Nakala




Mariamu, Mama wa Yesu, ana nafasi ya pekee sana katika Uislamu, na Mungu anamtangaza kuwa mwanamke bora zaidi kati ya wanadamu wote, ambaye alimchagua juu ya wanawake wengine wote kutokana na ucha mungu na kujitolea kwake.





“Na angalia pale Malaika walipo sema: ‘Ewe Maryamu! Kwa hakika Mwenyezi Mungu amekuteuwa, na akakutakasa, na akakutukuza kuliko wanawake wote.Ewe Maryamu! Mnyenyekee Mola Mlezi wako na usujudu na uiname pamoja na wainamao.’” (Kurani 3:42-43)





Pia alifanywa na Mungu kuwa mfano wa kufuata, kama alivyosema:





“Na Mariamu binti wa Imrani (Mwenyezi Mungu amepiga mfano kwa walio amini), aliye linda ubikira wake, na tukampulizia humo kutoka roho yetu, na akayasadiki maneno ya Mola wake Mlezi na Vitabu vyake, na alikuwa miongoni mwa wat'iifu.” (Kurani 66:12)





Hakika alikuwa mwanamke ambaye alifaa kuleta muujiza kama ule wa Yesu, ambaye alizaliwa bila baba. Alijulikana kwa uchamungu wake na usafi wake wa kimwili, na kama ingekuwa tofauti, basi hakuna ambaye angeamini madai yake ya kuzaa huku akiwa amebakia katika hali ya ubikira, imani na ukweli ambao Uislamu unashikilia kuwa ni wa kweli. Asili yake maalumu ilikuwa ule ambao miujiza mingi ilithibitisha kutoka utotoni mwake. Hebu tukumbuke kile ambacho Mungu alifunua kuhusiana na hadithi nzuri ya Mariamu.





Kipindi cha Utoto wa Mariamu


“Hakika Mwenyezi Mungu alimteuwa Adam na Nuhu na ukoo wa Ibrahim na ukoo wa Imran juu ya walimwengu wote.  Ni wazao wao kwa wao; na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia na Mwenye kujua. Alipo sema mke wa Imran: Mola wangu Mlezi! Nimekuwekea nadhiri kilichomo tumboni mwangu kuwa wakfu; basi nikubalie. Hakika Wewe ndiye Mwenye kusikia na Mwenye kujua.” (Kurani 3:33-35)





Mariamu alizaliwa kwa Imrani na mkewe Hannah ambaye alikuwa wa ukoo wa Daudi, hivyo alitoka katika familia ya Manabii, kuanzia Ibrahimu, Nuhu, hadi Adam, Amani na Baraka za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao wote. Kama ilivyotajwa katika mstari huo, alizaliwa kwa familia iliyochaguliwa ya Imrani, ambaye alizaliwa katika familia iliyochaguliwa ya Ibrahimu, ambaye pia alizaliwa katika familia iliyochaguliwa. Hannah alikuwa mwanamke tasa ambaye alitamani kupata mtoto, na aliweka nadhiri kwa Mungu kwamba, ikiwa angempa mtoto, atamweka wakfu kwa huduma yake Hekaluni. Mungu akajibu maombi yake, naye akapata mimba ya mtoto. Alipojifungua, alihuzunika, kwani mtoto wake alikuwa wa kike, na kwa kawaida wanaume walikuwa wakipewa huduma kwa Bait-ul-Maqdis.





“Basi alipo mzaa alisema: ‘Mola wangu Mlezi! Nimemzaa mwanamke... Na mwanamume si sawa na mwanamke.”





Alipoonyesha huzuni yake, Mungu alimkemea akisema:





“…Na Mwenyezi Mungu anajua sana aliye mzaa …” (Kurani 3:36)





…kwani Mungu alimchagua binti yake, Mariamu, kuwa mama wa moja ya miujiza mikuu ya uumbaji: kuzaliwa kwa Yesu na bikira, rehema na baraka za Mungu ziwe juu yake. Hannah akamuita mtoto wake Mariamu (Maryam kwa Kiarabu) na akamwomba Mungu amlinde yeye na mtoto wake kutoka kwa Shetani:





“…Na mimi nimemwita Maryamu. Nami namkinga kwako, yeye na uzao wake, uwalinde na Shet'ani aliye laaniwa.” (Kurani 3:36)





