Sunnah, kwa mujibu wa wasomi wa hadithi, ni kila kilichopokewa kutoka kwa Mtume kwa kauli zake, matendo yake, idhini zake za kimyakimya, utu wake, maelezo ya kimwili au wasifu wake. Haijalishi ikiwa habari inayohusiana inarejelea kitu kabla ya kuanza kwa utume wake wa kinabii, au baada yake.
Ufafanuzi wa maana hii:
Kauli za Mtume ni pamoja na kila alichosema Mtume kwa sababu mbalimbali katika nyakati tofauti. Kwa mfano, alisema:
“Hakika vitendo ni nia, na kila mtu atapata kulingana na alilokusudia.”
Matendo ya Mtume yanajumuisha kila alichofanya Mtume ambacho kilihusishwa na sisi kwa Maswahaba zake. Hii ni pamoja na jinsi alivyotawadha, jinsi alivyoswali, na jinsi alivyohiji.
Ridhaa za kimyakimya za Mtume ni pamoja na kila kitu ambacho Maswahaba wake walisema au walichofanya ambacho aidha alionyesha upendeleo kwake au angalau hakukipinga. Chochote ambacho kilikuwa na idhini ya kimyakimya ya Mtume ni sawa na kitu chochote alichosema au alichofanya mwenyewe.
Mfano wa hayo ni idhini waliyopewa Maswahaba walipotumia busara zao katika kuamua wakati wa kuswali kipindi cha Vita vya Bani Quraydhah. Mtume wa Mwenyezi Mungu aliwaambia:
“Mmoja wenu asiswali swalah yake ya alasiri mpaka afike Bani Quraizhah.”
Masahaba hawakufika Bani Quraydhah mpaka baada ya machweo. Baadhi yao waliyachukulia maneno ya Mtume kihalisi na wakaahirisha swala ya Alasiri, wakisema: “Hatutaswali mpaka tufike huko.” Wengine walielewa kwamba Mtume alikuwa akiwaambia kuwa wafanye haraka katika safari yao, hivyo wakasimama na kuswali Swalah ya Alasiri kwa wakati wake.
Mtume alielewa kuhusu yale makundi mawili yalichokuwa yameamua, lakini hakukosoa kundi hata moja kati yao.
Ama kwa wasifu wa Mtume, hii itajumuisha kauli ifuatayo ya Aisha (radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake):
“Mtume wa Mwenyezi Mungu hakuwa mchafu wala muovu, wala hakuwa na sauti kubwa sokoni. Hangeweza katu kulipa unyanyasaji wa wengine kwa unyanyasaji wake mwenyewe. Badala yake, alikuwa mvumilivu na mwenye kusamehe.”
Maelezo ya kimwili ya Mtume yanapatikana katika kauli kama ile iliyosimuliwa na Anas (radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake):
“Mtume wa Mwenyezi Mungu hakuwa mrefu kupita kiasi wala hakuwa mfupi. Hakuwa mweupe sana wala mweusi. Nywele zake hazikuwa za kujikunja kupita kiasi wala zilizonyooka.”
Uhusiano baina ya Sunnah na Ufunuo
Sunnah ni ufunuo kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwenda kwa Mtume wake. Mwenyezi Mungu anasema katika Kurani:
“…na aliyo kuteremshieni katika Kitabu na hikima…” (Kurani 2:231)
Hekima inahusu Sunnah. Mwanafaqihi mkubwa al-Shafi’i anasema: “Mwenyezi Mungu anakitaja Kitabu ambacho ni Quran. Nimesikia kutoka kwa watu ambao ninawaona kuwa wana mamlaka juu ya Kurani kwamba Hekima ni Sunnah ya Mtume wa Mwenyezi Mungu." Mungu anasema:
Hakika Mwenyezi Mungu amewafanyia hisani kubwa Waumini pale alipotuma Mtume miongoni mwao kutoka miongoni mwao, anaye wasomea Aya zake na awatakase na kuwafundisha Kitabu na hikima.
