Nakala

Uwezeshaji wa kimungu unalingana na mahitaji ya mwanadamu. Mungu hurahisisha upataji kadiri uhitaji wa wanadamu unavyoongezeka. Hewa, maji, na nuru ya jua ni vya lazima kwa ajili ya kuwepo kwa mwanadamu, na hivyo Mungu ameruhusu kupatikana kwake kwa vyote bila ugumu. Hitaji kuu zaidi la mwanadamu ni kumjua Muumba, na hivyo, Mungu amefanya iwe rahisi kumjua. Ushahidi wa Mungu, hata hivyo, hutofautiana katika asili yake. Kwa njia yake yenyewe, kila kitu katika uumbaji ni uthibitisho wa Muumba wake. Uthibitisho mwingine wa dhahiri sana hadi mtu yeyote wa kawaida anaweza ‘kumwona’ mara moja Muumba, kwa mfano, mzunguko wa uhai na kifo.  Wengine ‘wanaona’ kazi ya mikono ya Muumba katika umaridadi wa nadharia za hisabati, sanjari za ulimwengu mzima wa fizikia, na ukuzi wa kijusi:





"Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi na kukhitalifiana usiku na mchana ziko Ishara kwa wenye akili." (Kurani 3:190)





Kama vile uwepo wa Mungu, wanadamu wanahitaji ushahidi ili kuthibitisha ukweli wa manabii walionena kwa jina Lake. Muhammad, kama manabii waliomtangulia, alidai kuwa nabii wa mwisho wa Mungu kwa wanadamu. Kwa kawaida, ushahidi wa ukweli wake ni tofauti na mwingine. Baadhi ni dhahiri, nyingine huonekana tu baada ya kutafakari kwa kina.





Mwenyezi Mungu anasema ndani ya Kurani:





"…Haikutoshi kwamba Mola wako Mlezi kuwa Yeye ni Shahidi wa kila kitu?" (Kurani 41:53)





Ushahidi wa Kimungu peke yake unatosha bila ushahidi mwingine wowote. Shahidi wa Mungu kwa Muhammad upo katika:





(a)  Ufunuo wa Mungu uliopita kwa mitume wa mwanzo ulitabiri kutokea kwa Muhammad.





(b)  Matendo ya Mungu: miujiza na ‘ishara’ alizozitoa ili kuunga mkono madai ya Muhammad.





Haya yote yalianza vipi katika siku za mwanzo za Uislamu? Waumini wa mwanzo walisadikishwaje kwamba alikuwa nabii wa Mungu?





Mtu wa kwanza kuamini utume wa Muhammad alikuwa mke wake mwenyewe, Khadija. Aliporudi nyumbani akitetemeka kwa hofu baada ya kupata ufunuo wa Mwenyezi Mungu, alikuwa ni faraja yake:





"Kamwe! Mungu hatakuaibisha. Dumisha uhusiano mzuri na watu wa ukoo wako, saidia masikini, wahudumie wageni wako kwa ukarimu, na saidia wale waliopatwa na misiba." (Saheeh Al-Bukhari)





Alimuona mtu kwa mumewe, ambaye Mungu hatamdhalilisha, kwa sababu ya fadhila zake za uaminifu, haki, na kusaidia masikini.





Rafiki yake wa karibu zaidi, Abu Bakr ambaye alikuwa amemfahamu maisha yake yote na alikuwa wakikalibiana kwa kwa rika, aliamini mara tu aliposikia maneno, ‘Mimi ni Mtume wa Mungu’ bila ya uthibitisho wowote wa ziada zaidi ya kitabu kilicho wazi cha maisha ya rafiki yake.