Hakika Mungu aliikubali dua yake hii, na akampa Mariamu na mtoto wake atakayekuja hivi karibuni, Yesu, sifa maalumu - ambayo hakupewa yeyote kabla wala baada yake; hakuna hata mmoja wao aliyepatwa na mguso wa Shetani wakati wa kuzaliwa. Amesema Mtume Muhammad rehema na amani ziwe juu yake:





“Hakuna azaliwaye ambaye Shetani huwagusa katika kuzaliwa kwao, na hutoka huku akipiga kelele, isipo kuwa Maryamu na mwanawe (Yesu). (Ahmed)





Hapa, tunaweza kuona mara moja mfanano kati ya simulizi hii na nadharia ya Kikristo ya “Mimba Imara” ya Mariamu na Yesu, ingawa kuna tofauti kubwa kati ya hizo mbili. Uislamu hauenezi nadharia ya ‘dhambi ya asili’, na kwa hiyo haukubaliani na tafsiri hii ya jinsi walivyokuwa huru kutokana na mguso wa Shetani, bali kwamba hii ilikuwa ni neema iliyotolewa na Mungu kwa Mariamu na mwanawe Yesu. Akiwa kama manabii wengine, Yesu alilindwa asitende dhambi nzito. Ama Maryamu, hata tukichukua msimamo kuwa hakuwa nabii wa kike, lakini alipata ulinzi na mwongozo wa Mwenyezi Mungu ambao huwapa waumini wema.





“Tena Mola wake Mlezi akampokea kwa mapokeo mema na akamkuza makuzo mema, na akamfanya Zakariya awe mlezi wake.” (Kurani 3:37)





Baada ya kuzaliwa kwa Maryamu, mama yake Hannah alimpeleka Bait-ul-Maqdis na akamtoa kwa wale waliokuwa msikitini ili akue chini ya malezi yao. Wakijua fahari na uchamungu wa familia yao, waligombana ni nani angekuwa na heshima ya kumlea. Walikubaliana kupiga kura, na hakuwa mwingine ila nabii Zakaria aliyechaguliwa. Ilikuwa chini ya uangalizi wake na malezi ambayo alilelewa.





Miujiza katika Uwepo Wake na Kutembelewa na Malaika


Mariamu alipoanza kukua, hata nabii Zakaria aliona sifa maalumu za Mariamu, kutokana na miujiza mbalimbali iliyotokea mbele yake. Mary alipokuwa akikua, alipewa chumba cha faragha ndani ya msikiti ambapo angeweza kujitolea kwa ajili ya ibada ya Mungu. Wakati wowote Zakaria alipoingia chumbani ili kuona mahitaji yake, alikuta matunda mengi mbele yake, na sio kipindi cha msimu wake.





“Kila mara Zakariya alipo ingia chumbani kwake alimkuta na vyakula. Basi alimwambia: Ewe Maryamu! Unavipata wapi hivi? Naye akasema: Hivi vinatoka kwa Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye bila ya hisabu.” (Kurani 3:37)





Alitembelewa na malaika zaidi ya tukio moja. Mungu anatuambia kwamba malaika walimtembelea na kumjulisha juu ya hadhi yake ya na sifa kati ya wanadamu:





“Na angalia pale Malaika walipo sema: Ewe Maryamu! Kwa hakika Mwenyezi Mungu amekuteuwa, na akakutakasa (kutokana na ibada yako), na akakutukuza kuliko wanawake wote (kwa kukufanya kuwa mama wa nabii Yesu).  ‘Ewe Maryamu! Mnyenyekee Mola Mlezi wako na usujudu na uiname pamoja na wainamao.’” (Kurani 3:42-43)





Kwa sababu ya kutembelewa na malaika na kuchaguliwa kwake juu ya wanawake wengine, wengine wameshikilia kuwa Mariamu alikuwa nabii wa kike. Hata kama hakuwa hivyo, ambalo ni suala la mjadala, Uislamu bado unamwona kuwa na hadhi ya juu kabisa miongoni mwa wanawake wote kutokana na ucha mungu na kujitolea kwake, na kutokana na kuchaguliwa kwake kwa ajili ya kuzaliwa kwa Yesu kwa kimiujiza.Inaweza kuwashangaza watu wengi kujua ya kwamba Maryamu ni mmoja wa wanawake waliotukuzwa na kuheshimiwa sana katika Uislamu na kwamba Kurani vile vile imempatia yeye umuhimu mkubwa sana. Maryam ni jina la sura ya 19 ya Kurani, na Sura ya 3 ni Al Imran, iliyopewa jina la familia yake. Uislamu umeipatia hadhi kubwa sana familia yote ya Imran. Kurani inatuambia kuwa:





“Hakika Mwenyezi Mungu alimteuwa Adam na Nuhu na ukoo wa Ibrahim na ukoo wa Imran juu ya walimwengu wote.” (Kurani 3:33)





Mungu alimchagua Adamu na Nuhu kibinafsi, lakini alizichagua familia za Ibrahim na Imrani.