Imebainika kutokana na aya zilizotangulia kwamba Mwenyezi Mungu alimfunulia Mtume wake Kurani na Sunnah, na kwamba alimuamuru kuzifikisha zote mbili kwa watu. Hadithi ya Mtume pia inathibitisha kuwa Sunnah ni ufunuo. Imesimuliwa kutoka kwa Mak’hul kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu alisema:
“Mwenyezi Mungu alinipa Kurani na yaliyo kama hayo kutokana na hekima.”
Al-Miqdam b. Ma’di Karab anasimulia kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu alisema:
“Nimepewa Kitabu pamoja na kitu mfano wake.”
Hisani b. Atiyyah anasimulia kwamba Jibrili alikuwa akimjia Mtume na Sunnah kama vile alivyokuwa akimjia na Kurani.
Maoni yanayotoka kwa Mtume hayakuwa tu mawazo yake mwenyewe au mijadala juu ya jambo; ni kile ambacho Mungu alimfunulia. Kwa njia hii, Mtume alikuwa tofauti na watu wengine. Aliungwa mkono na ufunuo. Alipotumia fikra zake mwenyewe na kuwa sahihi, Mungu huthibitisha, na ikiwa atafanya kosa katika kufikiria kwake, Mungu alikuwa akimsahihisha na kumwongoza kwenye kweli.
Kwa sababu hii, inasimuliwa kwamba Khalifa Umar alisema akiwa kwenye mimbari: “Enyi watu! Maoni ya Mtume wa Mwenyezi Mungu yalikuwa sahihi kwa sababu tu Mwenyezi Mungu alimfunulia. Ila kwa maoni yetu, si chochote ila ni fikra na dhana tu.”
Ufunuo alioupata Mtume ulikuwa wa aina mbili:
A. Ufunuo wa taarifa: Mwenyezi Mungu humjulisha jambo kwa njia ya ufunuo kwa namna moja au nyingine kama ilivyotajwa katika aya ifuatayo ya Kurani:
“Na haikuwa kwa mwanaadamu kwamba Mwenyezi Mungu amsemeze ila kwa Wahyi (Ufunuo), au kwa nyuma ya pazia, au kumtuma Mjumbe. Naye humfunulia ayatakayo kwa idhini yake. Hakika Yeye ni Mtukufu, Mwenye hikima.” (Kurani 42:51)
Aishah alisimulia kwamba al-Harith b. Hisham alimuuliza Mtume jinsi ufunuo unavyomjia , na Mtume akajibu:
“Wakati mwingine, malaika huja kwangu kama mlio wa kengele, na hii ndiyo huwa ngumu zaidi kwangu. Inanielemea na ninaiweka kwenye kumbukumbu anayosema. Na wakati mwingine malaika anakuja kwangu katika umbo la mwanadamu na kusema nami na ninaweka kwenye kumbukumbu anayosema.”
Aishah anasema:
“Niliwahi kumwona wakati ufunuo ukimjia siku ya baridi sana. Ulipoisha, uso wake ulikuwa umejaa jasho.”
Wakati mwingine, alikuwa akiulizwa juu ya jambo fulani, lakini alikuwa akikaa kimya hadi ufunuo ulipomjia. Kwa mfano, wapagani wa Makkah walimuuliza kuhusu roho, lakini Mtume alinyamaza mpaka Mwenyezi Mungu alipoteremsha:
Na wanakuuliza khabari za Roho. Sema: 'Roho ni katika mambo ya Mola wangu Mlezi. Nanyi hamkupewa katika ilimu ila kidogo tu'. (Kurani 17:85)
Pia aliulizwa jinsi ya urithi unavyogawanywa, lakini hakujibu mpaka Mungu alipomfunulia:
“Mwenyezi Mungu anakuusieni juu ya watoto wenu…” (Kurani 4:11)
B. Ufunuo wa Uthibitisho: Hapa ndipo Mtume alipotumia hukumu yake katika jambo. Iwapo mawazo yake yalikuwa sahihi, ufunuo ulimjia kuthibitisha, na kama hakuwa sahihi, ufunuo ungekuja kumsahihisha, na kuwa kama ufunuo mwingine wowote wenye kuelimisha. Tofauti pekee hapa ni kwamba ufunuo ulikuja kama matokeo ya kitendo ambacho Mtume alikifanya kwanza peke yake.
