Nakala

Leo, watu wengi kote ulimwenguni wanautafuta ukweli; wanatafuta maana halisi katika maisha yao, na wanastaajabia maisha yanahusu nini hasa. Wanaume kwa wanawake huuliza swali, kwa nini nipo hapa? Katikati ya mateso na maumivu, wanadamu huomba kwa sauti ndogo au kubwa faraja, au kueleweka. Mara nyingi katikati ya starehe, mtu hutafuta kuelewa chanzo cha furaha hiyo. Wakati mwingine watu hutafakari kuukubali Uislamu kuwa dini yao ya kweli lakini hupambana na vizuizi.





Katika nyakati za furaha zaidi maishani au nyakati za dhiki zaidi, kimaumbile mtu hutafuta njia za kujikurubisha kwa Kiumbe Mkuu, kwa Mwenyezi Mungu. Hata wale ambao hujichukulia kuwa wao ni wakanamungu au wasioamini walipitia hatua fulani katika maisha yao kuhisi hisia ya kimaumbile (fitra) ya kuwa sehemu ya mpango mkuu.





Dini ya Uislamu imejengwa katika imani moja kuu ya msingi, kwamba kuna Mungu Mmoja. Yeye peke yake ndiye Mlezi Mwenye Kuruzuku na Muumba wa Ulimwengu. Yeye hana washirika, watoto, au wasaidizi. Yeye ndiye Mwingi wa Rehema, Mwenye Hekima zaidi na Mwadilifu zaidi. Yeye ndiye Mwenye Kusikia kila kitu, Mwenye Kuona kila kitu, na Mjuzi wa Kila kitu. Yeye ndiye wa Kwanza, Yeye ndiye wa Mwisho.





Ni faraja kufikiria kwamba majaribu yetu, dhiki zetu, na ushindi wetu katika maisha haya sio matendo nasibu ya ulimwengu mbaya usiopangwa. Imani ya Mungu, kuamini Mungu Mmoja, Muumba, na Mlezi Mwenye Kuruzuku vyote vinavyoishi ni haki ya kimsingi. Kujua kwa hakika kuwa uwepo wetu ni sehemu ya ulimwengu uliopangwa vizuri na kwamba maisha yataendelea kama yalivyopangwa ni dhana inayoleta utulivu na amani.





Uislamu ni dini inayoutazama uhai na kukumbusha kuwa ulimwengu huu ni mahali pa kuishi kwa muda mfupi na sababu yetu ya kuumbwa ni kumuabudu Mungu. Kauli hii inakaa kueleweka kiurahisi au sio? Itafahamika hivyo iwapo utakubali kuwa Mwenyezi Mungu ni Mmoja, na umwabudu Yeye ndipo kutapatikana amani na utulivu. Mwanadamu yeyote anaweza kuwa na ufahamu huu kwa kuamini kwa dhati kwamba hapana anayepaswa kuabudiwa isipokuwa Mwenyezi Mungu.





Inasikitisha kwamba katika karne hii mpya ya ujasiri, tunaendelea kuvuka mipaka na kugundua tena ulimwengu na fahari zake zote lakini tumemsahau Muumba, na tumesahau kuwa kweli maisha yalikusudiwa kuwa rahisi. Kutafuta uhusiano wetu na Mwenyezi Mungu na kuimarisha uhusiano na Yeye ni muhimu iwapo tutaishi kwa amani na kutupulia mbali pingu zinazotufunga kutuletea maumivu, fadhaa na huzuni.





Uislamu ulifunuliwa kwa watu wote, kila mahali na kwa wakati wote. Haukupelekwa kwa wanaume tu au kwa asili fulani au kabila fulani. Ni njia kamili ya maisha kulingana na mafundisho yanayopatikana katika Kurani na mwenendo sahihi wa Mtume Muhammad. Kwa mara nyingine tena, taarifa hii iko wazi au sio? Itafahamika hivyo iwapo utaelewa mwongozo uliofunuliwa na Muumba kwa viumbe wake. Ni mpango usio na hitilafu wa kupata furaha ya milele katika maisha haya na yajayo.