“Ni wazao wao kwa wao; na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia na Mwenye kujua.” (Kurani 3:34) 





Familia ya Imran inatokana na ukoo wa Ibrahim, familia ya Ibrahim wanatokana na ukoo wa Nuhu na Nuhu anatokana na ukoo wa Adam. Familia ya Imran pia inajumuisha watu wengi wanaojulikana na kuheshimiwa katika mila za Kikristo - Mitume Zakaria na Yohana (anayejulikana kama Mbatizaji), Mtume na Mjumbe Yesu na mamake, Maryamu.





Mwenyezi Mungu alimchagua Maryamu kuliko wanawake wote ulimwenguni. Alisema:





“Na angalia pale Malaika walipo sema: Ewe Maryamu! Kwa hakika Mwenyezi Mungu amekuteuwa, na akakutakasa, na akakutukuza kuliko wanawake wote.’” (Kurani 3:42)





Amesema Ali bin Abu Talib:





“Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu akisema yakuwa Maryamu, binti ya Imran alikuwa bora kati ya wanawake.” (Saheeh Al-Bukhari)





 Kwa Kiarabu jina la Maryamu linamaanisha mjakazi wa Mwenyezi Mungu, na kama tutakavyoona, Maryamu, mamake Yesu, alitolewa kumtumikia Mwenyezi Mungu hata kabla hajazaliwa.





Kuzaliwa kwa Maryamu


Biblia haina maelezo yoyote kuhusu kuzaliwa kwa Maryamu; hata hivyo, Kurani inatujulisha kwamba mke wa Imran alitoa wakfu mtoto wake ambaye hajazaliwa ili kumtumikia Mwenyezi Mungu. Mamake Maryamu, ambaye ni mke wa Imran, alijulikana kama Hana[1]. Aliyekuwa dada ya mke wa Mtume Zakaria. Hana na mumewe Imran walikuwa wameamini kuwa kamwe hawakujaaliwa kupata watoto, lakini siku moja Hana aliomba dua ya dhati kwa kuyenyekea kwa Mwenyezi Mungu abarikiwe mtoto, na kuweka nadhiri kwamba mtoto wake angetumika katika Nyumba ya Mwenyezi Mungu huko Yerusalemu. Mwenyezi Mungu alisikia maombi ya Hana na kumjaaliya kushika ujauzito. Hana alipotambua habari hizo tukufu alinyenyekea kwa Mwenyezi Mungu na kusema:





“Alipo sema mke wa Imran: Mola wangu Mlezi! Nimekuwekea nadhiri kilichomo tumboni mwangu kuwa wakfu; basi nikubalie. Hakika Wewe ndiye Mwenye kusikia na Mwenye kujua..” (Kurani 3:35)





Kuna mafunzo ya kujifunza kutokana na nadhiri ya Hana kwa Mwenyezi Mungu, mojawapo ikiwa ni utunzaji wa elimu ya kidini ya watoto wetu. Hana hakuwa na fikira ya ulimwengu huu, bali, alikuwa akijaribu kuhakikisha kuwa mtoto wake alikuwa karibu na Mwenyezi Mungu na vile vile katika ibada zake. Watu wema hawa wateule wa Mwenyezi Mungu, kama vile familia ya Imran, ni wazazi ambao tunapaswa kuwaiga. Mwenyezi Mungu anasema mara nyingi katika Kurani kwamba Yeye ndiye anayetupatia riziki, na anatuonya tujiepushe sisi pamoja na familia zetu kutokana na moto wa Jehanamu.