Mtu mwingine ambaye alikubali wito wake kwa kuusikiliza tu, alikuwa ‘Amr’[1]  Anasema:





"Nilikuwa nikifikiri kabla ya Uislamu kwamba watu ni wakosefu na hawakuwa juu ya kitu. Waliabudu sanamu. Wakati huohuo, nilisikia juu ya mtu mmoja akihubiri huko Makka; basi nikaenda kwake…nikamuuliza: ‘Wewe ni nani?’ Akasema: ‘Mimi ni Mtume.’ Nikasema tena: ‘Nabii ni nani?’ Akasema: ‘Mungu amenituma.’ Nikasema: Alikutuma na nini?’ Akasema: ‘Nimetumwa kuunganisha mafungamano, kuvunja masanamu, na kutangaza umoja wa Mwenyezi Mungu, bila kuwa na chochote kinachomshirikisha (katika ibada). Nani yu pamoja nawe katika hili?’ Akasema: ‘Mtu huru na mtumwa (akimaanisha Abu Bakr na Bilal, mtumwa, ambaye alikuwa ameukubali uislam kwa wakati huo)’ Nikasema: ‘Ninakusudia kukufuata wewe.’" (Saheeh Muslim)





Dimad alikuwa mganga wa jangwani aliyebobea katika magonjwa ya akili. Katika ziara yake huko Makka, aliwasikia watu wa Makka wakisema kwamba Muhammad (rehema na baraka za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake) alikuwa mwendawazimu! Akiwa na uhakika na ujuzi wake, alijiambia, ‘Kama ningemkuta mtu huyu, Mungu anaweza kumponya mkononi mwangu.’ Dimad alikutana na Mtume na akasema: ‘Muhammad, ninaweza kumlinda (mtu) anayeugua ugonjwa wa akili au kwa uchawi, na Mwenyezi Mungu humponya amtakaye kwa mkono wangu. Je, unatamani kuponywa?’ Mtume wa Mwenyezi Mungu akajibu, akianza na utangulizi wake wa kawaida wa hotuba zake:





"Hakika sifa na shukrani ni kwa Mungu. Tunamsifu na kumuomba msaada. Anaye muongoza Mwenyezi Mungu hakuna wa kumpoteza, na aliye potea hawezi kuongozwa. Nashuhudia hakuna anayestahiki kuabudiwa ila Mwenyezi Mungu, Yeye ni Mmoja, hana mshirika, na Muhammad ni mja na Mtume wake."





Dimad akiwa ameshtushwa na uzuri wa maneno hayo, akamwomba ayarudie, akasema, ‘Nimesikia maneno ya waganga, wachawi na washairi, lakini sijawahi kusikia maneno ya namna hii, yanafika kwenye kina cha bahari. Nipe mkono wako ili niweke kiapo cha utii wangu kwako juu ya Uislamu.[2]





Baada ya Jibrili kuleta ufunuo wa kwanza kwa Mtume Muhammad, Khadija, mke wake, alimchukua kwenda kumtembelea binamu yake mzee, Waraqa ibn Nawfal, msomi wa masuala ya Biblia, ili kujadiliana nae kuhusu tukio hilo. Waraqa alimtambua Muhammad kutokana na tabiri za Biblia na kuthibitisha:





"Huyu ndiye Mlinzi wa Siri (Malaika Jibrili) aliyekuja kwa Musa." (Saheeh Al-Bukhari)





Uso unaweza kuwa dirisha la roho. Abdullah ibn Salam, rabi mkuu wa Madina wa muda huo, aliutazama uso wa Mtume alipofika Madina, na akasema:





"Pindi nilipoutazama uso wake, nikajua siyo uso wa mtu mwongo!" (Saheeh Al-Bukhari)





      Wengi wa wale waliokuwa karibu na Mtume ambao hawakuukubali Uislamu hawakutilia shaka ukweli wake, lakini walikataa kufanya hivyo kwa sababu nyinginezo. Ami yake, Abu Talib, alimsaidia katika maisha yake yote, alikiri ukweli wa Muhammad, lakini alikataa kujitenga na dini ya babu zake kwa sababu ya aibu na hadhi ya kijamii.