Kurani na hadithi sahihi huelezea dhana ya Mwenyezi Mungu na kutoa maelezo ya kile kinachoruhusiwa na kile kilichokatazwa. Huelezea misingi ya tabia njema na maadili, na kutoa hukumu ya ibada. Husimulia hadithi kuhusu Mitume na watangulizi wetu wema, na huelezea Pepo na Jehanamu. Mwongozo huu uliteremshiwa wanadamu wote, na Mwenyezi Mungu mwenyewe anasema kwamba hataki kuwaweka wanadamu katika dhiki.





“Hapendi Mwenyezi Mungu kukutieni katika taabu; bali anataka kukutakaseni na kutimiza Neema Yake juu yenu ili mpate kushukuru.” (Kurani 5:6)





Tunaporudi na kumuomba Mungu, Yeye husikiliza na kujibu, na papo hapo ndipo ukweli ambao ni Uislamu, imani halisi ya kumpwekesha Mungu mmoja tu, hutudhihirikia. Hii yote iko wazi, na haipaswi kutatiza, lakini cha kusikitisha, sisi, wanadamu, tuna njia ya kufanya mambo kuwa magumu. Sisi ni wakaidi hali ya kuwa Mwenyezi Mungu daima huendelea kutuachia njia wazi kwa ajili yetu. 





Kukubali Uislamu kuwa dini moja ya kweli inapaswa kuwa rahisi. Hakuna Mungu mwingine isipokuwa Allah. Ni nini kinachoweza kuwa wazi kuliko taarifa hiyo? Hakuna jambo lisiloweza kueleweka, lakini wakati mwingine kwa kujaribu kufafanua upya mfumo wa imani kunaweza kuleta vitisho na hatari zenye vizuizi. Wakati mtu anakusudia kufanya Uislamu ni dini yake ya hiari aghlabu hushindwa kuukubali kwa sababu mbalimbali hata kama mioyo yao inawaambia ni ukweli.





Hivi sasa, ukweli wa Uislamu umefunikwa na kile kinachoonekana kuwa seti ya amri na kanuni ambazo zinaonekana kuwa ngumu kutimiza. Waislamu hawanywi pombe, Waislamu hawali nyama ya nguruwe, wanawake wa Kiislamu ni lazima wavae mitandio, Waislamu ni  lazima wasali mara tano kila siku. Wanaume na wanawake hujikuta wakitoa nyudhuru kama hizi, "Nisingeweza kuacha kunywa", au "Ningeona ugumu kusali kila siku seuze mara tano".





Hata hivyo, ukweli wa mambo ni kwamba pindi mtu anapokubali kuwa hapana mungu ila Allah na kukuza uhusiano na Yeye, basi masharti na kanuni huwa hazina thamani. Ni njia ya polepole ya kutaka kumridhisha Mwenyezi Mungu. Kwa wengine kukubali mwongozo wa maisha ya furaha huwachukua siku, hata saa, lakini kwa wengine huweza kuwachukua wiki, miezi, au hata miaka. Safari ya kila mtu katika Uislamu ni tofauti. Kila mtu ana upekee na uhusiano wa kila mtu na Mwenyezi Mungu unakuja kupitia matukio fulani ya kipekee. Safari moja sio sahihi zaidi kuliko nyingine.





Watu wengi wanaamini kuwa madhambi yao ni makubwa sana na ya mara kwa mara ambayo Mwenyezi Mungu hawezi kuyasamehe kamwe. Wanasita kukubali kile wanachojua ni ukweli kwa sababu wanaogopa kuwa hawataweza kujidhibiti na kuacha kufanya madhambi au uhalifu. Hata hivyo, Uislamu ni dini ya msamaha na Mwenyezi Mungu anapenda kusamehe. Ingawa madhambi ya wanadamu huweza kufikia mawingu angani, Mwenyezi Mungu atasamehe na ataendelea kusamehe hadi Dakika ya Mwisho itakapotufikia.





Iwapo mtu anaamini kwa dhati kwamba hakuna mungu ila Allah, anapaswa kuukubali Uislamu bila kuchelewa. Hata kama wanaamini wataendelea kutenda dhambi, au ikiwa kuna vipengele fulani vya Uislamu hawavielewi kwa ukamilifu. Imani ya Mungu mmoja ni imani muhimu sana katika Uislamu na endapo mtu ataimarisha uhusiano na Mungu, mabadiliko yatatokea katika maisha yao; mabadiliko ambayo hawangeamini yangewezekana.