Katika dua yake, Hana aliomba mtoto wake awe huru kutokana na shughuli zote za kikazi duniani. Kwa kuahidi kwamba mtoto wake atakuwa mtumwa wa Mwenyezi Mungu, Hana alikuwa akimhakikishia mtoto wake uhuru . Uhuru ni aina ya maisha ambayo kila mwanadamu anajitahidi kupata, lakini Hana alifahamu ya kwamba uhuru wa kweli unatokana na utiifu kamili kwa Mwenyezi Mungu.  Chanzo chake cha kutamani kupata mtoto wake ambaye hakuwa amezaliwa kilisababishwa na hili.  Hana alitaka mtoto wake awe mtu huru, ambaye hatokuwa mtumwa wa mtu yeyote ama mwenye matamanio, ila atakuwa mtumwa wa Mwenyezi Mungu tu. Baada ya muda, Hana alijifungua mtoto wa kike, na vile vile tena akanyenyekea kwa Mwenyezi Mungu katika sala na akasema;





 “‘Basi alipo mzaa alisema: Mola wangu Mlezi! Nimemzaa mwanamke - na Mwenyezi Mungu anajua sana aliye mzaa- Na mwanamume si sawa na mwanamke. Na mimi nimemwita Maryamu. Nami namkinga kwako, yeye na uzao wake, uwalinde na Shet'ani aliye laaniwa.” (Kurani 3:36)





Hana alimwita mtoto wake Maryamu. Kwa kuzingatia nadhiri yake kwa Mwenyezi Mungu, Hana alijipata akikabiliwa na hali ngumu. Haikuwa desturi ya wanawake kuhudumu katika Nyumba ya Maombi. Imran, babake Maryamu, alikuwa amefariki kabla ya kuzaliwa, kwa hivyo Hana alimwendea shemeji yake, Zakaria. ambaye alimfariji Hana kwa kumsaidia kuelewa hilo Mwenyezi Mungu alijua kuwa amejifungua msichana. Mtoto huyu wa kike, Maryamu, alitokana na uumbaji bora zaidi. Mtume Mohammad alitaja[2]  kwamba kila mtoto anapozaliwa Shetani humchoma na hivyo husababisha mtoto kulia kwa sauti kubwa. Hii ni ishara ya uhasama mkubwa baina ya wanadamu na Shetani; hata hivyo kulikuwa na tofauti mbili ya sheria hii. Shetani hakumpiga Maryamu vile vile na mwanawe Yesu[3], kutokana na dua ya mamake Maryamu.





Wakati rasmi ulipofika wa Maryamu kwenda kwenye Nyumba ya Maombi, kila mtu alitaka fursa ya kumtunza binti huyu wa Imran aliyekuwa mcha Mungu. Kama ilivyokuwa desturi ya wakati huo, wanaume hao walijaaliwa fadhila nyingi, na Mungu alihakikisha kuwa mlezi wake alikuwa Mtume Zakaria.





“Tena Mola wake Mlezi akampokea kwa mapokeo mema na akamkuza makuzo mema, na akamfanya Zakariya awe mlezi wake.” (Kurani 3:37)





Mtume Zakaria alihudumu katika Nyumba ya Mwenyezi Mungu na alikuwa mtu mwenye hekima na maarifa na aliyejitolea kufundisha.  Alikuwa na chumba kilichojengwa maalum kwa ajili ya Maryamu, ili aweze kumwabudu Mwenyezi Mungu na kufanya kazi zake za kila siku faraghani. Kama mlezi wake,Mtume Zakaria alimtembelea Maryamu kila siku, na siku moja alishangaa kuona matunda mabichi kwenye chumba chake. Inasemekana kwamba wakati wa majira ya baridi kali angekuwa na matunda mapya ya kiangazi na wakati wa kiangazi angekuwa na matunda mapya ya majira ya baridi kali.[4]  Mtume Zakaria alitaka kujua jinsi tunda lilivyofika pale, na Maryamu akamjibu, hakika ni Mwenyezi Mungu ndiye aliyempa riziki. Alisema:





“Hivi vinatoka kwa Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye bila ya hisabu.” (Kurani 3:37)





Fadhila za Maryamu kwa Mwenyezi Mungu wakati huo haukuwa na kifani, lakini imani yake ilikuwa karibu kujaribiwa





Aliyeheshimiwa na kupendwa na Waislamu wote na anayejulikana kama mwanamke mchamungu na msalihina, Maryamu, mamake Yesu alichaguliwa juu ya wanawake wote. Uislamu unakataa wazo la Kikristo kwamba Yesu ni sehemu ya utatu kuwa yeye ni Mungu, na unakataa kwa dhati kwamba Yesu ama mamake, Maryamu, wanastahili kuabudiwa. Kurani inatamka bayana kwamba hakuna mungu ila Mwenyezi Mungu.