Uchambuzi wa Kimantiki wa Dai Lake


      Kama ilivyojadiliwa hapo awali, Muhammad alitoa dai, ‘Mimi ni Mtume wa Mungu.’ Pengine alikuwa mkweli katika dai lake au hakuwa mkweli. Tutaanza kwa kuangalia dai la mwisho na kuchunguza uwezekano wote uliotolewa na wakosoaji wa zamani na wa sasa, tukijadili baadhi ya maoni yao potofu. Ni ikiwa tu uwezekano mwingine wote umekamilika ambapo mtu anaweza kudai kwamba uwezekano pekee uliobaki ni kwamba ulikuwa kweli katika kile alichodai. Pia tutaangalia Kurani inasemaje kuhusu suala hilo.





. Je, alikuwa Muongo?





Je, inawezekana kwa muongo kudai kwa muda wa miaka 23 kwa uhakika usiotikisika kwamba yeye ni nabii kama Ibrahimu, Musa na Yesu, kwamba hakutakuwako tena manabii baada yake, na kwamba andiko alilotumwa nalo kubaki kuwa muujiza wake wa kudumu hadi mwisho wa nyakati?





Mtu muongo atajikwaa wakati mwingine, labda kwa rafiki, labda kwa watu wa familia yake, mahali fulani atafanya makosa. Ujumbe wake, uliotolewa kwa zaidi ya miongo miwili, wakati mwingine utajipinga wenyewe . Lakini kile tunachokiona katika uhalisia ni kwamba andiko alilolileta linatangaza uhuru kutokana na kutofautiana kwa ndani, ujumbe wake ulibaki thabiti katika utume wake wote, na hata katikati ya vita, alitangaza utume wake![1]





Hadithi ya maisha yake ni kitabu kilichohifadhiwa kwa uwazi kwa kila mtu kuweza kukisoma. Kabla ya Uislamu, alijulikana sana kwa watu wake mwenyewe kuwa ni mwaminifu na mwenye kutegemewa, mtu mwaminifu, mtu mwadilifu, asiyesema uongo.[2] Ilikuwa ni kwa sababu hii wakamwita "Al-Ameen", au "Mwaminifu" Alipinga vikali kusema uongo na akaonya dhidi yake. Je, ingewezekana kwake kusema uongo thabiti kwa muda wa miaka 23, uongo wa kutisha sana ambao ungemfanya kuwa mtu wa kutengwa na jamii, wakati hakujulikana kamwe mwenye kusema uongo hata mara moja kwenye jambo lolote? Ni kinyume na saikolojia ya waongo.





Kama mtu angeuliza kwa nini mtu anajidai mtume na kusema uongo, jibu lao lingeweza kuwa moja kati ya mawili:





1)    Umaarufu, utukufu, mali, na hadhi.





2)    Maendeleo ya maadili.





      Kama tungesema kuwa Muhammad alidai utume kwa ajili ya umaarufu na hadhi, tungeona kuwa kile kilichotokea kilikuwa kinyume kabisa. Muhammad, kabla ya madai yake ya Utume, alikuwa na hadhi ya juu katika nyanja zote. Alikuwa wa kabila tukufu zaidi, wa familia tukufu, na alijulikana kwa ukweli wake. Baada ya madai yake, alikua mtu aliyetengwa na jamii. Kwa muda wa miaka 13 huko Makka, yeye na wafuasi wake walikabiliana na mateso makali, ambayo yalipelekea vifo vya baadhi ya wafuasi wake, kejeli, vikwazo, na kukatizwa mawasiliano na jamii.





      Kulikuwa na njia nyingine nyingi ambazo mtu angeweza kupata umaarufu katika jamii ya wakati huo, hasa kutokana na ushujaa, na ushairi. Kama Muhammad angetoa madai kwamba yeye mwenyewe ndiye aliyeandika Kurani, kama itakavyoelezwa baadaye, hilo lingetosha kwa jina lake na ushairi wake kuwekwa katika dhahabu na kutundikwa ndani ya Al-Kaaba milele, watu kutoka duniani kote wakimtukuza. Bali, alitangaza kwamba yeye hakuwa mwanzilishi wa ufunuo huu na kwamba ulitoka kwa Yule aliye juu, na kumfanya adhihakiwe katika wakati wake mpaka wakati wetu.