Katika matukio kama hayo, Mtume aliachwa atumie busara yake katika jambo. Ikiwa angechagua kilicho sawa, basi Mungu angethibitisha chaguo lake kupitia ufunuo. Ikiwa angechagua kwa makosa, Mungu angemsahihisha ili kulinda uaminifu-maadili ya imani. Mwenyezi Mungu asingemruhusu Mtume Wake kufikisha ujumbe usio sahihi kwa watu wengine, kwa kuwa hatua hii itawafanya wafuasi wake walifuate kosa hilo. Hili litakuwa kinyume na hekima ya kutuma Mitume, ambayo ni kuwa watu hawatakuwa na hoja juu ya Mwenyezi Mungu. Kwa njia hii, Mtume alilindwa kutokana na kutumbukia kwenye upotofu, kwani kama akikosea, ufunuo ulikuja kumsahihisha.
Maswahaba wa Mtume walijua kuwa uidhinishaji wa kimyakimya wa Mtume kwa hakika ulikuwa ni ridhaa ya Mwenyezi Mungu kwa sababu kama wangefanya jambo ambalo lipo kinyume na Uislamu wakati wa uhai wa Mtume, ufunuo ungeshuka na kulaani waliyoyafanya.
Jabir alisema: “Tulikuwa tukifanya jambo la kukatiza[1] zamani tangu Mtume wa Mwenyezi Mungu alipokuwa hai.” Sufyan, mmoja wa wapokezi wa Hadiyth hii, alisema: “Kama kitu kama hiki kingeharamishwa, Kurani ingekiharamisha.
Tofauti kati ya Sunnah na Kurani
Kurani ndio msingi wa Sheria ya Kiislamu. Ni hotuba ya Mwenyezi Mungu ya kimiujiza iliyofunuliwa kwa Mtume, rehema na baraka za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, kwa njia ya Malaika Gabrieli. Imepitishwa kwetu kwa minyororo mingi ya mamlaka hivyo ukweli wake wa kihistoria hauna shaka. Imeandikwa katika juzuu yake yenyewe, na usomaji wake ni aina ya ibada.
Sunnah, ni kila kitu isipokuwa Kurani kilichotoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu. Inafafanua na kutoa maelezo kwa sheria zinazopatikana katika Kurani. Pia inatoa mifano ya matumizi ya vitendo vya sheria hizi. Vile vile ni ufunuo wa moja kwa moja kutoka kwa Mwenyezi Mungu, au maamuzi ya Mtume ambayo yalithibitishwa kwa ufunuo. Kwa hiyo, chanzo cha Sunnah zote ni ufunuo.
Kurani ni ufunuo ambao unasomwa rasmi kama ibada, na Sunnah ni ufunuo ambao hausomwi rasmi. Sunnah, hata hivyo, ni kama Kurani kwa kuwa ni ufunuo unaopaswa kufuatwa na kuzingatiwa.
Kurani inapendekeza Sunnah kwa njia mbili. Kwa jambo moja, Kurani ina maneno kamili ya Mwenyezi Mungu, asili ya kimiujiza, hadi aya ya mwisho. Sunnah, hata hivyo, si lazima iwe na maneno halisi ya Mwenyezi Mungu, bali maana yake kama ilivyoelezwa na Mtume.
Nafasi ya Sunnah katika Sheria ya Kiislamu
Wakati wa uhai wa Mtume Kurani na Sunnah vilikuwa vyanzo pekee vya Sheria ya Kiislamu.