“Huyo ndiye Allah, Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wenu, hapana mungu ila Yeye, Muumba wa kila kitu. Basi muabuduni Yeye tu. Naye ni Mtegemewa wa kila kitu...” (Kurani 6:102)





Waislamu wanatakiwa, hata hivyo, kuwaamini na kuwapenda Mitume wote, akiwa ni pamoja na Mtume Yesu, ambaye ana nafasi maalum kwenye kanuni za imani za Kiislamu. Mamake, Maryamu, ana mahali pa heshima. Akiwa msichana, Maryamu alikwenda katika Nyumba ya Maombi huko Yerusalemu, maisha yake yote akiwa alijitolea kwa sala na ibada ya Mungu.





Maryamu Anapashwa Habari za Yesu


Wakati amejitenga na kila mtu, mtu mmoja alijitokeza mbele ya Maryamu. Mwenyezi Mungu alisema:





“Na akaweka pazia kujikinga nao. Tukampelekea Roho wetu, akajifananisha kwake sawa na mtu..” (Kurani 19:17)





Maryamu aliingiwa na hofu na kujaribu kukimbia. Alimwomba Mwenyezi Mungu akisema:





“(Maryamu) akasema: Hakika mimi najikinga kwa Mwingi wa Rehema aniepushe nawe, ukiwa ni mchamungu..”  (Malaika) akasema: Hakika mimi ni mwenye kutumwa na Mola wako Mlezi ili nikubashirie tunu ya mwana aliye takasika..” (Kurani 19:18-19)





Maryamu alistaajabishwa na kutatanishwa na maneno hayo. Hakuwa ameolewa, bali alikuwa bikira aliyejisitiri na kujilinda. Aliuliza kwa mshangao:





“‘Maryamu akasema: Mola wangu Mlezi! Vipi nitampata mwana na hali hajanigusa mwanaadamu? Mwenyezi Mungu akasema: Ndivyo vivyo hivyo, Mwenyezi Mungu huumba apendacho. Anapo hukumu jambo, huliambia: Kuwa! Likawa.” (Kurani 3:47)





Mwenyezi Mungu alimuumba Adam kwa vumbi la ardhi, bila mama wala baba. Alimuumba Hawa kutokana na ubavu wa Adam; na Yesu aliuumbwa bila ya baba, bali alikuwa na mama, Bikira Maryamu mchamungu. Mwenyezi Mungu, ambaye ni kauli ya lazima pindi anaposema ‘kitu Kiwe’ ili kukipatia uhai, alipuliza roho ya Yesu ndani ya tumbo la Maryamu kupitia Malaika Gabrieli.





“na tukampulizia humo[1] aliye linda ubikira wake,  kutoka roho yetu, na akayasadiki maneno ya Mola wake Mlezi...” (Kurani 66:12)





Ingawa katika Kurani na Biblia hadithi za Maryamu zina vipengele vingi vinavyofanana, maoni ambayo Maryamu alikuwa ameposwa au kuolewa yanakataliwa kabisa na Uislamu. Muda ulipita, na Maryamu aliogopa kusemwa na watu waliokuwa karibu naye. Aliwaza jinsi ya kwamba  watamuamini kuwa hakuna mwanaume aliyemgusa. Wanazuoni wengi katika Uislamu wanakubali kwamba muda wa ujauzito wa Maryamu ulikuwa wa kawaida.[2]  Kisha, wakati ulipowadia wa yeye kujifungua, Maryamu aliamua kuondoka Yerusalemu, na kusafiri kuelekea mjini Bethlehemu. Ingawa Maryamu aliyakumbuka maneno ya Mwenyezi Mungu, na kwa kuwa imani yake ilikuwa yenye nguvu na thabiti, msichana huyo alikuwa na hofu na wasiwasi. Lakini malaika JibriliKadhalikaz alimpatia hakikisho:





“Na pale Malaika walipo sema: Ewe Maryamu! Hakika Mwenyezi Mungu anakubashiria (mwana) kwa neno litokalo kwake. Jina lake ni Masihi Isa mwana wa Maryamu, mwenye hishima katika dunia na Akhera, na miongoni mwa walio karibishwa (kwa Mwenyezi Mungu).” (Kurani 3:45)





Kuzaliwa kwa Yesu


Uchungu wa kujifungua ulimfikisha kwenye mti wa mtende na akalikumbatia shina la mtende na kuendelea kulia kwa uchungu:





“Laiti ningeli kufa kabla ya haya, na nikawa niliye sahaulika kabisa!” (Kurani 19:23)





Maryamu alijifungua mtoto wake papo hapo, chini ya mti wa tende. Alikuwa amechoka baada ya kujifungua, na kujawa na dhiki na hofu, lakini hata hivyo alisikia sauti ikimuita. .