      Mtume alikuwa mume wa mfanyabiashara tajiri, na alifurahia starehe za maisha zilizopatikana kwake katika wakati wake. Lakini baada ya madai yake ya utume, akawa miongoni mwa watu masikini. Siku zilipita bila moto wa jiko kuwashwa ndani ya nyumba yake, na wakati fulani njaa ilimpeleka msikitini kwa matumaini ya kupata riziki. Viongozi wa Makka katika zama zake walimuahidi utajiri wa dunia ili aache ujumbe wake. Kwa kuwajibu ahadi yao, alisoma aya za Kurani.. Zifuatazo ni baadhi ya aya hizi:





"Hakika walio sema: Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu! Kisha wakanyooka sawa, hao huwateremkia Malaika wakawaambia: Msiogope, wala msihuzunike; nanyi furahini kwa Pepo mliyo kuwa mkiahidiwa. Sisi ni vipenzi vyenu katika maisha ya dunia na katika Akhera, na humo mtapata kinacho tamaniwa na nafsi zenu, na humo mtapata mtakavyo vitaka.Ni takrima itokayo kwa Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.Na ni nani mbora wa kusema kuliko aitaye kwa Mwenyezi Mungu na akatenda mema, na akasema: Hakika mimi ni katika Waislamu?  Mema na maovu hayalingani. Pinga uovu kwa lilio jema zaidi. Hapo yule ambaye baina yako naye pana uadui atakuwa kama rafiki jamaa wa kukuonea uchungu.  Lakini hawapewi wema huu ila wanao subiri, wala hawapewi ila wenye bahati kubwa." (Kurani 41:30-35)





Kama mtu angesema kuwa Muhammad alisema uongo na kudai utume ili kuleta mageuzi ya kimaadili na kidini katika jamii iliyojaa maovu, hoja hii yenyewe haina maana, kwani mtu anawezaje kuleta mageuzi ya kimaadili kwa njia ya uongo. Iwapo Muhammad alikuwa na shauku kubwa sana la kusimamisha na kuhubiri maadili na ibada iliyonyooka kwa Mungu Mmoja, basi je, angeweza kujidanganya kwa kufanya hivyo? Iwapo tutasema kuwa hilo haliwezekani, jibu pekee ni kwamba alikuwa anaongea ukweli. Uwezekano mwingine uliobaki ni kwamba alikuwa mwendawazimu.


Alikuwa Mwendawazimu?


Mtu ambaye amejihusisha na wagonjwa wa akili anajua kuwa watu wanaweza kutambuliwa kutokana na dalili zao. Muhammad hakuonyesha dalili zozote za ukichaa kipindi chochote cha maisha yake Hakuna rafiki, mke, au mwanafamilia aliyemshuku au kumwacha kwa sababu ya wazimu. Na kuhusu athari za Mtume kupokea ufunuo, kama vile kutokwa na jasho na mengine kama hayo, ilitokana na uzito wa Ujumbe ambao alilazimika kuubeba na sio kutokana na kifafa au tukio la ukichaa...





Kinyume chake kabisa, Muhammad alihubiri kwa muda mrefu na kuleta Sheria isiyojulikana katika ukamilifu wake na ugumu wake kwa Waarabu wa kale. Ikiwa nabii alikuwa mwendawazimu, ingekuwa dhahiri kwa wale walio karibu yake wakati mmoja katika kipindi cha miaka ishirini na tatu. Ni lini katika  historia mtu mwendawazimu alihubiri ujumbe wake wa kumwabudu Mungu Mmoja kwa muda wa miaka kumi, mitatu ambayo yeye na wafuasi wake walikaa uhamishoni, na hatimaye akawa mtawala wa nchi yake? Ni mwendawazimu gani amewahi kuziteka nyoyo na akili za watu waliokutana naye na kupata heshima ya wapinzani wake?