Kurani inatoa maamrisho ya jumla ambayo yaliunda msingi wa Sheria, bila kuingia katika maelezo yote na sheria ya pili, isipokuwa maagizo machache ambayo yamewekwa pamoja na kanuni za jumla. Maagizo haya hayawezi kubadilika kulingana na muda au kwa mabadiliko ya hali ya watu. Kurani vile vile, imekuja na kanuni za imani, imeweka matendo ya ibada, inataja hadithi za mataifa ya kale, na inatoa miongozo ya maadili.
Sunnah imekuja kwa kuafikiana na Kurani. Inafafanua maana ya kile kisichoeleweka katika maandiko, hutoa maelezo ya kile kinachoonyeshwa kwa maneno ya jumla, inabainisha kwa jumla, na inaelezea maagizo na malengo yake. Sunnah pia inakuja na maamrisho ambayo hayakutolewa na Kurani, lakini haya daima yanawiana na kanuni zake, na daima yanaendeleza malengo ambayo yameainishwa ndani ya Kurani.
Sunnah ni kielelezo cha kivitendo cha yale yaliyomo ndani ya Kurani. Usemi huu una sura nyingi. Wakati mwingine, huja kama kitendo kilichofanywa na Mtume. Wakati nyingine, ni kauli aliyoitoa akijibu jambo fulani. Wakati fulani, inachukua sura ya kauli au kitendo cha mmoja wa Maswahabah ambacho hakukizuiwa wala hakikukipingwa. Kinyume chake, alikaa kimya juu yake au alionyesha idhini yake kwa hilo.
Sunnah inaielezea na kuibainisha Kurani kwa njia nyingi. Inaeleza jinsi ya kufanya ibada na kutekeleza sheria ambazo zimetajwa katika Kurani. Mungu anawaamrisha waumini kusali bila kutaja nyakati ambazo maombi hayo yalipaswa kufanywa au namna ya kuyatekeleza. Mtume Mtukufu alilifafanua hili kupitia maombi yake mwenyewe na kwa kuwafundisha Waislamu jinsi ya kuswali. Akasema: “Swalini kama mlivyoniona nikiswali.”
Mwenyezi Mungu huifanya Hijja kuwa ni wajibu bila ya kueleza taratibu zake. Mtume wa Mwenyezi Mungu anafafanua hili kwa kusema:
“Fanyeni hajj kutoka kwangu”
Mwenyezi Mungu anaufanya ushuru wa Zakah kuwa ni wajibu bila ya kutaja ni aina gani ya mali na mazao yanayotozwa. Mungu pia hataji kiwango cha chini kabisa cha mali kinachofanya ushuru kuwa wa lazima. Sunnah, hata hivyo, inayaweka wazi haya yote.
Sunnah inabainisha kauli za jumla zinazopatikana ndani ya Kurani. Mungu anasema:
“Mwenyezi Mungu anakuusieni juu ya watoto wenu: Fungu la mwanamume ni kama fungu la wanawake wawili…” (Kurani 4:11)
Maneno haya ni ya jumla, yanatumika kwenye kila familia na kumfanya kila mtoto kuwa mrithi wa wazazi wake. Sunnah inaifanya hukumu hii kuwa maalum zaidi kwa kuwatenga watoto wa Mitume. Mtume wa Mwenyezi Mungu alisema:
“Sisi Manabii hatuwachi urithi. Tunachoacha nyuma huwa ni sadaka.”
Sunnah zinaelezea kauli zisizo na sifa ndani ya Kurani. Mungu anasema:
“… na hamkupata maji, basi tayamamuni vumbi lilio safi, na mpake nyuso zenu na mikono yenu… (Kurani 5:6)
Aya haijataja sehemu ya mkono, kutoa fursa ya mtu kuuliza iwapo inafaa kupangusa mikono hadi kwenye kifundo au sehemu ya mbele ya mkono. Sunnah inabainisha hili kwa kuonyesha kuwa ni kwenye kifundo cha mkono kwa sababu hivi ndivyo alivyofanya Mtume wa Mwenyezi Mungu alipotawadha mkavu.
Sunnah pia inakuja ikisisitiza yale yaliyomo ndani ya Kurani au inatoa sheria ya pili kwa sheria iliyotajwa humo. Hii ni pamoja na Hadeeth zote zinazoashiria kuwa Swala, ushuru wa Zaka, saumu na kuhiji ni wajibu.
