masahaba zake, anayejulikana zaidi kati yao akiwa ni Zaid ibn Thabit.[1] Wengine miongoni mwa waandishi wake wakuu walikuwa Ubayy ibn Ka'b, Ibn Mas'ud, Mu'awiyah ibn Abi-Sufyan, Khalid ibn Al-Waleed na Az-Zubayr ibn Al-Awwam.[2] Aya ziliandikwa juu ya ngozi, vipande, mifupa ya bega ya wanyama na mabua ya mitende.[3]
Ukusanyaji wa Kurani kwa namna ya kitabu ulifanyika punde tu baada ya vita vya Yamama (11AH/633 BK), baada ya kifo cha Mtume, wakati wa Ukhalifa wa Abu Bakr. Masahaba wengi wakawa mashahidi katika vita hivyo, na waliobaki wakaogopa kwamba iwapo nakala iliyoandikwa ya Kurani nzima haita tayarishwa, sehemu kubwa za Kurani zingeweza kupotea baada ya kifo cha wale waliokuwa wameihifadhi akilini. Kwa hivyo, kwa pendekezo la Umar kukusanya Kurani kwa namna ya kitabu, Zaid ibn Thabit alifanywa na Abu Bakr kuwa mkuu wa kamati ambayo ingekusanya pamoja rekodi zilizotawanyika za Kurani na kutayarisha msahafu- karatasi za kushikana ambazo zimebeba ufunuo wote .[4] Ili kulinda mkusanyiko kutokana na makosa, kamati hiyo ilikubali tu nyenzo ambazo zimeandikwa mbele ya Mtume mwenyewe, na ambazo zinaweza kuthibitishwa na angalau mashahidi wawili wa kuaminika ambao kwa kweli walikuwa wamesikia Mtume akisoma kifungu kinachohusika[5]. Baada ya kukamilika na kupitishwa kwa kauli moja na Masahaba wa Mtume, majarida haya yalitunzwa na Khalifa Abu Bakr (kifo. 13AH/634 BK), kisha kupitishwa kwa Khalifa Umar (13-23AH/634-644 BK), halafu binti wa Umar na mjane wa Mtume, Hafsah[6].
Khalifa wa tatu Uthman (23AH-35AH/644-656 BK) aliitisha kutoka kwa Hafsah mswada wa Kurani uliokuwa katika utunzaji wake, na kuamuru utengenezaji wa nakala kadhaa zilizoshikana (masaahif, kwa umoja: msahafu). Kazi hii ilikabidhiwa Sahaba Zaid ibn Thabit, Abdullah ibn Az-Zubair, Sa'eed ibn Al-'As, na Abdur-Rahman ibn Al-Harith ibn Hisham[7] .Baada ya kukamilishwa (mnamo 25AH/646 BK), Uthman alirudisha mswada wa awali kwa Hafsah na kupeleka nakala zingine katika majimbo makubwa ya Kiislamu.
Wasomi kadhaa wasio Waislamu ambao wamechunguza kwa kina suala la ukusanyaji na ulinzi wa Kurani pia wameshuhudia ukweli wake. John Burton, mwishoni mwa kazi yake kubwa katika mkusanyiko wa Kurani, anasema kwamba Kurani kama tulivyo nayo leo ni:
“…Nakala ambayo imefika kwetu imo katika namna ambayo iliandaliwa na kupitishwa na Mtume... Tuliyo nayo leo mikononi mwetu ni msahafu wa Muhammad.[8]
Kenneth Cragg anaeleza kuwa uwasilishaji wa Kurani kutoka kwa wakati wa ufunuo hadi leo umetokea katika “mlolongo hai usiovunjika wa ujitoaji.”[9] Schwally anakubali kuwa:
“Kuhusiana na vipande mbalimbali vya ufunuo, tunaweza kuwa na uhakika kwamba maandiko yao yamepitishwa kwa ujumla kama ilivyopatikana katika urithi wa Mtume.”[10]
Uaminifu wa kihistoria wa Kurani unabainika zaidi tukijua kuwa moja kati ya nakala zilizotumwa na Khalifa Uthman bado ipo leo. Iko katika Makavazi ya Jiji la Tashkent huko Uzbekistan, Asia ya Kati.[11] Kwa mujibu wa Mpango wa Kumbukumbu ya Dunia, UNESCO, tawi la Umoja wa Mataifa, 'ni toleo la uhakika, linalojulikana kama Msahafu wa Uthman.’[12]
Nakala pacha ya msahafu ulioko Tashkent inapatikana katika Maktaba ya Chuo Kikuu cha Columbia nchini Marekani.[13] Nakala hii ni ushahidi kwamba maandiko ya Kurani tuliyo nayo leo yanafanana na yale ya wakati wa Mtume na masahaba. Nakala ya msahafu iliyotumwa Syria (iliyonakiliwa kabla ya moto kuharibu Masjid ya Jaami ambapo ilikuwa mnamo mwaka wa 1310AH/1892 BK ) pia ipo katika Makavazi ya Topkapi mjini Istanbul [14], na mswada wa kale ulioandikwa juu ya ngozi ya swara upo kwenye Dar al-Kutub as-Sultaniyyah nchini Misri. Maandishi ya kale zaidi kutoka vipindi vyote vya historia ya Kiislamu yaliyopatikana katika Maktaba ya Kongres huko Washington, Makumbusho ya Chester Beatty huko Dublin (Ireland) na Makumbusho ya London yamefananishwa na yale ya Tashkent, Uturuki na Misri, huku matokeo yakihakikisha kuwa hakuna mabadiliko yoyote katika maandishi kutoka wakati wake wa awali wa uandishi.[15]
Taasisi ya Koranforschung, kwa mfano, katika Chuo Kikuu cha Munich (Ujerumani), ilikusanya zaidi ya nakala 42,000 kamili au isiyo kamili ya kale ya Kurani. Baada ya miaka hamsini ya utafiti, waliripoti kwamba hakukuwa na tofauti kati ya nakala mbalimbali, isipokuwa makosa ya mara kwa mara ya mnakili ambayo ingeweza kuhakikishwa kwa urahisi. Taasisi hii kwa bahati mbaya iliharibiwa na mabomu wakati wa vita vya pili vya Dunia.[16]
Hivyo, kutokana na juhudi za masahaba wa mwanzo, kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, Kurani kama tulivyo nayo leo inasomwa kwa namna ile ile ilivyofunuliwa.. Hili linafanya Kurani kuwa maandiko pekee ya kidini ambayo bado yanahifadhiwa kabisa na kueleweka katika lugha yake ya asili. Hakika, kama Sir William Muir anasema, “Pengine hakuna kitabu kingine duniani ambacho kimesalia kwa karne kumi na mbili (sasa kumi na nne) ikiwa na maandishi safi sana hivyo.”[17]
Ushahidi huo hapo juu unathibitisha ahadi ya Mungu katika Kurani:
“Hakika Sisi ndio tulio teremsha Ukumbusho huu, na hakika Sisi ndio tutao ulinda.” (Kurani 15:9)
Kurani imehifadhiwa kwa namna ya kimdomo na ya kimaandishi kwa jinsi ambayo hakuna kitabu kingine kimehifadhiwa, huku kila namna ikiwa kidhibiti kwa usahihi wa kingine.