Zaidi, masahaba wake wa karibu, Abu Bakr na Umar walitambuliwa kwa uwezo wao, uungwana, ujuzi, na uhodari. Walikuwa tayari kutoa chochote kwa ajili ya dini aliyoileta. Wakati mmoja, Abu Bakr, alileta mali zake zote anazomiliki kwa Muhammad, rehema na baraka za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na alipoulizwa alichowaachia familia yake, akajibu, ‘Niliwaachia Mungu na Mtume Wake!’





Abu Bakr, mfanyabiashara kwa taaluma, baada ya kuchaguliwa kuwa mtawala wa Waarabu wote baada ya Muhammad, alitumia dirhamu mbili tu juu yake na familia yake!





Umar akawa mtawala wa Uarabuni baada ya Abu Bakr na akaiteka Syria, Misri, na kuzitiisha Dola za Uajemi na Rumi. Alikuwa mtu anayejulikana kwa uadilifu wake. Je, mtu anawezaje kupendekeza watu hawa walikuwa wanamfuata mtu mwenye kichaa?





Mungu anapendekeza: simama mbele ya Mungu bila upendeleo au imani zilizotungwa hapo awali, na ujadiliane na mtu mwingine au ulifikirie mwenyewe, mtume huyu hana wazimu, yuko thabiti leo kama ulivyomjua kwa miaka arobaini.





"Sema: Mimi nakunasihini kwa jambo moja tu - ya kwamba msimame kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, wawili-wawili na mmoja-mmoja; kisha mfikiri. Mwenzenu huyu hana wazimu. Yeye si chochote ila ni Mwonyaji kwenu kabla ya kufika adhabu kali.’" (Kurani 34:46)





Watu wa Makka wa zamani walikataa mwito wake kutokana na ushabiki wa kikabila, na hawakuwa wakweli katika shutuma zao za kichaa chake. Hata leo, watu wengi wanakataa kumkubali Muhammad kama nabii kwa sababu tu alikuwa Mwarabu na kujifariji wenyewe kwa kusema lazima alikuwa mwendawazimu au alifanya kazi na shetani. Chuki yao kwa Waarabu inatafsiri katika kumkataa kwao Muhammad, ingawa Mwenyezi Mungu anasema:





"Bali huyu amekuja kwa Haki, na amewasadikisha Mitume." (Kurani 37:37)





Ingawa Waarabu wapagani walimjua Muhammad vizuri sana, lakini bado walimtupia tuhuma za ukichaa, kwakuwa waliichukulia dini yake kuwa ni kufuru dhidi ya mapokeo ya wazee wao.





"Na wanapo somewa Aya zetu zilizo wazi wanasema: Huyu si chochote ila ni mtu anaye taka kukuzuieni na waliyo kuwa wakiabudu baba zenu. Na wakasema: Haya si chochote ila ni uwongo ulio zuliwa. Na walio kufuru waliiambia Haki ilipo wajia: Haya si chochote ila ni uchawi ulio dhaahiri. Wala hatukuwapa Vitabu wavisome, wala hatukuwatumia Mwonyaji kabla yako wewe. Na walikadhibisha walio kuwa kabla yao. Na hawakufikilia hata sehemu moja katika kumi ya tulivyo wapa hao. Nao waliwakadhibisha Mitume wangu. Basi kuangamiza kwangu kulikuwa namna gani!" (Kurani 34:43-45)





Alikuwa Mshairi?