Katika makala ifuatayo tutajifunza kuwa kuna dhambi moja tu lisilosameheka na kwamba Mungu ni Mwingi wa Rehema, Mwenye Kusamehe tena na tena.





Tulihitimisha sehemu ya 1 ya makala hii kwa kupendekeza kwamba iwapo mtu anaamini kweli hapana mungu mwingine isipokuwa Allah, anapaswa kuukubali Uislamu mara moja. Kadhalika, tunaweka wazi ya kuwa Uislamu ni dini ya msamaha. Haijalishi ni madhambi mangapi ameyafanya mtu, asiweze kusamehewa. Mwenyezi Mungu ni mwingi wa Kusamehe, Mwingi wa Rehema na Kurani inasisitiza sifa hizi zaidi ya mara 70.





“Na ni vya Mwenyezi Mungu vyote vilivyomo katika Mbingu na vilivyomo katika Ardhi. Yeye humsamehe na humuadhibu amtakaye, na Mwenyezi Mungu ni Msamehevu, Mwenye kurehemu.” (Kurani 3:129)





Hata hivyo, kuna dhambi moja ambalo Mungu hatolisamehe na hilo ni dhambi la kumshirikisha Mwenyezi Mungu na washirika au wasaidizi wengine. Muislamu anaamini kuwa Mwenyezi Mungu ni Mmoja, hana washirika, vizazi, au wasaidizi. Yeye ndiye Pekee anayestahiki kuabudiwa.





“Sema (Ewe Muhammad), Yeye Mwenyezi Mungu ni wa pekee. Mwenyezi Mungu Mkusudiwa (Mwenye kutosheleza mahitaji yote, Ambaye viumbe vyote humhitaji, Hali na wala hanywi). Hakuzaa wala hakuzaliwa; Wala hana anayefanana naye hata mmoja.” (Kurani 112)





“Hakika Mwenyezi Mungu hasamehi kushirikishwa, na husamehe yaliyo duni ya hilo kwa amtakaye...” (Kurani 4:48)





Inaweza kuonekana ni jambo la ajabu kusema kuwa Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa Rehema, na kusisitiza kuwa Uislamu ni dini ya msamaha huku pia ukisema kuna dhambi moja halisameheki. Hili sio jambo geni ama dhana isiyo na mashiko pale unapoelewa kuwa dhambi hili kubwa haliwezi kusameheka iwapo mtu atakufa bila kutubia kwa Mwenyezi Mungu. Wakati wowote, hadi mtu mwenye dhambi avute pumzi yake ya mwisho, anaweza kumgeukia Mungu kwa dhati na kuomba msamaha, akijua kwamba hakika Mungu ni Mwingi wa Rehema na Mwenye kusamehe. Toba ya kweli inauhakikisha msamaha wa Mungu.





“Waambie wale walio kufuru, wakikoma (kukufuru) watasamehewa yaliyo kwisha pita...” (Kurani 8:38)





Mtume Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie, alisema: "Mwenyezi Mungu atakubali toba ya mja wake maadamu mtitigo wa kifo bado haujafika kooni mwake.”[1] Kadhalika, Mtume Muhammad alisema, "Uislamu hufuta yaliyokuja kabla yake (madhambi)”.[2]





Kama ilivyojadiliwa katika makala iliyopita, mara kwa mara mtu anapotafakari kuukubali Uislamu huchanganyikiwa au hata kuaibika na madhambi mengi waliyoyatenda wakati wa maisha yao. Watu wengine hushangaa ni vipi wanaweza kuwa watu wema, wenye maadili ilhali katika giza hujificha wakitenda madhambi yao na uhalifu wao.