“ Usihuzunike! Hakika Mola wako Mlezi amejaalia chini yako kijito kidogo cha maji; Na litikise kwako hilo shina la mtende, utakuangushia tende nzuri zilizo mbivu.Basi kula, na kunywa, na litue jicho lako...” (Kurani 19:24)





Mungu alimpa Maryamu maji, kijito kilitokea ghafla chini ya mahali alipokuwa ameketi. Kadhalika, alimpa chakula; kile alichotakiwa kufanya ni kutikisa shina la mti wa tende. Maryamu aliogopa na alijawa na hofu; alijihisi dhaifu sana baada ya kujifungua, kwa hiyo hakuna na nguvu ya kutikisa shina kubwa la mtende? Lakini Mwenyezi Mungu aliendelea kumpa Maryamu riziki. 





Tukio lililofuata kwa hakika lilikuwa la muujiza mwingine, na kama wanadamu tunajifunza somo kubwa kutokana na hili. Maryamu hakuhitaji kutikisa mti wa tende, jambo ambalo lisingewezekana; ilibidi atie juhudi tu. Alipojaribu kufuata amri ya Mwenyezi Mungu, tende mbivu zilianguka kutoka kwenye mti na Mwenyezi Mungu akamwambia Maryamu: “…basi kula, na kunywa, na litue jicho lako.” (Kurani 19:26)





 Sasa ilimbidi Maryamu amchukue mtoto wake mchanga na kuikabili familia yake. Bila shaka aliogopa, na Mwenyezi Mungu alijua hili vizuri. Hivyo alimwagiza anyamaze kimya. Haingewezekana kwa Maryamu kueleza jinsi ambavyo ghafla amekuwa mama wa mtoto mchanga. Kwa kuwa alikuwa hajaolewa, watu wake hawakuamini maelezo yake. Mungu alisema:





“Basi kula, na kunywa, na litue jicho lako. Na pindi ukimwona mtu yeyote basi sema: Hakika mimi nimeweka nadhiri kwa Mwenyezi Mungu ya kufunga; kwa hivyo leo sitasema na mtu.’” (Kurani 19:26)





Maryamu alifika  kwa watu wake akiwa amembeba mtoto, na hapo hapo wakaanza kumshutumu; wakasema, “Umefanya aibu gani? Umetoka katika familia nzuri, na wazazi wako walikuwa wachamungu.”





Kama vile Mungu alivyokuwa amemwagiza, Maryamu hakuzungumza, alinyoosha kidole tu kwa mtoto aliyekuwa mikononi mwake. Kisha Yesu, mwana wa Maryamu akasema. Kama mtoto mchanga, Yesu, Mtume wa Mungu alifanya muujiza wake wa kwanza. Kwa idhini ya Mwenyezi Mungu alisema:





“Akasema: Hakika mimi ni mtumwa wa Mwenyezi Mungu, amenipa Kitabu na amenifanya Nabii; Na amenijaalia ni mwenye kubarikiwa popote pale niwapo, Na ameniusia Swala na Zaka maadamu ni hai, na nimtendee wema mama yangu, wala hakunifanya niwe jeuri, mwovu.  Na amani iko juu yangu siku niliyo zaliwa, na siku nitakayo kufa, na siku nitakayo fufuliwa kuwa hai!” (Kurani 19:30-34)





Maryamu  ametajwa katika Kurani (5:75) kama siddqa (mkweli) lakini neno la Kiarabu siddiqa linamaanisha maana zaidi ya kusema ukweli . Lina maana ya kwamba mtu amefikia kiwango cha juu sana cha uadilifu. Pia lina maana kwamba mtu ni mkweli, si tu na yeye mwenyewe na wale walio karibu nao, bali  pia kwa Mungu. Maryamu alikuwa ni mwanamke aliyetimiza agano lake na Mwenyezi Mungu, ambaye alimuabudu kwa utiifu. Alikuwa mchamungu, aliyejisitiri, na msalihina; mwanamke aliyechaguliwa juu ya wanawake wengine wote kuwa mamake Yesu alikuwa ni Maryamu binti Imran.



Machapisho ya hivi karibuni

Uislamu Ni dini ya ma ...

Uislamu Ni dini ya maumbile na akili na furaha

UJUMBE KUTOKA KWA MUH ...

UJUMBE KUTOKA KWA MUHUBIRI MUISLAMU KWA MKRISTO

FADHILA YA KUFUNGA SI ...

FADHILA YA KUFUNGA SIKU SITA ZA SHAWAL