Mwenyezi Mungu anataja tuhuma zao ndani ya Kurani na anajibu:





"Au wanasema: Huyu ni mtunga mashairi, tunamtarajia kupatilizwa na dahari. Sema: Tarajieni, na mimi pia ni pamoja nanyi katika kutarajia.  Au hizo akili zao ndio zinawaamrisha haya, au wao basi ni watu majeuri tu?  Au ndio wanasema: Ameitunga hii! Bali basi tu hawaamini!" (Kurani 52:30-33)





Mwenyezi Mungu anawaeleza washairi wa wakati huo ili Mtume afananishwe nao:





"Na watungaji mashairi ni wapotofu ndio wanawafuata. Je! Huwaoni kwamba wao wanatangatanga katika kila bonde?[1], Na kwamba wao husema wasiyo yatenda? Isipo kuwa wale walio amini, na wakatenda mema, na wakamkumbuka Mwenyezi Mungu kwa wingi, na wakajitetea wanapo dhulumiwa. Na wanao dhulumu watakuja jua mgeuko gani watakao geuka." (Kurani 26:224-227)





Washairi wa Kiarabu walikuwa mbali zaidi na ukweli, waliongelea juu ya mvinyo, wanawake, vita, na tafrija, tofauti na Mtume ambaye analingania kwenye tabia njema, kumtumikia Mwenyezi Mungu, na kuwasaidia masikini. Muhammad alifuata mafundisho yake kabla ya mtu mwingine yeyote tofauti na washairi wa zamani au wanafalsafa wa siku hizi.





Kurani aliyoisoma Mtume ilikuwa tofauti na mashairi yoyote kwa mtindo wake. Waarabu wa wakati huo walikuwa na sheria kali kuhusiana na mahadhi, kibwagizo, silabi na hitimisho la kila ubeti wa ushairi. Kurani haikuafikiana na kanuni zozote zilizokuwa zikijulikana kwa wakati huo, lakini wakati huo huo, ilishinda aina yoyote ya maandiko ambayo Waarabu waliwahi kuyasikia. Baadhi yao walikuwa waislam baada ya kusikia Aya chache tu za Kurani , kutokana na ujuzi wake kuwa kiini cha kitu kizuri ambacho hakiwezi kutengenezwa na kiumbe yeyote.





Muhammad hakujulikana kamwe kuwa mkutunga shairi kabla ya Uislamu au baada ya utume. Bali Mtume alichukia sana jambo hilo. Mkusanyiko wa kauli zake, unaoitwa Sunna, umehifadhiwa madhubuti na upo tofauti kabisa katika maudhui yake ya kifasihi ukilinganisha na Kurani . Ghala la mashairi ya Kiarabu halina nakala zozote za Muhammad.





Alikuwa Mchawi?


Mtume Muhammad hakuwahi kujifunza wala kufanya uchawi. Badala yake, alilaani kitendo cha uchawi na kuwafundisha wafuasi wake jinsi ya kutafuta ulinzi dhidi yake.





Wachawi wana uhusiano mkubwa na shetani. Ushirikiano wao unawaruhusu kudanganya watu. Mashetani hueneza uwongo, dhambi, uchafu, uasherati, uovu, na kuharibu familia. Kurani inabainisha wale ambao mashetani huwashukia:





"Je! Nikwambieni nani wanawashukia Mashet'ani?   Wanamshukia kila mzushi mkubwa mwingi wa dhambi.  Wanawapelekea yale wanayo yasikia; na wengi wao ni waongo." (Kurani 26:221-223)





Mtume Muhammad alijulikana na kutambuliwa kuwa mtu mwadilifu mkweli wa neno lake ambaye hakujulikana kuwa amewahi kusema uwongo. Aliamrisha maadili mema na adabu njema. Hakuna mchawi katika historia ya kidunia aliyeleta maandiko kama ya Kurani au Sheria kama yake.



Machapisho ya hivi karibuni

Uislamu Ni dini ya ma ...

Uislamu Ni dini ya maumbile na akili na furaha

UJUMBE KUTOKA KWA MUH ...

UJUMBE KUTOKA KWA MUHUBIRI MUISLAMU KWA MKRISTO

FADHILA YA KUFUNGA SI ...

FADHILA YA KUFUNGA SIKU SITA ZA SHAWAL

Masuala kumi muhimu n ...

Masuala kumi muhimu na mafupi kuhusu mwezi wa Muharram