Mfano wa pale Sunnah inapotoa sheria saidizi kwa amri inayopatikana ndani ya Kurani ni hukumu inayopatikana katika Sunnah kwamba ni haramu kuuza tunda kabla halijaanza kuiva. Msingi wa sheria hii ni kauli ya Kurani:
Msile mali yenu baina yenu kwa dhulma, isipokuwa iwe biashara baina yenu kwa kuridhiana.
Sunnah ina hukumu ambazo hazikutajwa ndani ya Kurani na ambazo haziji kama ufafanuzi wa jambo lililotajwa ndani ya Kurani. Mfano wa hayo ni uharamu wa kula nyama ya punda na nyama ya wanyama wakali. Mfano mwingine wa hili ni uharamu wa kuoa mwanamke na shangazi yake kwa wakati mmoja. Hukumu hizi na nyinginezo zilizotolewa na Sunnah ni lazima zifuatwe.
Wajibu wa Kushikamana na Sunnah
Sharti la kuamini utume ni kukubali kuwa ni kweli kila alichosema Mtume wa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu aliwachagua Mitume wake miongoni mwa waja Wake ili kufikisha Sheria yake kwa wanadamu. Mungu anasema:
“…Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi kuliko wote kujua wapi anaweka ujumbe wake.…” (Kurani 6:124)
Mwenyezi Mungu pia anasema:
“…Basi lipo lolote juu ya Mitume isipo kuwa kubalighisha kwa uwazi?” (Kurani 16:35)
Mtume amehifadhiwa kutokana na upotovu katika matendo yake yote. Mungu ameulinda ulimi wake usiseme chochote isipokuwa ukweli. Mungu amevilinda viungo vyake visifanye lolote isipokuwa lililo sawa.
Mungu amemlinda dhidi ya kuonyesha kibali cha jambo lolote lililo kinyume na Sheria ya Kiislamu. Yeye ndiye aliyekamilika kwa uzuri zaidi kati ya Uumbaji wa Mungu. Hili liko wazi kutokana na jinsi Mwenyezi Mungu anavyomuelezea katika Kurani:
“Naapa kwa nyota inapo tua! Mwenzenu huyu hakupotea, wala hakukosea. Wala hatamki kwa matamanio. Hayakuwa haya ila ni ufunuo ulio funuliwa.” (Kurani 53:1-4)
Tunaona katika Hadiyth kwamba hakuna hali yoyote, hata ijaribiwe vipi, ingeweza kumzuia Mtume kusema ukweli. Kuwa na hasira hakujawahi kuathiri hotuba yake. Hakusema uwongo hata alipokuwa akitania. Masilahi yake mwenyewe hayakumshawishi kamwe ktokusema ukweli. Lengo pekee ambalo alitafuta lilikuwa ni radhi ya Mwenyezi Mungu.
Abdullah b. Amr b. al-Aas alisimulia kwamba alikuwa akiandika kila alichosema Mtume wa Mwenyezi Mungu. Kisha watu wa kabila la Quraish wakamkataza kufanya hivyo, wakasema: "unaandika kila anachokisema Mtume wa Mwenyezi Mungu, naye ni mtu anayesema kwa matamnio na kwa hasira?”
Abdullah b. Amr aliacha kuandika na akamwambia hili Mtume wa Mwenyezi Mungu ambaye alimwambia:
“Andika, kwani kwa Yule Ambaye nafsi yangu imo mkononi Mwake, hakika ukweli utokao katika huu ndiyo haki." ... na kunyooshea kinywa chake.
Kurani, Sunnah, na makubaliano ya mafaqihi yote yanaelekeza kwenye ukweli wa kumtii Mtume wa Mwenyezi Mungu ni wajibu. Mwenyezi Mungu anasema katika Kurani:
“Enyi mlio amini! Mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi. Na mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume, ikiwa mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. …” (Kurani 4:59)