Kuukubali Uislamu na kutamka maneno yanayojulikana kama Shahada au ushuhuda wa imani, (Nakiri “La ilah illa Allah, Muhammad rasoolu Allah.”[3]), hufuta rekodi kwenye kitabu cha mtu na kuwa safi. Anakuwa kama mtoto mchanga, huru kwa kutokuwa na dhambi kabisa. Ni mwanzo mpya, ambao madhambi ya zamani ya mtu hayawezi kamwe kumshika mtu mateka. Hakuna haja ya kuandamwa na madhambi yaliyotangulia. Kila Muislamu mgeni hutulika mzigo wake wa madhambi na kuwa huru kuishi maisha kulingana na imani ya kimsingi kwamba Mungu ni Mmoja





Pindi mtu akiachiliwa huru na hofu ya kuwa madhambi yao ya zamani au mtindo wao wa maisha unawazuia kuishi maisha mazuri, ndipo njia ya kuukubali Uislamu aghlabu inakuwa rahisi. Kujua kuwa Mwenyezi Mungu anaweza kumsamehe mtu yeyote, kwa lolote, kwa hakika ni tarajio linalofariji. Walakini, kuelewa umuhimu wa kutoabudu kitu chochote au mtu mwingine yeyote isipokuwa Mwenyezi Mungu ni jambo kuu kwa sababu ndio msingi wa Uislamu.





Mungu hakuumba wanadamu isipokuwa wamuabudu yeye peke yake (Kurani 51:56) na kujua jinsi ya kuweka ibada hiyo kuwa safi na isiyochafuliwa ni muhimu. Hata hivyo, maelezo yake aghlabu yatafahamika baada ya mtu kutambua ukweli adhimu wa njia ya maisha ambayo ni Uislamu.





“Na fuateni yaliyo bora kabisa katika yale yaliyo teremshwa kwenu kutoka kwa Mola wenu Mlezi, kabla haijakujieni adhabu kwa ghafla, na hali hamtambui. Isije ikasema nafsi: Ee majuto yangu kwa yale niliyo poteza upande wa Mwenyezi Mungu, na hakika nilikuwa miongoni mwa wanao fanya maskhara.” (Kurani 39:55-56)





Pindi tu mtu anapokubali ukweli wa Uislamu, na hivyo kukubali kwamba hapana mungu ila Mwenyezi Mungu Pekee, ana wakati wa yeye kujifunza kuhusu dini yake. Ana wakati wa yeye kuelewa uzuri wa mvuto na usahali wa Uislamu, pamoja na kujifunza kuhusu mitume na wajumbe wote wa Uislamu akiwemo mtume wa mwisho, Mtume Muhammad. Iwapo angepitisha Mwenyezi Mungu kwamba maisha ya mtu yangemalizika mara tu baada ya kukubali Uislamu inaweza kuonekana kama ishara ya huruma ya Mwenyezi Mungu; mtu safi kama mtoto mchanga atajaaliwa pepo ya milele; kwa rehema ya Mwenyezi Mungu, na hekima Yake isiyo na kikomo.





Wakati mtu anapotafakari kuukubali Uislamu, vizuizi vingi ambavyo alivifikiria sio chochote zaidi ya udanganyifu na hila kutoka kwa Shetani. Ni wazi kwamba mara tu mtu anapochaguliwa na Mungu, Shetani atafanya kila awezalo ili ampotoshe mtu huyo na kuwashambulia kwa minong'ono midogo na wasiwasi. Dini ya Uislamu ni zawadi, na kama vile zawadi nyingine yoyote lazima ikubaliwe, na ifunguliwe kabla ya kudhihirishwa  thamani halisi ya yaliyomo kufunuliwa. Uislamu ni njia ya maisha ambayo inafanikisha ndoto ya kupata neema ya milele Akhera. Hapana mungu ila Mwenyezi Mungu, Mmoja Pekee, wa Kwanza na wa Mwisho. Kumjua Yeye ndio ufunguo wa mafanikio na kuukubali Uislamu ni hatua ya kwanza katika safari ya kuelekea Akhera.



Machapisho ya hivi karibuni

Uislamu Ni dini ya ma ...

Uislamu Ni dini ya maumbile na akili na furaha

UJUMBE KUTOKA KWA MUH ...

UJUMBE KUTOKA KWA MUHUBIRI MUISLAMU KWA MKRISTO

FADHILA YA KUFUNGA SI ...

FADHILA YA KUFUNGA SIKU SITA ZA SHAWAL